Tuesday, November 29, 2016

NI MIAKA MITATU TOKA KIFO CHA NGULI TABU LEY


Mokolo mosusu ngai nakanisi
Naloti lokola ngai nakolala aah mama
Mokolo nakokufa
Mokolo nakokufa, nani akolela ngai ?
Nakoyeba te o tika namilela.
Liwa ya zamba soki mpe liwa ya mboka
Liwa ya mpasi soki mpe liwa ya mai O mama
Mokolo nakokufa
Kwa kifupi maana ya maneno haya ni;
Siku moja niliona kama nimeota siku yangu ya kufa,
Siku ya kufa nani atanililia? Sijui labda nitabiri.
Ntafia porini au nyumbani?
Kifo changu kitakuwa cha maumivu au kuzama majini?
Ahh siku yangu ya kufa.

Tabu Ley maarufu kwa jina na Rochereau, alizaliwa mwaka 1940 huko Bandundu katika Jamhuri ya Demokrasi ya Kongo. Alianza maisha akiitwa Pascal Emmanuel Sinamoyi Tabu, jina la Rocherau lilikuwa ni jina la utani toka shuleni na ndilo alilolitumia alipopeleka nyimbo zake za kwanza kwa Joseph Kabasele wakati akiomba kujiunga na bendi ya African Jazz. . Tabu Ley alianza maisha yake ya muziki mapema sana na 1954 akiwa na umri wa miaka 14 tu aliandika wimbo wake wa kwanza Bessama Muchacha,  ambao akaurekodi na kundi maarufu la African Jazz lililokuwa chini ya Joseph ‘Grande Kalle’ Kasebele, (asichanganywe na Pepe Kalle). Aliendelea na shule na hatimae alipomaliza High School 1959, ndipo alipojiunga rasmi na African Jazz. Alikuwa mmoj awapo wa walioimba ule wimbo utunzi wa Grande Kalle, na uliotikisa anga la Afrika miaka ya 60, Independence Cha Cha. Uliogeuka na kuwa wimbo rasmi wa kusherehekea uhuru wa kongo. 

Baada ya kiasi kama miaka minne alijiengua bendi hii na akiwa na mpiga gitaa mahiri Nicholaus Kassanda aka Dr Nico, wakaanzisha African Fiesta, ambapo alikuweko hadi 1965, wakati Kongo imewaka moto kimuziki na ushindani kuwa mkali sana, akaachana na Dr Nico na kuanzisha African Fiesta National au mara nyingine ikiitwa Africa Fiesta Flash, Wanamuziki kama Papa Wemba na Sam Mangwana ni kati ya wakongwe waliowahi kupitia katika kundi hili tishio.

 Kufikia mwaka wa 70, Tabu Ley alianzisha Orchestre Afrisa International wakati huo Afrisa na TPOK Jazz ndizo zilikuwa bendi maarufu zaidi Afrika. Afrisa waliteremsha vibao kama Sorozo, Kaful Mayay, Aon Aon, na Mose Konzo na  Tabu Ley aliweza hata kupata tuzo toka serikali za nchi kama Chad iliyompa heshima ya Officer of The National Order, wakati Senegal ilimpa heshima ya Knight of Senegal, na akawa sasa anaitwa Siegneur Rochereau. Katikati ya miaka ya 80 Tabu Ley aligundua kipaji cha mwanamama aliyekuja kutikisa anga za Afrika naye si mwingine ila Mbilia Bel, baadae Tabu alimuoa Mbilia a wakapata mtoto mmoja. Nyimbo kama Nadina, Nakei Nairobi zinaonyesha kipaji gani alikuwa nacho binti huyu aliyekuwa mzuri kwa sura, aliyejua pia kucheza na kutawala jukwaa vizuri. 1988 Tabu akamgundua muimbaji wa kike mwingine Faya Tess. Hapo Mbilia akaacha bendi na kuendelea na maisha yake ya muziki peke yake.
Kipindi hiki, mtindo wa Soukus uliokuwa na mapigo yenye mwendokasi zaidi ya lile rumba la Afrisa na TPOK Jazz ulianza kuzishika nyoyo za vijana, bendi hizi kubwa zikaanza kufifia.
Mwanzoni mwa miaka ya 90 Tabu Ley alihamia Marekani akaishi Kusini mwa California, akabadili muziki wake katika kujaribu kujikita zaidi katika soko la ‘Kimataifa’, akatunga nyimbo kama Muzina, Exil Ley, Babeti Soukous. 1996 Tabu Ley alishiriki katika album ya kundi la Africando na kushiriki katika wimbo Paquita wimbo aliyokuwa ameurekodi miaka ya 60 akiwa na African Fiesta. Tabu alipata cheo cha Uwaziri katika utawala wa Laurent Kabila baada ya kuondolewa kwa Mobutu. Hata baada ya kifo cha Laurent Kabila November  2005 Tabu alipewa cheo cha Vice-Governor in charge of political, administrative, and socio-cultural questions, kwenye jiji la Kinshasa.
Mwaka 2006  Tabu Ley  akashirikiana na rafiki yake wa  muda mrefu Maika munah na kutoa album yake ya mwisho iliyoitwa Tempelo, katika album hiyo kuna wimbo ambao ni kama kumbukumbu ya kote alikopita na pia akaimba wimbo mmoja na binti yake Melodie.
Mwaka 2008 alipata mshtuko wa moya na hakika kuanzia hapo hali yake haikutengenemaa mpaka kifo kilipomchukua siku ya Jumamosi Nov 30 2013, katika hospital ya St Luc Bsusells Ubelgiji. Matatizo ya kisukari na moyo yalisababisha kifo cha mbuyu huu wa muziki wa rumba. Inasemekana tabu Ley alikuwa na watoto wengi sana, inasemekana walifikia 104. Hata mwenyewe alipokuwa hai akiulizwa ana watoto wangapi hakujua. Watoto wake wachache walifuata nyayo za baba yao, akiwemo Melodie, binti aliyezaa na Mbilia Bel ambae sauti yake imo katika album ya mwisho ya Tabu Ley ‘Tempelo’ aliyoitoa mwaka 2006. Wengine katika muziki ni
 Pegguy Tabu, Abel Tabu, Philemon and Youssoupha Mabiki.
Youssoupha ni rapper anaeishi Paris, alizaliwa mwaka 1979 , mama yake alikuwa kutoka Senegal. Mwanae Marc Tabu ni mtangazaji kwenye TV moja huko Paris na ndie aliyetoa taarifa ya kwanza ya kifo cha baba yake kwenye ukurasa wake wa FACEBOO 2013.

No comments: