![]() |
| RIP Brother Zerno |
Tuesday, June 27, 2017
BROTHER ZENNO AFARIKI DUNIA
Friday, June 23, 2017
SHAABAN DEDE ANAUMWA AMELAZWA MWAISELA NO 5
MJUE BAKARI MAJENGO MWANAMUZIKI ALIYEANZA MUZIKI 1954, NA YUKO JUKWAANI MPAKA LEO
| Bakari Majengo akiwa na John Kitime kwenye msiba wa Mzee Manyema karibuni |
Nguli hao ni Salum Zahor, John Simon, Ally Adinani, Athuman Manicho, Ally Rashid, Kassim Mapili na wengine ni Mohammed Tungwa, Kassim Mponda na Mariam Nylon.
Mbali ya hao, kuna mwanamuziki mwingine nguli katika upulizaji wa 'Domo la Bata' Saxophone, aliyepitia bendi kadha wa kadha za muziki wa dansi, kwa jina Bakari Majengo.
Akiwa mmoja wa waasisi wa Shikamoo Jazz, Majengo amechangia mafanikio makubwa ndani ya bendi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuiongezea mashabiki na kuvuta mapromota nje ya nchi.
Majengo anamtaja mzungu aitwaye Ronnie Graham aliyekuwa anafanyakazi katika shirika la Help Age Tanzania, kuwa ndiye chanzo cha Shikamoo Jazz.
Ronnie akiwa HelpAge alikuwa na kamati iliyokuwa na wajumbe kama John Kitime, Mariam Hamdani, Mheshimiwa Mwabulambo marehemu Godigodi, marehemu Baranieki ambayo ndiyo iliyowezesha kuingiza vyombo vya muziki kutoka Uingereza na baada ya hapo Godigodi na Kitime ndio walienda nyumbani kwa Mzee Salum Zahoro na kumtaka akusanye wakongwe wenzie watengeneze kundi lililokuwa chini ya Helpage na kuwa ni njia moja wapo ya shirika hilo kuwezesha wazee kujitegemea.
Mzee Majengo anasema kuwa, tangu ajiunge na bendi hiyo ambayo awali maskani yake yalikuwa Tanzania Region, ameshasafiri nayo nchi kadhaa, zikiwamo Kenya na Uingereza.
Hatimae Ronnie aliamua kuiacha bendi hiyo kutokana na vituko vilivyofanywa na mmoja wa wazee hao bendi ilipoenda Uingereza, hivyo akaweza kuiondoa bendi kutoka mikono ya Helpage na kuikabidhi bendi kwa wanamuziki wajiendeleze wenyewe.
Kutokana na waanzilishi wengine kuwa wameshafariki, ni wanamuziki watatu tu wanaoiendesha Shikamoo Jazz Band sasa, ambao ni Salum Zahor, Ally Adinani na yeye mwenyewe.
Akizungumzia historia yake kimuziki,Bakari Majengo anasema kuwa, mwaka 1954 ndipo alipoanza kujiingiza kwenye fani hiyo kwa kujiunga na bendi ya Dar es Salaam Jazz, akiwa mkung’utaji tumba.
Kabla ya hapo, Majengo anasema kuwa, alikuwa akipiga ngoma kwenye vibendi vya watoto na kutumbuiza katika sherehe mbalimbali za kichama, kwenye ofisi za TANU.
Baadhi ya wanamuziki waliompokea Dar es Salaam Jazz, ni pamoja na Edward Salvu na Grey Sindo waliokuwa mahiri kwa upulizaji Sax, ambao kwa nyakati tofauti walichangia kumnoa kwenye chombo hicho.
Ilipofika mwaka 1963, marehemu King Michael Enock aliingia Dar Jazz na kumuongezea ujuzi wa kupuliza Sax kwa kiwango kikubwa.
Mwaka 1968 aliondoka Dar Jazz akiwa keshashiriki kupiga Sax kwenye vibao vingi, kikiwamo kile maarufu, ‘Mtoto Acha Kupiga Mayowe’, akajiunga na bendi ya Wakongo watupu iliyoitwa King Afrika.
Mwaka 1969 alijiunga na bendi nyingine ambayo nayo ilikuwa ya Wakongo, iliyoitwa 60 Zaire, kabla ya mwaka 1970 kuingia Nova Success ya Papaa Micky, saksafoni katika nyimbo kama Chlorida na kadhalika ni kazi ya Majengo.
Aliachana na Nova Success mwaka 1974, bendi ilipopata safari ya Swaziland ambapo yeye alishindwa kwenda kutokana na ajira aliyokuwa nayo katika kiwanda cha BATA Shoes, jijini Dar es Salaam.
Alifanyakazi kazi kwenye kiwanda cha BATA tangu mwaka 1963. Mwaka 1975 aliingia Maquis Original ‘Wana Kamanyola’ iliyokuwa chini ya mpulizaji Sax hodari, Chinyama Chiaza, akashiriki kurekodi vibao vingi zaidi vya bendi hiyo, huku mwenyewe akisifu kazi aliyoifanya katika wimbo ‘Nimepigwa Ngwala’.
Akiwa Maquis, mwaka 1986 alisimama kufanyakazi kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kifua na alipopata nafuu, alikwenda kumsaidia mwanamuziki Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kikii’ aliyekuwa kaanzisha bendi yake ya Orchestra Double O.
Chinyama alipobaini hilo, alimfuata na kumuomba arudi Maquis, ambapo siku aliyorejea kazini alikuta bendi iko chini ya Tshimanga Kalala Assosa ambaye wakati huo walikuwa hawajuani.
“Nilisalimiana naye kikawaida lakini nilipotaka kupanda jukwaani alinizuia akitaka nimsujudie kumuomba kwa vile yeye ndie Kiongozi, baada ya majibizano nilisusa na kusimama bendi,” anasema Majengo.
Majengo anasema kuwa, alipokuwa kasimama kuitumikia Maquis, siku moja alitembelea onesho la pamoja na OSS ‘Wana Power Iranda’ na mmiliki wa OSS, Huggo Kisima alipomuona akamvuta kwake, na Septemba 1986 alianza kazi rasmi na wanamuziki Muhidin Gurumo, Skassy Kasambulla na Abdallah Kimeza ndani ya OSS na kushiriki kurekodi nao vibao vingi .
Mwaka 1990 alirudi tena Maquis na kushiriki nao hadi mwaka 1993 alipoachia ngazi rasmi na kuwa mmoja wa waanzilishi wa Shikamoo Jazz.
Tofauti na wanamuziki wengi wanaotupa lawama kwa vyombo vya habari kuhusiana na kudidimia kwa dansi, Majengo anaweka wazi kuwa, ubinafsi wa wanamuziki wenyewe ndio chanzo.
Majengo anasema kuwa, kila mmoja kwenye muziki wa dansi anajijali yeye mwenyewe na wanamuziki wake tu na kwamba ushirikiano uliopo ni wa mdomoni si wa vitendo.
Faida aliyoyapata Majengo katika kazi ya muziki anayoielezea kuwa ni ngumu kufanikiwa kwa sasa, ni kufanikiwa kujenga nyumba maeneo ya Kigogo Luhanga, jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wa familia, Majengo anayefurahia watoto wake kutorithi kazi yake ya muziki, ana mke na watoto watano, ambao ni Selemani, Kassim, Juma, Zubeda na Tunu.
Alizaliwa mwaka 1943, Kariakoo, jijini Dar es Salaam na kupata elimu ya msingi katika shule ya Mchikichini kwa miaka miwili ya 1949 na 50.
Mwaka 1955 ilipoanzishwa shule ya Magomeni Mzimuni, alilazimika kuanza tena darasa la kwanza hadi la nane mwaka 1962.
JOHN KITIME NA WAKONGWE KATIKA PICHA
Monday, June 19, 2017
MAZISHI YA MZEE AHMED MANYEMA YAFANYIKA LEO MCHANA
Saturday, June 17, 2017
MZEE MANYEMA HATUNAE TENA
Mzee Ahmed Manyema hatunae tena, amefariki leo alfajiri katika hospitali ya Mwananyamala. Ni siku chache tu toka kufariki kwa Halila Tongolanga, ambaye walikuwa wote na mzee huyu katika bendi ya Les Mwenge. Mzee Manyema alitunga na kushiriki wimbo wa Chukulubu akiwa Les Mwenge. Wimbo alioimba akishirikiana na Fredy Siame. Sauti ya Manyema pia ilikuwemo katika nyimbo za Tanga Inter 1978, nyimbo kama Zubeda, Vicky. Halafu alishiriki na Chamwino Bendi alipotunga na kuimba wimbo maarufu wa Waganga wa kienyeji. Mzee Manyema pia alipitia Jkt Kimbunga na Dar Jazz wakati ikiwa chini ya King Michael Enock,ambapo alitunga wimbo wa Kaka Jirekebishe.Katika miaka ya karibuni alikuwa katika kundi la Sinza Sound, kundi ambalo lilipiga katika hoteli ya Johannesburg Sinza Mori kwa muda mrefu
MUNGU AMLAZE PEMA PEPONI
Monday, June 5, 2017
MWILI WA TONGOLANGA WASAFIRISHWA KUELEKEA TANDAHIMBA, BALOZI WA MSUMBIJI AJITOKEZA KUMUAGA
| Balozi wa Msumbiji Bi Monica Patricio Clemente akiaga sanduku lililokuwa na mwili wa Halila Tongolanga |
Shukrani za pekee zimfikie Mbunge wa Tandahimba Mheshimiwa Katani Ahmed Katani, kwani kwa juhudi zake Tongolanga alisafirishwa akiwa hai kutoka Ndanda hadi Dar es Salaam kwa matibabu, na pia ndie aliyeusafirisha mwili wa mwanamuziki huyu kwenda Mchichila kwa ajili ya mazishi.
![]() |
| Toka kushoto Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Nyangamale, Balozi wa Msumbiji nchini, Katibu Mtendaji wa BASATA, Mbunge wa Tandahimba Mhe Katani Katani, afisa wa Ubalozi wa Msumbiji |
| Mpiga Kinanda Geophrey Kumburu, Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza, Katibu Mkuu wa CHAMUDATA Hassan Msumari |
| John Kitime, wanamuziki wa Makondeko Six, Mngereza, KumburuAdd caption |
| Sanduku alilolazwa Halila Tongolanga likitayarishwa kuingizwa kwenye gari la kusafirisha kuelekea Mcjichila |
| Sanduku likiingizwa kwenye gari |

