Mara ya kwanza kukutana uso kwa uso na Hemedi Maneti ilikuwa ni wakati Vijana Jazz band ilipita Iringa ikielekea Songea mwaka 1989. Wakti huo nilikuwa mwanamuziki wa Tancut Almasi Orchestra, na kama ilivyokuwa ada miaka ile, bendi ikipita katika mji ambao kuna bendi wanamuziki walikuwa wakipiga muziki pamoja. Tuliongea nae machache lakini aliongea kuhusu kufurahishwa na setting ya vyombo vyetu, alisema inafanya vyombo vyote visikike. Wakati huo hatukujua lakini kumbe alikuwa kishaongea na Shaaban Wanted, Mohamed Gotagota na Mohamed Shaweji ili wajiunge na Vijana Jazz band, na hakika walihamia bendi hiyo wiki chache zilizofuata.
Katika mlolongo huohuo nilijikuta nikiitwa kujiunga na Vijana Jazz Band mwezi wa September mwaka huohuo na kufikia Oktober 1989 niliwasili Dar es Salaam kujiunga na Vijana Jazz Band. Siku ya kwanza nilipofika Vijana maneti alinipa shilingi 300 za kuanza maisha. Nitafute guest house ya kuishi na chakula kwa wiki moja. Hiyo ndiyo kumbukumbu yangu ya kwanza ya Maneti ambaye miezi michache baadae, tarehe 31 May 1990 siku ya Alhamisi majira ya saa kumi na moja jioni, Hemed Maneti alifariki katika hospitali ya Mwananyamala. Alikuwa ameanza kuwa na matatizo ya afya miezi kadhaa kabla ya hapo na hatimae kupelekwa Tanga kwa ajili ya matibabu. Hali yake ilipozidi kuwa mbaya alirudishwa kwa ndege kuwasili Dar Jumatano 30 May na kupelekwa moja kwa moja hospitali ya Mwananyamala ambapo alilala na kufariki kesho yake. Marehemu alisafirishwa kwenda kuzikwa Tanga siku moja baadae.
Wimbo wa mwisho kurekodi ulikuwa wimbo Nelson Mandela uliotungwa nami, ukiwa wimbo uliokuwa matayarisho ya ziara ya Nelson Mandela.
Thursday, June 1, 2017
Friday, May 26, 2017
URAFIKI WA MUZIKI NA SIASA ULIANZA ENZI ZA UKOLONI
Miaka michache baada ya Tanganyika kupata Uhuru, nchi yetu ikabadili mfumo wa siasa na kuwa na siasa ya chama kimoja. Hivyo chama cha TANU kikawa ndicho chama pekee cha siasa nchini. Katika mtiririko huo wa siasa ya chama kimoja, vyama vingine mbalimbali vilivyokuwa si vya kisiasa, vikaunganishwa ili kuwa kwa namna moja au nyingine chini ya TANU, hivyo kukaweko na muungano kama National Union of Tanganyika Workers (NUTA) kwa ajili ya vyama vya wafanyakazi, Cooperative Union of Tanganyika (CUT), muungano wa vyama vya ushirika, TANU Youth League (TYL) chama cha vijana, na kadhalika. Pia jeshi likaundwa upya na kukaundwa Tanzania Peoples Defence Force (TPDF) baada ya vurugu ya jeshi la awali la lililorithiwa kutoka kwa wakoloni lililoitwaTanganyika Rifles, na baadae jeshi jingine la kujitolea lililoitwa National Service likaanzishwa. Hakika mabadiliko yalikuwa mengi sana katika miaka saba ya kwanza baada ya Uhuru wa Tanganyika, likiwemo pia tukio kubwa la muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Mabadiliko haya mengi na ya muda mfupi yaligusa kila sekta ikiwemo sekta ya muziki. Katika miaka hii, kulikuwa na aina mbalimbali za muziki uliokuwa ukipendwa , ukiwemo muziki wa dansi, taarab, kwaya na ngoma za asili. Muziki wa dansi ulikuwa umejikita hasa mijini, bendi zikiwa mali za watu binafsi au taasisi binafsi. Lakini baada ya mabadiliko hayo niliyo yataja hapo juu, vyombo vya umma vikaanza kuzindua vikundi vyao vya muziki. Kati ya bendi za kwanza kuanzishwa kupitia mfumo hu, zilikuwa ni NUTA Jazz Band ikijitambulisha kwa mtindo wa msondo, Polisi Jazz Band na mtindo wa Vangavanga, National Service Jazz Band na mtindo wa Kimbunga, baadaye bendi hii ikaja kuitwa Kimbunga Stereo, baada ya bendi nyingine ya National Service kuanzishwa katika kambi ya jeshi hilo huko Mafinga Iringa, ambayo iliitwa National Service Kimulimuli. Jeshi la wananchi nalo likaanzisha bendi Mwenge Jazz Band wana Paselepa, na hivyo hivyo Jeshi la Magereza wakawa na Magereza Jazz Band waliokuja kuwa namtindo wa Super Mnyanyuo na hata idara ya Uhamiaji nayo ilianzisha bendi maarufu ya Uhamiaji Jazz Band iliyokuwa na mtindo wao wa Hamahama. Vijana wa chama cha Tanu, walianzisha TANU Youth League Jazz Band, iliyokuja kupata jina la Vijana Jazz Band baadae. TYL ilianzisha pia bendi nyingi katika wilaya mbalimbali nchini, kama vile Mbeya lringa, Mwanza, Moshi, Lindi, Songea, Bagamoyo, Tunduru, Biharamulo, Nachingwea, Njombe, Same na kadhalika. Muungano wa vyama vya Ushirika nayo pia ikaja kuwa na bendi iliyokuja kuwa maarufu sana, Washirika Tanzania Stars. Mashirika ya umma nayo yakaanzisha bendi, Urafiki Jazz Band, ilikuwa mali ya kiwanda cha nguo cha Friendship Textile Mills, shirika la State Trading Corporation likaja na STC Jazz Band ambayo baadae ilikuja kuitwa Biashara Jazz band. Kampuni ya mabasi ya Usafiri Dar es Salaam ikazindua bendi yao ya UDA Jazz Band,
National Insurance Corporation, shirika la bima nalo likaanzisha Bima Jazz Band ambayo wanamuziki wake awali wengi walikuwa wanamuziki wa BAT Jazz Band mali ya kampuni ya sigara ya British American Tobacco (BAT), kampuni iliyokufa na kuzaliwa kampuni ya Tanzania Cigarette Company (TCC). Mwaka 1978. Tanzania Taxi and Transport Service (TTTS) wakaanzisha bendi yao waliyoiita Mlimani Park Orchestra, jina la Mlimani lilitokana na bendi kuanzia Mlalakuwa jirani na chuo kikuu cha Dar es Salaam maarufu kwa jina la Mlimani, bendi hii ilikuja kubadili jina baada ya kuchukuliwa na Dar es Salaam Development Corporation (DDC) na kuitwa DDC Mlimani Park Orchestra mwaka 1982. Mashirika ya umma na idara za serikali zilianzisha bendi hizi hasa kwa ajili ya kuburudisha wafanyakazi wake, lakini pia na kutambua uwezo wa muziki katika kusambaza ujumbe ambao mashirika haya yalitaka uwafikie wananchi, na mwisho bendi hizi zilikuwa ni vitega uchumi. Bendi za mashirika kama Urafiki Jazz Band, Biashara Jazz Band, na Bima Lee, kwa mfano zilifanya kazi za kutangaza biashara za kampuni zao na bendi zilizunguka kila wilaya nchini, na hata kwenye vitongoji vidogo kabisa. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), lilikuwa na bendi tatu ikiwemo Kimbunga Stereo ikiwa kambi ya Mgulani, Kimulimuli katika kambi ya Mafinga, na kambi ya Makutopora nayo pia ikawa na bendi yake. Kulikuwa na bendi za Polisi maarufu kama Usalama jazz Band huko Bukoba na Moshi, wakati Polisi Jazz band ilikuwa Dar es Salaam. Kuna hata Kurugenzi za mikoa zilizoanzisha bendi zilizokuja kuwa maarufu, bendi za Kurugenzi Arusha na Kurugenzi Dodoma ni kati ya bendi hizo. Kwa kuwa chama cha siasa kilikuwa kimoja tu, bendi zote hizi, pamoja na bendi zilizokuwa za watu au vikundi binafsi zilishiriki kikamilifu katika kutangaza mambo yote ya siasa wakati ule. Kimsingi hakukuwa na mabadiliko sana kwa jambo hili, kwani mahusiano kati ya wanamuziki na siasa yalianza toka wakati wa kupigania Uhuru, wazee kama marehemu Mzee Nnauye walitumia sana muziki kuhamasisha wananchi kuunga mkono juhudi za kumuondoa mkoloni. Uhusiano huu uliongezeka sana mara baada ya Uhuru kwa bendi kutunga nyimbo nyingi za uzalendo na kuhamasisha ujenzi wa Taifa jipya. Mpaka kufikia mwishoni mwa miaka ya 1980, kila wakati wa kurekodi nyimbo mpya bendi zilikuwa japo na wimbo mmoja wa siasa katika kila nyimbo sita. Radio ya Taifa ilizipiga sana nyimbo hizi na zikafahamika nchini kote.RTD wakati huo ilikuwa ni ngazi moja kubwa ya kutangaza nyimbo za bendi za hapa nchini. Takwimu moja iliyofanywa July 1968, ilionyesha kuwa asilimia 84% ya nyimbo zilizoombwa na wasikilizaji katika vipindi vitatu vya Idhaa ya Kiswahili ya RTD, zilikuwa ni nyimbo za Kiswahili, kutoka Tanzania, na nyingi zikiwa nyimbo za siasa. Bendi hazikuongelea tu siasa za ndani ya nchi bali ziliongea pia kuhusu siasa zilizokuwa zikiendelea ulimwenguni na hasa kuhusiana kupigania uhuru wa nchi zilizokuwa bado zinatawaliwa Afrika. Vijana Jazz Band ndio ilikuwa bendi kubwa ya kuelezea mipango, sera na maanuzi ya chama tawala, bendi ilikuwa mstari wa mbele kwenye kampeni za uchaguzi na kutunga nyimbo nyingi za kupigia debe mgombea wa chama tawala. Bila kusahau bendi zilifanya kazi kubwa ya kuwahamasisha askari na wananchi wakati wa vita ya Kagera, baada ya vita vikundi vya muziki vya JKT, JWTZ na Magereza, vilizunguka sehemu mbalimbali nchini Uganda kupiga muziki kuwahamasisha watu kurudi kutoka mafichoni.
Mwisho lazima nitoe mfano wa bendi binafsi zilivyokuwa zinashiriki katika siasa. Bendi kama Kilwa Jazz band ilikuwa moja ya bendi iliyotumika sana na wanasiasa wa TANU kuhamasisha watu juhudhuria mikutano ya kisiasa, na hata katika mikutano ya kuchangia chama. Kilwa Jazz ndio ilikuwa bendi rasmi iliyopiga muziki siku ya sherehe za mwaka wa pili wa Uhuru 1962, na ndio bendi iliyopelekwa na serikali kwenye sherehe za Uhuru wa Malawi mwaka July 6, 1964.
Monday, May 1, 2017
MSONDO KUTENGENEZA HISTORIA?
HABARI ambazo hazijathibitishwa zimesema kuwa bendi ya Msongo Ngoma Music imechukuliwa tena na Chama cha Wafanyakazi, na itaitwa TUCTA Jazz Band 'Msondo Ngoma'. Hii itakuwa historia ya mambo mengi, kwanza kurudi kwa uhusiano kati ya bendi hii na vyama vya wafanyakazi. Bendi hii ilianzishwa na chama cha wafanya kazi cha NUTA mwaka 1964 na kuitwa NUTA Jazz Band, na kubadilika kuwa JUWATA Jazz Band baada ya mabadiliko yaliyozaa Jumuiya ya Wafanya kazi Tanzania (JUWATA). Baada ya mabadiliko mengine yaliyoleta chombo kilichoitwa Organization of Tanzania Trade Unions (OTTU), bendi ikabadili jina na kuitwa Ottu Jazz band, kwa muda mfupi kulikuweko mabadiliko mengine yaliyoleta Tanzania Federation of Free Trade Unions (TFTU), na bendi ikachukuliwa na TFTU. Hatimae bendi ikajikuta iko huru ikiendeshwa na wanamuziki wenyewe na ndipo ilipojipa jima la Msondo Ngoma Music Band, na kama inavyosikika inaweza sasa tena ikaitwa TUCTA Jazz Band.hakika itakuwa moja ya bendi ambazo zimewahi kubadili jina mara nyingi kuliko bendi nyingine duniani.
Friday, April 28, 2017
SI KWELI KUWA HARRISON SATCHMO SIWALE ALIFIA GEREZANI,
![]() |
| Mar. Harrison Siwale-Satchmo |
...................... SIKILIZA HAPA GUITAR LA MZEE SIWALE...................
Tarehe 8 September 2013, niliandika katika blog hii habari niliyoipa kichwa cha habari, Harrison Siwale aliishia wapi? Ni habari ya kusikitisha.
Tarehe 8 September 2013, niliandika katika blog hii habari niliyoipa kichwa cha habari, Harrison Siwale aliishia wapi? Ni habari ya kusikitisha.
Niliandika hivi-----Nimetoka kuongea na Mzee mmoja ambaye nilimuomba anitafutie habari za Harrison Siwale aka ‘Satchmo’, ambaye alikuwa mpiga rhythm mahiri na maarufu sana katika miaka ya sabini, Harrison alikuwa na staili ya pekee ya upigaji wa gitaa wa kudokoa nyuzi na kupata aina ya pekee ya mlio wa gitaa. Kati ya nyimbo ambazo upigaji huu unasikika ni katika nyimbo za Jamhuri Jazz Band kama vile Mganga 1 na 2, Blandina na kadhalika. Pamoja na bendi nyingine Harisson aliwahi kupigia Atomic na Jamhuri Jazz Band zote za Tanga, na kisha kuvuka mpaka na kuwa na makazi Mombasa kwa muda mrefu ambako aliendelea na muziki. Kwa kadri ya maelezo niliyopewa leo na huyu Mzee niliyemuomba anitafutie habari ili nijue yu wapi huyu mwanamuziki siku hizi? Haya ndio aliyonambia.
'Baada ya kufa kwa yale makundi ya Simba wa Nyika na Les Wanyika, Harrison Siwale alianza kupiga muziki wa Injili katika eneo la Kilifi. Akawemo katika kundi lililokuwa likifanya maonyesho yake katika miji mingi ikiwemo Mombasa na Nairobi. Umahiri wake wa kazi ukamfanya mwenye vyombo vya hilo kundi alilokuwemo Harrison kumuamini sana na kumuachia awe kiongozi wa kundi hilo na kuwa huru kuzunguka sehemu mbalimbali. Inasemekana Harrison akapata tamaa ya kuingia mitini na vyombo vile, hivyo ghafla akapotea. Taarifa zikamfikia mwenye vyombo kuwa vyombo vyake viko njiani kuvushwa kungia Tanzania kupitia mji wa Lungalunga. Mwenye vyombo akaweka mtego hapo na Harrison akakamatwa hapo akiwa na vyombo hivyo, kesi ilifika mahakamani na akahukumiwa kifungo cha miaka mitatu'. Baada ya hapa kuna hadithi mbili, moja ikisema alifia gerezani Shimo la Tewa, na nyingine ikisema alifariki baada ya kumaliza kifungo chake.
Je, nini hasa kilitokea? Najaribu kuwasiliana na watu mbalimbali kupata hadithi zaidi kuhusu mwanamuziki huyu.
HATIMAE (2017 APRIL).... Kwa bahati sana nimeweza kuanza kuwasiliana na mtoto wa Harrison Satchmo Siwale, ambae tuliweza kukutana kupitia facebook. Kijana huyu ambaye jina lake ni Salehe Siwale aliweza kunambia kuwa baba yake alimuoa mama yao na walizaliwa vijana wawili yeye na kaka yake.
Na niliweza kupata taarifa za ziada baada ya kuniunganisha na mama yake ambaye ndie alikuwa mke wa Mzee Siwale nikaweza kuongea nae mubashara kupitia video call ya whatsapp. Kwanza kabisa mama huyo ansema kuwa katika kipindi alichoishi na Mzee Siwale hakuwahi kufungwa wala kuzungumzia kuwa aliwahi kufungwa. Na Mzee Siwale alifariki katika Kitongoji cha Rongai huko Nakuru na kuzikwa tarehe 31/3/2013. Ukiangalia kuwa taarifa ya awali niliyopewa ilikuwa katika miezi michache baada ya kifo chake, niwazi si kweli kuwa alifia Gerezani na kama angekuwa aliwahi kufungwa hakika mkewe angekuwa anajua.
Mungu Amlaze Pema Mchungaji Harrison ‘Satchmo’ Siwale
Saturday, April 22, 2017
KIFO CHA SOKOINE KILIIKUTA ORCHESTRA MAMBO BADO IKO SHINYANGA
Mwaka 1984 nilikuwa mwanamuziki wa bendi ya Orchestra Mambo Bado, bendi iliyokuwa inaongozwa na Tchimanga Kalala Assossa. Bendi ilikuwa ni moja ya bendi zilizokuwa pendwa wakati huo, mtindo wa bendi ulikuwa unajulikana kama Bomoa. Neno hili lilitokana na wimbo wa Bomoa Tutajenga Kesho, wimbo ambao baadae kwa sababu ambazo mpaka leo sizijui, ulikuja kupigwa marufuku na Umoja wa Vijana wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati ule, usisike kwenye radio ya Taifa, redio ambao ilikuwa pekee wakati huo. Orchestra Mambo Bado ilikuwa na watu ishirini hivi, Tchimanga Assossa kiongozi na mwimbaji. George Mzee muimbaji, Lucas Faustin muimbaji, Jenipher Ndesile muimbaji, Banza Tax muimbaji, Athumani Cholilo muimbaji, John Kitime muimbaji, Likisi Matola mpiga gitaa la bezi, Andre Milongo akipiga gitaa la second solo, Huluka Uvuruge na Kazembe wa Kazembe wapiga gitaa la solo, William Maselenge akiwa kwenye gitaa la rhythm. Kulikuweko na wacheza show wanne, mafundi mitambo watatu na mweka hazina mmoja na meneja wa bendi. Masikani ya bendi yalikuwa katika ukumbi wa Lango la Chuma, Mabibo Dar es Salaam
Tarehe 12 April 1984, kundi zima lilitua katika mji wa Shinyanga baada ya kuwasili hapo kwa treni kutokea Dar es Salaam. Kwa taratibu za miaka hiyo, pamoja na ratiba ya ziara ya bendi kutangazwa kwenye gazeti la Uhuru, meneja wa bendi alikuwa akilazimika kutangulia mji ambao dansi litapigwa kuwahi kufanya mikataba na kumbi ambazo dansi lingepigwa na pia kufuatilia vibali mbalimbali vya kuruhusu onyesho kufanyika. Mawasiliano yalikuwa magumu na urasimu ulikuwa mkubwa. Haikuwa kazi rahisi maana miaka hiyo ili bendi isafiri ililazimika kupata kibali cha Afisa Utamaduni wa Mkoa ambao ni masikani ya bendi kuruhusu bendi kutoka nje ya Mkoa na kisha kibali hicho kupelekwa kwa Ofisa Utamaduni wa Mkoa ambao bendi inakwenda, nae baada ya kuruhusu bendi kuingia mkoani kwake, unaomba kibali cha Afisa Utamaduni wa Wilaya unakotaka kupiga muziki ili nae akuruhusu kufanya onyesho kwenye wilaya yake. Baada ya hapo meneja hutafuta na mtu ambaye ana spika ya mkononi, megaphone kuikodisha na kisha kutafuta mtu wa kutangaza onyesho. Ili kubana matumizi kuna mara nyingine wanamuziki wenyewe ililazimika wapite mtaani na spika hiyo kujitangaza. Kulikuwa na mji kama Mpanda wakati huo, ambapo mtangazaji hakuwa na megaphone, mtu maalumu alipita mtaa kwa mtaa akiwa na ngoma ambao aliipiga watu wakikusanyika basi anatangaza ujio wa bendi katika mji wao.
Tarehe 12 April 1984, Orchestra Mambo Bado iliwasili Shinyanga kwa treni ikitokea Dar es Salaam, kuanza ziara ya Kanda ya Ziwa. Wanamuziki tulionyeshwa vyumba vya kulala, mambo yalionekana kuwa yatakuwa mazuri kwa siku ile, matangazo yalikuwa yamebandikwa kwenye nguzo za umeme sehemu mbalimbali za mji, na hali ya kuonyesha kuwa watu walikuwa na taarifa ya ujio wetu ilikuwa dhahiri. Ilikuwa ni muda wa saa kumi hivi ilipotangazwa kuwa nchi imepata msiba mkubwa sana. Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine amefariki katika ajali ya gari jirani na Morogoro. Kwanza ilikuwa ni mshtuko, halafu akili ilipotulia tulijua kuwa na sisi kama bendi tunaingia kwenye tatizo kubwa sana, tulikuwa na nauli ya kuja tu mpaka Shinyanga, na fedha ya kula ya siku moja tulikuwa tunategemea kupiga dansi ili kuweza kulipa malazi ya siku hiyo na kupata fedha ya kula na kuendelea na safari kesho yake, tukitegemea mapato mengine makubwa katika maonyesho ya Mwanza wikiendi iliyokuwa inafuata. Hayo yote tulijua sasa yameharibika, tulirudisha vyumba vyote mara moja na kubaki na viwili tu kimoja kikiwa cha wasichana waliokuwa kwenye bendi, wengine wote ikalazimu tuhamishie mizigo yetu chumba kingine. Baadae tulikaa na Afisa Utamaduni kutafakari kama dansi lingeweza kulia siku ile, na kama halitalia nini hatima ya watu hawa 20 wageni kutoka Dar es Salaam? Kama kiasi cha saa moja jioni, Afisa Utamaduni akaruhusu tupige dansi ili tuweze kupata nauli ya kurudi Dar es Salaam, kwani ilijulikana wazi kitaanza kipindi cha maombolezo ambacho hakuna mtu alijua kitaisha lini, hivyo hakukuwa na sababu ya kuendelea na safari kutoka hapo. Vipindi vya maombolezo huwa ni vipindi ambavyo pamoja na mambo mengine shughuli za muziki husimamishwa. Kwa wanamuziki na wale wanaotegemea shughuli za muziki na familia zao, kipindi hiki huwa kigumu sana. Lakini kinaleta ukakasi akilini kwani shughuli za kupiga muziki kwenye kumbi husimamishwa, madisco hufungwa na vikundi vya muziki haviruhusiwi kufanya kazi lakini radio huendelea kupiga muziki uleule ambao umezuiwa kwenye kumbi, sehemu za starehe kama baa huendelea kupiga muziki na kufanya biashara zao bila tatizo ila wanamuziki ndio huzuiwa kufanya shughuli zao kwa maelezo kuwa ni kipindi cha maombolezo. Nakumbuka sana misiba mikubwa ya viongozi wetu ukiwemo wa Baba wa Taifa kwa sababu kubwa mbili, kwanza uchungu wa kupoteza kiongozi wetu na njaa iliyofuatia baada ya hapo.
Saturday, March 25, 2017
MIAKA 22 TOKA KIFO CHA NGULI MARIJANI RAJABU
ALHAMISI, Machi 23 mwaka 1995 ni siku isiyosahaulika kwa wapenzi wa muziki wa zamani nchini. Siku hiyo ndipo tulipompoteza mwanamuziki kipenzi chetu, Marijani Rajabu. Alizikwa kesho yake Ijumaa Machi 24 kwenye makaburi ya Kisutu.
Historia ya gwiji huyu inaanzia siku alipozaliwa tarehe 3 Machi mwaka 1955, katika eneo la Kariakoo. Mama yake alikuwa mama wa nyumbani wakati baba yake alikuwa na shughuli za uchapishaji. Maisha yake ya utoto yalikuwa ya kawaida ila alikuwa kipenda sana uimbaji wa Tabu Ley na mwimbaji mmoja wa Guinea Sorry Kandia. Alisoma shule ya Msingi ikiambatana na elimu ya Madrasa. Mwaka 1970 Akiwa bado shuleni, utaona umri wake ulikuwa miaka 15 tu, alijiunga na STC Jazz, ikiwa chini ya mpiga gitaa maarufu wakati huo Raphael Sabuni, kabla ya hapo bendi hii ilikuwa unajulikana kama The Jets. Katika bendi hii Marijani aliweza kutoka nje ya Tanzania kwa mara ya kwanza ambapo alikwenda Nairobi na kurekodi nyimbo zilizotoka katika label ya Phillips., hili jambo la mwanafunzi kusafiri na bendi likaleta shida na kwa vile STC ilikuwa mali ya umma akaachishwa kazi na mwaka1972 alijiunga na The Trippers ya David Mussa ambayo kwa wakati huo ilikuwa inapiga zaidi nyimbo za hoteli na za kukopi na muimbaji wao kiongozi wakati huo alikuwa Ali Rajabu. Hapa ndipo ubora wake ulifunguka haswa na kuweza kuinyanyua Trippers, ambayo sasa ilibadili jina na kuwa Safari trippers kutokana na msimamo wa serikali wakati huo wa kutaka majina ya nyumbani yatumike bala ya yale ya kigeni na kuwa moja ya bendi maarufu za wakati huo. Waliweza kutoa vibao vilivyopendwa mfululizo na kuweza kuzunguka nchi nzima. Vibao kama Rosa nenda shule, Georgina,Mkuki moyoni, viliweza kuuza zaidi ya nakala 10000 za santuri na hivyo kuwezesha bendi kuwa na vyombo vyake vizuri. Bendi wakati huo ikiwa na wanahisa wanne, ambao kwa bahati mbaya wakati bendi ndio iko juu, wakakosa kuelewana na ukawa ndio mwisho wa bendi hiyo. Marijani alishiriki kutunga, kuimba nyimbo karibu zote za Trippers sanjari na kupiga gitaa kwa baadhi ya nyimbo. Mfano wimbo Olila ambao alipiga rhythm na kuimba.
Mwaka 1976, Marijani na baadhi ya wanamuziki wa Trippers waliamua kuihama bendi na kwenda baadaye kuasisi Dar es salaam International chini ya umiliki wa Mzee Zakaria Ndabemeye ambaye bado yu hai hadi sasa. Baadhi ya wanamuziki hao ni pamoja na Abel Baltazar kutoka Msondo, Kassimu Mponda kutoka Trippers, Abdallah Gama, Joseph Mulenga, Haruna Lwali na George Kessy Omojo waliokuwa wanapiga muziki Magot pale, Said Mohamed kutoka Polisi Jazz, Cosmas Chidumule kutoka Urafiki, Belesa Kakere kutoka Biashara Jazz, Joseph Bernard kutoka Trippers, Ali Rajabu kutoka Trippers, na King Michael Enock kutoka Dar es salaam Jazz. Akiwa Dar Inter alishiriki kutunga nyimbo mbili, Betty na Sikitiko. Hata hivyo kama waswahili wanavyosema mafahari wawili hawakai zizi moja ndivyo ilivyotokea kati yake na Abel Balthazal kiasi cha hatimaye Marijani kufukuzwa ndani ya bendi kutokana na ubishi kuhusu wimbo aliotunga Marijani, kuna maelezo kuwa wimbo ulionekana unafanana na wimbo fulani toka Kongo na hivyo Marijani akatakiwa aubadilishe na ndipo ugomvi ukaanza. Hata hivyo mwishoni mwa mwaka 1978, Marijani alirejeshwa tena kundini kutokana na rundo la wanamuziki wa Dar Inter kuihama bendi kwa kishindo kikubwa na kwenda kuifungua bendi mpya kabisa ya Orchestra Mlimani Park. Aliporejeshwa Marijani alikuja na wanamuziki wengi wapya wakati huo kama akina Christopher Kasongo, Mohamed Tungwa, Mafumu Bilal, Hamis Milambo, Athuman Momba, Mzee Alex Kanyimbo na wengine na kuja na mtindo wa Super Bomboka. Katika kudhihirisha hasira zake kwa Abel, Marijani alimtungia Abel wimbo wa kumnanga ukiitwa Kidudu mtu ambao hata hivyo RTD waliukataa kuurekodi, jambo lililokuwa kawaida enzi hizo kwa redio kukataa wimbo. Sifa nyingine ambayo Marijani alikuwa nayo ni kuibua wanamuziki chipukizi kama alivyofanya mwaka 1983 alipomuibua kutoka Tanga kijana Mkuu Waziri Kungugu Kitanda Milima almaaruf Fresh Jumbe ambaye kwa hakika kabisa Marijani hakujutia kumchukua kijana huyo. Alimuamini kupita maelezo kiasi kwamba wakati mwingine alikuwa akimuachia bendi aongoze na yeye anapumzika nyumbani. Mbali na Fresh, wanamuziki wengine ni kama vile Tino Masinge, Mohamed Mwinyikondo, Juma Choka na wengine kibao. Ni vizuri kuelezea hapa kuwa kadri ya maelezo yake mwenyewe marehemu baada ya kurekodi Zuena na Mwanameka na nuimbo nyingine katika album hiyo alichoambulia ni malipo ya nauli toka RTD ya sh 2500/- tu. Kilichosikitisha zaidi ni kuwa nyimbo zao tisa ziliuzwa kwa kampuni ya Polygram bila ridhaa yao.
Hata hivyo safari ya Dar International ilikoma mwaka 1987 kutokana na sababu za kawaida za kufa kwa bendi lakini kubwa ni uchakavu wa vyombo. Hata hivyo Marijani aliendelea kufanya muziki na kwa kipindi kifupi amewahi kucheza na Kurugenzi ya Arusha na Mwenge Jazz ambayo alirekodi nayo wimbo mmoja wa Ukimwi na hata kupitia bendi ya Watafiti ambayo hatimae ilikuja kuwa 38.. Mwaka huohuo wa 1987 Marijani na Muhidin Maalim Gurumo waliliongoza kundi la wanamuziki zaidi ya 50 kutunga nyimbo maalum hasa kwa maadhimisho ya miaka 10 ya CCM na 20 ya Azimio la Arusha. Naizungumzia Tanzania All Stars. Aidha mwaka 1994 aliwahi kurekodi zong zing na marehemu Eddy Sheggy. Bendi yake ya mwisho ilikuwa ni Africulture ama Mahepe Ngoma ya Wajanja, iliyokuwa mali ya Rogers Malila, alikokuwa na wanamuziki kadhaa kama akina Hassan Kunyata, Mgosi na wengine. Bado Marijani ataendelea kukumbukwa na wapenda muziki kote nchini na hata Afrika kwa ujumla kwa nyimbo zake zenye mafundisho na tamu huku akienzi utamaduni na ngoma za kwao Kigoma.
ANGALIA VIDEO MARIJANI LIVE
Saturday, March 18, 2017
AMRI BILA TAFITI ZINAATHIRI SANA SEKTA YA MUZIKI
KATIKA shughuli ambazo watu wengi huona ni rahisi kuendesha na kutoa maamuzi bila utafiti ni soka na muziki. Ukisikiliza mazungumzo baada ya mechi za soka ndipo utakaposikia watu wanavyotoa ushauri au kukosoa wachezaji, kocha refa, chama cha mpira wa miguu, hakika ingewezekana watu hawa wakapata mamlaka, maamuzi yangekuwa ya ajabu sana.
Hali kadhalika kwenye muziki. Kwa mfano ukiuliza, kwanini muziki wa bendi hauna umaarufu kama zamani? Hakika ukipita kila mtaa utapata majibu, wengine watakwambia kosa la vyombo vya utangazaji , wengine watakwambia wanamuziki wenyewe , wengine watakwambia serikali, na pia utapewa maelekezo mbalimbali ya nini kifanyike. Bahati nzuri majibu haya ya mtaani hayana madhara kwani huishia hapo hapo. Lakini bahati mbaya huja pale ambapo viongozi wenye mamlaka nao hugeuka wataalamu wa muziki na wao kutoa maamuzi kadri ya mtizamo wao, lakini maamuzi yao huwa amri, na amri inapotolewa bila utafiti wa kutosha madhara yake yanaweza kuendelea miaka mingi baadae. Ninaloweza kusema kwa uhakika, ni kuwa muziki wa Tanzania leo ungekuwa katika nafasi ya juu zaidi duniani kama isingekuwa maamuzi ambayo yalitolewa bila utafiti miaka ya nyuma. Labda nitoe mifano kadhaa. Mpaka miaka ya 70, wanamuziki wa Tanzania walikuwa wakienda sambamba na wanamuziki wa nchi nyingine nyingi Afrika, licha ya kutokuwa na miundo mbinu muhimu katika maendeleo ya muziki kama vile kutokuwa na kampuni za kurekodi na kutengeneza santuri. Lakini kimuziki, wanamuziki wa kipindi hiki walikuwa bega kwa bega na wenzao ambao walikuwa na miundo mbinu stahiki. Tanzania tulikuwa na bendi ambazo zilikuwa zinapiga muziki wa rumba, nyimbo nyingi za wakati huo mpaka leo bado zinasifika na kupendwa katika anga za muziki. Pia tulikuwa na wanamuziki vijana ambao wengi wao walikuwa mashuleni, hawa wakiwa na mtizamo mpana zaidi wa kutambulika duniani, wanamuziki hawa kama ilivyokuwa sehemu nyingi Afrika walianza kupiga muziki uliojulikana kama Afro Rock, muziki ambao ulichanganya mahadhi ya muziki asili wa Kitanzania na mapigo ya kizungu, wakifuatia nyayo za kundi la Osibisa, na wanamuziki kama Ransome Fela Kuti. Kukawa na makundi kama Afro 70, Trippers, Sun Burst, The Jets na kadhalika kwa kuyataja machache, makundi ambayo yalianza kuingiza muziki wa Tanzania kwenye soko kubwa zaidi la Kimataifa, kwa mfano wimbo wa Weekend wa Afro70 uliingia kwenye Top Ten Nigeria miaka hiyo, wakati huo muziki wa Nigeria haukuwa na umaarufu wowote nchini kwetu. Kwa kuwa vijana hawa wengi walikuwa bado shuleni, na kufuatana na maadili ya wakati ule, wanafunzi hawakuruhusiwa kushiriki madansa ya usiku, hivyo basi kulikuweko na utamaduni wa madansa ya mchana yaliyoitwa Bugi. Hapo vijana walikusanyika kupiga muziki wao kila mwisho wa wiki, shughuli zikianza saa nane mchana na kuisha saa kumi na mbili jioni. Lakini siku moja kiongozi mmoja akatokea na kupiga marufuku Bugi, hivyo kuwaondoa wanamuziki vijana wengi kwenye muziki kwani wasingeruhusiwa kushiriki madansi ya usiku. Wakati vijana hao wanaacha muziki, vijana wengine Afrika waliendelea mbele. Hata majirani zetu Kenya na Zambia wakawa na wanamuziki wengi walioweza kuingia katika soko la Kimataifa, wanamuziki wetu walikosa fursa hiyo. Pengo hili linaendelea kuwepo mpaka leo. Kuziba pengo hilo kunahitaji kutafiti tulipojikwaa na kuangalia tunafanya nini kurekebisha hali iliyopo. Swala la kupiga marufuku kazi za muziki si jambo geni katika historia ya muziki, kulikuwa na maamuzi kadhaa ya kisiasa pia ambayo pia hayakuwa na utafiti hivyo kudhoofisha maendeleo ya muziki Tanzania. Kwa mfano kulishawahi kutolewa amri ya kupiga marufuku wacheza show, wakati huo karibu bendi zote kubwa za muziki wa rumba kote Afrika Mashariki na Kati zilihakikisha kuwa zinakuwa na kundi la wacheza show, na waimbaji maarufu kama Mbilia Bel na Tshala Mwana wote awali walikuwa ni wacheza show. Kwa kipindi kirefu kulikuweko na sinto fahamu ya wacheza show na ikalazimika taaluma hiyo irudi kinyemela kwani makundi yote ya muziki kutoka nje yalipokuja nchini yalisindikizana na wacheza show. Nyimbo kadhaa ziliwahi kupigwa marufuku na hatimae kuja kuonekana ni za muhimu katika jamii, ukiwemo wimbo maarufu wa Super Matimila, Mambo kwa Soksi, ambao ulipigwa marufuku na baade kuonekana ni wimbo muhimu kuhamasisha watu kutumia kinga katika zama hizi za balaa la Ukimwi. Upigaji marufuku wa tungo unakwaza watunzi na kuishia kutunga nyimbo nyepesi ambazo zina uhakika wa kutokupigwa marufuku. Katika miaka ya karibuni kumewahi kufanyika maamuzi kadhaa yasiyokuwa na utafiti kwa mfano, serikali iliwahi kununua mashine iliyoitwa Mastering Mixer kwa gharama ya shilingi milioni 50, kwa maelezo kuwa ndio itakayowezesha kumaliza wizi wa kazi za muziki. Sio siri wizi uko palepale. Hayo yalikuwa maamuzi bila utafiti, ni vizuri kujua hiyo ‘mixer’ iko wapi ili kutathmini ni matokeo ya uamuzi huu uliogharimiwa na serikali. Uamuzi mwingine ulikuwa ni ule wa kutunga sheria ya kuweka stempu za TRA kwenye kazi za sanaa, kwa maelezo kuwa utamaliza wizi wa kazi za muziki na filamu. Si mara moja taarifa imatolewa kuwa serikali ilitoa milioni 20 kwa mtafiti toka ‘Chuo Kikuu’ kuhakiki kuwa njia hiyo ndio itamaliza wizi wa kazi za sanaa, hakuna ‘mtafiti’ anayejitokeza kuwa alipokea fedha na kufanya utafiti huo, wala hakuna nakala ya utafiti huo, ni aina nyingine ya maamuzi bila utafiti na matokeo yake wizi wa kazi za sanaa umeenea kila kona nchini na mauzo halali ya kazi za muziki yamepotea. Ushauri tu kwa viongozi kuwa muziki si shughuli ya kubahatisha ina misingi yake, ni muhimu kwa manufaa ya Taifa, umefika wakati wa kufanya utafiti kwanza kabla ya kutoa maamuzi.
Subscribe to:
Posts (Atom)




