Friday, June 2, 2017

HABARI NJEMA, HALILA TONGOLANGA AMEPATA USAFIRI WA KUJA DAR ES SALAAM NA YUKO NJIANI, ANATEGEMEA KUFIKIA HOSPITALI TA REGENCY

MWANAMUZIKI HALILA TONGOLANGA AMEWEZA KUPATA BAHATI YA KUPATA USAFIRI UTAKAOMLETA KWENYE MATIBABU DAR ES SALAAM. TONGOLANGA ANATEGEMEWA KUFIKIA HOSPITALI YA REGENCY. ANASINDIKIZWA NA WADOGO ZAKE WAWILI. TUZIDI KUMUOMBEA NDUGU YETU

Thursday, June 1, 2017

HALILA TONGOLANGA ANAUMWA ANAHITAJI MSAADA WA HARAKA SANA


MWANAMUZIKI HALILA TONGOLANGA MTUNZI WA WIMBO MAARUFU WA KILA MUNU AVE NA KWAO, AMEUGUA GHAFLA AKIWA KATIKA ZIARA YA MUZIKI MIKOA YA KUSINI. ANATAKIWA KURUDISHWA DAR ES SALAAM MAPEMA APATE MATIBABU YA HARAKA MUHIMBILI. KWA SASA AMELAZWA KATIKA HOSPITALI YA NDANDA. ANAE ONA AMEGUSWA NA ANAWEZA KUTOA USAFIRI AU MSAADA WOWOTE  APIGE SIMU 0713644439 ILI KUWASILIANA NA KATIBU MTENDAJI WA BARAZA LA SANAA LA TAIFA.

NI MIAKA 27 TOKA KIFO CHA HEMEDI MANETI

Picha niliyoipiga tukiwa chumba cha maiti Muhimbili, mbele yetu ulikuwa mwili wa Hemedi Maneti. Kati ya waliopo kwenye picha ni marehemu Mzee jacob John, mwenye shati jeusi na marehemu Salum Faya mwenye jaketi jekundu
Mara ya kwanza kukutana uso kwa uso na Hemedi Maneti ilikuwa ni wakati Vijana Jazz band ilipita Iringa  ikielekea Songea mwaka 1989. Wakti huo nilikuwa mwanamuziki wa Tancut Almasi Orchestra, na kama ilivyokuwa ada miaka ile, bendi ikipita katika mji ambao kuna bendi wanamuziki walikuwa wakipiga muziki pamoja. Tuliongea nae machache lakini aliongea kuhusu kufurahishwa na setting ya vyombo vyetu, alisema inafanya vyombo vyote visikike. Wakati huo hatukujua lakini kumbe alikuwa kishaongea na Shaaban Wanted, Mohamed Gotagota na Mohamed Shaweji ili wajiunge na Vijana Jazz band, na hakika walihamia bendi hiyo wiki chache zilizofuata.
Katika mlolongo huohuo nilijikuta nikiitwa kujiunga na Vijana Jazz Band mwezi wa September mwaka huohuo na kufikia Oktober 1989 niliwasili Dar es Salaam kujiunga na Vijana Jazz Band. Siku ya kwanza nilipofika Vijana maneti alinipa shilingi 300 za kuanza maisha. Nitafute guest house ya kuishi na chakula kwa wiki moja. Hiyo ndiyo kumbukumbu yangu ya kwanza ya Maneti ambaye miezi michache baadae, tarehe 31 May 1990 siku ya Alhamisi majira ya saa kumi na moja jioni, Hemed Maneti alifariki katika hospitali ya Mwananyamala.  Alikuwa ameanza kuwa na matatizo ya afya miezi kadhaa kabla ya hapo na  hatimae kupelekwa Tanga kwa ajili ya matibabu. Hali yake ilipozidi kuwa mbaya alirudishwa kwa ndege  kuwasili Dar Jumatano 30 May na kupelekwa moja kwa moja hospitali ya Mwananyamala ambapo alilala na kufariki kesho yake. Marehemu alisafirishwa kwenda kuzikwa Tanga siku moja baadae.
Wimbo wa mwisho kurekodi ulikuwa wimbo Nelson Mandela uliotungwa nami, ukiwa wimbo uliokuwa matayarisho ya ziara ya Nelson Mandela.

Friday, May 26, 2017

URAFIKI WA MUZIKI NA SIASA ULIANZA ENZI ZA UKOLONI



 
Miaka michache baada ya Tanganyika kupata Uhuru, nchi yetu ikabadili mfumo wa siasa na kuwa na siasa ya chama kimoja. Hivyo chama cha TANU kikawa ndicho chama pekee cha siasa nchini. Katika mtiririko huo wa siasa ya chama kimoja,  vyama vingine mbalimbali vilivyokuwa si vya kisiasa, vikaunganishwa ili kuwa kwa namna moja au nyingine chini ya TANU, hivyo kukaweko na muungano kama National Union of Tanganyika Workers (NUTA) kwa ajili ya vyama vya wafanyakazi, Cooperative Union of Tanganyika (CUT), muungano wa vyama vya  ushirika, TANU Youth League (TYL) chama cha vijana,  na kadhalika. Pia jeshi likaundwa upya na kukaundwa Tanzania Peoples Defence Force (TPDF) baada ya vurugu ya jeshi la awali la lililorithiwa kutoka kwa wakoloni lililoitwaTanganyika Rifles, na baadae jeshi jingine la kujitolea lililoitwa National Service likaanzishwa. Hakika mabadiliko yalikuwa mengi sana katika miaka saba ya kwanza baada ya Uhuru wa Tanganyika, likiwemo pia tukio kubwa la muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.  Mabadiliko haya mengi na ya muda mfupi yaligusa kila sekta ikiwemo sekta ya muziki. Katika miaka hii, kulikuwa na aina mbalimbali za muziki uliokuwa ukipendwa , ukiwemo muziki wa dansi, taarab, kwaya na ngoma za asili. Muziki wa dansi  ulikuwa umejikita hasa mijini, bendi zikiwa mali za watu binafsi au taasisi binafsi. Lakini baada ya mabadiliko hayo niliyo yataja hapo juu, vyombo vya umma vikaanza kuzindua vikundi vyao vya muziki. Kati ya bendi za kwanza kuanzishwa kupitia mfumo hu, zilikuwa ni NUTA Jazz Band ikijitambulisha kwa mtindo wa msondo, Polisi Jazz Band na mtindo wa Vangavanga, National Service Jazz Band na mtindo wa Kimbunga, baadaye bendi hii ikaja kuitwa Kimbunga Stereo, baada ya bendi nyingine ya National Service kuanzishwa katika kambi ya jeshi hilo huko Mafinga Iringa, ambayo iliitwa National Service Kimulimuli. Jeshi la wananchi nalo likaanzisha bendi Mwenge Jazz Band wana Paselepa, na hivyo hivyo Jeshi la Magereza wakawa na Magereza Jazz Band waliokuja kuwa namtindo wa Super Mnyanyuo na hata idara ya Uhamiaji nayo ilianzisha bendi maarufu ya Uhamiaji Jazz Band iliyokuwa na mtindo wao wa Hamahama. Vijana wa chama cha Tanu, walianzisha TANU Youth League Jazz Band, iliyokuja kupata jina la Vijana  Jazz Band baadae. TYL ilianzisha pia bendi nyingi katika wilaya mbalimbali nchini, kama vile Mbeya lringa, Mwanza, Moshi, Lindi, Songea, Bagamoyo, Tunduru, Biharamulo, Nachingwea, Njombe, Same na kadhalika. Muungano wa vyama vya Ushirika nayo pia ikaja kuwa na bendi iliyokuja kuwa maarufu sana, Washirika Tanzania Stars. Mashirika ya umma nayo yakaanzisha bendi, Urafiki Jazz Band, ilikuwa mali ya kiwanda cha nguo cha Friendship Textile Mills, shirika la State Trading Corporation likaja na STC Jazz Band ambayo baadae ilikuja kuitwa Biashara Jazz band. Kampuni ya mabasi ya Usafiri Dar es Salaam ikazindua bendi yao ya UDA Jazz Band,
National Insurance Corporation, shirika la bima nalo likaanzisha Bima Jazz Band ambayo wanamuziki wake awali wengi walikuwa wanamuziki wa BAT Jazz Band mali ya  kampuni ya sigara ya British American Tobacco (BAT), kampuni iliyokufa na kuzaliwa kampuni ya Tanzania Cigarette Company (TCC). Mwaka 1978. Tanzania Taxi and Transport Service (TTTS) wakaanzisha bendi yao waliyoiita Mlimani Park Orchestra, jina la Mlimani lilitokana na bendi kuanzia Mlalakuwa jirani na chuo kikuu cha Dar es Salaam maarufu kwa jina la Mlimani, bendi hii ilikuja kubadili jina baada ya kuchukuliwa na Dar es Salaam Development Corporation (DDC) na kuitwa DDC Mlimani Park Orchestra mwaka 1982. Mashirika ya umma na idara za serikali zilianzisha bendi hizi hasa kwa ajili ya kuburudisha  wafanyakazi wake, lakini pia na kutambua uwezo wa muziki katika kusambaza ujumbe ambao mashirika haya yalitaka uwafikie wananchi, na mwisho bendi hizi zilikuwa ni vitega uchumi. Bendi za mashirika kama Urafiki Jazz Band, Biashara Jazz Band, na Bima Lee, kwa mfano zilifanya kazi za kutangaza biashara za kampuni zao na bendi zilizunguka kila wilaya nchini, na hata kwenye vitongoji vidogo kabisa. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), lilikuwa na bendi tatu ikiwemo Kimbunga Stereo ikiwa kambi ya Mgulani, Kimulimuli katika kambi ya Mafinga, na kambi ya Makutopora nayo pia ikawa na bendi yake. Kulikuwa na bendi za Polisi maarufu kama Usalama jazz Band  huko Bukoba na Moshi, wakati Polisi Jazz band ilikuwa Dar es Salaam. Kuna hata Kurugenzi za mikoa zilizoanzisha bendi zilizokuja kuwa maarufu, bendi za Kurugenzi Arusha na Kurugenzi Dodoma ni kati ya bendi hizo. Kwa kuwa chama cha siasa kilikuwa kimoja tu, bendi zote hizi, pamoja na bendi zilizokuwa za watu au vikundi binafsi zilishiriki kikamilifu katika kutangaza mambo yote ya siasa wakati ule. Kimsingi hakukuwa na mabadiliko sana kwa jambo hili, kwani mahusiano kati ya wanamuziki na siasa yalianza toka wakati wa kupigania Uhuru, wazee kama marehemu Mzee Nnauye walitumia sana muziki kuhamasisha wananchi kuunga mkono juhudi za kumuondoa mkoloni. Uhusiano huu uliongezeka sana mara baada ya Uhuru kwa bendi kutunga nyimbo nyingi za uzalendo na kuhamasisha ujenzi wa Taifa jipya. Mpaka kufikia mwishoni mwa miaka ya 1980, kila wakati wa kurekodi nyimbo mpya bendi zilikuwa japo na wimbo mmoja wa siasa katika kila nyimbo sita. Radio ya Taifa ilizipiga sana nyimbo hizi na zikafahamika nchini kote.RTD wakati huo ilikuwa ni ngazi moja kubwa ya kutangaza nyimbo za bendi za hapa nchini. Takwimu moja iliyofanywa July 1968, ilionyesha kuwa asilimia  84% ya nyimbo zilizoombwa na wasikilizaji katika vipindi vitatu vya Idhaa ya Kiswahili ya RTD, zilikuwa ni nyimbo za Kiswahili, kutoka Tanzania, na nyingi zikiwa nyimbo za siasa. Bendi hazikuongelea tu siasa za ndani ya nchi bali ziliongea pia kuhusu siasa zilizokuwa zikiendelea ulimwenguni na hasa kuhusiana kupigania uhuru wa nchi zilizokuwa bado zinatawaliwa Afrika. Vijana Jazz Band ndio ilikuwa bendi kubwa ya kuelezea mipango, sera na maanuzi ya chama tawala, bendi ilikuwa mstari wa mbele kwenye kampeni za uchaguzi na kutunga nyimbo nyingi za kupigia debe mgombea wa chama tawala. Bila kusahau bendi zilifanya kazi kubwa ya kuwahamasisha askari na wananchi wakati wa vita ya Kagera, baada ya vita vikundi vya muziki vya JKT, JWTZ na Magereza, vilizunguka sehemu mbalimbali nchini Uganda kupiga muziki kuwahamasisha watu kurudi kutoka mafichoni.
Mwisho lazima nitoe mfano wa bendi binafsi zilivyokuwa zinashiriki katika siasa. Bendi kama Kilwa Jazz band ilikuwa moja ya bendi iliyotumika sana na wanasiasa wa TANU kuhamasisha watu juhudhuria mikutano ya kisiasa, na hata katika mikutano ya kuchangia chama. Kilwa Jazz ndio ilikuwa bendi rasmi iliyopiga muziki siku ya sherehe za mwaka wa pili wa Uhuru 1962, na ndio bendi iliyopelekwa na serikali kwenye sherehe za Uhuru wa Malawi mwaka July 6, 1964.

Monday, May 1, 2017

MSONDO KUTENGENEZA HISTORIA?

HABARI ambazo hazijathibitishwa zimesema kuwa bendi ya Msongo Ngoma Music imechukuliwa tena na Chama cha Wafanyakazi, na itaitwa TUCTA Jazz Band 'Msondo Ngoma'.  Hii itakuwa historia ya mambo mengi, kwanza kurudi kwa uhusiano kati ya bendi hii na vyama vya wafanyakazi. Bendi hii ilianzishwa na chama cha wafanya kazi cha NUTA mwaka 1964 na kuitwa NUTA Jazz Band, na kubadilika kuwa JUWATA Jazz Band baada ya mabadiliko yaliyozaa Jumuiya ya Wafanya kazi Tanzania (JUWATA). Baada ya mabadiliko mengine yaliyoleta chombo kilichoitwa Organization of Tanzania Trade Unions (OTTU), bendi ikabadili jina na kuitwa Ottu Jazz band, kwa muda mfupi kulikuweko mabadiliko mengine yaliyoleta Tanzania Federation of Free Trade Unions (TFTU), na bendi ikachukuliwa na TFTU. Hatimae bendi ikajikuta iko huru ikiendeshwa na wanamuziki wenyewe na ndipo ilipojipa jima la Msondo Ngoma Music Band, na kama inavyosikika inaweza sasa tena ikaitwa TUCTA Jazz Band.hakika itakuwa moja ya bendi ambazo zimewahi kubadili jina mara nyingi kuliko bendi nyingine duniani.

Friday, April 28, 2017

SI KWELI KUWA HARRISON SATCHMO SIWALE ALIFIA GEREZANI,


Mar. Harrison Siwale-Satchmo

...................... SIKILIZA HAPA GUITAR LA MZEE SIWALE...................
 
Tarehe 8 September 2013, niliandika katika blog hii habari niliyoipa kichwa cha habari, Harrison Siwale aliishia wapi? Ni habari ya kusikitisha.

Niliandika hivi-----Nimetoka kuongea na Mzee mmoja ambaye nilimuomba anitafutie habari za Harrison Siwale  aka ‘Satchmo’, ambaye alikuwa mpiga rhythm mahiri na maarufu sana katika miaka ya sabini, Harrison alikuwa na staili ya pekee ya upigaji wa gitaa wa kudokoa nyuzi na kupata aina ya pekee ya mlio wa gitaa. Kati ya nyimbo ambazo upigaji huu unasikika ni katika nyimbo za Jamhuri Jazz Band kama vile Mganga 1  na 2, Blandina na kadhalika. Pamoja na bendi nyingine Harisson aliwahi kupigia Atomic na Jamhuri Jazz Band zote za Tanga, na kisha kuvuka mpaka na kuwa na makazi Mombasa kwa muda mrefu ambako aliendelea na muziki. Kwa kadri ya maelezo niliyopewa leo na huyu Mzee niliyemuomba anitafutie habari ili nijue yu wapi huyu mwanamuziki siku hizi? Haya ndio aliyonambia.



'Baada ya kufa kwa yale makundi ya Simba wa Nyika na Les Wanyika, Harrison Siwale alianza kupiga muziki wa Injili katika eneo la Kilifi. Akawemo katika kundi lililokuwa likifanya maonyesho yake katika miji mingi ikiwemo Mombasa na Nairobi. Umahiri wake wa kazi ukamfanya mwenye vyombo vya hilo kundi alilokuwemo Harrison kumuamini sana na kumuachia awe kiongozi wa kundi hilo na kuwa huru kuzunguka sehemu mbalimbali. Inasemekana Harrison akapata tamaa ya kuingia mitini na vyombo vile, hivyo ghafla akapotea. Taarifa zikamfikia mwenye vyombo kuwa vyombo vyake viko njiani kuvushwa kungia Tanzania kupitia mji wa Lungalunga. Mwenye vyombo akaweka mtego hapo na Harrison akakamatwa hapo akiwa na vyombo hivyo, kesi ilifika mahakamani na akahukumiwa kifungo cha miaka mitatu'. Baada ya hapa kuna hadithi mbili, moja ikisema alifia gerezani Shimo la Tewa, na nyingine ikisema alifariki baada ya kumaliza kifungo chake.

Je, nini hasa kilitokea? Najaribu kuwasiliana na watu mbalimbali kupata hadithi zaidi kuhusu mwanamuziki huyu.

HATIMAE (2017 APRIL).... Kwa bahati sana nimeweza kuanza kuwasiliana na mtoto wa Harrison Satchmo Siwale, ambae tuliweza kukutana kupitia facebook. Kijana huyu ambaye jina lake ni Salehe Siwale aliweza kunambia kuwa baba yake alimuoa mama yao na walizaliwa vijana wawili yeye na kaka yake.

Na niliweza kupata taarifa za ziada baada ya kuniunganisha na mama yake ambaye ndie alikuwa mke wa Mzee Siwale nikaweza kuongea nae mubashara kupitia video call ya whatsapp. Kwanza kabisa mama huyo ansema kuwa katika kipindi alichoishi na Mzee Siwale hakuwahi kufungwa wala kuzungumzia kuwa aliwahi kufungwa. Na Mzee Siwale alifariki katika Kitongoji cha Rongai  huko Nakuru na kuzikwa tarehe 31/3/2013. Ukiangalia kuwa taarifa ya awali niliyopewa ilikuwa katika miezi michache baada ya kifo chake, niwazi si kweli kuwa alifia Gerezani na kama angekuwa aliwahi kufungwa hakika mkewe angekuwa anajua.

Mungu Amlaze Pema Mchungaji Harrison ‘Satchmo’ Siwale








Saturday, April 22, 2017

KIFO CHA SOKOINE KILIIKUTA ORCHESTRA MAMBO BADO IKO SHINYANGA


Mwaka 1984 nilikuwa mwanamuziki wa bendi ya Orchestra Mambo Bado, bendi iliyokuwa inaongozwa na Tchimanga Kalala Assossa. Bendi ilikuwa ni moja ya bendi zilizokuwa pendwa wakati huo, mtindo wa bendi ulikuwa unajulikana kama Bomoa. Neno hili lilitokana na wimbo wa Bomoa Tutajenga Kesho, wimbo ambao  baadae kwa sababu ambazo mpaka leo sizijui, ulikuja kupigwa marufuku na Umoja wa Vijana wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati ule, usisike kwenye radio ya Taifa, redio ambao ilikuwa pekee wakati huo. Orchestra Mambo Bado ilikuwa na watu ishirini hivi, Tchimanga Assossa kiongozi na mwimbaji. George Mzee muimbaji, Lucas Faustin muimbaji, Jenipher Ndesile muimbaji, Banza Tax muimbaji, Athumani Cholilo muimbaji, John Kitime muimbaji, Likisi Matola mpiga gitaa la bezi, Andre Milongo akipiga gitaa la second solo, Huluka Uvuruge na Kazembe wa Kazembe wapiga gitaa la solo, William Maselenge akiwa kwenye gitaa la rhythm. Kulikuweko na wacheza show wanne, mafundi mitambo watatu na mweka hazina mmoja na meneja wa bendi. Masikani ya bendi yalikuwa katika ukumbi wa Lango la Chuma, Mabibo Dar es Salaam
Tarehe 12 April 1984, kundi zima lilitua katika mji wa Shinyanga baada ya kuwasili hapo kwa treni kutokea Dar es Salaam. Kwa taratibu za miaka hiyo, pamoja na ratiba ya ziara ya bendi kutangazwa kwenye gazeti la Uhuru, meneja wa bendi alikuwa akilazimika kutangulia mji ambao dansi litapigwa kuwahi kufanya mikataba na kumbi  ambazo dansi lingepigwa na pia kufuatilia vibali mbalimbali vya kuruhusu onyesho kufanyika. Mawasiliano yalikuwa magumu na urasimu ulikuwa mkubwa. Haikuwa kazi rahisi maana miaka hiyo ili bendi isafiri ililazimika kupata  kibali cha Afisa Utamaduni wa Mkoa ambao ni masikani ya bendi kuruhusu bendi kutoka nje ya Mkoa na kisha kibali hicho kupelekwa kwa Ofisa Utamaduni wa Mkoa ambao bendi inakwenda, nae baada ya kuruhusu bendi kuingia mkoani kwake, unaomba kibali cha Afisa Utamaduni wa Wilaya unakotaka kupiga muziki ili nae akuruhusu kufanya onyesho kwenye wilaya yake. Baada ya hapo meneja hutafuta na mtu ambaye ana spika ya mkononi, megaphone kuikodisha na kisha kutafuta mtu wa kutangaza onyesho. Ili kubana matumizi kuna mara nyingine wanamuziki wenyewe ililazimika wapite mtaani na spika hiyo kujitangaza. Kulikuwa na mji kama Mpanda wakati huo, ambapo mtangazaji hakuwa na megaphone, mtu maalumu alipita mtaa kwa mtaa akiwa na ngoma ambao aliipiga watu wakikusanyika basi anatangaza ujio wa bendi katika mji wao.
Tarehe 12 April 1984, Orchestra Mambo Bado iliwasili Shinyanga kwa treni ikitokea Dar es Salaam, kuanza ziara ya Kanda ya Ziwa. Wanamuziki tulionyeshwa vyumba vya kulala, mambo yalionekana kuwa yatakuwa mazuri kwa siku ile, matangazo yalikuwa yamebandikwa kwenye nguzo za umeme sehemu mbalimbali za mji, na hali ya kuonyesha kuwa watu walikuwa na taarifa ya ujio wetu ilikuwa dhahiri. Ilikuwa ni muda wa saa kumi hivi ilipotangazwa kuwa nchi imepata msiba mkubwa sana. Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine amefariki katika ajali ya gari jirani na Morogoro. Kwanza ilikuwa ni mshtuko, halafu akili ilipotulia tulijua kuwa na sisi kama bendi tunaingia kwenye tatizo kubwa sana, tulikuwa na nauli ya kuja tu mpaka Shinyanga, na fedha ya kula ya siku moja tulikuwa tunategemea kupiga dansi ili kuweza kulipa malazi ya siku hiyo na kupata fedha ya kula na kuendelea na safari kesho yake, tukitegemea mapato mengine makubwa katika maonyesho ya Mwanza wikiendi iliyokuwa inafuata. Hayo yote tulijua sasa yameharibika, tulirudisha vyumba vyote mara moja na kubaki na viwili tu kimoja kikiwa cha wasichana waliokuwa kwenye bendi, wengine wote ikalazimu tuhamishie mizigo yetu chumba kingine. Baadae tulikaa na Afisa Utamaduni kutafakari kama dansi lingeweza kulia siku ile, na kama halitalia nini hatima ya watu hawa 20 wageni kutoka Dar es Salaam? Kama kiasi cha saa moja jioni, Afisa Utamaduni akaruhusu tupige dansi ili tuweze kupata nauli ya kurudi Dar es Salaam, kwani ilijulikana wazi kitaanza kipindi cha maombolezo ambacho hakuna mtu alijua kitaisha lini,  hivyo hakukuwa na sababu ya kuendelea na safari kutoka hapo. Vipindi vya maombolezo huwa ni vipindi ambavyo pamoja na mambo mengine shughuli za muziki husimamishwa. Kwa wanamuziki na wale wanaotegemea shughuli za muziki na familia zao, kipindi hiki huwa kigumu sana. Lakini kinaleta ukakasi akilini kwani shughuli za kupiga muziki kwenye kumbi husimamishwa, madisco hufungwa na vikundi vya muziki haviruhusiwi kufanya  kazi lakini radio huendelea kupiga muziki uleule ambao umezuiwa kwenye kumbi, sehemu za starehe kama baa huendelea kupiga muziki na kufanya biashara zao bila tatizo ila wanamuziki ndio huzuiwa kufanya shughuli zao kwa maelezo kuwa ni kipindi cha maombolezo. Nakumbuka sana misiba  mikubwa ya viongozi wetu ukiwemo wa Baba wa Taifa kwa sababu kubwa mbili, kwanza uchungu wa kupoteza kiongozi wetu na njaa iliyofuatia baada ya hapo.