Friday, December 20, 2013

UNAKIJUA KILICHOIUA ORCHESTRA SOSOLISO? ANGALIA NA VIDEO YA LIVE SHOW ZAO



Miaka ile ya mwanzoni ya 70, Kiamwangana Mateta Verckys, aliyejulikana kama mpiga sax mwenye mapafu ya chuma, alikuwa ndio katika umaarufu wa hali ya juu bendi yake ikitoa kibao baada ya kibao ambavyo vyote vilitingisha nchi yake ya Kongo na nchi za jirani, Tanzania ikiwa mojawapo. Kama methali ya Kiswahili isemayo ‘ngoma ikivuma sana hupasuka’ ndicho kilichotokea kwa bendi yake ya Orchestre Veve, waimbaji wake nyota watatu wakaona wanabanwa, wakachoropoka na kuanzisha kundi lao.  Matadidi " Buana Kitoko " Mario, Bonghat Tshekabu "Saak Sakoul" na Masengo Djeskain Loko,          ( labda niseme hapa bendi ya Mapacha Watatu ilipoanza nilikuwa napata kumbukumbu ya kundi hili, kuna mengi walifanana). Nyota hawa wakaanzisha bendi walioiita Orchestra Sosoliso Trio Madjesi . Bendi hii changa ilipata umaarufu mkubwa mara baada ya kuanza. Maonyesho ya Trio Madjesi kwenye maeneo kama vile Place de la Voix du Zaire au maeneo ya Itaga katikati ya jiji la Kinshasa ilikuwa moto chini, watu waliumizana kwa  kujazana kwenye maonyesho ya hawa vijana, kuna siku walikuwa wanafanya onyesho, na kundi la vijana wakawa wamepanda kwenye paa la kanisa la Mtakatifu Andrew  maeneo ya Mature, ili wawaangalie, paala kanisa likavunjika, kukaweko na majeruhi na inasemekana hata vifo. 
Trio Madjes na Sosoliso wakaendelea kuwasha moto na vipao vyao, wakaanza kupata mialiko hata nje ya Kongo. Wakongwe wa muziki wa Kongo hawakufurahia umaarufu wa ghafla waliokuwa wakipata hawa vijana, wakaapa lazima kulimaliza kundi hili, na hasa kundi lilipopata mwaliko wa kukaribishwa Paris na kupiga katika ukumbi wa Olympia, wazee waliokuwa wakijiita  the Three Musketeers Luambo Makiadi Franco, Tabu Ley Rochereau na Kiamwangana Mateta Verckys wakaona kama vile utawala wao katika muziki wa Kongo unataka kuingiliwa na mpango ukaundwa wa kuimaliza Sosoliso. Katibu mipango mmoja akapenyezwa kwa ujanja na kujiunga na bendi hii, hivyo wazee wakawa wanapata kila plani inayofanywa na vijana hawa.
Siku moja Trio Madjesi wakakaribishwa kwenye onyesho walilolifanya Bangui CAR, walipolipwa fedha zao kwa pesa ya Kifaransa, wakaamua kubadilisha fedha zao kuwa za Zaire kwa njia ya magendo badala ya kutumia benkii ya Zaire ili wapate fedha nzuri, jambo ambalo lilikuwa ni kosa la jinai. Three Musketeers wakapewa taarifa, haraka sana mambo yakasukwa na chama cha wanamuziki cha Kongo wakati huo kikiitwa UMUZA-Union des Musiciens du Zaïre kikatoa adhabu ya kuifungia bendi ya Sosoliso na viongozi wake kutofanya shughuli za muziki kwa miezi sita, safari ya Paris ikafa na mwanzo wa mwisho wa Sosoliso ukawadia.
Baada ya muda Matadidi Mario akaamua kurudi kwao Angola. Loko Masengo akahamia Congo Brazzaville, Saak Sakoul akapanda ndege na kuelkea Ufaransa. Wanamuziki nao wakasambaratika mpiga gitaa Makoso akajiunga na TP OK Jazz . Katibu Mipango aliyeimaliza bendi, Manzenza Nsalamu Nsala akarudi kwa  Luambo Makiadi kamaliza kazi aliyotumwa.

Friday, December 13, 2013

GURUMO 53-TAMASHA LA KUSTAAFU MUHIDIN MAALI GURUMO

Wanamuziki kadhaa wenye heshima katika muziki wa dansi watakuweko katika Tamasha la Gurumo 53, ambalo ni tamasha la kustaafu muziki  mwanamuziki mkongwe Muhidin Maalim Gurumo. Kati ya wanamuziki watakao panda jukwaani ni  Komandoo Hamza Kalala, Mzee Makassy, wanamuziki nyota waliowahi kutamba na bendi ya DDC Mlimani Park , Cosmas Chidumule, Abdallah Gama, Hussein Jumbe, Mashaka Shaaban, Kalamazoo, Henry Mkanyia na Karama Legesu. Wengine ni Ali Yahaya na Boniface Kachala, Tshimanga Kalala Assossa, Shaaban Lendi na Ibrahim Mwinchande. Pia wapulizaji wakongwe Majengo na King Maluu watakuweko na wote kwa pamoja wataporomosha show kubwa Jumamosi hii ndani ya TCC Club Chang’ombe. Wakali hao  jana Alhamisi walihitimisha mazoezi ya nyimbo tano watakazopiga katika tamasha hilo. Mazoezi hayo makali yalifanyika Amana Club ambako kwa wiki nzima wanamuziki watakaoshiriki tamasha hilo wamekuwa wakikutana hapo na kupiga mazoezi ya kufa mtu. Baadhi ya nyimbo zilizofanyiwa mazoezi ni  pamoja na “Selina” utunzi wake Gurumo kwa kushirikiana na marehemu Joseph Mulenga, “Barua kutoka kwa Mama” uliotungwa na Cosmas Chidumule na “Gama” (Tshimanga Kalala Assossa). Tamasha la Gurumo 53 ni maalum kwa ajili ya kuhitimisha miaka 53 ya utumishi uliotukuka katika muziki wa dansi kwa Muhidin Maalim Gurumo ambaye ametangaza rasmi kustaafu muziki. Wasanii wengine wanaoshiriki mazoezi hayo ni Miraji Shakashia, Hafsa Kazinja, Juma Katundu, Edo Sanga. Burudani zingine zitakazokuwepo siku hiyo ni pamoja na bendi za Msondo Ngoma Music Band, Talent Band, na Twanga Pepeta.

Sunday, December 8, 2013

MZEE CHEKECHA HATUNAE TENA


WAPENZI WA MAQUIS WATAMKUMBUKA MKONGWE HUYU MZEE MWEMA ALIYEKUJA FAHAMIKA ZAIDI KAMA MZEE CHEKECHA.
PICHA MBILI HAPO JUU NI ZA MZEE CHEKECHA AKIWA KWENYE MAZISHI YA KABEYA BADU MIEZI MICHACHE ILIYOPITA. HABARI ZILIZOTUFIKIA PUNDE NI KUWA MZEE ALIFIA HOSPITALI YA AMANA SIKU YA IJUMAA  TAREHE 6 DESEMBA NA KUZIKWA MAKABURI YA MAGOMENI KAGERA
MUNGU AILAZE PEMA PEPONI ROHO YA MZEE MWEMA MUDJANGA

Friday, December 6, 2013

UPANGA NI ENEO MUHIMU KATIKA HISTORIA YA MUZIKI WA TANZANIA Jeff


Jeff kwa sasa yuko Mlimani Park Orchestra
Upanga ni eneo muhimu sana katika historia ya muziki Tanzania. Hata katika miaka ya karibuni kulizuka kilichoitwa East Coast, muungano fulani wa wasanii wa Bongoflava toka maeneo ya Upanga, hii haikuwa mara ya kwanza kwa Upanga kuwa na wanamuziki waliotingisha mji. Enzi hizo za muziki wa soul, vijana wa Upanga walilipa eneo hili la mji jina la Soulville.Kwenye kona ya barabara ya Mindu na United Nations, nyumbani kwa familia ya Jengo, hapo ndipo palikuwa mahala pa mazoezi pa kundi lile la Groove Makers. Baadhi ya wanamuziki wa kundi hili walikuwa Mohamed Maharage, Joseph Jengo, Emmanuel Jengo, Herbert Lukindo, Willy Makame, na mpiga Drums ambae mpaka leo yupo katika anga za muziki Jeff. Kipindi hiki kilikuwa ni wakati wa muziki wa soul na kundi hili lilikuwa kundi la ubora wa juu wakati huo. Upanga ilikuwa na kundi jingine The Strokers, hili lilikuwa na awamu mbili, awamu ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Donald Max, David Max, Harry Chopeta, Vincet Chopeta, Pino Makame na Ochiwa na Freddy Lukindo.

Awamu ya pili ya kundi hili lilkuwa na Sajula Lukindo,Onesmo Kibira,Innocent Galinoma,Ben Galinoma, Denis Pad,Francis Kasambala,Vicent na Harry Chopeta, Ally Mwarabu, Sabri Mmanga na wengineo. Barlocks ni Bendi nyingine i
liyochipukia Upanga, jina la Barlockslilitokana na kuweko kwa kundi laBarkeys ambalo leo linaitwa Tanzanites.Barlocks walikuwa wakitumia vyombo vya Barkeys kwani kwa wakati huo bendi hizi zilikuwa kama mkubwa na mdogo. Barlocks hiyo ya awamu ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Jimmy Jumba,Pimbi Sokoine, huyu alipewa jina la utani Pimbi kutokana na kuwa mrefu sana, Said Mbonde kaka yake Amina Mbonde mwanamuziki mwingine muimbaji,Sajula Lukindo, Abraham. Kulikuweko na makundi mengine mengi hapo Upanga, kamaWhite HorseAquarius hapa walikuweko producer maarufu Hendrico Figueredo, Joe Ball,Joel De Souza, Mark De Souza,Roy Figueredo, Yustus Pereira,Mike De Souza. Baadhi ya wanamuziki wake walienda na kuungana na wengine Arusha na kuvuma sana na kundi la Crimson Rage, baadae wakarudi Dar na kujiita Strange. Baadhi ya kumbi walizokuwa wakipiga zilikuwa DI, Marine,Gymkhana,Maggot, St Joseph na kwenye shule mbalimbali. 
(Picha ya juu-Emmanuel 'Emmy' Jengo, Joseph 'Joe' Jengo, Herbert 'Herby' Lukindo. Kati-Jeff 'Funky' nyuma yake ni Willy Makame. Picha ya chini Willy Makame)

Thursday, December 5, 2013

UTAMU WA MAGITAA KATIKA BENDI ZETU- rythm guitar

Katika mfumo wa awali bendi, ambao uliigwa toka Cuba, zilikuwa zikitumia magitaa matatu, Solo, Rythm na Bass. Gitaa la solo lilikuwa na sauti ya juu huku rythm ikiwa na sauti nzito kidogo ya kati, na mwisho Bass likiwa na sauti nzito kuliko magitaa mengine. Kimuundo gitaa la rythm na la solo hakuna tofauti. Yote yana nyuzi 6,lakini katika kutyuni kwenye amplifier, gitaa la rythm hunyimwa treble kiasi na kuongezewa bass kiasi ili kuwa zito na si kali kama gitaa la solo, ambalo huwa na treble zaidi ya magitaa mengine, na pia hujitokeza zaidi. Inasemekana kaka yake Dr Nico Kasanda, ndie aliyeanzisha mtindo wa kuongeza gitaa la nne lililoitwa second solo, au wenyewe wakiliita Mi solo. Hili lilikuwa likipigwa kwa mifumo mbalimbali katika bendi mbali mbali. Bendi nyingine zilitumia second solo kama gitaa lililokuwa linajibizana na solo, na bendi nyingine lilikuwa linajibizana na rythm. Bendi ya Cuban Marimba chini ya Juma Kilaza liliongeza ubunifu na kuongeza gitaa la 5 na kuliita chord guitar. 
Leo tuzungumzie gitaa la rythm. Chombo hiki bado kinapigwa katika bendi nyingi lakini umaaarufu wake umeshuka sana. Katika kipindi cha miaka ya 60 na 70, gitaa hili lilikuwa na umuhimu mkubwa na wapigaji wake waliweza kubuni staili zao wenyewe na kufanya bendi kuwa na utamu tofauti na bendi nyingine. Kwa upande wa Kongo wapigaji kama Mpia Mongongo au Porthos wa Conca success ya Johhny Bokelo Isenge, Vata Mombasa wa Lipua lipua na wengine wengi kila moja alibuni staili yake na kufanya kila bendi kuwa na utamu tofauti, hapa kwetu  Satchmo, hilo ndio lilikuwa jina la kisanii la Harrison Siwale mpiga rythm wa Jamhuri Jazz, yeye alikuwa na staili peke yake ya kupiga rythm, sikumbuki kusikia mtu mwingine akipiga rythm ya aina yake kabla ya hapo. Rythm yake ilitawala nyimbo za Jamhuri wakati huo. Kumbuka wimbo kama Mganga no 1 na 2, au Blandina. Marehemu Mzee Kasim Kaluwona nae alikuwa na staili tofauti ya upigaji uliyoifanya Tabora Jazz kuwa na staili yake peke yake, kumbuka gitaa lake katika wimbo Asha, au Dada Lemmy. Charles Kazembe akiwa na Morogoro Jazz anakumbukwa katika upigaji wa rythm kwenye nyimbo kama Wajomba Wamechacha. Hao ni wachache tu kulikoweko na wengi marufu. Katika kipindi hiki huko Zaire kulikuwa na mipigo mbalimbali ya gitaa la rythm, ila kitu kipya kikaanzishwa ambapo katika ufungaji wa nyuzi ,wapiga rythm wakauondoa uzi namba nne na kuweka uzi namba moja, hivyo kukawa na nyuzi namba moja 2 katika gitaa, hapo ndipo akina Vata Mombasa wakaweza kuleta utamu mpya katika upigaji wa rythm. Wimbo wa Kumbora wa BAT ni wimbo ambao rythm ilipigwa kwa staili hiyo na nyimbo nyingi za wakati wa mwanzoni mwa miaka ya sabini zilipigwa na rythm iliyofungwa nyuzi za stail hiyo. Wakati huo Orchestra Kiam wakawa wanajivunia kupiga rythm kwa spidi kali sana,vibao kama Kamiki, Bomoto ni ushahidi wa kazi hizo. Utamu wa ufungaji wa nyuzi kwa staili hii uliweza kusikika vizuri katika gitaa lililopigwa mwanzo kabisa wa wimbo Andoya. Leo vionjo vya upigaji huo vinarudi kwa njia ya ajabu sana. Vikundi vya taarab vimeanza 'kuachia rythm' gitaa moja kubaki linapiga peke yake, japo wao hupiga gitaa la solo lakini staili wanayoipiga ni ya gitaa la rythm enzi ya miaka ya sabini. Jambo ambalo ni wazi watu bado wanapenda sana staili hiyo, japo bendi zinaonekana kuitupa staili hiyo. Siku hizi kelele huwa nyingi kiasi unaweza ukatembelea bendi 3 ukaona mtu anapiga gitaa la rythm lakini husikii, kwa hiyo hata thamani ya rythm katika bendi haipo, hata wanamuziki wanaojisifu kwa kupiga rythm ni wachache wengi hudai wao wapiga gitaa bila kutaja rythm kwani inaonekana ni chombo kisicho muhimu.

SHAW HASSAN SHAW RWAMBOH..MPIGA KINANDA MKONGWE

Shaw Hassan Shaw
Kwa wapenzi wa Vijana Jazz wanakumbuka vile vipande vya kinanda vilivyokuwa vikianzisha zile nyimbo mbili alizokuwa akiimba Kida Waziri, Penzi Haligawanyiki na Shingo feni, mpigaji wake alikuwa Shaw Hassan Shaw Rwamboh. Mwanamuziki huyu alizaliwa tarehe 25 September 1959, Dar Es Salaam. Alianza kujifunza kupiga gitaa na wenzie kando ya Ziwa Tanganyika huko Kigoma, wakitumia magitaa ya tajiri mmoja aliyekuwa na meli ya uvuvi. Alipokuja Dar es Salaam akakutana na mwanamuziki Zahir Ally Zorro, Zahir ndiye aliyeboresha upigaji wake wa gitaa kiasi cha kukubaliwa na Patrick Balisidya kupiga gitaa la rythm katika bendi yake ya pili PAMA Band, chini ya Afro70.
Hassan Shaw wa kwanza kulia aliyenyoosha mkono. Mwendeshaji wa blog hii John Kitime wa kwanza aliyesimama kushoto. Hapa wakiwa Stadium Morogoro.
Ni chini ya malezi ya Patrick alipojifunza kupiga Keybords (Kinanda). Baada ya hapo aliacha muziki na kujiunga na Dar Technical College. Lakini 1980 alijiunga na Vijana Jazz kama mpiga Keyboards, alishirikiana na wanamuziki wengi lakini wengi kwa mapenzi ya Mungu,  wametangulia mbele ya haki. Baadhi ya waliobaki kati ya aliyokuwa nao wakati huo ni John Kitime, Kida Waziri, Saad Ally Mnara, Hamisi Mirambo, Huluka Uvuruge, Hassan Dalali, Hamza Kalala na Rashid Pembe. Mwaka 1990 alijiunga na Orchestra Safari Sound, chini ya Maalim Muhidin Gurumo (MJOMBA), na Marehemu Abel Baltazar, hapa alikutana na wanamuziki kama Benno Villa Anthony na Mhina Panduka (Toto Tundu) .Aliacha bendi baada ya miezi sita tu, mwenyewe anasema, ‘….kutokana na muhusika kutozingatia mkataba wangu…’. Alihamia Zanzibar na kujiunga na bendi iliyokuwa ikipiga Mawimbini Hotel, hakukaa sana kwani Washirika Tanzania Stars walimwita. Hapa akakutana na mwalimu wake wa gitaa Zahir Ally, Ally Choki, Musemba wa Minyugu,Tofi Mvambe, Abdul Salvador na wengine, ilitokea kutoelewana baina ya wanamuziki na yeye kama kiongozi wa bendi ilibidi aachie ngazi kuepusha bendi kuzidi kujichanganya. Baada ya hapo Kanku Kelly ambaye ni mume wa dada wa mke wake alimuita ajiunge na Kilimanjaro Connection Band. Anasema Kanku alimvumilia sana kwa kuwa alikuwa hajawahi kufanya kazi ya kukopi nyimbo za wanamuziki wengine wakubwa duniani, hatimae akaweza kujiendeleza na kuweza kumudu kupiga vitu vikubwa, bendi hii ya Kanku  ilikua inazunguka kwa kupiga muziki hotel mbalimbali katika nchi za Malaysia, Singapore, Indonesia, Thailand na Japan jambo ambalo lilifanya aone kila kitu ni kigeni kila alipokwenda. Katika bendi hiyo alishirikiana na akina Kanku Kelly, Mafumu Bilal, Maneno Uvuruge, Burhan Adinan, Shomari Fabrice, Bob Sija, Fally Mbutu, Raysure boy, Delphin Mununga na Kinguti System. Baadaye Shaw, Kinguti na Burhan Muba waliamua kuanzisha kundi dogo wakitumia sequencer keyboards na kumuaga Kanku Kelly. Group hili lilijiita Jambo Survivors Band, bendi ambayo itakumbukwa  kwa ule wimbo Maprosoo ulioimbwa na MlasiFeruzi ambao uliokuwa katika album ya MAPROSOO.
Mlasi feruzi
Baada ya hapo bendi ikaanza kuzunguka nchi mbalimbali ikipiga katika mahotelini. Wameshapita Oman , Fujairah, U.A.E, Singapore, Malaysia na sasa wapo Thailand. Shaw anasema wanamuziki ambao hatawasahau kwa kuwa wamemfikisha alipo ni Zahir Ally Zorro, Marehem Patrick Balisdya, Waziri Ally, Kinguti System, Burhan Muba na Kanku Kelly. Kituko ambacho hawezi kusahau ni nchini Malasyia wakati akiwa na Kanku Kelly na ikiwa ni mara ya kwanza kwake kupiga muziki akiwa amezungukwa na watu weupe watupu. Anasema nyimbo zote zilipotea kichwani akawa hakumbuki hata nyimbo moja aliyokuwa kafanyia mazoezi

BENDI ZA UPANGA- THE GROOVEMAKERS

Picha hii ina maana nyingi kwa wapenzi wa Groove Makers. Hapa ni wakali wawili wa GrooveMakers wakiwa katika mazoezi ya Karate. Hakuna zawadi kwa kuwataja japo itakuwa vizuri kupata taarifa ya kipindi hiki. MMOJA NI BALOZI MWENYE HESHIMA KUBWA NCHINI.

BENDI ZILIZOANZIA UPANGA- THE STROKERS


The Strokers, hili lilikuwa kundi jingine la wanamuziki wa Upanga. The Strokers lilikuwa na awamu mbili, ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Donald Max, David Max, Harry Chopeta, Vincet Chopeta, Pino Makame na Ochiwa na Freddy Lukindo. Awamu ya pili ya kundi hili ilikuwa na Sajula Lukindo,Onesmo Kibira,Innocent Galinoma,Ben Galinoma, Denis Pad,Francis Kasambala,Vicent na Harry Chopeta, Ally Mwarabu, Sabri Mmanga na wengineo. Pichani ni awamu ya kwanza ya Strokers. Waliosimama, Pino Makame, Freddie Lukindo, David Max. Waliokaa (?),Harry Chopeta, Vincet Chotepa.

Wednesday, December 4, 2013

MOKOLO NA KOKUFA ULITUNGWA NA NANI?



Kuna kitendawili kikubwa cha nani alitunga wimbo wa Mokolo Nakokufa  kuna wanosema ni wimbo uliotungwa na  Wendo Kolosay maarufu kama Papa Wendo na aliuimba mwaka 1966  kwenye msiba wa Paul Mwanga kule Kongo Brazzaville, na aliyempigia gitaa alikuwa Honoré Liengo. Rochereau  alikuweko siku hiyo na akamkaribisha Mzee Wendo auimbe wimbo huo na African Fiesta National. Kwa kuwa Wendo alikuwa na matatizo ya fedha wakati huo akakubali haraka, na Rochereau akamuahidi Wendo kuwa atampa haki zake zote za utunzi, hatimae Rochereau akaurekodi wimbo huo kwa jina lake na arrangement yake, hili ni jambo ambalo hujitokeza mara nyingi katika bendi za Afrika ambapo kiongozi huweka jina lake katika tungo zilizorekodiwa. Wendo aliendelea kuweko katika kundi la Africana Fiesta National kwa miaka miwili mpaka pale lilipotokea kasheshe Brussels Ubelgiji  baada ya bendi kuwa huko kwa mualiko wa ubalozi wa Kongo na bendi kutapeliwa malipo ya safari hiyo, Rochereau akawaacha wanamuziki wengine huko wasijue la kufanya moja wapo alikuwa Mzee Wendo, na ndipo Wendo akaiacha bendi hiyo na  akajiunga na mwanamuziki mwingine maarufu Dewayon.Mpaka mwaka 1990 alipokuwa akiulizwa ni utunzi wake gani alioupenda kuliko wote, Mzee Wendo daima alikuwa akisema Mokolo  Nakokufa.
Sam Mangwana alikuwa mmoja ya wanamuziki waliokuweko African Fiesta National wakati Wendo alipokuja kujiunga na kundi hilo, nae alipourekodi wimbo huu tena aliandika mtunzi ni Wendo kolosay.  Unaweza kuusikiliza wimbo huu version ya Sam Mangwana na maelezo ya ziada kupitia link hii http://www.rdctube.com/mokolo-nakokufa-minha-angola-sam-mangwana/

Huyu Wendo Kolosoy ni nani?

Antoine Wendo Kolosoy (alizaliwa tarehe 25 Aprili mwaka 1925 na kufariki July 28 mwaka 2008).  Wendo alizaliwa wilaya ya Mai-Ndombe magharibi ya Kongo. Alipofikisha umri wa miaka saba baba yake alifariki na muda mfupi baadae mama yake ambaye nae alikuwa muimbaji akafariki pia, hivyo Wendo akapelekwa kuishi katika kituo cha watoto yatima kilichokuwa kikiendeshwa na Society of the Missionaries of Africa. Akiwa na umri wa miaka 11 akaanza kupiga gitaa, lakini alipofikisha umri wa miaka 12/13 akafukuzwa katika kituo hicho kutokana na kutunga nyimbo ambazo hazikuwapendeza wafadhili wake akaanza kupiga muziki wa kuburudisha wasafiri katika pantoni  zilizokuwa zikifanya kazi katika Mto Kongo.  Pamoja na kuwa alibatizwa kwa jina la Antoine Kalosoyi, alipewa jina la Wendo kutokana na jina la mmoja wa watawala wa Uingereza aliyeitwa Duke of Windsor, hilo Windsor lilianza kubadilika na kuwa Wendo Sor na hatimae Wendo peke yake kubakia. Na katika utu uzima wake alikuja kuitwa Papa Wendo. Kwenye mwaka 1941 alianza kupiga muziki katika jiji la Leopordville (Kinshasa) akiwa na bendi yake ya Victoria Bakolo Miziki na wakati huo akakutana mmoja ya wale ndugu wawili wa Kigiriki walioanzisha record label ya kwanza Kongo, Nicolas Jeronimidis na kukubaliana kutoa nyimbo zake chini ya label ya Ngoma. Mwaka 1948 akiwa na mpiga gitaa Henri Bowane walifyatua kibao ambacho kiliweza kupata umaarufu hata nje ya Kongo, kibao hicho  kiliitwa Marie-Louise, kibao hiki kilipendwa sana katika nchi za Afrika Magharibi. Wendo aliendelea kuimba nyimbo nyingi kwa lugha mbalimbali ikiwemo Kiswahili.  Kwa kipindi kirefu sana Wendo alipotea katika ulimwengu wa  muziki japo kwa muda alikuweko African Fiesta National akiwa na Tabu Ley na Sam Mangwana. 

Baada ya Laurent Kabila na baadae mwanae Joseph Kabila kushika madaraka Kongo walimsaidia  mzee huyu kuanza kurekodi tena na kuanza kufanya maonyesho. Nilibahatika kukutana nae Ivory Coast mwaka 1998 wakati wa tamasha la MASA Cultural Festival akiwa na kundi lake alilokuwa bado akiliita Victoria Bakolo Miziki. Onyesho lake la mwisho alilifanya mwaka 2004 na hatimae kufariki 2008.