Saturday, September 16, 2017

BURIANI SHABANI YOHANA MWANASANDE- SHABAN WANTED HATUNAE TENA

Jana mchana, siku ya Ijumaa nikiwa njiani natoka Tanga muda mfupi tu baada ya kupita Hale nilipigiwa simu na James Mawila, mpiga drums wa Msondo akinitaarifu kuwa Albert Chikopa, mwanamuziki mwenzetu aliyeko Botswana ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kuwa mpiga gitaa Shabani Yohana amefariki. Niliingia haraka katika ukurasa huo na kukuta habari hizo, pia Chikopa alikuwa ameweka namba ya mtu ambaye ana taarifa zaidi. Nilimpigia mtu huyo na alisema kuwa habari hizo ni kweli na kuwa Shabani alifariki akiwa peke yake chumbani na hivyo ilikuwa ni baada ya siku mbili ndipo jambo hilo lilipojulikana na hivyo polisi walikuwa wakitafuta ndugu zake. Bahati nzuri Rashid Pembe aliweza kumpata nduguye na taratibu za mazishi zinaendelea. Mpaka sasa kuna jitihada za kujaribu kurudisha mwili wa Shabani nyumbani. Michango inaendelea Botswana na hapa nyumbani katika makundi ya wapenzi wa muziki wa rumba.
Nilikutana na Shabani mara ya kwanza katika bendi ya Tancut Almasi Orchestra, yeye akitokea bendi ya Orchestra Vinavina, nami nikitokea Orchestra Seleleka, tulikuwa kati wa watu wa kwanza kujiunga na bendi hiyo hatimae wakaja kujiunga wanamuziki wengine kina Mafumu Bilali, Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa na pamoja tukaja kujenga bendi ambayo iliweza kuporomosha muziki mzuri sana. Katika album ya kwanza ya Tancut Almasi karibu nyimbo zote solo lilipigwa na Shabani Yohana kasoro wimbo wa Kiwele ambapo solo lilipigwa na Kawelee Mutimwana ambaye pia ndie aliyekuwa  mtunzi wa wimbo huo. Nyimbo hizo zilikuwa 
Nimemkaribisha nyoka
Kashasha
Tutasele
Kuwajibiika
Big Four
Mtaulage
Na hata album ya pili solo la Shabani linatambulika sana kwenye wimbo Masafa Marefu, lakini pia alipiga solo kwenye wimbo wa Wifi.
Shabani alihamia vijana Jazz band 1988 ambapo akapewa jina la Wanted, na katika bendi hii aliendelea kwa miaka 6 kuburudisha watu kwa ufanisi wake katika kupiga gitaa hili, nyimbo kama Ogopa Tapeli, Aza, Mama Wa Kambo Mundinde, Wifi Zangu, Penzi haligawanyiki, Thereza, Shoga, Heshima ya mtu na nyimbo nyingine nyingi za bendi hii. Baada ya safari ya Ujerumani ambapo tulikwenda mimi John Kitime, Mzee Small, Abadallah Mgonahazelu, Baker Semhando, na yeye mwenyewe Shabani, ndipo mwenzetu alipotutaarifu kuwa anataka kuhama bendi. Vijana Jazz tulimfanyia party ya kumuagana kumnunulia zawadi, jambo ambalo halikuwa la kawaida, na baada ya hapo akahamia Ngorongoro Heroes, huko nako alitingisha jiji kwa gitaa lake katika nyimbo za bendi hiyo. Hatimae akahamia Botswana, ambako kwa mujibu wa maandiko kwenye facebook baada ya kusikia kifo chake wanamuziki wa huko wameendelea kusifia ubora aliokuwa nao.
Mipango ya maziko inaendelea, jaribio kubwa ni kuchangishana kurudisha mwili wake hapa nyumbani. 
MUNGU AMLAZE PEMA SHABANI YOHANA WANTED

No comments: