Sunday, April 22, 2018

KILA ZAMA NA AINA YAKE YA UTUNZI WA MUZIKI




Wanamuziki wakongwe wakiwa mazoezini



Hapa kazi tuu, King Kiki akiwa katika mazoezi ya wimbo mpya
Juzi nilikuwa naongea na msanii maarufu ambaye ana wimbo ambao kwa sasa haukosi kupigwa hewani mara tatu kwa siku. Kizazi chake wanasema ametoka. Nilikuwa na maswali machache kwa ‘supastaa’ huyu. Nilipokuwa nausikiliza wimbo wake nimependa sana uimbaji wake lakini nilikuwa shida kuelewa mpangilio wa vyombo katika muziki huo, hivyo nilitaka kujua aina ya vyombo alivyotumia na  pia kujua alikuwa ana sababu gani kutumia vyombo hivyo. Kifupi tu alishangaa swali hilo na alikuwa hana jibu. Alisema aliyepanga hivyo vyombo si yeye bali producer wake. Jibu lake lilinirudisha nyuma sana wakati nikiwa katika bendi miaka ya 80 jinsi tulivyokuwa tukitunga na hatimae kurekodi nyimbo, hakika taratibu zilikuwa tofauti. Katika zama hizi msanii hutunga ‘mistari’ yake na kufanya mazoezi ya kuuimba peke yake kisha huingia studio ambako ‘producer humtengenezea muziki au maarufu ‘beat’ kutoka hapo wimbo huenda hewani. Hali ilikuwa tofauti sana huko nyuma.  Labda nirudishe picha miaka ya 80 mwishoni nilipokuwa bendi ya Tancut Almasi iliyokuwa na masikani yake Iringa.  Mwanamuziki yoyote mwenye uwezo wa kutunga aliruhusiwa kutunga wimbo, watunzi walikuwa wa aina tofauti, watunzi maarufu  mapacha Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa walikuwa wakitunga pamoja, hivyo walikuwa wakileta wimbo ambao umekwisha pangwa sauti za uimbaji na hata magitaa ya kusindikiza, ambayo waliyaimba kwa mdomo, na hivyo kurahisisha kidogo utengenezaji wa wimbo mzima. Lakini watunzi wengine walikuja tu na mashahiri na kutegemea watu wengine watunge sauti na kupanga vyombo. Lakini kitu cha kwanza ambacho  kilikuwa kinafanyika kwa tungo yoyote ile,  ilikuwa ni mtunzi kuyasoma mashahiri yake mbele ya watu wote, na hapo mashahiri yalianza kuchambuliwa  kuona kama yalikuwa na mistari iliyoleta maana na iko katika Kiswahili fasaha, na  hata kuangalia maadili katika tungo hiyo. Baada ya hapo ndipo mtunzi alianza kuuimba wimbo huo wakati waimbaji wenzie wakimsikiliza, na kuchangia hapa na pale kuboresha melodia hiyo.  Baada ya hapo waimbaji walianza kupangiana sauti ili kuleta muafaka katika wimbo huo. Wakati huo mpiga gitaa mmoja mara nyingi mpiga gitaa la rhythm, alikuwa akisindikizana na waimbaji wakati wa kuanza kujenga njia za wimbo huo.  Baada ya hapo wapiga magitaa wote walikaa pembeni na kupanga magitaa yao.  Vyombo vya upulizaji vilifuata na hatimae wimbo ulikuwa tayari. Bendi iliufanyia mazoezi kati ya wiki moja au mbili kabla ya kuanza kuupiga hadharani.  Siku ambayo wimbo ulikuwa unapigwa kwa mara ya kwanza hadharani, kila mmwanamuziki wakiwemo mafundi mitambo hata marafiki wa karibu wa bendi walikuwa wakiangalia wimbo umepokelewa vipi na wapenzi, wimbo ukionekana umepigwa mara mbili au tatu lakini haujapokelewa vizuri, wimbo huo ulirudishwa tena mazoezini au mara nyingine ulikufa hapohapo na haukupigwa tena, labda mtunzi angeupika tena. Wimbo ukipata bahati ya kurudi mazoezini watu waliulizana kwanini haukupokelewa vizuri, na kwa kweli watu walikuwa wanapeana ukweli kiasi cha kwamba mara nyingi baada ya kufanyiwa marekebisho wimbo uliweza kupokelewa vizuri na kuingizwa katika orodha ya nyimbo za kurekodiwa. Nyimbo zilipigwa ukumbini kwa muda wa miezi kadhaa kabla ya kurekodiwa, hivyo ‘kuuivisha’ kwa maboresho ya hapa na pale kila ulipopigwa ukumbini. Bendi zilikuwa zikirekodi nyimbo zao katika studio za RTD, taratibu zilizokuweko ni kuwa kabla ya kupangiwa siku ya kuingia studio, bendi zililazimika kupeleka RTD mashahiri ya nyimbo zote ambazo zinatakiwa kurekodiwa. Huko kulikuwa na kamati ambayo iliyapitia mashahiri hayo na kuidhinisha kurekodiwa au kukataa kurekodiwa nyimbo ambazo zilionyesha kuwa na tungo tata. Nyimbo nyingi zilipita bila kupingwa kwa kuwa bendi zilikuwa zinafanya kikao cha ndani cha kuangalia upya mashahiri kabla ya kuyapeleka RTD. Lakini pamoja na matayarisho hayo,  bado nyimbo kadhaa zilikwama au nyingine kukatazwa kurushwa hewani japo zilikuwa zimepita katika kamati ya awali. Siku hizi mtu anaweza kuchukua mwezi mzima kurekodi wimbo mmoja, hali haikuwa hivyo zamani. RTD walikuwa wakitoa siku mbili kwa kila bendi kuwa studio. Siku ya kwanza kurekodi nyimbo zote, hata kama ni 15. Na muda wa mwisho kuwa studio ilikuwa ni saa 12 jioni, hivyo ilikuwa muhimu kufanya sana mazoezi kabla ya kuingia studio ili kutumia vyema muda huo. Siku ya pili bendi ilishiriki katika kurekodi kipindi cha Klabu Raha Leo Show. Ni wazi ukielewa aina ya ugumu wa taratibu za kurekodi na kuona kuwa nyimbo zilizorekodiwa katika mazingira hayo bado ni maarufu miaka hamsini baada ya kurekodiwa, mtu unaelewa ubora wa wanamuziki katika miaka hiyo.  Kutokana na aina ya kurekodi hii mwanamuziki ulijua kabisa ni vyombo gani vimetumiwa katika wimbo wako na kwanini chombo fulani kimepigwa katika sehemu fulani. Hakika kila zama na vitabu vyqake.

No comments: