Friday, December 20, 2013

UNAKIJUA KILICHOIUA ORCHESTRA SOSOLISO? ANGALIA NA VIDEO YA LIVE SHOW ZAO



Miaka ile ya mwanzoni ya 70, Kiamwangana Mateta Verckys, aliyejulikana kama mpiga sax mwenye mapafu ya chuma, alikuwa ndio katika umaarufu wa hali ya juu bendi yake ikitoa kibao baada ya kibao ambavyo vyote vilitingisha nchi yake ya Kongo na nchi za jirani, Tanzania ikiwa mojawapo. Kama methali ya Kiswahili isemayo ‘ngoma ikivuma sana hupasuka’ ndicho kilichotokea kwa bendi yake ya Orchestre Veve, waimbaji wake nyota watatu wakaona wanabanwa, wakachoropoka na kuanzisha kundi lao.  Matadidi " Buana Kitoko " Mario, Bonghat Tshekabu "Saak Sakoul" na Masengo Djeskain Loko,          ( labda niseme hapa bendi ya Mapacha Watatu ilipoanza nilikuwa napata kumbukumbu ya kundi hili, kuna mengi walifanana). Nyota hawa wakaanzisha bendi walioiita Orchestra Sosoliso Trio Madjesi . Bendi hii changa ilipata umaarufu mkubwa mara baada ya kuanza. Maonyesho ya Trio Madjesi kwenye maeneo kama vile Place de la Voix du Zaire au maeneo ya Itaga katikati ya jiji la Kinshasa ilikuwa moto chini, watu waliumizana kwa  kujazana kwenye maonyesho ya hawa vijana, kuna siku walikuwa wanafanya onyesho, na kundi la vijana wakawa wamepanda kwenye paa la kanisa la Mtakatifu Andrew  maeneo ya Mature, ili wawaangalie, paala kanisa likavunjika, kukaweko na majeruhi na inasemekana hata vifo. 
Trio Madjes na Sosoliso wakaendelea kuwasha moto na vipao vyao, wakaanza kupata mialiko hata nje ya Kongo. Wakongwe wa muziki wa Kongo hawakufurahia umaarufu wa ghafla waliokuwa wakipata hawa vijana, wakaapa lazima kulimaliza kundi hili, na hasa kundi lilipopata mwaliko wa kukaribishwa Paris na kupiga katika ukumbi wa Olympia, wazee waliokuwa wakijiita  the Three Musketeers Luambo Makiadi Franco, Tabu Ley Rochereau na Kiamwangana Mateta Verckys wakaona kama vile utawala wao katika muziki wa Kongo unataka kuingiliwa na mpango ukaundwa wa kuimaliza Sosoliso. Katibu mipango mmoja akapenyezwa kwa ujanja na kujiunga na bendi hii, hivyo wazee wakawa wanapata kila plani inayofanywa na vijana hawa.
Siku moja Trio Madjesi wakakaribishwa kwenye onyesho walilolifanya Bangui CAR, walipolipwa fedha zao kwa pesa ya Kifaransa, wakaamua kubadilisha fedha zao kuwa za Zaire kwa njia ya magendo badala ya kutumia benkii ya Zaire ili wapate fedha nzuri, jambo ambalo lilikuwa ni kosa la jinai. Three Musketeers wakapewa taarifa, haraka sana mambo yakasukwa na chama cha wanamuziki cha Kongo wakati huo kikiitwa UMUZA-Union des Musiciens du Zaïre kikatoa adhabu ya kuifungia bendi ya Sosoliso na viongozi wake kutofanya shughuli za muziki kwa miezi sita, safari ya Paris ikafa na mwanzo wa mwisho wa Sosoliso ukawadia.
Baada ya muda Matadidi Mario akaamua kurudi kwao Angola. Loko Masengo akahamia Congo Brazzaville, Saak Sakoul akapanda ndege na kuelkea Ufaransa. Wanamuziki nao wakasambaratika mpiga gitaa Makoso akajiunga na TP OK Jazz . Katibu Mipango aliyeimaliza bendi, Manzenza Nsalamu Nsala akarudi kwa  Luambo Makiadi kamaliza kazi aliyotumwa.

No comments: