Wednesday, December 14, 2016

MWISHO WA LUTUMBA SIMARO KATIKA TP OK JAZZ


BANNING EYRE ni mwandishi Mmarekani aliyefanya mazungumzo na mwanamuziki Lutumba Simaro mpiga gitaa wa kundi la OK Jazz, kuna mengi ya kujifunza kwa wanamuziki wa Tanzania
SWALI: Nini kinaendelea katika muziki wa Kongo siku hizi?
SIMARO: Kinachoendelea sasa sikipingi, mi ndio baba yao, hawa vijana kuna kitu walichoingiza katika muziki. Wameleta damu mpya na ujana kweli lakini,kuna monotony mno, Huwezi kutofautisha bendi moja na nyingine. Wanavyoimba, wanavyocheza na wanavyopiga mgitaa katika kile wanachoita seben. Kuna mtangazaji mmoja anaitwa Gaspar wa Studio Maximum, ana kipindi kimoja ambapo nilikuwa nasikia wimbo wa Werrason lakini alikuwa JB anecheza na wimbo wa JB ukichezwa show na Werra, kwa kweli huwezi kuona tofauti ya muziki wa hawa wawili.
Enzi za OK Jazz, Franco alikuwa mtunzi mzuri sana, mimi nikajiunga nikaleta style yangu, Josky alipokuja nae akaleta staili yake. Ndombe nae pia akaja na staili yake. Wote tulikuwa OK Jazz, gitaa la Franco ndilo lilitawala na kuweka nembo ya staili zetu mbalimbali. Papa Wemba akiimba najua ni Papa Wemba ana staili yake. Mdogo wangu Kofi nae anastaili yake, Zaiko ya Nyoka Longo pia wana staili yao
Kama wangeweza kunisikiliza ningewaambia hivi hawa vijana wanajitoa Wenge na kuanzisha makundi yao, ni muhimu kuja na utofauti, wana waimbaji wazuri sana, watunzi wazuri na wamepata bahati kuweza kurekodi katika studio za kisasa wana jukumu la kuendeleza ubunifu. Wakati wetu wa enzi za Vicky Longomba, Mujos na Kabasele, kama we ni mwimbaji ulilazimika kuimba aina mbalimbali za muziki. Muziki wa Ulaya au Marekan na kwa staili mbalimbali. Mtu akiomba Tango, unapiga Tango , ukitakiwa kuimba Waltz uliimba style hiyo, lakini waimbaji wetu wa sasa, hakuna kitu. Na wapiga magitaa pia, tulikuwa na wapiga magitaa wakali kama Papa Noel, na Tino Baroza, na hata Franco. Wapiga magitaa siku hizi ukiwauliza unamfahamu Nico Kasanda? Tuno Baroza? Kimya kinatawala. Muhimu kujua staili zao ili kujitafutia stail mpya. Nina mpiga gitaa ana miaka 20, wiki iliyopita nilimpa sanduku zima la santuri akafanye mazoezi, nashukuru ameanza kuniuliza maswali mengi kuhusu upigaji mbalimbali. Utunzi nao unapwaya pia utakuta wimbo unataja majina ya watu 200, wanaita “mabanga”, nawauliza majina mengi ya nini wananiambia hawa huwa wanawalipa vizuri.
Vijana wana bahati wana teknolojia nzuri, wana TV nyingi na nzuri za kuweza kuwafanyia promotion, Wakati wetu tulikuwa na radio moja tu, hivyo ililazimu kufanya kazi nzuri ili ujulikane. Nawakumbuka Soki Dianzenza na Soki Vangu walikuja na kitu kipya, Nyboma, Pepe Kalle wote watakumbukwa kwa aina yao ya uimbaji.
Nimeitafsiri kwa ruksa ya Banning Eyre. Kwa habari nyingi zaidi angalia <www.afropop.org>

Monday, December 5, 2016

SITI BINTI SADI SUPER STAR WA KWELI



Kwa kila hali Siti Binti Sadi anastahili kuenziwa. Kwa akina mama, mwanamke huyu shujaa aliyetoka katika familia maskini ya kijijini, ataenziwa kwa kuwa aliweza kushinda mfumo uliokuwa ukizuia wanawake kujichagulia mfumo wa maisha yao, na kuweza kujitokeza kufanya yale ambayo hayakuwezekana kwa mwanamke wa aina yake kabla. Alijitokeza na kuwa mwanamke mwimbaji mwenye nguvu za kuendesha shughuli za muziki katika mfumo uliotawaliwa na wanaume.
Kwa akina mama wanamuziki katika Taarabu, alikuwa ndio ufunguo ya mfumo uliopo ambao taarab inaongozwa na waimbaji wa kike.

Alikuwa ndie mwasisi wa kuimba taarab kwa Kiswahili.
Kwa wanamuziki wote kwa ujumla Siti Binti Sadi ni super star wa kweli.
- Alirekodi santuri zaidi ya 150
- Alikuwa wa kwanza kwenda kurekodi nyimbo zake India May 1928
- Umaarufu wake ulisababisha Columbia Records ya India kujenga studio Zanzibar katika enzi yake ili tu kumrekodi.
Oktoba 1936 aliwahi kufanya onyesho moja huko Pangani na kupata shilingi 1200/-. Kwa thamani ya pesa wakati ule, mtu aliweza kupanga chumba kwa shilingi 1 kwa mwezi. Na Pangani ilikuwa na wastani wa watu 1500. Si rahisi msanii yoyote wa leo hapa nchini kuweza kufikia Usuper Star huo.Kufanya onyesho na kuteka mji mzima.
Siti alizaliwa mnamo mwaka 1880 na kufariki 1950.
































Tuesday, November 29, 2016

NI MIAKA MITATU TOKA KIFO CHA NGULI TABU LEY


Mokolo mosusu ngai nakanisi
Naloti lokola ngai nakolala aah mama
Mokolo nakokufa
Mokolo nakokufa, nani akolela ngai ?
Nakoyeba te o tika namilela.
Liwa ya zamba soki mpe liwa ya mboka
Liwa ya mpasi soki mpe liwa ya mai O mama
Mokolo nakokufa
Kwa kifupi maana ya maneno haya ni;
Siku moja niliona kama nimeota siku yangu ya kufa,
Siku ya kufa nani atanililia? Sijui labda nitabiri.
Ntafia porini au nyumbani?
Kifo changu kitakuwa cha maumivu au kuzama majini?
Ahh siku yangu ya kufa.

Tabu Ley maarufu kwa jina na Rochereau, alizaliwa mwaka 1940 huko Bandundu katika Jamhuri ya Demokrasi ya Kongo. Alianza maisha akiitwa Pascal Emmanuel Sinamoyi Tabu, jina la Rocherau lilikuwa ni jina la utani toka shuleni na ndilo alilolitumia alipopeleka nyimbo zake za kwanza kwa Joseph Kabasele wakati akiomba kujiunga na bendi ya African Jazz. . Tabu Ley alianza maisha yake ya muziki mapema sana na 1954 akiwa na umri wa miaka 14 tu aliandika wimbo wake wa kwanza Bessama Muchacha,  ambao akaurekodi na kundi maarufu la African Jazz lililokuwa chini ya Joseph ‘Grande Kalle’ Kasebele, (asichanganywe na Pepe Kalle). Aliendelea na shule na hatimae alipomaliza High School 1959, ndipo alipojiunga rasmi na African Jazz. Alikuwa mmoj awapo wa walioimba ule wimbo utunzi wa Grande Kalle, na uliotikisa anga la Afrika miaka ya 60, Independence Cha Cha. Uliogeuka na kuwa wimbo rasmi wa kusherehekea uhuru wa kongo. 

Baada ya kiasi kama miaka minne alijiengua bendi hii na akiwa na mpiga gitaa mahiri Nicholaus Kassanda aka Dr Nico, wakaanzisha African Fiesta, ambapo alikuweko hadi 1965, wakati Kongo imewaka moto kimuziki na ushindani kuwa mkali sana, akaachana na Dr Nico na kuanzisha African Fiesta National au mara nyingine ikiitwa Africa Fiesta Flash, Wanamuziki kama Papa Wemba na Sam Mangwana ni kati ya wakongwe waliowahi kupitia katika kundi hili tishio.

 Kufikia mwaka wa 70, Tabu Ley alianzisha Orchestre Afrisa International wakati huo Afrisa na TPOK Jazz ndizo zilikuwa bendi maarufu zaidi Afrika. Afrisa waliteremsha vibao kama Sorozo, Kaful Mayay, Aon Aon, na Mose Konzo na  Tabu Ley aliweza hata kupata tuzo toka serikali za nchi kama Chad iliyompa heshima ya Officer of The National Order, wakati Senegal ilimpa heshima ya Knight of Senegal, na akawa sasa anaitwa Siegneur Rochereau. Katikati ya miaka ya 80 Tabu Ley aligundua kipaji cha mwanamama aliyekuja kutikisa anga za Afrika naye si mwingine ila Mbilia Bel, baadae Tabu alimuoa Mbilia a wakapata mtoto mmoja. Nyimbo kama Nadina, Nakei Nairobi zinaonyesha kipaji gani alikuwa nacho binti huyu aliyekuwa mzuri kwa sura, aliyejua pia kucheza na kutawala jukwaa vizuri. 1988 Tabu akamgundua muimbaji wa kike mwingine Faya Tess. Hapo Mbilia akaacha bendi na kuendelea na maisha yake ya muziki peke yake.
Kipindi hiki, mtindo wa Soukus uliokuwa na mapigo yenye mwendokasi zaidi ya lile rumba la Afrisa na TPOK Jazz ulianza kuzishika nyoyo za vijana, bendi hizi kubwa zikaanza kufifia.
Mwanzoni mwa miaka ya 90 Tabu Ley alihamia Marekani akaishi Kusini mwa California, akabadili muziki wake katika kujaribu kujikita zaidi katika soko la ‘Kimataifa’, akatunga nyimbo kama Muzina, Exil Ley, Babeti Soukous. 1996 Tabu Ley alishiriki katika album ya kundi la Africando na kushiriki katika wimbo Paquita wimbo aliyokuwa ameurekodi miaka ya 60 akiwa na African Fiesta. Tabu alipata cheo cha Uwaziri katika utawala wa Laurent Kabila baada ya kuondolewa kwa Mobutu. Hata baada ya kifo cha Laurent Kabila November  2005 Tabu alipewa cheo cha Vice-Governor in charge of political, administrative, and socio-cultural questions, kwenye jiji la Kinshasa.
Mwaka 2006  Tabu Ley  akashirikiana na rafiki yake wa  muda mrefu Maika munah na kutoa album yake ya mwisho iliyoitwa Tempelo, katika album hiyo kuna wimbo ambao ni kama kumbukumbu ya kote alikopita na pia akaimba wimbo mmoja na binti yake Melodie.
Mwaka 2008 alipata mshtuko wa moya na hakika kuanzia hapo hali yake haikutengenemaa mpaka kifo kilipomchukua siku ya Jumamosi Nov 30 2013, katika hospital ya St Luc Bsusells Ubelgiji. Matatizo ya kisukari na moyo yalisababisha kifo cha mbuyu huu wa muziki wa rumba. Inasemekana tabu Ley alikuwa na watoto wengi sana, inasemekana walifikia 104. Hata mwenyewe alipokuwa hai akiulizwa ana watoto wangapi hakujua. Watoto wake wachache walifuata nyayo za baba yao, akiwemo Melodie, binti aliyezaa na Mbilia Bel ambae sauti yake imo katika album ya mwisho ya Tabu Ley ‘Tempelo’ aliyoitoa mwaka 2006. Wengine katika muziki ni
 Pegguy Tabu, Abel Tabu, Philemon and Youssoupha Mabiki.
Youssoupha ni rapper anaeishi Paris, alizaliwa mwaka 1979 , mama yake alikuwa kutoka Senegal. Mwanae Marc Tabu ni mtangazaji kwenye TV moja huko Paris na ndie aliyetoa taarifa ya kwanza ya kifo cha baba yake kwenye ukurasa wake wa FACEBOO 2013.

Saturday, November 12, 2016

RAJABU OMARY KUNGUBAYA APATA MGUU WA BANDIA KUTOKA KWA WAPENZI WA MUZIKI WA ZAMANI


Marehemu Omary Kungubaya
Rajabu Kungubaya
Rajabu Omary Kungubaya, mtoto wa marehemu Omary Kungubaya, mwanamuziki ambaye alipata umaarufu kutokana na wimbo wake wa ‘ Salamu za wagonjwa’ uliokuwa wimbo wa kufungua na kufunga kipindi cha salamu za wagonjwa kilichokuwa kikirushwa na Radio Tanzania, leo amepokea mguu wa bandia ili kumsaidia kutokana na mguu wake wa kulia kuwa umekatwa kutokana na ajali ya bodaboda. Wanamuziki John Kitime na Mjusi Shemboza walimuona Rajabu kwa mara ya kwanza siku walipoenda kumzika Mzee Kungubaya na kuona umuhimu wa kumsaidia Rajabu kutokana na  hali yake ya kutegemea magongo wakati wa kutembea. Kwa kutumia kundi a Whatsapp la ZAMA ZILE, (kundi la wapenzi wa muziki wa zamani wanaosikiliza kipindi cha ZAMA ZILE kinachoendeshwa na John Kitime kupitia EFM 93.7fm kila Jumapili kuanzia saa 2-5 usiku), wanakikundi waliweza kuchanga fedha zilizowezesha kijana huyu kupata mguu wa bandia.
 Rajabu ni mchangamfu anaeonekana kupendwa na kila mtu, kutokana na majirani zake wote kumuunga mkono ikiwemo serikali ya mtaa wake. Mwenyekiti wa serikali ya mtaa akiwa na wajumbe wengine wa serikali ya mtaa wake wote walimsifu kwa tabia yake ambayo walisema ilikuwa ni mfano hasa kwa jitihada zake za kutunza familia yake. Mke wa marehemu Mzee Kungubaya, ambaye ni mama mzazi wa Rajabu alisema yeye alikuwa anategemea kuishi kwa kufanya kazi za kibarua katika sehemu ambazo kuna ujenzi unaendelea, hufanya kazi kama kubeba maji na zege kuwasaidia wajenzi. Marehemu Kungubaya ameacha watoto wakiwemo wadogo ambao mmoja yuko shule ya chekechekea na mwingine darasa la 6, wote hawa wanamtegemea sasa kaka yao ambae ana mguu mmoja. Rajabu alikatika mguu kutokana na gari kuovertake na kumfuata upande wake na kumgonga wakati akiwa kwenye bodaboda, aliyemgonga, jina na namba ya simu ipo aliahidi kumsaidia lakini hajatimiza ahadi zake kwa kijaa huyu aliyempa ulemavu wa maisha.


Saturday, October 29, 2016

EXCLUSIVE- ANGALIA PAMBAMOTO LILIVYOKUWA LIKICHEZWA MIAKA YA 90 -VIDEO