Friday, May 26, 2017

URAFIKI WA MUZIKI NA SIASA ULIANZA ENZI ZA UKOLONI



 
Miaka michache baada ya Tanganyika kupata Uhuru, nchi yetu ikabadili mfumo wa siasa na kuwa na siasa ya chama kimoja. Hivyo chama cha TANU kikawa ndicho chama pekee cha siasa nchini. Katika mtiririko huo wa siasa ya chama kimoja,  vyama vingine mbalimbali vilivyokuwa si vya kisiasa, vikaunganishwa ili kuwa kwa namna moja au nyingine chini ya TANU, hivyo kukaweko na muungano kama National Union of Tanganyika Workers (NUTA) kwa ajili ya vyama vya wafanyakazi, Cooperative Union of Tanganyika (CUT), muungano wa vyama vya  ushirika, TANU Youth League (TYL) chama cha vijana,  na kadhalika. Pia jeshi likaundwa upya na kukaundwa Tanzania Peoples Defence Force (TPDF) baada ya vurugu ya jeshi la awali la lililorithiwa kutoka kwa wakoloni lililoitwaTanganyika Rifles, na baadae jeshi jingine la kujitolea lililoitwa National Service likaanzishwa. Hakika mabadiliko yalikuwa mengi sana katika miaka saba ya kwanza baada ya Uhuru wa Tanganyika, likiwemo pia tukio kubwa la muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.  Mabadiliko haya mengi na ya muda mfupi yaligusa kila sekta ikiwemo sekta ya muziki. Katika miaka hii, kulikuwa na aina mbalimbali za muziki uliokuwa ukipendwa , ukiwemo muziki wa dansi, taarab, kwaya na ngoma za asili. Muziki wa dansi  ulikuwa umejikita hasa mijini, bendi zikiwa mali za watu binafsi au taasisi binafsi. Lakini baada ya mabadiliko hayo niliyo yataja hapo juu, vyombo vya umma vikaanza kuzindua vikundi vyao vya muziki. Kati ya bendi za kwanza kuanzishwa kupitia mfumo hu, zilikuwa ni NUTA Jazz Band ikijitambulisha kwa mtindo wa msondo, Polisi Jazz Band na mtindo wa Vangavanga, National Service Jazz Band na mtindo wa Kimbunga, baadaye bendi hii ikaja kuitwa Kimbunga Stereo, baada ya bendi nyingine ya National Service kuanzishwa katika kambi ya jeshi hilo huko Mafinga Iringa, ambayo iliitwa National Service Kimulimuli. Jeshi la wananchi nalo likaanzisha bendi Mwenge Jazz Band wana Paselepa, na hivyo hivyo Jeshi la Magereza wakawa na Magereza Jazz Band waliokuja kuwa namtindo wa Super Mnyanyuo na hata idara ya Uhamiaji nayo ilianzisha bendi maarufu ya Uhamiaji Jazz Band iliyokuwa na mtindo wao wa Hamahama. Vijana wa chama cha Tanu, walianzisha TANU Youth League Jazz Band, iliyokuja kupata jina la Vijana  Jazz Band baadae. TYL ilianzisha pia bendi nyingi katika wilaya mbalimbali nchini, kama vile Mbeya lringa, Mwanza, Moshi, Lindi, Songea, Bagamoyo, Tunduru, Biharamulo, Nachingwea, Njombe, Same na kadhalika. Muungano wa vyama vya Ushirika nayo pia ikaja kuwa na bendi iliyokuja kuwa maarufu sana, Washirika Tanzania Stars. Mashirika ya umma nayo yakaanzisha bendi, Urafiki Jazz Band, ilikuwa mali ya kiwanda cha nguo cha Friendship Textile Mills, shirika la State Trading Corporation likaja na STC Jazz Band ambayo baadae ilikuja kuitwa Biashara Jazz band. Kampuni ya mabasi ya Usafiri Dar es Salaam ikazindua bendi yao ya UDA Jazz Band,
National Insurance Corporation, shirika la bima nalo likaanzisha Bima Jazz Band ambayo wanamuziki wake awali wengi walikuwa wanamuziki wa BAT Jazz Band mali ya  kampuni ya sigara ya British American Tobacco (BAT), kampuni iliyokufa na kuzaliwa kampuni ya Tanzania Cigarette Company (TCC). Mwaka 1978. Tanzania Taxi and Transport Service (TTTS) wakaanzisha bendi yao waliyoiita Mlimani Park Orchestra, jina la Mlimani lilitokana na bendi kuanzia Mlalakuwa jirani na chuo kikuu cha Dar es Salaam maarufu kwa jina la Mlimani, bendi hii ilikuja kubadili jina baada ya kuchukuliwa na Dar es Salaam Development Corporation (DDC) na kuitwa DDC Mlimani Park Orchestra mwaka 1982. Mashirika ya umma na idara za serikali zilianzisha bendi hizi hasa kwa ajili ya kuburudisha  wafanyakazi wake, lakini pia na kutambua uwezo wa muziki katika kusambaza ujumbe ambao mashirika haya yalitaka uwafikie wananchi, na mwisho bendi hizi zilikuwa ni vitega uchumi. Bendi za mashirika kama Urafiki Jazz Band, Biashara Jazz Band, na Bima Lee, kwa mfano zilifanya kazi za kutangaza biashara za kampuni zao na bendi zilizunguka kila wilaya nchini, na hata kwenye vitongoji vidogo kabisa. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), lilikuwa na bendi tatu ikiwemo Kimbunga Stereo ikiwa kambi ya Mgulani, Kimulimuli katika kambi ya Mafinga, na kambi ya Makutopora nayo pia ikawa na bendi yake. Kulikuwa na bendi za Polisi maarufu kama Usalama jazz Band  huko Bukoba na Moshi, wakati Polisi Jazz band ilikuwa Dar es Salaam. Kuna hata Kurugenzi za mikoa zilizoanzisha bendi zilizokuja kuwa maarufu, bendi za Kurugenzi Arusha na Kurugenzi Dodoma ni kati ya bendi hizo. Kwa kuwa chama cha siasa kilikuwa kimoja tu, bendi zote hizi, pamoja na bendi zilizokuwa za watu au vikundi binafsi zilishiriki kikamilifu katika kutangaza mambo yote ya siasa wakati ule. Kimsingi hakukuwa na mabadiliko sana kwa jambo hili, kwani mahusiano kati ya wanamuziki na siasa yalianza toka wakati wa kupigania Uhuru, wazee kama marehemu Mzee Nnauye walitumia sana muziki kuhamasisha wananchi kuunga mkono juhudi za kumuondoa mkoloni. Uhusiano huu uliongezeka sana mara baada ya Uhuru kwa bendi kutunga nyimbo nyingi za uzalendo na kuhamasisha ujenzi wa Taifa jipya. Mpaka kufikia mwishoni mwa miaka ya 1980, kila wakati wa kurekodi nyimbo mpya bendi zilikuwa japo na wimbo mmoja wa siasa katika kila nyimbo sita. Radio ya Taifa ilizipiga sana nyimbo hizi na zikafahamika nchini kote.RTD wakati huo ilikuwa ni ngazi moja kubwa ya kutangaza nyimbo za bendi za hapa nchini. Takwimu moja iliyofanywa July 1968, ilionyesha kuwa asilimia  84% ya nyimbo zilizoombwa na wasikilizaji katika vipindi vitatu vya Idhaa ya Kiswahili ya RTD, zilikuwa ni nyimbo za Kiswahili, kutoka Tanzania, na nyingi zikiwa nyimbo za siasa. Bendi hazikuongelea tu siasa za ndani ya nchi bali ziliongea pia kuhusu siasa zilizokuwa zikiendelea ulimwenguni na hasa kuhusiana kupigania uhuru wa nchi zilizokuwa bado zinatawaliwa Afrika. Vijana Jazz Band ndio ilikuwa bendi kubwa ya kuelezea mipango, sera na maanuzi ya chama tawala, bendi ilikuwa mstari wa mbele kwenye kampeni za uchaguzi na kutunga nyimbo nyingi za kupigia debe mgombea wa chama tawala. Bila kusahau bendi zilifanya kazi kubwa ya kuwahamasisha askari na wananchi wakati wa vita ya Kagera, baada ya vita vikundi vya muziki vya JKT, JWTZ na Magereza, vilizunguka sehemu mbalimbali nchini Uganda kupiga muziki kuwahamasisha watu kurudi kutoka mafichoni.
Mwisho lazima nitoe mfano wa bendi binafsi zilivyokuwa zinashiriki katika siasa. Bendi kama Kilwa Jazz band ilikuwa moja ya bendi iliyotumika sana na wanasiasa wa TANU kuhamasisha watu juhudhuria mikutano ya kisiasa, na hata katika mikutano ya kuchangia chama. Kilwa Jazz ndio ilikuwa bendi rasmi iliyopiga muziki siku ya sherehe za mwaka wa pili wa Uhuru 1962, na ndio bendi iliyopelekwa na serikali kwenye sherehe za Uhuru wa Malawi mwaka July 6, 1964.

No comments: