Friday, October 13, 2017

MUZIKI ENZI ZA NYERERE

LEO ni miaka 18 toka Kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mungu amlaze pema Mwalimu. Vyombo vya habari vinaeleza mengi kuhusu hali ya maisha ilivyokuwa zama za Enzi ya Nyerere, kwa tuliekuweko enzi hizo tunaona mengi yanayosemwa ni ya kweli na mengi si sahihi, mengine yanatungwa ili kufanikisha azma fulani, mengine si kweli kwa kuwa mtoa habari hakuweko au alihadithiwa na mtu ambaye hakuwa mkweli au pengine hakumbuki vizuri, lakini hiyo ndio hali halisi kutokana na kuwa mengi yaliyokuwa yakitendeka wakati ule hayakuwekwa katika maandishi kutokana na uwoga wa kusema ukweli enzi hizo, uchache wa vyombo huru vya mawasiliano, na kutokana na ukweli kuwa hata sasa ni vizuri uchunge unachosema kuhusu Mwalimu hasa kama ni mwanasiasa unaweza ukajikuta unatengwa na jamii ukionekana unakinzana na Mwalimu!!!!. Lakini mimi si mwanasiasa ni mwanamuziki, na leo nitasimulia ilikuwaje kuwa mwanamuziki enzi za Mwalimu. Mimi ni mzaliwa wa Iringa, nilipata bahati kuzaliwa katika nyumba ambayo muziki ulikuwa sehemu kubwa ya maisha. Moja ya starehe kubwa ya wazazi wangu ilikuwa muziki, baba yangu alikuwa mpiga gitaa mzuri aliyerekodi nyimbo zake kwa mara ya kwanza Tanganyika Broadcasting Services (TBC) mwaka 1960 na nyimbo hizo kupigwa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha Jimbo Letu, 16 May 1960. baba alilipwa shilingi 40. Hili ni ushahidi kuwa kabla ya Uhuru wanamuziki walilipwa mirabaha kila nyimbo zao zilipopigwa katika redio miaka hiyo. Niliwahi kumuona baba pia akipiga accordeon, trumpet na saxophone, ila chombo chake haswa kilikuwa gitaa lisilotumia umeme, acoustic guitar, ambalo alikuwa akipiga katika  mtindo wa Folk Music, au mtindo wa kupiga gitaa kwa kutumia vionjo vya utamaduni asili wa mpigaji, nae tungo zake zilitokana na utamaduni wa kabila lake la Kihehe. Hivyo nilipokuwa mdogo nilishirikishwa kuimba wakati akipiga gitaa na kuupenda muziki toka nikiwa na umri mdogo. Pia nyumbani tulikuwa na radio na gramaphone iliyokuwa na santuri za muziki aina mbalimbali,muziki wa Kiswahili, Kihindi, Kiingereza na muziki toka Afrika ya Kusini na Kongo, hivyo muziki ulikuwa masikioni muda mwingi wa maisha yangu ya awali.  Nilianza shule mwaka uleule ambapo Tanganyika ilipata Uhuru, nakumbuka tulifagia barabara za jirani na shule yetu kisha kuzimwagia maji siku moja kabla ya Uhuru, ili siku ya Uhuru kusiwe na vumbi.
Shuleni kulikuwa na kipindi kilichoitwa ‘Kuimba’, mwalimu alihakikisha anafundisha japo wimbo mmoja kwa wiki, vitabu maalumu vilikuwepo vikiwa na nyimbo zilizokuwa na mafunzo ya maisha, kuheshimu wazazi, wakubwa, kupenda shule na kadhalika. Somo hili lilikuweko katika ngazi zote za shule za msingi, na kulikuweko waalimu wengi waliokuwa wakijua kusoma na kuandika muziki kwa nota hivyo wanafunzi kupewa elimu ya muziki zaidi ya kuimba nyimbo. Shule zote zilikuwa na bendi ya shule. Ambayo kila asubuhi bendi  ilipiga muziki wakati wanafunzi wakikaguliwa kama wamekuja shuleni wasafi, moja ya ndoto zangu ilikuwakuja kuwa mmoja wa wana bendi ya shule. Nilitamani aidha kuwa mpiga ngoma au mpiga filimbi na kubwa kuliko yote ni kupata bahati kuwa mshika kifimbo. Shule zilishindana kwa kuzivalisha bendi mavazi bora na upigaji kuwa makini na hivyo siku za sikukuu kila shule ilijitahidi bendi yake ndio iwe bora. Hakika nakumbuka raha iliyokuwepo wakati shule mbalimbali zilipokutana siku ya siku kuu au kukiwa na maandamo na kisha kila bendi kupita mbele ya mgeni wa heshima, wanafunzi tulijitahidi kuwa wasafi, wakakamavu na wenye nidhamu ili shule yetu ishinde.  

Kila shule ilikuwa na vikundi vya kwaya, ngoma za asili na nyingine kuwa na bendi za muziki wa kisasa. Nilisoma shule iliyokuwa na wahindi wengi, Iringa Aga Khan Primary School, bila kujali kabila wote tulicheza ngoma za asili. Hakika kulikuwa na wahindi wanajua kucheza sindimba kuliko waswahili. Siasa ya Ujamaa iliingia wakati niko darasa la saba. Mambo mengi yalibadilika, nyimbo, ngoma ngonjera, mashahiri yakanza kuwa ni ya kisiasa, nyimbo nyingi za kiasili zikapewa maneno ya kisiasa, maafisa utamaduni ndio walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha hili, kwa kuzunguka kuhamasisha na hata kutoa adhabu kwa vikundi vilivyoonekana havitaki kuimba nyimbo za siasa. Mashuleni tulianza kuimba nyimbo za siasa kwa uwingi zaidi, somo la kuimba lilikuwa likifundisha nyimbo za siasa tu. Kwaya zilizokuwa na nyimbo mbalimbali za siasa kutoka kila upande wa nchi, zilirekodiwa na Radio ya Taifa ambayo kwa wakati huu iliitwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Uzalendo ulikuwa ndio ‘habari ya mjini’. Kila mwisho wa onyesho la muziki bendi zililazimika kupiga ule wimbo wa ‘Chama cha Mapinduzi chajenga nchi’. TANU Youth League (TYL) ilikuwa na matawi kila mahala. Kimuziki TYL ilichangia sana, kwani kila kwenye tawi la TYL lazima kulikuwa na kundi la muziki aidha kwaya au ngoma, na mara nyingi vyote na sehemu nyingi TYL pia ilinunua vyombo vya bendi na hivyo karibu kila wilaya ilikuwa na bendi. Hapa ndipo wanamuziki wengi maarufu wa miaka hiyo na ambao nyimbo zao bado maarufu mpaka leo walikotokea. Pale Iringa, vyombo vya TYL hatimae viliishia kuwa chini ya shule ya Sekondari ya Mkwawa na hivyo pale kulikuwa na bendi nzuri sana ambayo iliweza kuja kurekodi RTD ikiwa na mtindo wao wa Ligija, kati ya waliokuwa wanamuziki wa bendi hiyo, mpia solo ni mzazi wa producer mmoja maarufu wa Bongo fleva na hata yeye alikuja kuwa na bendi yake TZ Brothers, mpiga rythmambaye  kwa sasa ana chuo kikubwa cha muziki pale Tabata, wakati muimbaji mmoja wa bendi hiyo alianzisha bendi maarufu pale Arusha.  Mashirika ya umma, taasisi mbalimbali za kiserikali zilihamasishwa kuwa na vikundi vya utamaduni ambavyo ndani yake kulikuwa na kwaya, bendi na ngoma za asili. Vingi vilikuja kuwa maarufu nchi nzima, kama vile BIMA, vikundi vya majeshi yote, DDC, TANCUT, UDA, URAFIKI ana kadhalika. Pamoja na kutoa burudani vikundi hivi vilijenga uzalendo kwa vijana wa wakati ule. Hakika uzalendo kwa sasa si moja ya vipaumbele na matokeo ya hili ni janga kubwa kwa Taifa .

No comments: