Sunday, November 12, 2017

JE UTAMU WA GITAA LA RYTHM UTAWEZA KURUDI TENA?

Harrison Siwale (Satchmo) mpiga rythm, Mbaraka Mwinyishehe mpiga solo, Abdul Mketema mpuliza saksafoni
Katika mfumo wa awali kuanzia miaka ya 50,  bendi zilikuwa  na mfumo wa kutumia magitaa matatu, Solo, rythm na Bass. Gitaa la solo lilikuwa na sauti ya juu, huku rythm ikiwa na sauti nzito kidogo ya kati, na mwisho Bass likiwa na sauti nzito kuliko magitaa mengine. Kimuundo gitaa la rythm na la solo hakuna tofauti. Yote yana nyuzi 6,lakini katika kutyuni kwenye amplifier, gitaa la rythm hunyimwa treble (ukali) kiasi na kuongeza bass zaidi kuliko gitaa la solo ambalo huwa na treble zaidi ya magitaa mengine. Mwanzoni mwa miaka ya 60 likaanza kutumika gitaa la nne lililojulikana kama 'second solo' au Wakongo waliliita 'mi solo'. Inasemekana kaka yake mpiga solo maarufu wa Kongo wa enzi hizo Dr Nico, ndie aliyeanzisha mtindo wa kuongeza gitaa hilo la nne. Hili lilikuwa likipigwa kwa mifumo mbalimbali katika bendi mbali mbali. Bendi nyingine zilitumia second solo kama gitaa lililokuwa linajibizana na solo, na bendi nyingine lilikuwa linajibizana na rythm,na hata kulikuweko mfumo ambapo gitaa hilo aidha lilikuwa likipiga 'harmony ya gitaa la solo au ya gitaa la rythm. Bendi nyingine , mfano  Cuban Marimba chini ya Juma Kilaza liliongeza ubunifu na kuongeza gitaa la 5 na kuliita 'chord guitar'. Ubunifu huu uliongeza sana uzito wa muziki na hata kuleta ladha mbalimbali za muziki wa dansi. Na uamuzi wa aina ya mpangilio wa magitaa uliweza kuleta tofauti kubwa kati yabendi moja na nyingine.
Lakini katika makala ya leo tuzungumzie gitaa la rythm. Chombo hiki bado kinapigwa katika bendi nyingi lakini umuhimu wake umeshuka sana. Katika kipindi cha miaka ya 60 na 70, gitaa hili lilikuwa na umuhimu mkubwa na wapigaji wake waliweza kubuni staili zao wenyewe. N kujijengea sifa kubwa. Kati ya wapiga rythm maarufu alikuweko Satchmo, hilo ndio lilikuwa jina la kisanii la Harrison Siwale, huyu alikuwa Mzambia aliyekuja weka masikani yake katika mji wa Tanga. Alipitia bendi kubwa za Tanga ikiwemo Atomic Jazz Band na hatimae Jamhuri Jazz Band. Satchmo alikuwa na staili peke yake ya kupiga rythm, sikumbuki kusikia mtu mwingine akipiga rythm ya aina yake kabla ya hapo, lakini hakika wapiga rythm wengi walichukua mtindo wake na kubuni vionjo vya aina yao. Rythm yake ilitawala nyimbo za Jamhuri Jazz Band wakati huo. Ufundi wake unaonekana sana katika nyimbo kama Mganga no 1 na 2, au Blandina. Kule Tabora  Mzee Kasim Kaluwona nae alikuwa na staili tofauti ya upigaji wa gitaa la rythm uliyoifanya Tabora Jazz kuwa na staili yake peke yake, kumbuka gitaa lake katika wimbo Asha, au Dada Lemmy. Charles Kazembe akiwa na Morogoro Jazz anakumbukwa katika upigaji wa rythm kwenye nyimbo kama Wajomba Wamechacha. Hao ni wachache tu kulikoweko na wengi marufu. Katika kipindi hiki huko Zaire kulikuwa na mipigo mbalimbali ya gitaa la rythm, ila kitu kipya kikaanzishwa ambapo katika ufungaji wa nyuzi ,wapiga rythm wakauondoa uzi namba nne katika gitaa hilo na kuweka uzi namba moja, hivyo kukawa na nyuzi namba moja 2 katika gitaa moja, hapo ndipo akina Vata Mombasa wakaweza kuleta utamu mpya katika upigaji wa rythm, ufungaji wa aina hii wa nyuzi za gitaa ulifahamika kama 'double string'. Wakati huo Orchestra Kiam wakawa wanajivunia kupiga rythm kwa spidi kali sana,vibao kama Kamiki, Bomoto ni ushahidi wa kazi hizo. Utamu wa ufungaji wa nyuzi kwa staili hii uliweza kusikika vizuri katika gitaa lililopigwa mwanzo kabisa wa wimbo Andoya. Umuhimu wa gitaa la rythm ulikuwa ukionekana kwa bendi nyingi kuwa na mtindo wa 'kuachia rythm', huo ulikuwa ni mpangilio ambapo gitaa la rythm liliachwa lipige peke yake wakati magitaa mengine yakiwa kimya. Hapo mpiga rythm aliachiwa kucheza na gitaa alivyotaka na  kuonyesha umahiri wake wote. Mtindo huu ulipendwa sana na wapenzi wa muziki. Utaratibu huu umerudi kwa njia ya ajabu sana, bendi nyingi za  taarab vimeanza 'kuachia rythm' lakini kwa kuwa bendi hizo hazitumii tena gitaa la rythm , jukumu hili linafanywa na mpiga solo, tena vipande vingi vinavyopigwa ni vile vilivyopigwa na bendi za zamani!!  matokeo ni yaleyale, wapenzi wa muziki hupanda mzuka na kucheza sana wakati wa kipindi hicho. 
Kwa ujumla bendi nyingi za dansi hazitilii umuhimu tena gitaa la rythm. Kinanda kimechukua nafasi ya gitaa hili. Kuna bendi ambazo zinalo gitaa la rythm lakini kwa mfumo wa sasa wa muimbaji kuchukua nafasi kubwa ya wimbo gitaa hilo limerudishwa nyuma sana. Lakini kwenye muziki kila kitu kina utamu wake kamwe chombo kimoja hakiwezi kuziba pengo la chombo kingine.

No comments: