Tuesday, August 15, 2017

Penzi shubiri 1

Sehemu ya Kwanza
 

Julai 22, 2004 – Moshi, Kilimanjaro.
NILIKUWA nimejilaza kwenye sofa kubwa, nikiwa nimevaa bukta yangu nyepesi na flana ya kukata mikono, kifuani mwangu kulining’inia cheni ya dhahabu iliyong’ara barabara, huku macho yangu nikiwa nimeyaelekeza kwenye TV yangu kubwa ya rangi iliyokuwa pale sebuleni kwangu, iliyokuwa inaonyesha mwanadada mrembo Celine Dion na wimbo wake wa I’m Alive. Wimbo huo kipenzi changu cha moyo wangu, Josephine alikuwa anaupenda sana. Nikatamani atoke mapema huko bafuni ili auone na kuusikiliza.

Ghafla simu ya mpenzi wangu, Josephine ambayo ilikuwa pale mezani iliita! Sikung’amua mara moja kuwa ilikuwa ni simu au ni ujumbe mfupi wa maneno. Kwa kuwa mimi na mpenzi wangu Josephine tunaaminiana, niliamua kuiendea simu ili nipokee!
Baada ya kuifikia niligundua ilikuwa siyo simu bali ni ujumbe mfupi wa maneno. Ilikuwa ni kawaida yetu kila mmoja kuangalia simu ya mwenzake, kutokana na sababu hiyo, sikuona woga kufungua ule ujumbe mfupi uliokuwemo na kuanza kusoma.

Kila nilipomaliza kusoma neno moja, ndivyo jazba ilivyozidi kunipanda. Nusura nipate uchizi. Uso wangu ulikuwa umechora makunyanzi makubwa mithili ya matuta kutokana na jazba iliyokuwa inaendelea kunipanda kila nukta moja ilipoondoka.
Sikuamini yaliyotokea kuwa ni kweli au nilikuwa ndotoni, nilikuwa naombea iwe ndoto na sio kweli. Hasira ikanijaa. Unaweza kudhani labda ni hadithi ya kufikirika, lakini haikuwa hivyo bali ilikuwa ni ukweli halisi.

“Shit…! Huyu mpuuzi ananitania siyo? Ngoja atoke huko bafuni,” niliwaza.
Nilikaa kimya nikiwa nimeishikilia ile simu, nisijue la kufanya. Niliduwaa. Nikawa namsubiri kwa hamu sana atoke bafuni ili anieleze vizuri.
Kitambo kidogo Josephine akatamalaki sebuleni mwangu akiwa na upande mmoja wa khanga ya Zanzibar, meno yake meupe aliyaachilia kinywani mwake. Utepe wa maji kwenye khanga yake uliosababisha kuuchora umbo la mwili wake kama lilivyo, lilimfanya aonekane mzuri.
Ni kweli alikuwa mzuri!
Alitegemea kunipagawisha kwa umbo lake. Ndivyo anavyofanya mara nyingi. Lakini sasa hakuwa na thamani tena mbele yangu. Nilikuwa namwonea kinyaa!

Akanisogelea pale nilipokuwa na kuanza kunipigapiga kifuani huku akichezea garden love yangu.
Nikamwonya!
“Naomba niache tafadhali!” nilimwambia, akadhani namtania.
“Una nini tena honey?”aliniuliza kwa sauti yake ya mahaba.
Sauti hiyo ilikuwa na thamani zamani na siyo sasa. Sasa ilikuwa ni kero na makelele masikioni mwangu.
Sikumjibu.

“Mbona unakuwa hivyo Masumbuko? Au kuna taarifa ya msiba umesikia?”
Akaniongezea hasira mara mbili, nilimwambia neno moja tu.
“Ondoka mbele yangu Jose…”
Hakusikia!
Nikamwonya tena, hakujali, akabetua midomo yake akaniambia:
“Lakini mpenzi kwani kun…….” sikumpa nafasi ya kumalizia ujinga wake, nilimgeukia kisha nikamwangalia kwa hasira kali ambayo ilikuwa wazi kabisa kisha nikamsindikiza na kibao kikubwa kilichompata bara-bara usoni mwake. 
Akaanza kulia, tena kwa sauti ya juu, nikaenda mpaka mlangoni nikaufunga mlango wangu na kurudi tena ndani.
“Hivi ni kitu gani umetaka nikakunyima wewe mwanaharamu?” nilimwuliza kwa hasira.
“Yaani leo umefika hatua ya kuniita mimi mwanaharamu…..eti. …Masumbuko uharamu wangu ni nini haswa niambie basi!” alianiambia kwa kunikaripia huku akiendelea kulia kilio cha kwikwii.
“Unataka kujua uharamu wako siyo?” Nilihoji kwa hasira.
“Nd..i..ooo,” akaniambia.

“Nd…i…oooooooooo,” nikamjibu kwa kejeli.
Nikampa ile simu na kumwonyesha ile meseji na kumwambia aisome kwa sauti!
Hakusoma kwa sauti!
Aliogopa!
Alivyomaliza tu aliniangukia miguuni mwangu na kunitaka radhi, huku akidai kuwa ni wapambe wasiopenda mapenzi yetu ndiyo wanataka kutuchonganisha.

“Mimi siyo mpuuzi kama unavyodhani, wala mimi si limbukeni wa mapenzi kiasi hicho, haiwezekani mapenzi yaniumize na kuninyanyasa kiasi hiki, yaani mimi ninakupenda kwa moyo wangu wote nakugharamia kwa kila utakacho, nafanya kazi usiku na mchana ili nimudu kukutimizia mahitaji yako yote, lakini wewe leo hii unanifanyia hivi sio? 
“Sawa mimi sina haja nawe tena, endelea na maisha yako kama kawaida, sawa Josephine?” nilimwambia kwa hasira huku nikiwa nimeishika ile simu yake mkononi mwangu.
Hasira ilinishika, jazba ikanipanda, hamu ya kuendelea na Josephine ilinitoka kabisa. Nilimwonea kinyaa, nilihisi harufu ya damu, tena damu mbichi! Sio siri sikumuhutaji tena Josephine.

Midomo ya Josephine ikaanza kutingishika, alikuwa kama anamung’unya mamung’unya! Akaanza kuongea!
“Sikiliza nikuambie Masumbuko ni wambea hao ambao hawapendi mapenzi yetu yaendelee, mimi sina mwingine zaidi yako mpenzi wangu Masu…naomba uniamini tafadhali mpenzi wangu usiniache tafadhali mpenzi nakuomba,” aliniambia huku machozi yakimtiririka mashavuni mwake mithili ya vijito vidogo. 
Alikuwa akilia umbea, kwani si ni kweli kuwa aliandikiwa ujumbe kwenye simu yake akitakiwa kukutana na huyo mpuuzi mwenzake kwenye nyumba ya kulala wageni.

“Sidhani kama kuna utakachoniambia nikuelewe, unalia unafiki tu kwa hiyo wewe una marafiki wanafiki? Sawa labda unao na ukayaandika majina yao kwenye simu yako sio?” nilimwuliza kwa jazba ya wazi kabisa ambayo hapakuwa na njia ya kuficha hasira yenyewe.

Baada ya kumshawishi kwa muda mrefu aniambie ukweli aliamua kunieleza ukweli halisi.
“Samahani sana mpenzi ni tamaa tu ndio imeniponza, ni kweli kuwa nina mahusiano na Gabby lakini alinishawishi kwa pesa zake naomba unisamehe na kuanzia leo naachana naye kabisa…naomba uniamini mpenzi,” ilikuwa ni kama ndio amewasha moto wa kifuu nikamvutia nje na kumtoa chumbani mwangu.

Ghafla nilikurupuka usingizi. Nikapekecha macho mara kadhaa, nilikuwa nahema sana, ilikuwa ni ndoto! Ni ndoto lakini ilikuwa ni tukio lililowahi kunitokea kipindi cha nyuma. Hakika sikuipenda ile ndoto, kwa sababu ilikuwa inanikumbusha machungu ambayo nilikuwa nimeshayasahau.
Nilichukia, nikaanza kulia! Baada ya muda niliona kulia sio suluhisho. Nikanyamaza.
Nikayatupa macho yangu kwenye saa iliyokuwa ukutani, ilionyesha kuwa ilikuwa tayari ni saa kumi na mbili unusu za asubuhi.
Macho yanitoka pima!

Baada ya kushtuka nilitulia kwa muda, nikatingisha kichwa kwa nguvu kisha nikatumbulia macho saa yangu ya ukutani, sikuamini nilichokiona kwenye saa yangu, haikuwa kawaida yangu kuchelewa kuamka kiasi kile. Nilishazoea kuamka saa kumi na moja kamili za alfajiri kila siku.

Sikutaka kupoteza muda niliingia maliwatoni na kujiswafi kabla ya kujitayarishia kifungua kinywa mezani. Baada ya kupata kufungua kinywa niliingia kabatini na kuchagua nguo maridadi za kuvaa. Baada ya kuvaa nikakiendea kioo ili kunihakikishia umaridadi niliokuwa nao. Ebwana…eh! Si-mchezo, kweli nilipendeza haswa.

Muda mfupi baadaye tayari nilikuwa nimeshafika kwa mzee Moringe, sehemu ambayo huwa ninapaki gari langu baada ya mizunguko ya siku nzima ya kutafuta abiria ambao kwa hakika si wote huwa wastaarabu.
“Shikamoo,” nilimsalimia mara baada ya kunifungulia geti.
“Marhaba Masumbuko, umechelewa sana leo, sio kawaida yako nini kimekusibu?” aliniuliza  mzee Moringe kwa utani na kejeli.
Mzee Moringe anapenda sana mizaha ingawa ni kweli nilichelewa lakini aliamua kunichemsha bongo kidogo.
“Ah! Nilipitiwa tu mzee, usingizi wa leo kiboko!” nilimwambia.
Mzee Moringe huwa ana kawaida ya kulaza magari nyumbani kwake, alijenga eneo kubwa lenye uzio na walinzi wawili wakakamavu maalum kwa ajili ya kazi hiyo ya ulinzi wa magari.

Tayari mvi zilianza kutapakaa karibu kila eneo la kichwa chake. Nilimpatia fedha zake akanipa stakabadhi nikawasha gari nikatoweka maeneo yale kabisa.
Muda mfupi baadaye nilikuwa nimeshafika katika kituo changu cha kusubiri abiria, eneo la kituo cha mabasi ya mikoani mjini Moshi. Kipindi hicho nilikuwa naishi Oysterbay. Kabla hata sijafikisha dakika tano tangu nifike pale kijiweni kwangu, simu yangu ya mkononi iliita. Niliingiza mkono mfukoni na kuitoa. 
Jina nilokutana nalo kwenye kioo cha simu yangu lilikuwa faraja kubwa sana kwangu. Jina lile lilinipa uhakika wa kuishi maisha ya starehe kwa siku mbili tatu hivi, kwenye kioo cha simu kilionyesha jina lililoandikwa Shams.
Huyu ni mfanyabiashara ambaye kila alipokuwa akija Moshi hunichukua kwa siku zote atakazokuwa hapa nikimpeleka kila kona ya sehemu aliyotaka. Alinilipa ujira wa kutosha na starehe za kila aina.
Nikambonyeza kitufe cha kupokea simu nikaanza kuzungumza na sauti ya upande wa pili.
“Haloo!” Ndio sauti iliyopenyeza kwenye ngoma za masikio yangu.
“Haloo bro Shams vipi?”
“Salama mimi nimeshafika hapa Moshi nipo hotelini naomba uje tafadhali kuna mahali nataka kwenda.”
“Sawa bro…kwa hiyo umefika lini? Nilijidai kumbamiza swali.”

“Jana jioni… weka mafuta full tank.”
 “Sawa bro, nipe dakika tatu nitakuwa hapo.”
“Sawa!”
Tukakata simu zetu.
Nilivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu, udenda wa furaha ukaanza kunitoka sikumuaga mtu yeyote pale kijiweni, nilichokifanya ni kuingia garini, nikawasha, nikaingiza gia namba moja nikatokomea kwenye kituo cha mafuta.

Kitambo kidogo nilikuwa hotelini kwa Shams, nikaegesha gari nikatoa simu yangu, nikapekua kwenye orodha ya majina yaliyopo kwenye simu, nilipokutana na jina la Shams nikabonyeza kitufe cha kupiga simu. Baada ya mazungumzo yangu na Shams aliniambia tayari ameshajitayarisha hivyo nimsubiri pale pale nje.
Muda si muda Shams akatamalaki akiwa amevaa suruali maridadi ya kijivu, shati la rangi ya damu ya mzee, viatu vilivyochongoka mbele, kifuani ilining’inia tai maridadi kabisa kiufupi ni kwamba Shams alipendeza haswa!

“Za siku nyingi bwana?” Ndio swali la kwanza kuniuliza baada ya kuniona.
“Salama habari za wapi? Mbeya, Tanga, Dar, Iringa… au…”
kabla sijamalizia sentensi yangu alishadakia.
“Nimetoka Dodoma bwana!” alibainisha.
“Ok! Habari za Dom?” Nilimwambia huku nikijichekesha.

“Nzuri tu, sasa nipeleke Soweto kwanza nikamsalimie mtoto Linna baada ya hapo tutakwenda Majengo nikamsalimie Halima. Halafu ratiba nyingine tutapanga baadaye!” alisema.
“Sawa brother!”
Gari sikuwa nimelizima !

Lilikuwa silence!
Nikaingia garini nikatupia gia, nikaondoa gari. Safari ya Soweto ikaanza. Haikuchukua muda mrefu tulikuwa getini mwa nyumba anayoishi mrembo Linna.
Nilipiga honi mfululizo mpaka Linna akaja kufungua geti.
Linna kweli kiboko!
Alikuwa Linna kweli!
Binti wa Kitanga, mtoto mweupe asiye na doa, siyo mrefu, wala sio mfupi. Asikudanganye mtu Linna alikuwa mrembo haswa!
Huko nyuma balaa!
Mtoto wa watu alikuwa kajaliwa, nisije kusahau miye nikawanyima uhondo, tabasamu lake mh! Usisikie. Kila akiachia tabasamu vijishimo huonekana mashavuni mwake.
Lafudhi yake ya kitanga ndio-funga kazi, akianza kuzungumza utatamani aendelee kuzungumza huku ukimsikiliza kwa makini neno moja-moja likiburudisha ngoma za masikio yako.
Sijui kama ni kweli!
Ila mimi naamini hivyo!
Sasa, sio lazima na wewe uamini kama mimi, lakini mapenzi ya siku hizi pesa bwana. Nadhani pesa ndio zimesababisha Shams akawa na ujasiri wa kumtongoza binti mrembo kama Linna. Pesa hizo hizo ndizo zilizomfanya Linna kumkubali Shams.
Ebwanae, pesa sabuni ya roho rafiki yangu.
Baada ya mlango mdogo wa geti kufunguliwa nyuso zetu zilikutana na sura yenye furaha na bashasha haswa! Alikuwa Linna na upande wa khaga nyepesi macho yetu kwa pamoja yalipata burudani bila malipo yeyote!
“Karibuni jamani!” ndio neno alilotamka baada ya kutuona.
“Ahsante!” tuliitika kwa pamoja.
Lina aliusogelea mlango wa gari akaufungua ili Shams atoke.
Shams akatoka!
Ile kutoka tu, akarukiwa almanusra ule upande wa khanga udondoke chini, wakabaki wamekumbatiana kwa takribani dakika nzima na sekunde kadhaa, macho ya husuda yakinitoka, mshawasha wa mapenzi ukanipanda nikatamani mimi ndio niwe Shams.
Nilimwonea wivu!
Ghafla wakaachiana.
Linna akaingia ndani, Shams akanisogelea kisha akafungua pochi yake akatoa noti tatu za shilingi elfu kumi kumi, akanikabidhi.
Sikuamini!
Ndiyo ilivyokuwa!
Nikawa kimya nisijue nini cha kufanya, midomo ya Shams ikafunguka. Akaanza kuzungumza.

“Sasa, Masumbuko endelea na mizunguko yako nitakupigia nikikuhitaji baadaye ila jiandae vizuri usiku tutakwenda club au vipi?” aliniambia kwa mapozi ya kipesa.
Ni halali pia kuwa na mapozi ya kipesa kama yale kwa sababu alikuwa nazo.
“Sawa!” niliitika.
Nilimsindikiza kwa macho mpaka akatokomea ndani. Nifanye nini sasa, zaidi ya kuwasha gari na kuondoka?
Nikatambaa zangu!
***

Baada ya kufanya mipango yote kwa siri, tuliamua tukapumzike Marangu Mtoni, twende huko siku ya week-end tukafurahie maisha!
Kila nikiufikiria uzuri wa Linna nazidi kuchanganyikiwa, siyo siri Linna ni mrembo jamani! Tamaa ya mapenzi ilinizidi, mshawasha wa mapenzi ukanipanda nikaamua kumweleza hisia zilizoko katikati ya moyo wangu.

No comments: