Thursday, October 12, 2017

IMANI ZA UCHAWI KATIKA TASNIA YA MUZIKI




Imani ya uchawi ni utamaduni ambao umekuweko katika  jamii zote za binaadamu kwa maelfu ya miaka. Historia na maandiko ya dini mbalimbali yanatukumbusha hilo na kulilaani. Huwa inategemewa kuwa kadri maendeleo na elimu yanavyoongezeka ndio imani hiyo inavyopungua na kupotea, lakini ni wazi safari bado ni ndefu kwani ukipita katika mitaa mingi utaona vibao vikiashiria waganga wanaoweza kutibu magonjwa mbalimbali, na hata kutangaza ‘kusafisha nyota’, ‘kuondoa majini’ na kadhalika.

Tasnia ya muziki kwa kuwa ni sehemu ya jamii,  haijakwepa kuguswa na tatizo hilo. Kutokana na mimi mwenyewe kufanya kazi katika bendi mbalimbali niliona na kusikia vituko vingi vilivyohusishwa na imani ya uchawi. Mara ya kwanza kuanza kuona vitimbi hivi ‘live’ ni nilipojiunga na bendi moja ambayo ilikuja kuwa maarufu sana wakati wake. Kwa mara ya kwanza nilishuhudia kiongozi wa bendi yangu akiwa na katibu wake wakiwa wanafukiza kwenye radio majani fulani wakati kipindi cha Misakato kikiwa hewani. Misakato kilikuwa ni kipindi kilichokuwa hewani kila Jumanne saa tatu na robo asubuhi, katika redio ya RTD, kikiporomosha nyimbo mpya zilizorekodiwa na pia kutoa maelezo kuhusu wanamuziki walioshiriki. Siku hiyo vibao ambavyo tulikuwa tumerekodi  vilikuwa vikirushwa hewani kwa mara ya kwanza, ndipo viongozi wangu hawa nikawakuta wakiwa katika shughuli ya kufukiza radio,  kwa imani kuwa kwa kufanya hivyo, vibao hivyo vitatikisa wasikilizaji wake. Baada ya hapo vituko vingi viliendelea hatimae tulimzoea kiongozi wa bendi yetu kuwa ni mshirikina. Kuna wakati aliletwa mganga ambaye alidaiwa aliwahi kuifanya timu moja maarufu ya soka, ishinde kombe  na kuwa bingwa wa Taifa, kutokana na sifa hizo bendi ilimchukua kwa mkataba na kazi yake ikawa ni kukaa mlangoni akijifanya ni muuza machungwa, hapo alitakiwa afanye vimbwanga vyake ili wateja wengi waingie kwenye muziki. Yeye alidai kila anapomenya chungwa kwa kuunganisha maganda basi na wateja nao wataingia katika ukumbi kwa kuunganika, huyu alikaa nasi kiasi cha kuweza kuwa  katika misafara mbalimbali ya bendi kulipokuwa na ziara za mikoani. Harakati za bendi kutafuta umaarufu kwa uchawi ilifikia mpaka bendi ikasafiri hadi kwenda Mpanda, ambako viongozi wa bendi walikwenda kwa mganga na kufanya mambo yao yalihusisha na hata kumchinja mbuzi ambaye nadhani masharti yalikuwa ni sisi wanamuziki wote tule kipande cha mbuzi yule wa kafala. Sijajua mpaka leo viongozi walifanya nini na nyama ya mbuzi yule maana wanamuziki walifanya mgomo wa kumla yule mbuzi. Kiongozi wa bendi katika safari hiyo, alichanjwa shingo yote na akawa na mikrofon ambayo wengine wote tulikatazwa kuitumia iwapo jukwaani na sikuona mtu akiigusa  mpaka nilipoacha bendi. Ushirikina una matatizo ya kufanya watu wasiaminiane hata kwenye bendi yenyewe, haikuchukua muda mrefu bendi ilipoanza kupoteza umaarufu, Kiongozi wa bendi akaaitisha mkutano na kutuambia kuwa kuanguka kwa bendi kunatokana na mmoja wetu kuiloga bendi, hapo ikatolewa tishio kuwa mtuhumiwa asipojitaja mwenyewe na kuomba msamaha mganga atamfanya awe kichaa. Jambo ambalo liliungwa mkono na wote kuwa kama ni kweli kuna mtu namna hiyo basi apate uchizi. Hakuna aliyekumbwa na tatizo hilo mpaka leo.

Miezi michache baadae, wanamuziki wawili walioamua kuacha bendi walirudisha uniform zao shati zikiwa zimechanywa kwenye kwapa na suruali kuchanywa kwenye maungio ya miguu kwa imani kuwa hizo ndizo sehemu zenye jasho kwa hiyo zingeweza kutumiwa na bendi kiuchawi kuwaharibia maisha.

Katika mizunguko kwenye bendi mbalimbali, nilikuwa katika bendi ambapo siku kukiwa na mpambano wa kupiga bendi zaidi ya moja katika ukumbi mmoja, basi hapo mganga maalumu lazima atafutwe ili kuilinda bendi isimalizwe na wapinzani. Ilikuwa inaaminika kuwa katika mpambano wa bendi, uchawi hutumika kuimaliza bendi ambayo itakuwa haina kinga. Kwa siku hiyo ndani ya spika kuliwekwa tunguli na hirizi mbalimbali tayari kwa mpambano.

Kwa ukweli kabisa hata wanamuziki kutembeleana mara nyingine ilikuwa ni vigumu, kwani ukionekana mwanamuziki wa bendi nyingine katika ukumbi, basi bendi iliyo jukwaani haina raha, anaweza hata akatumwa mtu kufuatilia kila utakachofanya. Na ilikuwa vigumu kuruhusiwa kugusa vyombo vya bendi nyingine kwa wasiwasi wa kuwa unaweza ukaloga kile chombo.

Kulikuwa na hadithi nyingi kuhusu ni kiasi gani bendi ziliweza kufanya ili kupata wateja. Kuna bendi ambayo ilisifika kuwa kila wakimaliza kupiga walipita katika kumbi na kuokota vizibo vya chupa, mifupa, na hata kupata maji toka chooni kwenda kuloga ili wale walioingia wasiingie bendi yoyote kasoro yao. Bendi nyingine zilidaiwa kuwa ziliweka mkataba ambapo zililazimika kutoa kafala ya mtu kila mwaka, hivyo viongozi wa bendi kufiwa na watoto, na hata wanamuziki wageni katika bendi hizo kukutwa na mauti ambayo, kwa chini chini yalidaiwa ni katika kutoa kafala.

Bendi mbili ambazo zilikuwa na upinzani mkubwa katika jiji la Dar es Salaam zilidaiwa hata kutaka kuweka uchawi katika chanzo cha maji Dar es Salaam , na kujikuta wakitaka kuumbuana hadharani kuhusu hilo.

Kama nilivyosema imani ya uchawi huleta kutokuaminiana na hata madhara makubwa ya kutuhumiana mambo ambayo mara nyingi hayana ukweli wowote. Kuna mwanamuziki niliyejaribu kumshawishi aingie katika bendi niliyokuwa nikipigia , alikataa katakata kwa kuwa alidai mmoja wa wanamuziki katika bendi ni mchawi. Mwanamuziki mmoja aliwahi kuhadithia jinsi alivyopita uchochoro wa nyumba ya mwanamuziki mwenzake akashangaa kusikia jina lake likitajwa na mwenzie aliyekuwa chumbani kwake na kusema,’ Nyota ya …….izimike kama kaa hili’, akadai alichungulia katika ufa na akakuta mwenzie anatumbukiza kaa la moto kwenye maji. Ugonjwa wa ukimwi ulipoanza kuuwa wanamuziki kwa mara ya kwanza mara nyingi ulihusishwa na uchawi. Rafiki yangu mmoja nilipomtembelea wakati akiwa hoi kitandani akanambia,’Nikupe siri? Mi ntakufa lakini nauawa na wanamuziki wenzangu kwenye bendi. Nimepata mganga kanitajia na majina kabisa’. Miezi michache baadae mwanamuziki huyu kabla hajafariki alinambia,’Mjomba sijalogwa wala nini, udude huu, unaniua udude’. Alifariki siku chache baada ya kunambia haya. Mungu amlaze Pema peponi Mjomba.


Kitu ambacho kimenishangaza karibuni tuhuma kuwa kuna wanamuziki wa kizazi kipya wanaendeleza imani hii ya ushirikina. Producer maarufu amejitokeza na kuwakanya wasifanye mambo hayo kwenye studio yake. Na siku chache baada ya hapo tena mwanamuziki mwingine wa muziki huo kawataja ambao aliwaita wabaya wake wanaomloga.!!!!!!! Nikaona loh kumbe shughuli bado inaendelea, wanamuziki hawa wenye umri mdogo tayari wamekwisha jenga imani ya kulogana katika enzi hizi za dijitali, safari bado ndefu sana

Wednesday, October 11, 2017

MWEZI MMOJA BAADA YA KUFARIKI, SHABAN WANTED AZIKWA KIJIJINI KWAO KWAMGHWE

Hatimae mwezi mmoja baada ya kufariki, Cloud Yohana Mwanasande maarufu kwa jina la  Shabani Yohana Wanted amezikwa kijijini kwao Kwamgwe Michungwani Muheza. Mazishi haya yamekamilisha safari ya mwezi mmoja toka alipofariki 12/13 Septemba 2017 huko Gaberone Botswana, tarehe maalumu ya kifo chake pia ikiwa na utata kutokana na kutokujulikana uhakika siku ya kifo kwani mwili wake ulikutwa chumbani kwake akiwa amekwishafariki. Shabani alikuwa anaishi peke yake. Mwili wa Shabani ulichukuliwa na polisi na zikaanza taratibu za kupata ndugu zake, ambapo walipopatikana, awali waliruhusu Shabani azikwe hukohuko Botswana, lakini wanamuziki na wapenzi wa Shaban kule Botswana waliamua kuwa lazima warudishe maiti Tanzania, na hivyo kuanzisha michango hukohuko na hata kufanya onyesho kubwa la muziki kuhakikisha zinapatikana fedha za kusafirisha mwili mpaka Dar es Salaam.
kwa upande wa Tanzania, wanamuziki waliunda kamati ya mazishi ya Shabani ikiongozwa na John Kitime na Rashidi Pembe, Kitime aliwahi kuwa katika bendi moja na Shabani Yohana kati ya mwaka 1988 hadi 1994. Kwanza wakiwa Tancut Almasi Orchestra na baadae Vijana Jazz Band wakiwa pamoja na Rashid Pembe. Kazi ya kamati hii ilikuwa ni kupokea mwili, kusafirisha, na hatimae kwenda kumzika Shabani.
Michango ilihamasishwa na watu mbalimbali waliweza kuchangia yakiwemo makundi ya whatsapp ya Kavasha na Zama Zile, wapenzi wa muziki, Umoja wa Vijana ambapo Shabani alikuwa ni mwajiriwa na kiongozi wa bendi ya Vijana kwa miaka minne, BASATA, wanamuziki wenyewe. Na hii iliwezesha kufanikisha kukamilisha safari ndefu ya Shabani Yohana ambaye jina lake rasmi lilikuwa Cloud Yohana Mwanasande.
Nichukue nafasi hii kuwashukuru wote waliofanikisha kazi hii hapa nchini na kule Botswana. Mungu awabariki na hakika familia ya Shabani imetoa shukrani kubwa kwa kurudishiwa ndugu yao na kuweza kumzika katika makaburi ambayo mama yake mzazi wa marehemu pia amezikwa.

Zifuatazo ni picha mbalimbali za mazishi ya Shabani
Kupokelewa kwa sanduku lenye mwili wa Shaba Yohana Swissport Uwanja wa ndege Dar



Vikao vya wanamuziki kupanga namna ya kupata fedha za kusafirisha mwili wa Shabani kwenda kuzikwa Kwamgwe





Mwili wawasili kijijini Kwamgwe na kuingizwa nyumbani kwao Shabani

Rashid Pembe akiwa na Mzee Masongi , mzee aliyewalea wanamuziki wengi maarufu akiwemo Shaaban wanted



Ibada nyumbani kwa marehemu






Ibada katika kanisani Kwamgwe








Dada wa Shabani akiwa ameketi pembeni ya sanduku muda mfupi kabla ya kuzika








John kitime akiweka shada kwa niaba ya wanamuziki

Dada wa marehemu akiweka shada

Kaka wa marehemu Hamisi Yohana akiweka shada

Mjomba akiweka shada



Edina Pambamoto na Tabu Mambosasa wakiweka shada



Hassan Msumari akiweka shada


Shada kwa niaba ya Vijana Jazz band











Picha baada ya mazishi



Safari ya kurudi Dar es Slaaam

Monday, October 9, 2017

MWILI WA SHABAN YOHANA 'WANTED' WAPOKELEWA TANZANIA MAZISHI KUWA MICHUNGWANI JUMATANO

Sanduku lenye mwili wa Shaban Yohana Wanted lilipokelewa na wanamuziki wa Tanzania jana asubuhi katika ofisi za Swissport Dar es Salaam. Mwili wa mwanamuziki huyo ambaye aliefia Gaberone Botswana tarehe 14/9/2017 ulifanikiwa kufika Tanzania kutokana na juhudi za wanamuziki wenzake na wadau wa muziki walioko huko Botswana. Walioupokea mwili huo walikuwa ni John Kitime, Rashid pembe, Hassan Msumari na mwanamuziki wa kike Sholinder Mwezimpya. Maiti ilipelekwa hospitali ya Muhimbili kuhifadhiwa. Baada ya hapo wanamuziki walikutana Vijana Social Hall kupanga mikakati ya jinsi ya kufikisha mwili kijijini kwao Shaban. Wanamuziki, wadau wa muziki, Baraza la Sanaa la Taifa, Umoja wa Vijana, Mheshimiwa William Ngeleja Mbunge wa Sengerema, Dekula Kahanga Vumbi vikundi vya Whatsap vya Zamazile  na Kavasha ni kati ya walioweza kuchangia ili kufanikisha taratibu za kukamilisha safari ya Shaban Yohana Wanted.
Shabani atazikwa kesho Jumatano 11/10/2017, Michungwani Muheza. Safari ya kwenda huko itaanzia Muhimbili saa kumi na mbili asubuhi. wanamuziki kadhaa watamsindikiza mwenzao katika safari yake ya mwisho.

Wanamuziki waakiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Shaka Hamdu Shaka wakipanga kukamilisha safari ya mwisho ya Shaban Yohana. Shaban alikuwa kiongozi wa bendi ya Vijana Jazz  kuanzia mwaka 1990 hadi 1995.




Sunday, October 8, 2017

MWILI WA SHABANI YOHANA WAAGWA BOTSWANA KUWASILI DAR, ALFAJIRI 9 OKTOBA 2017

Wednesday, October 4, 2017

HATIMAE MWILI WA SHABAAN YOHANA WANTED KUWASILI NCHINI KWA AJILI YA MAZISHI

HATIMAE mwili wa Shabani Yohana Mwanasande, aliyejulikana kwa jina la Shaban Wanted utawasili alfajiri  Jumatatu 9 Oktoba 2017. Shaban Yohana ambae jina lake halisi ni Cloud Yohana Mwanasande alifariki akiwa peke yake chumbani kwake huko Botswana kati ya tarehe 12 na 13 Septemba 2017, jambo lililofanya mwili wake kuwa chini ya vyombo vya usalama kwa muda mrefu. Shukrani kubwa zitolewe kwa jamaii ya Watanzania na wanamuziki wenzake wa huko Botswana kwa kuchangishana na hata kufanya onyesho maalumu la muziki ili kuweza kupta fedha za kufikisha mwili Dar es Salaam. Mwili wa Shabani utapokelewa na wanamuziki wa Tanzania Jumatatu na kisha kupelekwa Muhimbili na kesho yake Jumanne mipango ya kuusafirisha kwenda kwa mazishi Michungwani Muheza itafanyika. Bado michango inahitajika kumalizia safari ya mwisho ya Shabani Wanted. Na atakaeguswa anaombwa kutuma michango kupitia namba 0713274747 na 0763722557 zilizosajiliwa kwa jina la John Kitime.
Shabani Yohana atakumbukwa kwa nyimbo zake alizorekodi kati ya mwaka 1988 hadi 1995 akiwa katika bendi za Tancut Almasi Orchestra, Vijana Jazz Band, na Ngorongoro Heroes. Baadhi ya nyimbo ambazo alipiga gitaa la solo na  bado ni maarufu ni;
Nimemkaribisha Nyoka - Tancut Almasi Orch
Masafa Marefu -Tancut Almasi Orch
Azza- Vijana Jazz Band
Penzi Haligawanyiki -Vijana Jazz Band
Thereza -Vijana Jazz Band
Kamwembwe - Ngorongoro Heroes
Naachia Ngazi - Ngorongoro Heroes
Shime tushirikiane kumzika mpendwa wetu 

Saturday, September 16, 2017

BURIANI SHABANI YOHANA MWANASANDE- SHABAN WANTED HATUNAE TENA

Jana mchana, siku ya Ijumaa nikiwa njiani natoka Tanga muda mfupi tu baada ya kupita Hale nilipigiwa simu na James Mawila, mpiga drums wa Msondo akinitaarifu kuwa Albert Chikopa, mwanamuziki mwenzetu aliyeko Botswana ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kuwa mpiga gitaa Shabani Yohana amefariki. Niliingia haraka katika ukurasa huo na kukuta habari hizo, pia Chikopa alikuwa ameweka namba ya mtu ambaye ana taarifa zaidi. Nilimpigia mtu huyo na alisema kuwa habari hizo ni kweli na kuwa Shabani alifariki akiwa peke yake chumbani na hivyo ilikuwa ni baada ya siku mbili ndipo jambo hilo lilipojulikana na hivyo polisi walikuwa wakitafuta ndugu zake. Bahati nzuri Rashid Pembe aliweza kumpata nduguye na taratibu za mazishi zinaendelea. Mpaka sasa kuna jitihada za kujaribu kurudisha mwili wa Shabani nyumbani. Michango inaendelea Botswana na hapa nyumbani katika makundi ya wapenzi wa muziki wa rumba.
Nilikutana na Shabani mara ya kwanza katika bendi ya Tancut Almasi Orchestra, yeye akitokea bendi ya Orchestra Vinavina, nami nikitokea Orchestra Seleleka, tulikuwa kati wa watu wa kwanza kujiunga na bendi hiyo hatimae wakaja kujiunga wanamuziki wengine kina Mafumu Bilali, Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa na pamoja tukaja kujenga bendi ambayo iliweza kuporomosha muziki mzuri sana. Katika album ya kwanza ya Tancut Almasi karibu nyimbo zote solo lilipigwa na Shabani Yohana kasoro wimbo wa Kiwele ambapo solo lilipigwa na Kawelee Mutimwana ambaye pia ndie aliyekuwa  mtunzi wa wimbo huo. Nyimbo hizo zilikuwa 
Nimemkaribisha nyoka
Kashasha
Tutasele
Kuwajibiika
Big Four
Mtaulage
Na hata album ya pili solo la Shabani linatambulika sana kwenye wimbo Masafa Marefu, lakini pia alipiga solo kwenye wimbo wa Wifi.
Shabani alihamia vijana Jazz band 1988 ambapo akapewa jina la Wanted, na katika bendi hii aliendelea kwa miaka 6 kuburudisha watu kwa ufanisi wake katika kupiga gitaa hili, nyimbo kama Ogopa Tapeli, Aza, Mama Wa Kambo Mundinde, Wifi Zangu, Penzi haligawanyiki, Thereza, Shoga, Heshima ya mtu na nyimbo nyingine nyingi za bendi hii. Baada ya safari ya Ujerumani ambapo tulikwenda mimi John Kitime, Mzee Small, Abadallah Mgonahazelu, Baker Semhando, na yeye mwenyewe Shabani, ndipo mwenzetu alipotutaarifu kuwa anataka kuhama bendi. Vijana Jazz tulimfanyia party ya kumuagana kumnunulia zawadi, jambo ambalo halikuwa la kawaida, na baada ya hapo akahamia Ngorongoro Heroes, huko nako alitingisha jiji kwa gitaa lake katika nyimbo za bendi hiyo. Hatimae akahamia Botswana, ambako kwa mujibu wa maandiko kwenye facebook baada ya kusikia kifo chake wanamuziki wa huko wameendelea kusifia ubora aliokuwa nao.
Mipango ya maziko inaendelea, jaribio kubwa ni kuchangishana kurudisha mwili wake hapa nyumbani. 
MUNGU AMLAZE PEMA SHABANI YOHANA WANTED

Thursday, September 7, 2017

UNAKUMBUKA SOCIAL EVENINGS?

KWA wengi waliokuwa wakisoma sekondari miaka ya 60 na 70, moja ya siku zilizokuwa zikisubiriwa kwa hamu ilikuwa siku ya ‘Social Evening’. Siku hii ilikuwa ndio siku ambayo wanafunzi walipata nafasi kusakata dansi na kupata marafiki wapya, na mara nyingine hata kuachwa na marafiki wa zamani. Mara nyingi dansi hili liliambatana na kualika wanafunzi kutoka shule nyingine za jirani. Na kawaida ilikuwa shule ya wavulana kualika wanafunzi kutoka shule ya wasichana na shule ya wasichana kualika wanafunzi kutoka shule ya wavulana. Matayarisho yalikuwa yanaanza mapema kwa waalikaji kuandika barua kwa Mwalimu Mkuu au mwalimu wa ‘Social’ wa shule wanayotaka kuialika. Baada ya hapo kazi kubwa ni kukusanya michango kutoka kwa wanafunzi wanaotaka kushiriki siku hiyo. Michango hii kazi yake ilikuwa kununua viburudisho kwa wageni; soda, biskuti au hata maandazi, na pia kununua betri za ‘player’ ya kupigia muziki. Umeme ulikuwa nadra kwenye mashule mengi. Kamati ya starehe ilikuwa ‘busy’ kutafuta santuri mpya, kwa kuazima popote pale, na kama kuna mwalimu ana record player ilikuwa jambo la heri sana.  Ukumbi ulipigwa deki vizuri ili wageni wakifika wasije wakawadharau. Hatimae siku huwadia, social evening mara nyingi zilikuwa Jumamosi kuanzia saa nane mchana na kuisha kati ya saa moja mpaka mbili usiku. Wageni hukaribishwa na burudani huanza. Baada ya hotuba na kugawa vinywaji, wenyeji huleta burudani kama vile kucheza jiving, baada ya hapo ‘Dada mkuu’ au mwenyekiti wa kamati ya social wa shule moja hufungua dansi na mwenzie wa upande wa pili. Na ndipo wengine mnajitosa kusaka mapatna. Kawaida ya miaka hiyo mwanaume unamfuata msichana kisha unainama kidogo kumuomba ucheze nae, anaweza akakubali au kukataa. Katika shughuli hizi waalimu wa kuangalia nidhamu walikuwa wakishiriki kuangalia kuwa maadili yanafuatwa. Wakati mnacheza mwalimu anapitapita kuangalia kama ‘hamsogeleani ‘ sana.  Kama nilivyosema hapo juu, muziki ulitoka kwenye record player ambayo ilikuwa na spika moja ndogo hivyo haikuwa na sauti kubwa. Ukiona ukubwa wa maspika siku hizi, unabaki kushangaa, tuliwezaje wanafunzi 200 hadi 300 kucheza muziki na kuusikia vizuri kwa kutumia spika moja  ya player yenye betri 6. Spika ambayo ili itoe bezi ililazimika kuwekwa juu ya pipa. Kulikuwa na nidhamu kubwa sana katika uchezaji, kulikuwa hakuna kupiga kelele, unasikia viatu tu vikisaga chini kwa kufuata mdundo wa muziki. Swala la kuwa pombe haikuhusika katika burudani hizi ni moja ya sababu ya kuwezekana kwa nidhamu hii. Mazungumzo yalikuwa ya chini chini mara nyingi yakihusu masomo.
Katika miaka ya 60 santuri za nyimbo kutoka Congo ndizo zilikuwa maarufu, magwiji wa muziki kama akina Franco, Johhny Bokelo, Dr Nico, Bavon Marie Marie na bendi zao maarufu, Ok Jazz, Negro Success, Co Bantuo, Conga Success na kadhalika, ndizo zilikuwa pendwa wakati huo. Kutoka  Marekani wanamuziki wa muziki wa country kama Skeeter Davis, Jim Reeves, Connie Francis ndio walitawala social evenings. Wavulana kwa wasichana walishiriki kuandika maneno ya nyimbo hizo kwenye madaftari yao na kubadilishana madaftari. Nyimbo maarufu katika madaftari ya wavulana zilikuwa ni nyimbo za Kikongo. Tambola na Mokili wa Johhny Bokelo na Conga Success na Bougie ya Motema wa Dr Nico na African Fiesta zilikuwa hazikosekana kwenye madaftari ya wavulana, wakati akina dada walipendelea sana kuandika maneno ya nyimbo za Skeeter Davis na Dark City Sisters kutoka Afrika ya Kusini. Kama nilivyosema hapo juu, umeme tu ulikuwa tatizo kweye shule nyingi, hivyo swala la kuwaona na kuwajua wanamuziki waliokuwa wakiporomosha muziki huo lilikuwa nadra sana. Magazeti yalikuwa machache, vyombo ambavyo siku hizi vinaonekana ni kawaida kabisa kama radio na TV navyo vilikuwa nadra sana. Lakini kwa njia ya ajabu watu walikuwa wanajua namna ya kucheza staili za muziki mbalimbali!! Chacha, pachanga, charanga, baadae soul, bumping na kadhalika. Kwenye shule mbalimbali kulikuwa na wanafunzi ambao walikuwa wanapata bahati kuwa na ndugu au marafiki ambao walikuwa wakibahatisha kuwafundisha uchezaji mbalimbali wakati wa likizo, basi mwanafunzi wa aina hiyo anakuwa maarufu sana mara arudipo shule na watu wote wanaanza kumuiga  uchezaji ili kujitayarisha kwa social evening.
Ili kujaribu kuwarudishia kumbukumbu wazee walioshiriki haya miaka hiyo na kuwaonyesha wale ambao hawakupitia  enzi hizo nimetayarisha ‘social evening’ kila Ijumaa kwenye ukumbi wa Salender Bridge Upanga, Dar es Salaam, kuanzia tarehe 8 Septemba 2017. Kuanzia saa moja jioni na kuendelea siku hiyo na kila Ijumaa baada ya hapo, muziki utarudishwa nyuma enzi za miaka ya 60,70, na 80. Saa moja usiku utaanza muziki laini, zikipigwa nyimbo laini zilizokuwa maarufu, hivyo sauti za Skeeter Davis, Bobby Bare, Jim Reeves, zitasikika tena, baada ya hapo kutakuwa na maonyesho ya video mbalimbali za wanamuziki wa zamani wakiwa jukwaani. Franco, Tabu Ley, Dr Nico, Bella bella, Lipua Lipua, na kutoka hapa kwetu video za Maquis enzi ya marehemu Chinyama Chiaza, Vijana Jazz, Simba wa Nyika na kadhalika, hatimae dansi rasmi litaanza kwa muziki wa aina mbalimbali na watakaofika wataweza tena kucheza nyimbo ambazo pengine hawajawahi kuzisikia tena toka walipocheza muziki walipokuwa sekondari miaka ya 60. Jioni hiyo itakuwa pia ya kukutana na marafiki na jamaa ambao wamepoteana miaka mingi na kukumbushana vituko vya ujana wao, hakika sasa imepatikana nafasi ya wazee nao kujipatia mahala pa kwenda kupata burudani ya enzi zao.