Thursday, December 5, 2013

UTAMU WA MAGITAA KATIKA BENDI ZETU- rythm guitar

Katika mfumo wa awali bendi, ambao uliigwa toka Cuba, zilikuwa zikitumia magitaa matatu, Solo, Rythm na Bass. Gitaa la solo lilikuwa na sauti ya juu huku rythm ikiwa na sauti nzito kidogo ya kati, na mwisho Bass likiwa na sauti nzito kuliko magitaa mengine. Kimuundo gitaa la rythm na la solo hakuna tofauti. Yote yana nyuzi 6,lakini katika kutyuni kwenye amplifier, gitaa la rythm hunyimwa treble kiasi na kuongezewa bass kiasi ili kuwa zito na si kali kama gitaa la solo, ambalo huwa na treble zaidi ya magitaa mengine, na pia hujitokeza zaidi. Inasemekana kaka yake Dr Nico Kasanda, ndie aliyeanzisha mtindo wa kuongeza gitaa la nne lililoitwa second solo, au wenyewe wakiliita Mi solo. Hili lilikuwa likipigwa kwa mifumo mbalimbali katika bendi mbali mbali. Bendi nyingine zilitumia second solo kama gitaa lililokuwa linajibizana na solo, na bendi nyingine lilikuwa linajibizana na rythm. Bendi ya Cuban Marimba chini ya Juma Kilaza liliongeza ubunifu na kuongeza gitaa la 5 na kuliita chord guitar. 
Leo tuzungumzie gitaa la rythm. Chombo hiki bado kinapigwa katika bendi nyingi lakini umaaarufu wake umeshuka sana. Katika kipindi cha miaka ya 60 na 70, gitaa hili lilikuwa na umuhimu mkubwa na wapigaji wake waliweza kubuni staili zao wenyewe na kufanya bendi kuwa na utamu tofauti na bendi nyingine. Kwa upande wa Kongo wapigaji kama Mpia Mongongo au Porthos wa Conca success ya Johhny Bokelo Isenge, Vata Mombasa wa Lipua lipua na wengine wengi kila moja alibuni staili yake na kufanya kila bendi kuwa na utamu tofauti, hapa kwetu  Satchmo, hilo ndio lilikuwa jina la kisanii la Harrison Siwale mpiga rythm wa Jamhuri Jazz, yeye alikuwa na staili peke yake ya kupiga rythm, sikumbuki kusikia mtu mwingine akipiga rythm ya aina yake kabla ya hapo. Rythm yake ilitawala nyimbo za Jamhuri wakati huo. Kumbuka wimbo kama Mganga no 1 na 2, au Blandina. Marehemu Mzee Kasim Kaluwona nae alikuwa na staili tofauti ya upigaji uliyoifanya Tabora Jazz kuwa na staili yake peke yake, kumbuka gitaa lake katika wimbo Asha, au Dada Lemmy. Charles Kazembe akiwa na Morogoro Jazz anakumbukwa katika upigaji wa rythm kwenye nyimbo kama Wajomba Wamechacha. Hao ni wachache tu kulikoweko na wengi marufu. Katika kipindi hiki huko Zaire kulikuwa na mipigo mbalimbali ya gitaa la rythm, ila kitu kipya kikaanzishwa ambapo katika ufungaji wa nyuzi ,wapiga rythm wakauondoa uzi namba nne na kuweka uzi namba moja, hivyo kukawa na nyuzi namba moja 2 katika gitaa, hapo ndipo akina Vata Mombasa wakaweza kuleta utamu mpya katika upigaji wa rythm. Wimbo wa Kumbora wa BAT ni wimbo ambao rythm ilipigwa kwa staili hiyo na nyimbo nyingi za wakati wa mwanzoni mwa miaka ya sabini zilipigwa na rythm iliyofungwa nyuzi za stail hiyo. Wakati huo Orchestra Kiam wakawa wanajivunia kupiga rythm kwa spidi kali sana,vibao kama Kamiki, Bomoto ni ushahidi wa kazi hizo. Utamu wa ufungaji wa nyuzi kwa staili hii uliweza kusikika vizuri katika gitaa lililopigwa mwanzo kabisa wa wimbo Andoya. Leo vionjo vya upigaji huo vinarudi kwa njia ya ajabu sana. Vikundi vya taarab vimeanza 'kuachia rythm' gitaa moja kubaki linapiga peke yake, japo wao hupiga gitaa la solo lakini staili wanayoipiga ni ya gitaa la rythm enzi ya miaka ya sabini. Jambo ambalo ni wazi watu bado wanapenda sana staili hiyo, japo bendi zinaonekana kuitupa staili hiyo. Siku hizi kelele huwa nyingi kiasi unaweza ukatembelea bendi 3 ukaona mtu anapiga gitaa la rythm lakini husikii, kwa hiyo hata thamani ya rythm katika bendi haipo, hata wanamuziki wanaojisifu kwa kupiga rythm ni wachache wengi hudai wao wapiga gitaa bila kutaja rythm kwani inaonekana ni chombo kisicho muhimu.

No comments: