Friday, October 13, 2017

MUZIKI ENZI ZA NYERERE

LEO ni miaka 18 toka Kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mungu amlaze pema Mwalimu. Vyombo vya habari vinaeleza mengi kuhusu hali ya maisha ilivyokuwa zama za Enzi ya Nyerere, kwa tuliekuweko enzi hizo tunaona mengi yanayosemwa ni ya kweli na mengi si sahihi, mengine yanatungwa ili kufanikisha azma fulani, mengine si kweli kwa kuwa mtoa habari hakuweko au alihadithiwa na mtu ambaye hakuwa mkweli au pengine hakumbuki vizuri, lakini hiyo ndio hali halisi kutokana na kuwa mengi yaliyokuwa yakitendeka wakati ule hayakuwekwa katika maandishi kutokana na uwoga wa kusema ukweli enzi hizo, uchache wa vyombo huru vya mawasiliano, na kutokana na ukweli kuwa hata sasa ni vizuri uchunge unachosema kuhusu Mwalimu hasa kama ni mwanasiasa unaweza ukajikuta unatengwa na jamii ukionekana unakinzana na Mwalimu!!!!. Lakini mimi si mwanasiasa ni mwanamuziki, na leo nitasimulia ilikuwaje kuwa mwanamuziki enzi za Mwalimu. Mimi ni mzaliwa wa Iringa, nilipata bahati kuzaliwa katika nyumba ambayo muziki ulikuwa sehemu kubwa ya maisha. Moja ya starehe kubwa ya wazazi wangu ilikuwa muziki, baba yangu alikuwa mpiga gitaa mzuri aliyerekodi nyimbo zake kwa mara ya kwanza Tanganyika Broadcasting Services (TBC) mwaka 1960 na nyimbo hizo kupigwa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha Jimbo Letu, 16 May 1960. baba alilipwa shilingi 40. Hili ni ushahidi kuwa kabla ya Uhuru wanamuziki walilipwa mirabaha kila nyimbo zao zilipopigwa katika redio miaka hiyo. Niliwahi kumuona baba pia akipiga accordeon, trumpet na saxophone, ila chombo chake haswa kilikuwa gitaa lisilotumia umeme, acoustic guitar, ambalo alikuwa akipiga katika  mtindo wa Folk Music, au mtindo wa kupiga gitaa kwa kutumia vionjo vya utamaduni asili wa mpigaji, nae tungo zake zilitokana na utamaduni wa kabila lake la Kihehe. Hivyo nilipokuwa mdogo nilishirikishwa kuimba wakati akipiga gitaa na kuupenda muziki toka nikiwa na umri mdogo. Pia nyumbani tulikuwa na radio na gramaphone iliyokuwa na santuri za muziki aina mbalimbali,muziki wa Kiswahili, Kihindi, Kiingereza na muziki toka Afrika ya Kusini na Kongo, hivyo muziki ulikuwa masikioni muda mwingi wa maisha yangu ya awali.  Nilianza shule mwaka uleule ambapo Tanganyika ilipata Uhuru, nakumbuka tulifagia barabara za jirani na shule yetu kisha kuzimwagia maji siku moja kabla ya Uhuru, ili siku ya Uhuru kusiwe na vumbi.
Shuleni kulikuwa na kipindi kilichoitwa ‘Kuimba’, mwalimu alihakikisha anafundisha japo wimbo mmoja kwa wiki, vitabu maalumu vilikuwepo vikiwa na nyimbo zilizokuwa na mafunzo ya maisha, kuheshimu wazazi, wakubwa, kupenda shule na kadhalika. Somo hili lilikuweko katika ngazi zote za shule za msingi, na kulikuweko waalimu wengi waliokuwa wakijua kusoma na kuandika muziki kwa nota hivyo wanafunzi kupewa elimu ya muziki zaidi ya kuimba nyimbo. Shule zote zilikuwa na bendi ya shule. Ambayo kila asubuhi bendi  ilipiga muziki wakati wanafunzi wakikaguliwa kama wamekuja shuleni wasafi, moja ya ndoto zangu ilikuwakuja kuwa mmoja wa wana bendi ya shule. Nilitamani aidha kuwa mpiga ngoma au mpiga filimbi na kubwa kuliko yote ni kupata bahati kuwa mshika kifimbo. Shule zilishindana kwa kuzivalisha bendi mavazi bora na upigaji kuwa makini na hivyo siku za sikukuu kila shule ilijitahidi bendi yake ndio iwe bora. Hakika nakumbuka raha iliyokuwepo wakati shule mbalimbali zilipokutana siku ya siku kuu au kukiwa na maandamo na kisha kila bendi kupita mbele ya mgeni wa heshima, wanafunzi tulijitahidi kuwa wasafi, wakakamavu na wenye nidhamu ili shule yetu ishinde.  

Kila shule ilikuwa na vikundi vya kwaya, ngoma za asili na nyingine kuwa na bendi za muziki wa kisasa. Nilisoma shule iliyokuwa na wahindi wengi, Iringa Aga Khan Primary School, bila kujali kabila wote tulicheza ngoma za asili. Hakika kulikuwa na wahindi wanajua kucheza sindimba kuliko waswahili. Siasa ya Ujamaa iliingia wakati niko darasa la saba. Mambo mengi yalibadilika, nyimbo, ngoma ngonjera, mashahiri yakanza kuwa ni ya kisiasa, nyimbo nyingi za kiasili zikapewa maneno ya kisiasa, maafisa utamaduni ndio walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha hili, kwa kuzunguka kuhamasisha na hata kutoa adhabu kwa vikundi vilivyoonekana havitaki kuimba nyimbo za siasa. Mashuleni tulianza kuimba nyimbo za siasa kwa uwingi zaidi, somo la kuimba lilikuwa likifundisha nyimbo za siasa tu. Kwaya zilizokuwa na nyimbo mbalimbali za siasa kutoka kila upande wa nchi, zilirekodiwa na Radio ya Taifa ambayo kwa wakati huu iliitwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Uzalendo ulikuwa ndio ‘habari ya mjini’. Kila mwisho wa onyesho la muziki bendi zililazimika kupiga ule wimbo wa ‘Chama cha Mapinduzi chajenga nchi’. TANU Youth League (TYL) ilikuwa na matawi kila mahala. Kimuziki TYL ilichangia sana, kwani kila kwenye tawi la TYL lazima kulikuwa na kundi la muziki aidha kwaya au ngoma, na mara nyingi vyote na sehemu nyingi TYL pia ilinunua vyombo vya bendi na hivyo karibu kila wilaya ilikuwa na bendi. Hapa ndipo wanamuziki wengi maarufu wa miaka hiyo na ambao nyimbo zao bado maarufu mpaka leo walikotokea. Pale Iringa, vyombo vya TYL hatimae viliishia kuwa chini ya shule ya Sekondari ya Mkwawa na hivyo pale kulikuwa na bendi nzuri sana ambayo iliweza kuja kurekodi RTD ikiwa na mtindo wao wa Ligija, kati ya waliokuwa wanamuziki wa bendi hiyo, mpia solo ni mzazi wa producer mmoja maarufu wa Bongo fleva na hata yeye alikuja kuwa na bendi yake TZ Brothers, mpiga rythmambaye  kwa sasa ana chuo kikubwa cha muziki pale Tabata, wakati muimbaji mmoja wa bendi hiyo alianzisha bendi maarufu pale Arusha.  Mashirika ya umma, taasisi mbalimbali za kiserikali zilihamasishwa kuwa na vikundi vya utamaduni ambavyo ndani yake kulikuwa na kwaya, bendi na ngoma za asili. Vingi vilikuja kuwa maarufu nchi nzima, kama vile BIMA, vikundi vya majeshi yote, DDC, TANCUT, UDA, URAFIKI ana kadhalika. Pamoja na kutoa burudani vikundi hivi vilijenga uzalendo kwa vijana wa wakati ule. Hakika uzalendo kwa sasa si moja ya vipaumbele na matokeo ya hili ni janga kubwa kwa Taifa .

Miaka 28 bila Franco Luambo Luanzo Makiadi

Franco Luambo Luanzo
François Luambo Luanzo Makiadi  alizaliwa 6 July 1938, katika kijiji cha Soni Bata magharibi mwa jimbo la Bas Zaire huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Wakati akiwa bado mchanga wazazi wake walihamia jiji la Leopodville ambalo sasa linaitwa Kinshasa. Baba yake aliitwa Joseph Emongo alikuwa mfanyakazi wa shirika la reli, wakati huo mama yake alikuwa akiuza maandazi sokoni. Alipofikia umri wa miaka saba alitengeza gitaa lake akawa analipiga kwenye genge la mama yake ili kuita wateja. Mwanamuziki maarufu Paul Ebengo Dewayon ndie aliyegundua kipaji cha mtoto huyu na kuanza kumfundisha rasmi namna ya kupiga gitaa. Mwaka 1950 akiwa na umri mdogo wa miaka 12 alichukuliwa rasmi kama mwanamuziki wa bendi ya Watam iliyokuwa inaongozwa na Dewayon. Kipaji chake kiliwashangaza wengi hasa kwa vile alikuwa akionekana umbo lake likilingana na ukubwa wa gitaa analolipiga, lakini akiwa analipiga kwa umakini mkubwa. Akiwa na miaka 15 alirekodi wimbo wake wa kwanza ulioitwa Bolingo na ngai na Beatrice (Mapenzi yangu kwa Beatrice). Wimbo huu aliutunga alipojiunga na bendi iliyokuwa inamilikiwa na Studio za Loningisa. Kiongozi wa bendi hiyo Henri Bowane ndie aliyeanza kufupisha jina la mwanamuziki huyu na kumuita Franco, jina alilokuja kujulikana nalo maisha yake yote. Mwaka 1955 alianzisha bendi akishirikiana na Jean Serge Essous, bendi ilizinduliwa katika ukumbi wa OK Bar, hatimae bendi ilichukua jina la OK Jazz kwa heshima ya bar ambapo ilizinduliwa.Katika muda mfupi ikiwa na mwimbaji Vicky Longomba(Baba yake Lovy Longomba) walianza kuwa bendi pinzani ya bendi kongwe ya African Jazz iliyokuwa inaongozwa na Joseph Kabasele maarufu kwa sifa ya Grand Kalle. Mwaka 1958 Franco aliteuliwa kuwa kiongozi na mtunzi mkuu wa Ok Jazz,  kundi alilokuja kulijenga kwa kuanzia watu 6 hadi kufikia  watu 30 kwenye mwaka 1980. Franco mwenyewe alikuwa anasema OK Jazz iliweza kutoa album 150 katika miaka 30 ya bendi hiyo.Mwaka 1958 Franco alifungwa kwa mara ya kwanza kwa kosa la uendeshaji mbaya wa gari, lakini siku ya kutoka kwake jela ilikuwa kama shujaa katoka vitani, inasemekana sababu ya kufungwa ilikuwa ya kisiasa zaidi kwani alikuwa katunga wimbo ambao haukupendeza wakoloni wakati ule. 1960 Vicky Longomba aliacha bendi. Lakini wakati huo Kongo ilikuwa kwenye vuguvugu za kutafuta uhuru na nchi ilikuwa si shwari Franco akahamia Ubelgiji. Baada ya Mobutu Sese Seko kushika nchi na kukawa na amani katika nchi iliyoitwa sasa Zaire,  Franco akarudi kwao mwaka 1966. Akashiriki katika Tamasha la Sanaa Za Afrika lililofanyika Kinshasa 1966 na Franco akawa kipenzi cha serikali ya Mobutu.
Franco hakuwa tu mwanamuziki mzuri bali pia aliendesha vizuri sana biashara zake za kurekodi na kampuni alizozianzisha wakati huo. Alikuwa na lebo kama (Surboum OK Jazz, Epanza Makita, Boma Bango and Éditions Populaires). Katika miaka ya 70 muziki wa Kongo ulishika kasi sana Afrika na Franco akiongoza jahazi kwa nyimbo kama Infidelité Mado,  na akaendeleza kupiga mitindo mbalimbali kama Bolelo na muziki uliotokana na ngoma za asili toka Kongo zikichanganywa na mapigo kutoka Cuba na kuanza upigaji wa gitaa uliokuja itwa Sebene.
 
Bavon  Marie Marie
Mwaka 1970 Franco alimpoteza mdogo wake ambaye nae alikuwa mpiga gitaa mashuhuri Bavon Marie-Marie Siongo ambaye alifariki katika ajali ya gari. Lilikuwa pigo kubwa kwa Franco kwa miezi kadhaa aliaacha hata kupiga muziki. Baada ya hapo OK Jazz ilibadili jina na sasa kuitwa TP OK Jazz na mwaka 1973 kutoa kibao kingine kilichotikisa Afrika, AZDA.  Wimbo huu kwanza ulirekodiwa kama tangazo kwa ajili ya  kampuni ya Volkswagen VW. Mahusiano yake na Mobutu yalikuwa na mawimbi mara wakipatana mara wakikosana kutokana na Franco kuwa anatumia nyimbo zake kukosoa serikali ya Mobutu. 1970 Franco alikuwa ni Rais wa wanamuziki wa Kongo na pia kuajiliwa na kampuni ya kugawa mirabaha ya wanamuziki. Aliendelea kutajirika kwa kuweza hata kunua ardhi nchini Ufaransa, Ubergiji na Kongo, na kuwa na nightclub 4 kubwa kuliko zote Kinshasa kwa wakati huo na kufanya club mojawapo
kuwa ndio makao makuu yake. Hapo ilijengwa studio kubwa, office na apartment za kuishi kadhaa. Mwaka 1978 alitiwa mbaroni  tena baada ya kugundulika kuwa alikuwa anasambaza nyimbo zenye matusi ambazo hakuzipitisha katika  kamati ya kuchunguza mashairi kama ilivyokuwa kawaida wakati ule. Kufikia kipindi hiki TPOK Jazz  ilikuwa kubwa kiasi iliweza kumeguka kuwa mbili moja ikifanya kazi Afrika wakati nyingine ikiwa inafanya maonyesho Ulaya. !983 Franco alifanya maonyesho kadhaa Marekani lakini hayakufanikiwa haijajulikana mpaka leo sababu za kushindikana huko. Katikati ya miaka ya 70 Franco alibadili dini na kuwa Muislam na kupewa jina la Abubakkar Siddiki, japo hakuonekana kufuata taratibu zozote za Kiislamu na akaendelea kuitwa Franco. 1980, Franco alitajwa kama ndie Grand Master wa muziki wa Kongo na serikali ya nchi hiyo, nyimbo zake nyingi zikaanza kuwa zinasifia utawala ulikuweko madarakani. 1985 Franco alitoa wimbo ambao uliuza kuliko nyimbo zake zote, wimbo ulioitwa Mario,  wimbo ambao ulikuwa ni hadithi ya mwanaume kijana  ambae alikuwa anategemea akina mama watu wazima wamlee.
Franco
1987 zilianza habari kuwa Franco anaumwa sana, na kwa mwaka ule alitoa wimbo mmoja Attention Na SIDA
 (Jihadhari na UKIMWI), wimbo huu ukaanzisha maneno kuwa pengine Franco amekwisha pata ugonjwa huu. Franco akawa taratibu anakosekana kwenye shughuli za bendi nayo ikaanza kumeguka kutokana na kutokuwa na uongozi thabiti. Franco tena akarudi kwenye dini yake ya awali ya Roman Catholic. Tarehe 12 Oktoba 1989, Franco alifariki katika hospitali moja Ubelgiji. Mwili wake ukarudishwa Kongo, sanduku likiwa limefunikwa bendera ya Taifa lake na kupitishwa katika mitaa ya Kinshasa na kuagwa na maelfu ya wapenzi wake. Serikali ikatangaza siku 4 za maombolezo ambapo redio ya serikali ilipiga nyimbo za Franco tu. Franco alizikwa tarehe17 Oktoba 1989. Alifariki akiwa na miaka 51. Mungu amlaze pema peponi


Thursday, October 12, 2017

PICHA ZA ZIADA ZA MAZISHI YA SHABANI YOHANA WANTED

 JITIHADA ZA WANAMUZIKI HAWA WAKONGWE ZILIFANIKISHA MAZISHI YA MWANAMUZIKI MWENZAO.






 HATIMAE SAFARI YA KWENDA MICHUNGWANI KWA MAZISHI ILIANZA


  KWAMGWE KIJIJI ALIKOZIKWA SHABANI YOHANA WANTED






 WANAMUZIKI WALIKUTANA NA MZEE MASONGI











 IBADA  YA MAZISHI NYUMBANI









 KANISANI










 MAZISHI









































 PICHA BAADA YA MAZISHI














 KURUDI NYUMBANI