Sunday, August 13, 2017

MIAKA 13 TOKA KIFO CHA PATRICK BALISIDYA


Jina Patrick Balisdya halitakuwa geni kabisa kwa wadau wa blog hii,lazima roho zimeanza kuwadunda kama inavyokuwa kwangu kila nikimkumbuka Blai. Patrick Pama Balisidya alizaliwa Mvumi Dodoma tarehe 18 April 1946. Kabila lake alikuwa Mgogo , kabila ambalo lina wanamuziki wengi maarufu kutokana na muziki kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kabila hilo. Mama yake alikuwa anapiga kinanda kanisani na hivyo basi kutokana na asili ya kabila lake na pia kutokana na mama yake, hakika huyu angeweza kujisifu kuwa muziki uko katika damu yake. Mdau mmoja alitutaarifu kuwa Balisidya alikuwa kiongozi wa Bendi ya shuleni kwake Dodoma secondary School. Ambapo kutoka hapo alijiunga na Chuo cha Ufundi , na baada ya kumaliza mafunzo alifanya kazi hiyo kwa muda na 1967 akawa tayari anapiga muziki Dar Es Salaam Jazz B. Bendi hii ilikuwa inafanya kazi nzuri hivyo kuanza kuwa tishio kwa bendi kongwe Dar Jazz, na hivyo uongozi wa Dar Jazz ukaamua kuivunja bendi hiyo kabla haijaipoteza kabisa bendi kaka. Patrick hakufurahishwa kwa hiyo kufikia mwaka 1970 Patrick alikuwa ameanzisha kikosi chake mwenyewe Afro70, kikiwa na mtindo wake Afrosa. Alikuwa mbunifu katika muziki wake, na kwa muda mrefu alikwepa sana kuingia katika wimbi la kufuata mapigo ya Kikongo kitu ambacho hata wakati huo bendi nyingi zilikifanya, japokuwa kukutana na Franco wakati alipofanya moja ya ziara zake nchini humu 1973 kulimfanya abadili mtindo kwa kipindi kifupi na katika nyimbo moja wapo aliiga kabisa solo la Franco alilolipiga kwenye wimbo wake Georgette. Afro70 iliwakilisha wanamuziki wa Tanzania katika maonyesho ya mtu mweusi Lagos, Nigeria. (FESTAC festival 1977).  Baada ya kushinda safari ya kwenda Festac Afro 70 walianza kuzunguka mikoani kuonyesha umahiri wao, na hii ilikuwa kwa agizo la serikali, bahati mbaya wakati wa kurudi Dar gari lao lilipata ajali na vyombo vyake vyote vilihalibika katika ajali ya gari. Serikali ilikuwa imenunua vyombo vipya kwa ajili ya kuanzisha bendi ya Wizara ya Utamaduni wakati huo, vyombo hivyo ilikabidhiwa Afro 70 kuvitumia FESTAC. Aliporudi kutoka Nigeria Patrick aliamuliwa arudishe hivyo vyombo serikalini. Pia baada ya kurudi Festac bendi ilianza kusambaratika na kitendo cha kunyang'anya vyombo ilikuwa  kutangaza rasmi kifo cha Afro70. Vyombo hivyo vilitumika kuanzisha bendi ya Asilia Jazz ambayo ilikuwa Bendi ya Wizara ya Utamaduni na Vijana. Balisdya alitumia muda mwingi kujaribu kudai haki yake hiyo ambayo ilimkwepa mpaka mwisho wa maisha. Mwaka 1979, Balisidya alikwenda Sweden na kushirikiana na kikundi cha Archimedes akatoa album nzuri sana iliyoitwa Bado Kidogo. Kuna wakati Patrick alijiunga na Orchestre Safari Sound, (Masantula) na kupiga piano katika ule wimbo maarufu, ‘Unambie siri’, Patrick pia alikuwa mpigaji mahiri wa keyboards na gitaa. Kwa kweli nyimbo za Patrick zilizokuwa juu katika chati ni nyingi. Harusi, Dirishani, Weekend, Tausi, Pesa, Nakupenda kama Lulu, Ni mashaka na mahangaiko, Afrika. Patrick alifariki tarehe 7, Agosti 2004 na kuzikwa 12 Aug katika makaburi ya Buguruni Malapa. Daima tutakukumbuka Patrick Pama Balisidya, Mungu akulaze pema peponi


No comments: