Thursday, June 29, 2017

HATIMAE MWANAMUZIKI MKONGWE BROTHER ZENNO AZIKWA

MWANAMUZIKI  na mchambuzi wa muziki wa charanga maarufu kwa jina la Brother Zeno hatimae amezikwa na makaburi jirani na alipokuwa akiishi kule Mbagala Kibondemaji. Zerno ambaye alikuwa muimbaji mzuri atakumbukwa kwa kuwa mmoja wa waanzilishi wa bendi ya Dar es Salaam Jazz B, bendi iliyokuwa ikiongozwa na Patrick Balisidya, ambayo ilianza kufanikiwa kwa kasina kuanza kuwa tishio kwa Dar es Salaam Jazz Band A, chini ya Michael Enoch, bendi ikavunjwa na wanamuziki wengine wakaingizwa Dar Jazz A, lakini Patrick akakasirika na kutokomea , baadae akaja kuanzisha Afro 70 na kufanya mambo makubwa. Baadae Brother Zeno alijiunga na Shirika la Bima ya Taifa, na baada ya kujiunga kampuni hiyo ndie aliyetoa msukumo wa kuanzishwa kwa bendi katika shirika hilo, Bima Jazz Band na hivyo pia kupewa kazi ya kutafuta wanamuziki wa kujiunga na bendi hiyo na yeye mwenyewe kuwa kati ya wanamuziki waanzilishi wa kundi hilo lililokuja kujizolea umaarufu mkubwa. Kati ya wanamuziki wa kwanza katika bendi hiyo waliobaki hai sasa ni wawili tu baada ya kifo cha Zeno. 







Binti pekee wa marehemu akiwa na mumewe wakiweka shada la maua







Baadhi ya wanamuziki waliohudhuria mazishi ya Brother Zeno


Aliyekaa ni Abdallah Mbosanga mmoja ya wanamuziki wawili waliobaki hai wa bendi ya Bima Jazz band ya kwanza. Mwingine ni Duncan Ndumbalo

Tuesday, June 27, 2017

KIPOFU WA MAISHA sehemu ya 1




MSOMAJI HII NI STORY YA KUSISIMUA YA BWANA ERICK MOSHA AMBAE AMEPATA SHIDA SANA KATIKA MAISHA YAKE AKIWA KATIKA SAFARI YA KUTAFUTA  ELIMU MKOANO DODOMA.INALIZA SANA
Ilikua ni asubuhi na mapema ubaridi unaopuliza katika mkoa wa na upepo wa msimu katika mkoa wa Kilimanjaro. Ambapo mama erik na mwanae wakiwa wapo katika hali ya majonzi katika kuagana kwani kijana Erick alikua anaelekea mkoani  Dodoma kwa masomo baada ya kupata nafasi ya kusomea uwalimu kwatika chuo hicho
Mama erik  nenda mwanangu kasome maana elimu ndio kila kitu katika maisha yako (huku akilia )maisha ni magumu sana mwanangu unatakiwa ujitume kadri uwezavyo nitajitahd kuuza ndizi ili usome mwanangu..
Erick nimekuelewa mama yangu nitajituma mama sema najickia vibaya mama kukuacha katika hii hali ya upweke nani atakusaidia hata kukatia majani au kulisha ng`ombe zetu mama yangu?
Mama Erick mwanangu usiniofie mimi huku (akfuta machozi)
Erick sawa mama yangu ila nitakukumbuka sana lakin hatuna budi mama baki salama
Mama alinipa elfu ishirini kama nauli ya mimi kutoka pale kuelekea chuoni udom kwani huko nilipanga kufikia kwa mjomba wangu alieitwa Joshua moshikwani ndie angekua mwenyeji wangu kabla ya kufika chuo. Nakumbuka niliondoka siku ile ndo ilikua mara ya mwisho kumuona mama yangu kipenzi ambae mpaka leo namkumbuka kwani ndie muhimili wangu wa pekee…
Nilibaatika kuzaliwa peke yangu na kulelew na mzazi mmoja Baba yangu aliuwawa wakati bado nikiwa mdogo sana nikiwa na umri wa miaka miwili.siijui raha ya kuwa na baba kama watu wengine. Nililelewa na mama kwa kipindi chote hali ya kuwa hali ya nyumbani ilikua ngumu kwani mama yangu hakuopataga bahati ya kusoma katika uschana wake hivyo alikua mama wa nyumbani na alijitoa sana katika malezi yangu hasa kwenye swala la elimu mama yangu alikuwa akinisih nisome sana ili nikomboe maisha ya nyumbani na kufkia ndoto zangu kwa ujimla.
Nilitoka moja kwa moja nikimuaga mama na kwenda moja kwa moja ambapo nilidandia tatu (daladala)ilionifikisha mpaka  njia panda ya machame ambapo nlisubiri gari znazotoka boma znazoelekea mkoani Dodoma ili kufika kwa mjomba joshua tyr kwa maandalizi ya masomo yangu
Nakumbuka nikiwa njiani nilijinyima kula hali ya kuwa gari nliopanda ilikua mbovu na inasimama mara kwa mara kutokana na ubovu wa safari hiyo.Nilifika mkoani Dodoma majira ya saa 2 usiku nikiwa na njaa sana  moja kwa moja nlielekea katika taxi kadhaa ambazo zilikua karibu na stendi ya mkoa wa Dodoma ambapo niliulizia dereva aitwae Joshua moshakwakua nilikua sina hata simu ya mawasiliano
Kwakua mjomba wangu alikua dereva na alikua maarufu kidogo  maeneo hayo haikua tabu kumpata.Baada ya nusu saa hivi mjomba alifika na alionekana akiwa amelewa akijipiga kifua “jombaa langu limekuja mweshmiwa wa baadae toto pekee la dada yangu” alioneshwa kufurai sana kutokana nay eye na mama yangu kupendana sana . “shkamoo mjomba “ nilimsalimia  lakin alinijibu “shkamoo makelele “ Erick twende zetu kwanza ukapumzike umechoka na safari mimi nina ofa za bia nimeacha huko “ sikumjibu  chochote bali nilionyesha sura ya kukubaliana na wazo lake ambapo nilipanda TAXI yake kuu kuu Nakumbuka sana siku ile katika maisha yangu ni siku ambayo sitaisahau katika maisha yangu  ilikua ni may 16 mwaka 2014 laiti ningejua kama ile siku ingekua  vile basi nisinge hangaika kuitafuta elimu ningalibaki mgombani tu na mama yangu kipenzi.
Tukiwa na mjomba Joshua tunatoka maeneo ya standi ya mkoa Dodoma nikiwa mgeni kidogo nakumbuka tulielekea  magharibi kidogo na stendi mbele kidogo na shule ya sekondari  Dodoma na mbele kidogo ya Bunge la nchi yetu kulikua na mtaa unaitwa makole kama skosei ndipo tulismamishawa na watu wawili ambapo walikua na mwonekano kama abiriA  kwakua nilikua nimekaa siti ya mbele pembeni na dereva  mjomba aliamua kusmamisha gari
“tusiache vichwa pesa ya kufunga hesabu hii mwanangu” aliyasema mjomba  huku akisimamisha gari wale watu walifinguA  mlango na kuingia ndani ya gari walidai kuwa wanataka kuelekea eneo la area d maeneo ya karibu na mlima walitaka kujua bei mjomba aliwambia waandae elfu 5000 maana hata sisi tulikua tukielekea maeneo hayo hayo  bila kusita gari ilirudi tena barabarani na kuanza kuelekea palipotakiwa
Lakini tukiwa njiani Yule abiria wa kiume alipiga simu na kuongea maneno ambayo yalintisha kidogo
“mkuu mzigo tunio lakini viumbe ni viwili andaa mazingira “ kasha akakata simu bila kupata majibu kwa aliempigia au mwitikio  lakini sikujali na nikaendelea kuutazama uzuri wa mkoa wa Dodoma  nakumbuka mjomba aliuliza hali ya mama na watu wengne ambao walikua marafiki pale kijijin alionesha uchangamfu mkubwa pia Nadhani ni kutokana na pombe ilio kichwani.
Tukiwa eneo la ukimya na kama pori eneo ambalo liliitwa area d ghafla tuliona watu watatu wamesimama na kujitandaza  barabarani ghafla abiria tuliokua nao kwenye gari wote wawili wakituambia kwa sauti “simamisha gari mpo chini ya ulinzi” mwanamkwe alimnyooshea njomba silaa ndogo ya moto na Yule mwanaume alitoa panga ambalo aliliweka usawa wa shingo yangu  nilishtuka sana
“hapa asimamishi gari mtu na  leo mmekosea namba  nasema labda tufe woote”  aliyasema hayo maneno mjomba huku akiongeza spidi ya gari straight kuelekea pale wale watu watatu walikua wamesimama  kulizinga gari . nikiwa nimeshikwa na butwaa na nikiusoma mchezo unavokua  nakumbuka wale watu baada ya kuona gari inakuja speed na hakuna dalili ya kusmama waliamua kutoka barabani
“neema uwa huyo mshenzi fyatua ya utosi tumalizee” ilikuz ni sauti ya Yule  mwanaume ghafla gari lilipoteza uelekieo na kuingia porini katika zile purukushani za vitisho. Nikiwa nmapigo ya moyo yanaenda mbio na nikijishkilia vizuri kutokana na kuyumba na mwendo kasi wa gari  niliskia kishindo kikubwa sana katika maskio  ambacho kilipelekea mvurugano ndani ya gari  …..sikumbuki nini kilitokea lakini nlikua nipo chini navuja damu maeneo ya shingo na maumiv makali pia. Nilinitahd kuinuka lakn nilishindwa nilijarib kugeuza kichwa pia niliskia maumivu makali sana . nilijaribu kupaza sauti kuomba msaada lakin niliskia maumiv makali shingoni na pia sauti haikutoka.. nilibaki natokwa na machozi huku nikiwa najihisi kama maskio yangu yameziba………
Mpendwa msomaji usikose sehemu ya pili ya mkasa huu wa kweli wa Erick mosha


JANETH Short story

                                                     JANETH                                      

                                           story fupi ya kujifunza

 

Kengele ya kutoka darasani iligongwa, wanafunzi wa shule ya msingi wakaanza kutoka madarasani huku wakifukuzana wengine wakipiga kelele ilimradi shwangwe tu.

Ilikuwa mara yangu ya kwanza kufundisha shule za hatua hiyo.

Ilikuwa ni shule ya serikali.

Jicho langu liliangukia katika sura ya msichana mdogo, nguo zake chafu. Alikuwa analia.

Alikuwa peke yake na hakuwa na yeyote wa kumbembeleza.

Mimi kama mwalimu sikutaka kujisogeza karibu naye sana. Kwanza nilikuwa mgeni.

Nikaachana naye.

Siku iliyofuata tukio kama lile likajirudia. Msichana yuleyule wakati ule uleule wa kutawanyika, alikuwa analia sana. Mwishowe aliondoka huku akiwa analia.

“Mbona mwenzenu analia?” nilimuuliza mwanafunzi mmoja.

“Huyo ni mama kulialia..” alinijibu huku anacheka.

Haikuniingia akilini hata kidogo kuwa yule binti analia bila sababu.

Siku ya tatu nikaanza kujiweka karibu naye.

Muda wa mapumziko nilimwita nikamnunulia chai, alikuwa ananiogopa na hakutaka kuniangalia machoni.

Sikumuuliza lolote juu ya tabia yake ya kulia lia kila anaporuhusiwa kurejea nyumbani.

Hata siku hiyo pia alilia vilevile. Wenzake wakawa wanamzomea.

Akili yangu iligoma kuamini kuwa binti yule analia bila sababu.

Kwanini alie wakati wa kutawanyika tu?? Hapana si bure.

Nikaendelea kujiweka karibu naye. Mkuu wa shule akafikishiwa taarifa kuwa nina mahusiano ya kimapenzi na yule mtoto.

Moyo wangu na Mungu pekee ndio walikuwa mashahidi. Nilikosa cha kujibu.

Nilijaribu kujiweka mbali naye lakini moyo ulinambia kuwa kuna jambo natakiwa kulijua.

Nikaendelea kuwa karibu naye. Hatimaye mkuu wa shule akanisimamisha kufundisha pale kwa tabia yangu ya kufanya mapenzi na mwanafunzi.

Nilijitetea lakini sikueleweka. Nikamwachia Mungu……

Licha ya kusimamishwa kazi, niliendelea kufuatilia nyendo za yule binti aliyeitwa Janeth.

Kila alipotoka shule nilimvizia njiani na kumnunulia chakula, kisha tunazungumza kidogo.

Aliponiamini kama kaka yake ndipo nikajieleza dukuduku langu.

“Janeth…” nilimuita.

“Bee kaka ….” Aliitika huku akinitazama.

“Nyumbani unaishi na wazazi.”

“Ndio naishi na mama..baba huwa anasafiri safari.”

“Mama yako ana watoto wangapi?”

“Mama yangu alikufa….alikufa nikiwa mdogo hata simkumbuki” Alijibu kwa sauti ya chini.

“Kwa hiyo unaishi na mama mdogo.”

“Ndio.”

“Unampenda mama mdogo?”

Swali hili likaikatisha furaha ya Janeth. Akaanza kulia, alilia bila kukoma, Janeth alilia kwa uchungu hadi nikajisikia vibaya. Nilimbembeleza kisha sikumuuliza tena.

Siku zikaenda bila kumuuliza chochote..

Baada ya siku kumi, ilikuwa siku ya michezo pale shuleni, hivyo hapakuwa na masomo.

Janeth alichelewa kuja shule, nilimngoja uwanjani, hadi alipofika majira ya saa nne.

Nikamwambia twende kunywa chai.

Siku hiyo nilimpeleka mbali kidogo, tukanywa chai, kisha tukakaa mahali palipokuwa wazi.

Nikaleta tena mjadala mezani.

Ni kuhusu maisha ya Janeth.

Alikataa kabisa kusema lolote, nilimshawishi sana.

“Usiogope mimi ni kaka yako.” Nilimpooza.

Janeth badala ya kusimulia akaanza kulia tena.

“Ataniua mama nikisemaaaa” alilalamika.

Nikambembeleza hatimaye akanieleza jinsi anavyonyanyaswa na mama yake.

“Mama hanipendi hata kidogo, ananipiga na kuninyima chakula, hapendi nije shule, vyombo tunavyotumia usiku hataki nivioshe usiku na hataki niwahi kuamka asubuhi, nikiamka natakiwa kufanya kazi zote, kufagia uwanja, kudeki nyumba, kuosha vyombo kisha ndipo nije shule. Baba akiwepo anajidai kunijali sana…”

Alijieleza.

“Ni hayo tu Janeth….niambie kila kitu.”

“Akijua ananiua alisema….”

“Kwani amewahi kukutesa vipi..”

Ni hapa Janeth alivyozungumza huku analia kilio ambacho hakitatoka masikioni mwangu kamwe.

Siku moja, alichelewa kuamka, ilikuwa siku ya mapumziko.

Mama yake alipomwamsha, aliitika na kupitiwa usingizi tena.

Mama aliporejea mara ya pili, alikuwa na mti mkavu, alimpiga nao kichwani na popote pale katika mwili, alipoona hiyo haitoshi akamvua nguo, akausokomeza katika sehemu za siri, aliuigiza hovyohovyo, ukuni huo ulikuwa wa moto.

Yeyote mwenye moyo wa nyama ajifikirie ukuni wa moto ukazamishwa sehemu za siri za mtoto wa darasa la sita.

Nilitokwa machozi.

Nikawahi kujifuta hakuona.

“Baba yeye alisemaje….”

“Baba ni mkali na hapendi kunisikiliza na mama aliniambia nikiambia mtu ananiua mara moja.” Alijibu kwa huzuni.

“Nikija na dada yangu tunaweza kukuona ulivyounguzwa..”

“Ndio…” alinijibu.

Sikutaka kulaza damu nikampigia simu rafiki yangu wa kike.

Nikamuuliza kama yupo kwake, alikuwepo.

Nikaongozana na Janeth.

Tukafika, Janeth akatoa nguo zote.

Ilihitaji moyo wa kiuaji sana kutazama mwili wa Janeth mara mbilimbili.

Alitisha, hakika alikuwa ameunguzwa vibaya na vidonda vilikuwa havijapona vizuri.

Dada yule alishindwa kujizuia alimlazimisha Janeth twende kwa mama yake amkabiri na kumpa kipigo. Nikamzuia.

Hata mimi nilikuwa na hasira kali. Lakini sikutaka kuiruhusu ifanye kazi.

Nikachukua kamera, nikampiga picha Janeth katika yale makovu.

Mbio mbio nikaenda polisi, kituo cha haki za watoto nikaelezea mkasa ule huku nikishindwa kujizuia machozi.

Nikawaonyesha na picha.

Tukaongozana nao hadi nyumbani kwao Janeth.

Mama yule akakamatwa bila kutarajia.

Nilitamani kumrukia nimng’ate lakini haikuruhusiwa.

Sheria ikafuata mkondo. Janeth akaanza kupokea tiba.

Yule mama akahukumiwa kwenda jela miaka sita..hadi sasa yupo jela.

Mume wake alitozwa faini kubwa kwa kosa la kutofuatilia maendeleo ya mtoto wake kiafya……..

Mimi nilirudishwa kazini, kwa heshima kubwa. Heshima ya nkumkomboa mtoto.

***Akina JANETH wapo mtaani kwako…..usiwaangalie na kuwaacha tu…hebu jaribu KUWA SAUTI YAO….hawawezi kusema…hebu sema badala yao…….wanalia kisikie kilio chao…….

BROTHER ZENNO AFARIKI DUNIA

RIP Brother Zerno
Hakika siku za karibuni zimekuwa ngumu kwa wapenzi wa muziki wa zamani, mfululizo wa misiba na wanamuziki kuugua kumekuwa ni habari karibu kila siku. Mchambuzi mahiri wa muziki wa Charanga Zerno Andrew Lucas, aliyefahamika zaidi kwa jina Brother Zeno, amefariki dunia asubuhi leo katika hospitali ya Temeke,  Brother Zeno  aliyekuwa akishirikiana na 'Mzee wa Macharanga' Charles Hillary enzi hizo Radio One, alikuwa na ufahamu mkubwa wa muziki wa kutoka Cuba na hivyo kuwa mpenzi mkubwa wa watu waliopenda muziki huo. Brother Zeno amesumbuliwa karibu mwaka mzima na tatizo la moyo na katika siku zake za chache mwisho alikuwa akipumua kwa msaada wa mashine, alitegemewa angepata nafuu na kuhamishiwa Muhimbili kwa matibabu zaidi lakini Mungu amekuwa na mipango mingine.
Msiba wa Mzee utakuwa nyumbani kwake Mbagala Kibonde Maji na mazishi yatakuwa kesho 28/6/2017 saa kumi hukohuko Mbagala

Friday, June 23, 2017

SHAABAN DEDE ANAUMWA AMELAZWA MWAISELA NO 5

Mwanamuziki mkongwe Shaaban Dede 'Kamchape' amelazwa leo katika hospitali ya Muhimbili wadi ya Mwaisela No 5. Wapenzi wa muziki tumkumbuke katika swala zetu.

MJUE BAKARI MAJENGO MWANAMUZIKI ALIYEANZA MUZIKI 1954, NA YUKO JUKWAANI MPAKA LEO

Bakari Majengo akiwa na John Kitime kwenye msiba wa Mzee Manyema karibuni
SHIKAMOO Jazz Band ‘Wana Chelachela’, ni kundi la muiziki wa dansi lililoanzishwa mwaka 1993 kwa kujumuisha baadhi ya nguli wa muziki huyo kutoka katika bendi nyingine kadhaa.
Nguli hao ni Salum Zahor, John Simon, Ally Adinani, Athuman Manicho, Ally Rashid, Kassim Mapili na wengine ni Mohammed Tungwa, Kassim Mponda na Mariam Nylon.
Mbali ya hao, kuna mwanamuziki mwingine nguli katika upulizaji wa 'Domo la Bata' Saxophone, aliyepitia bendi kadha wa kadha za muziki wa dansi, kwa jina Bakari Majengo.
Akiwa mmoja wa waasisi wa Shikamoo Jazz, Majengo amechangia mafanikio makubwa ndani ya bendi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuiongezea mashabiki na kuvuta mapromota nje ya nchi.
Majengo anamtaja mzungu aitwaye Ronnie Graham aliyekuwa anafanyakazi katika shirika la Help Age Tanzania, kuwa ndiye chanzo cha Shikamoo Jazz.
Ronnie akiwa HelpAge alikuwa na kamati iliyokuwa na wajumbe kama John Kitime, Mariam Hamdani, Mheshimiwa Mwabulambo marehemu Godigodi, marehemu Baranieki ambayo ndiyo iliyowezesha kuingiza vyombo vya muziki kutoka Uingereza na baada ya hapo Godigodi na Kitime ndio walienda nyumbani kwa Mzee Salum Zahoro na kumtaka akusanye wakongwe wenzie watengeneze kundi lililokuwa chini ya Helpage na kuwa ni njia moja wapo ya shirika hilo kuwezesha wazee kujitegemea.
Mzee Majengo anasema kuwa, tangu ajiunge na bendi hiyo ambayo awali maskani yake yalikuwa Tanzania Region, ameshasafiri nayo nchi kadhaa, zikiwamo Kenya na Uingereza.
Hatimae Ronnie aliamua kuiacha bendi hiyo kutokana na vituko vilivyofanywa na mmoja wa wazee hao bendi ilipoenda Uingereza, hivyo akaweza kuiondoa bendi kutoka mikono ya Helpage na kuikabidhi bendi kwa wanamuziki  wajiendeleze wenyewe.
Kutokana na waanzilishi wengine kuwa wameshafariki, ni wanamuziki watatu tu wanaoiendesha Shikamoo Jazz Band sasa, ambao ni Salum Zahor, Ally Adinani na yeye mwenyewe.
Akizungumzia historia yake kimuziki,Bakari Majengo anasema kuwa, mwaka 1954 ndipo alipoanza kujiingiza kwenye fani hiyo kwa kujiunga na bendi ya Dar es Salaam Jazz, akiwa mkung’utaji tumba.
Kabla ya hapo, Majengo anasema kuwa, alikuwa akipiga ngoma kwenye vibendi vya watoto na kutumbuiza katika sherehe mbalimbali za kichama, kwenye ofisi za TANU.
Baadhi ya wanamuziki waliompokea Dar es Salaam Jazz, ni pamoja na Edward Salvu na Grey Sindo waliokuwa mahiri kwa upulizaji Sax, ambao kwa nyakati tofauti walichangia kumnoa kwenye chombo hicho.
Ilipofika mwaka 1963, marehemu King Michael Enock aliingia Dar Jazz na kumuongezea ujuzi wa kupuliza Sax kwa kiwango kikubwa.
Mwaka 1968 aliondoka Dar Jazz akiwa keshashiriki kupiga Sax kwenye vibao vingi, kikiwamo kile maarufu, ‘Mtoto Acha Kupiga Mayowe’, akajiunga na bendi ya Wakongo watupu iliyoitwa King Afrika.
Mwaka 1969 alijiunga na bendi nyingine ambayo nayo ilikuwa ya Wakongo, iliyoitwa 60 Zaire, kabla ya mwaka 1970 kuingia Nova Success ya Papaa Micky, saksafoni katika nyimbo kama Chlorida na kadhalika ni kazi ya Majengo.
Aliachana na Nova Success mwaka 1974, bendi ilipopata safari ya Swaziland ambapo yeye alishindwa kwenda kutokana na ajira aliyokuwa nayo katika kiwanda cha BATA Shoes, jijini Dar es Salaam.
Alifanyakazi kazi kwenye kiwanda cha BATA tangu mwaka 1963. Mwaka 1975 aliingia Maquis Original ‘Wana Kamanyola’ iliyokuwa chini ya mpulizaji Sax hodari, Chinyama Chiaza, akashiriki kurekodi vibao vingi zaidi vya bendi hiyo, huku mwenyewe akisifu kazi aliyoifanya katika wimbo ‘Nimepigwa Ngwala’.
Akiwa Maquis, mwaka 1986 alisimama kufanyakazi kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kifua na alipopata nafuu, alikwenda kumsaidia mwanamuziki Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kikii’ aliyekuwa kaanzisha bendi yake ya Orchestra Double O.
Chinyama alipobaini hilo, alimfuata na kumuomba arudi Maquis, ambapo siku aliyorejea kazini alikuta bendi iko chini ya Tshimanga Kalala Assosa ambaye wakati huo walikuwa hawajuani.
“Nilisalimiana naye kikawaida lakini nilipotaka kupanda jukwaani alinizuia akitaka nimsujudie kumuomba kwa vile yeye ndie Kiongozi, baada ya majibizano nilisusa na kusimama bendi,” anasema Majengo.
Majengo anasema kuwa, alipokuwa kasimama kuitumikia Maquis, siku moja alitembelea onesho la pamoja na OSS ‘Wana Power Iranda’ na mmiliki wa OSS, Huggo Kisima alipomuona akamvuta kwake, na Septemba 1986 alianza kazi rasmi na wanamuziki Muhidin Gurumo, Skassy Kasambulla na Abdallah Kimeza ndani ya OSS na kushiriki kurekodi nao vibao vingi .
Mwaka 1990 alirudi tena Maquis na kushiriki nao hadi mwaka 1993 alipoachia ngazi rasmi na kuwa mmoja wa waanzilishi wa Shikamoo Jazz.
Tofauti na wanamuziki wengi wanaotupa lawama kwa vyombo vya habari kuhusiana na kudidimia kwa dansi, Majengo anaweka wazi kuwa, ubinafsi wa wanamuziki wenyewe ndio chanzo.
Majengo anasema kuwa, kila mmoja kwenye muziki wa dansi anajijali yeye mwenyewe na wanamuziki wake tu na kwamba ushirikiano uliopo ni wa mdomoni si wa vitendo.
Faida aliyoyapata Majengo katika kazi ya muziki anayoielezea kuwa ni ngumu kufanikiwa kwa sasa, ni kufanikiwa kujenga nyumba maeneo ya Kigogo Luhanga, jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wa familia, Majengo anayefurahia watoto wake kutorithi kazi yake ya muziki, ana mke na watoto watano, ambao ni Selemani, Kassim, Juma, Zubeda na Tunu.
Alizaliwa mwaka 1943, Kariakoo, jijini Dar es Salaam na kupata elimu ya msingi katika shule ya Mchikichini kwa miaka miwili ya 1949 na 50.
Mwaka 1955 ilipoanzishwa shule ya Magomeni Mzimuni, alilazimika kuanza tena darasa la kwanza hadi la nane mwaka 1962.



JOHN KITIME NA WAKONGWE KATIKA PICHA

Bakari Majengo na John Kitime

Kiniki Kieto, King Kiki na Abdul Salvador

John Kitime na Innocent Nganyagwa

John Kitime na Rashid Pembe

Monday, June 19, 2017

MAZISHI YA MZEE AHMED MANYEMA YAFANYIKA LEO MCHANA

HATIMAE mwili wa Ahmad Manyema umelazwa katika nyumba yake ya milele. Mzee Hamad manyema mwimbaji na mtunzi wa miaka mingi, amezikwa leo katika makaburi ya Mabibo Makutano. Watu wengi wakiwemo wanacham wa CUF tawi la Chechnya, ambako alikuwa mwanachama mzuri wa chama hicho, wanamuziki wengi wakongwe, na majirani wengi  walihudhuria mazishi haya. Ahamed Manyema alifia katika hospitali ya Mwananyamala alfajiri ya Jumapili. Mungu Amlaze Pema Peponi

Saturday, June 17, 2017

MZEE MANYEMA HATUNAE TENA

Mzee Ahmed Manyema hatunae tena, amefariki leo alfajiri katika hospitali ya Mwananyamala. Ni siku chache tu toka kufariki kwa Halila Tongolanga, ambaye walikuwa wote na mzee huyu katika bendi ya Les Mwenge. Mzee Manyema alitunga na kushiriki wimbo wa Chukulubu akiwa  Les Mwenge. Wimbo alioimba akishirikiana na Fredy Siame. Sauti ya Manyema pia ilikuwemo katika nyimbo za Tanga Inter 1978, nyimbo kama Zubeda, Vicky. Halafu alishiriki na Chamwino Bendi alipotunga na kuimba wimbo maarufu wa Waganga wa kienyeji. Mzee Manyema pia alipitia  Jkt Kimbunga na Dar Jazz wakati ikiwa chini ya King Michael Enock,ambapo alitunga wimbo wa Kaka Jirekebishe.Katika miaka ya karibuni alikuwa katika kundi la Sinza Sound, kundi ambalo lilipiga katika hoteli ya Johannesburg Sinza Mori kwa muda mrefu
MUNGU AMLAZE PEMA PEPONI

Monday, June 5, 2017

MWILI WA TONGOLANGA WASAFIRISHWA KUELEKEA TANDAHIMBA, BALOZI WA MSUMBIJI AJITOKEZA KUMUAGA


Halila Tongolanga amefariki jana usiku katika hospitali ya Muhimbili. Alikuwa mwanamuziki wa siku nyingi na alifahamika kwanza  kwa wengi baada ya kuanza kusikika kibao chake cha lugha ya Kimakonde cha Kila munu ave na kwao, chenye tafsiri ya ‘Kila mtu ana kwao’ ambacho alikirekodi akiwa bendi ya jeshi ya CTU Monduli, iliyojulikana kama  Les Mwenge. Kwa kifupi ni kuwa baada ya hapo aliitwa kujiunga na bendi iliyokuwa mali ya Dr Alex Khalid, iliyokuwa ikiitwa Makondeko Six. Wakati huo Dr Khalid alikuwa na sehemu kubwa ya burudani iliyokuwa pia na ukumbi na ilikuwa inaitwa Makondeko ikawa na bendi ya watu sita hivyo bendi hiyo ikaitwa Makondeko Six. Bendi hii awali ilikuwa ikipiga muziki kwa kufuata nyayo za bendi ya Tatu Nane, lakini Dr Khalid baada ya kuona bendi haina umaarufu kutokana na aina ya muziki iliyokuwa ikipiga, ndipo alipomuita Halila Tongolanga nae akaja na baadhi ya wanamuziki wakajiunga na kuanzisha kundi lililoendelea kutumia jina la Makondeko Six japo wanamuziki walikuwa wengi zaidi ya sita. Na ndipo katika kundi hili lilikuwa na wanamuziki wengine kama Innocent Nganyagwa, Anna mwaole wakaweza kurekodi tena wimbo wa Kila Munu Ave na kwao na kundi kupata umaarufu mkubwa mpaka baada ya kusambaratika kwa Makondeko baada ya kifo cha Dr Alex Khalid, lakini Tongolanga aliendelea kutumia jina la Makondeko.
Baadhi ya wanamuziki waliowahi kufanya kazi na Tongolanga katika kundi la makondeko Six, wakiwa wanasubiri kusafirisha mwili wa mpendwa wao.Toka kushoto, mpiga bezi Innocent Nganyagwa, Meneja wa bendi Said Mahadula, mpiga solo Fadhili Ally, mpiga drums Hamza Waninga
                       Tongolanga amefanya kazi nyingi za muziki ikiwemo kuwa mmoja wa kundi lililoundwa na wanamuziki wengine mahiri kama Moshi William, Muhidin Mwalim, Huluka Uvuruge, Kandaya na wengine lililojulikana kama Bana mwambe, ambapo waliweza kutoka nyimbo nyingi nzuri sana wakati biashara ya kuuza album ilipokuwa ina faida. Tongolanga ameagwa na wapenzi wa muziki ndugu na marafiki, lakini kulikuwa na uhaba mkubwa wa wanamuziki wenzie katika kundi lililokuja kumuaga mwanamuziki huyu. Waliojitokeza hasa ni wanamuziki wale tu ambao waliwahi kupiga nae katika kundi la Makondeko na Bana Mwambe na wanamuziki wengine wachache wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Muziki John Kitime, Katibu Mkuu wa Chamudara Hassan Msumari. Serikali iliwakilishwa na Katibu Mtendaji wa BASATA.  Katika jambo moja kubwa lililotokea wakati wa kuaga mwili ni kujitokeza kwa balozi wa Msumbiiji Bi Monica Patricio Clemente aliyefika Muhimbili kuaga mwili wa Tongolanga akiwa amesindikizwa na maafisa wengine, na pia Balozi huo alitoa rambirambi zake kama Balozi na alitoa rambirambi kutoka kwa Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji. Hili lilikumbusha usemi wa wahenga ‘Nabii hathaminiwi kwao.’ Taarifa zilizopatikana pale ni kuwa Tongolanga alikuwa mtu maarufu sana nchini Msumbiji, na aliyekuwa ni msanii muhimu wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu nchini humo.
Balozi wa Msumbiji Bi Monica Patricio Clemente akiaga sanduku lililokuwa na mwili wa Halila Tongolanga

Nilipokutana nae kwa mara ya mwisho akiwa kitandani Tongolanda kwa sauti ya uchovu alinambia alikuwa na mengi ya kunambia, wakati tunasubiri taratib kukamilika za kuanza kusafirisha mwili, Innocent Nganyagwa ambaye alikuwa mmoja ya wanamuziki waliotengeneza kundi la Makondeko Six alinambia Tongolanga alikuwa amepanga kufanya onyesho la ‘Usiku wa Makondeko’ na alikuwa na mipango mingine mikubwa ya kufanya kupitia kipaji chake. Pengine ndiyo hayo aliyotaka kunambia Mungu pekee anajua. 
Shukrani za pekee zimfikie Mbunge wa Tandahimba Mheshimiwa Katani Ahmed Katani, kwani kwa juhudi zake Tongolanga alisafirishwa akiwa hai kutoka Ndanda hadi Dar es Salaam kwa matibabu, na pia ndie aliyeusafirisha mwili wa mwanamuziki huyu kwenda Mchichila kwa ajili ya mazishi.
Toka kushoto Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Nyangamale, Balozi wa Msumbiji nchini, Katibu Mtendaji wa BASATA, Mbunge wa Tandahimba Mhe Katani Katani, afisa wa Ubalozi wa Msumbiji

Tongolanga anategemewa kuzikwa kijijini kwao Mchichila kesho Junanne 6 Juni 2017.

Mungu Amlaze Pema Halila Tongolanga 
Mpiga Kinanda Geophrey Kumburu, Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza, Katibu Mkuu wa CHAMUDATA Hassan Msumari
John Kitime, wanamuziki wa Makondeko Six, Mngereza, KumburuAdd caption

Sanduku alilolazwa Halila Tongolanga likitayarishwa kuingizwa kwenye gari la kusafirisha kuelekea Mcjichila




Sanduku likiingizwa kwenye gari


Sunday, June 4, 2017

MWANAMUZIKI HALILA TONGOLANGA AFARIKI DUNIA

HALILA TONGOLANGA, mwanamuziki wa siku nyingi ambaye alikuwa amelazwa katika hospitali ya Muhimbili amefariki dunia usiku wa kuamkia leo. Halila alikuwa amesafirishwa kutokea Ndanda kuja Muhimbili akihisiwa kuwa na matatizo ya figo. Licha ya kuwa alifika Muhimbili juzi Ijumaa usiku, lakini alikuwa hakufanyiwa vipimo vyovyote vikubwa mpaka umauti unamkuta. Jana Jumapili ililazimika kuanza kufanya jitihada za kupata daktari ambaye angemshughulikia kwa karibu zaidi, na daktari alipatikana ambaye aliahidi angeanza kufwatilia swala lake leo asubuhi lakini mapenzi ya Mungu yalikuwa tofauti. Juzi nilipomuona alinambia kuwa ana mengi anataka kunambia, lakini moja aliloweza kunambia pale ni kuwa yeye anajihisi ana kansa, 'Nilimuuliza anajuaje hilo, kwa vile hajapimwa hakuwa na jibu"
Wengi tutamkumbuka Tongolanga kwa wimbo wake wa Kimakonde aliouimba kwa mara ya kwanza akiwa na Les Mwenge 'Kila Munu Ave Na Kwao"
 Mwili wa marehemu unategemewa kusafirishwa leo saa tano kuelekea kwao Newala. Habari zaidi  zitawafikia kupia hapa
Mungu amlaze Pema peponi Halila Tongolanga


Saturday, June 3, 2017

TONGOLANGA ANASUBIRI VIPIMO

Katibu Mtendaji wa BASATA mwenye kitenge akiwa na Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi, walipomtembelea Tongolanga asubuhi ya leo.
Halila Tongolanga kwa kweli anaumwa. Kwa maelezo ya mdogo wake, ni mwezi wa tatu sasa anaingia na kutoka hospitali mbalimbali. Mpaka jana alikuwa katika hospitali ya Ndanda, na kwa msaada wa Mbunge wa Tandahimba aliweza kupatiwa Ambulance na kufikishwa Muhimbili ambako amelazwa Kibasila No 10. Mpaka jioni ya leo alikuwa anasubiri vipimo.
Tongolanga ndie mtunzi na mwimbaji wa wimbo maarufu wa 'Kilamunu ave na kwao' aliouimba kwanza akiwa Les Mwenge bendi iliyo mali ya JWTZ.

NIDHAMU NA MAENDELEO YA MUZIKI KATIKA BENDI ZETU


Miezi michache iliyopita rafiki yangu mmoja alinambia ameamua kuunda bendi mpya kabisa, alikuwa na lengo la kuleta muziki mpya kabisa katika anga ya muziki Tanzania. Aliongea kwa furaha na ni wazi alikuwa ana nia ya kufanya kitu kikubwa, maana alikuwa amegharamia fedha nyingi kununua vifaa vipya kabisa vya kuanzisha bendi. Mwezi mmoja baada ya mazoezi kuanza alinitafuta na kunambia ameamua kuvunja bendi na vyombo anauza. Nilipomuuliza kwanini kabadili mawazo katika kipindi kifupi vile, hata onyesho moja halijafanyika? Akanijibu. ’Wanamuziki wamenishinda, wana matatizo makubwa ya ndhamu’. Kiukweli sikushangaa sana kwani jambo hili si geni kabisa kwenye tasnia ya muziki kwa siku hizi. Mfumo wa uendeshaji bendi siku hizi ni tofauti sana na miaka ya nyuma.

Nichukue mfano wa bendi Vijana jazz Band, bendi ambayo nilijiunga mwaka 1989. Kujiunga na bendi hii kulitokana na mwaliko niliyoupata kupitia kwa muimbaji rafiki yangu Marehemu Mohamed Shaweji. Shaweji tulikuwa wote Tancut Almasi Orchestra kisha yeye akaniacha kule na na kujiunga na Vijana Jazz Band, yeye na muimbaji mwingine Marehemu Gota gota wakiwa wamemfuata mpiga gitaa Shaaban ‘Wanted’ Yohana, aliyetoka Tancut pia na kuhamia Vijana Jazz Band miezi michache kabla. Hivyo siku moja nikiwa na bendi ya Tancut Almasi kwenye onyesho kwenye ukumbi wa CCM kata ya 14 Temeke, Shaweji alikuja na kunambia kuwa Hemed Maneti, kiongozi wa Vijana Jazz Band alikuwa anataka nijiunge na bendi yake. Nilikubali na mwezi Oktoba 1989 nilijiunga na Vijana Jazz. Kufikia mwezi wa Desemba mwaka huohuo nikawa nimepewa wadhifa wa kuwa Band Master, kazi za Band Master ni kuangalia nidhamu ya jumla ya wanamuziki, ikiwemo mahudhurio mazoezini na kazini, uchelewaji, ulevi, usafi binafsi wa mwanamuziki na pia kupanga ratiba ya nyimbo ambazo zinatakiwa kupigwa katika onyesho.  Kwa mfumo uliokuweko, Band Master aliweza kumsimamisha mwanamuziki yoyote aliyekiuka sheria za bendi, au kutoa adhabu ya kukatwa fedha kutoka kwenye mafao yake ya kila wiki ikiwa ni adhabu kwa makosa mbalimbali. Nguvu hizi zilifanya wanamuziki kuwa na nidhamu wakati wote wawapo kwenye shughuli za bendi. Ikumbukwe kuwa katika bendi kulikuweko na kiongozi mkuu Band Leader. Huyu alikuwa na mamlaka ya kufukuza mtu kazi na pia kuajiri na ndie anaepanga hata ukubwa wa mshahara, lakini alikuwa haingilii madaraka ya Stage Master. Kwa kawaida wanamuziki waliona ni heri matatizo yao yaishie kwa Band Master kwani yakifika kwa Band Leader yanakuwa ndio yamefika hatua ya mwisho isiyo na rufaa na inaweza kuwa hasara kubwa. Ili kuonyesha Band Master alivyokuwa na nafasi ya pekee, siku moja wakati niko Vijana jazz band, ilikuwa twende kwenye moja ya maonesho na kuna gari ilikuwa inatupitia wote majumbani kwetu, tulipofika nyumbani kwa Band Leader Hemed Maneti, alitoka nje akiwa na karatasi kutoka hospitali akaja kunitaarifu kama Band Master, kuwa hataweza kuja kazini kwani anaumwa, Maneti alikuwa Band Leader lakini alikuwa akiheshimu nafasi ya Band Master, tena nilikuwa bado mgeni katika bendi. Hii ilikuwa ni ishara wazi kwa wanamuziki wengine kuwa Band Master lazima aheshimiwe na wote.

Hali si hivi katika bendi nyingi siku hizi. Ngumu kujua nani mwenye madaraka gani kwani bendi zinakuwa na mwenye bendi, mkurugenzi wa bendi, meneja, maseneta, kiongozi wa bendi, wadau wa bendi. Wote hawa wana mamlaka zisizo na mipaka, wanaweza kuamua wimbo gani upigwe, wanaweza kuamua nani atimuliwe au nani aingizwe kwenye bendi, mmoja akimsimamisha mwanamuziki kwa utovu wa nidhamu mwingine anaweza akamrudisha, hakuna mtu mwenye amri ya mwisho kuhusu lolote lile, hivyo nidhamu imeshuka sana, na pasipo na nidhamu si rahisi kuweko na maendeleo yoyote yenye tija.

Sasa nizungumzie kosa la rafiki yangu aliyetaka kuanzisha bendi na ikamshinda, kwanza baada ya kununua vyombo, aliaanza kutafuta wanamuziki akisaidiana na watu wake wa karibu, kisha akamteua kiongozi wa bendi, ambae kimsingi kilikuwa kilemba cha ukoka kwani rafiki yangu ndie aliyekuwa na amri ya mwisho kuhusu lolote katika bendi. Na kwa kuwa hakuwa na muda wa kushinda kila mahala na bendi, kundi likawa halina kiongozi mwenye mamalaka  na mwisho kila mtu akawa anafanya lake, walevi wakalewa sana, wachelewaji wakendelea na uchelewaji wao, hakukuwa na mtu aliyekuwa na uwezo wa kutoa mwelekeo wa bendi kinidhamu wala kimuziki. Muziki wa bendi kwa ujumla umekumbwa na tatizo hili la kukosa uongozi, maamuzi mengi yanafanyika kwa vikao, hata maamuzi yale ambayo ni ya kitaaluma yanangoja makubaliano ya wengi, na kwa mtindo huu bendi zitachelewa sana kujikwamua kwenye tope ambalo zimenasa.  Ushauri kwa wanaotaka kufungua bendi, ni bora kumtafuta mwanamuziki mmoja ambaye unaamini anaweza kutengeneza muziki unaoutaka au unaodhani utakuletea biashara kisha umwachie aijege hiyo bendi na wanamuziki anaoona yeye wanafaa, hapa tayari utakuwa umejenga utawala unaoeleweka. Mwenye vyombo usiingilie moja kwa moja mambo ya bendi, wanamuziki wakishajua kuwa kiongozi wa bendi hana mamlaka kamili, nidhamu inavunjika.

Friday, June 2, 2017

HALILA TONGOLANGA AMELAZWA MUHIMBILI WODI YA KIBASILA


HALILA TONGOLANGA ALIWASILI DAR JANA USIKU NA KUFIKIA REGENCY HOSPITAL AMBAKO WALISHAURI KUWA AHAMISHIWE MUHIMBILI. KWA SASA AMEPEWA KITANDA. AMELAZWA KIBASILA NO 10. KWA MAWASILIANO UNAWEZA KUPATA TAARIFA ZAIDI KWA KUPIGA NAMBA YA MDOGO WAKE UWESU TONGOLANGA NI 0789800656

HABARI NJEMA, HALILA TONGOLANGA AMEPATA USAFIRI WA KUJA DAR ES SALAAM NA YUKO NJIANI, ANATEGEMEA KUFIKIA HOSPITALI TA REGENCY

MWANAMUZIKI HALILA TONGOLANGA AMEWEZA KUPATA BAHATI YA KUPATA USAFIRI UTAKAOMLETA KWENYE MATIBABU DAR ES SALAAM. TONGOLANGA ANATEGEMEWA KUFIKIA HOSPITALI YA REGENCY. ANASINDIKIZWA NA WADOGO ZAKE WAWILI. TUZIDI KUMUOMBEA NDUGU YETU