Hatimae mwezi mmoja baada ya kufariki, Cloud Yohana Mwanasande maarufu kwa jina la Shabani Yohana Wanted amezikwa kijijini kwao Kwamgwe Michungwani Muheza. Mazishi haya yamekamilisha safari ya mwezi mmoja toka alipofariki 12/13 Septemba 2017 huko Gaberone Botswana, tarehe maalumu ya kifo chake pia ikiwa na utata kutokana na kutokujulikana uhakika siku ya kifo kwani mwili wake ulikutwa chumbani kwake akiwa amekwishafariki. Shabani alikuwa anaishi peke yake. Mwili wa Shabani ulichukuliwa na polisi na zikaanza taratibu za kupata ndugu zake, ambapo walipopatikana, awali waliruhusu Shabani azikwe hukohuko Botswana, lakini wanamuziki na wapenzi wa Shaban kule Botswana waliamua kuwa lazima warudishe maiti Tanzania, na hivyo kuanzisha michango hukohuko na hata kufanya onyesho kubwa la muziki kuhakikisha zinapatikana fedha za kusafirisha mwili mpaka Dar es Salaam.
kwa upande wa Tanzania, wanamuziki waliunda kamati ya mazishi ya Shabani ikiongozwa na John Kitime na Rashidi Pembe, Kitime aliwahi kuwa katika bendi moja na Shabani Yohana kati ya mwaka 1988 hadi 1994. Kwanza wakiwa Tancut Almasi Orchestra na baadae Vijana Jazz Band wakiwa pamoja na Rashid Pembe. Kazi ya kamati hii ilikuwa ni kupokea mwili, kusafirisha, na hatimae kwenda kumzika Shabani.
Michango ilihamasishwa na watu mbalimbali waliweza kuchangia yakiwemo makundi ya whatsapp ya Kavasha na Zama Zile, wapenzi wa muziki, Umoja wa Vijana ambapo Shabani alikuwa ni mwajiriwa na kiongozi wa bendi ya Vijana kwa miaka minne, BASATA, wanamuziki wenyewe. Na hii iliwezesha kufanikisha kukamilisha safari ndefu ya Shabani Yohana ambaye jina lake rasmi lilikuwa Cloud Yohana Mwanasande.
Nichukue nafasi hii kuwashukuru wote waliofanikisha kazi hii hapa nchini na kule Botswana. Mungu awabariki na hakika familia ya Shabani imetoa shukrani kubwa kwa kurudishiwa ndugu yao na kuweza kumzika katika makaburi ambayo mama yake mzazi wa marehemu pia amezikwa.
Zifuatazo ni picha mbalimbali za mazishi ya Shabani
|
Kupokelewa kwa sanduku lenye mwili wa Shaba Yohana Swissport Uwanja wa ndege Dar |
|
Vikao vya wanamuziki kupanga namna ya kupata fedha za kusafirisha mwili wa Shabani kwenda kuzikwa Kwamgwe |
|
Mwili wawasili kijijini Kwamgwe na kuingizwa nyumbani kwao Shabani |
|
Rashid Pembe akiwa na Mzee Masongi , mzee aliyewalea wanamuziki wengi maarufu akiwemo Shaaban wanted |
|
Ibada nyumbani kwa marehemu |
|
Ibada katika kanisani Kwamgwe |
|
Dada wa Shabani akiwa ameketi pembeni ya sanduku muda mfupi kabla ya kuzika |
|
John kitime akiweka shada kwa niaba ya wanamuziki |
|
Dada wa marehemu akiweka shada |
|
Kaka wa marehemu Hamisi Yohana akiweka shada |
|
Mjomba akiweka shada |
|
Edina Pambamoto na Tabu Mambosasa wakiweka shada |
|
Hassan Msumari akiweka shada |
|
Shada kwa niaba ya Vijana Jazz band |
|
Picha baada ya mazishi |
|
Safari ya kurudi Dar es Slaaam |
No comments: