FRANKLIN alikuwa mtoto wa mwanamuziki Aubin Boukaka wa kundi la "The Gaiety ", na mkewe Yvonne Ntsatouabaka aliyekuwa MC maarufu kwenye misiba na pia alikuwa mwanamuziki muimbaji. François Boukaka aliyekuja julikana kama Franklin alizaliwa tarehe 10 Oktoba, 1940. Yeye ndie alikuwa mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wanane wavulana watatu na wasichana watano. Elimu yake yote aliipata katika shule mbalimbali nchini kwake Congo Brazzaville. Franklin alianza mambo ya muziki 1955 katika kundi lililojiita Sexy Jazz lililoongozwa na Miguel Samba, baadae akaanzisha kundi la Negro Band. Hatimae katika safari yake ya muziki akaungana na wakali wengine kama Edo Clary Lutula, Jeannot Bombenga, Tabu Ley , Mutshipile "Casino", André Kambite " Damoiseau ", Papa Bouanga, Charles Kibongue katika lile kundi maarufu la African Jazz, sauti ya Franklin imo katika nyimbo kama Mwana mawa , Catalina cha cha na Marie José zilizotungwa na Tabu Ley. Mwaka 1959 kundi la African Jazz lilimeguka baada ya wanamuziki wengine walipohamia Brussels wakifuatana na wanasiasa wa Kongo kwenye mazungumzo ya awali ya uhuru wa Kongo. Wanamuziki wote waliobaki akiwemo Jeannot Bombenga, kasoro Tabu Ley wakajiunga na kuanzisha kundi jingine lililotingisha Africa lililoitwa Vox Africa, Franklin Boukaka na Jeannot Bombenga wakiimba. Baada ya hapo Franklin akaaliacha kundi hili na kurudi kwao Brazzaville ambako 1962 akawa mmoja wa wanamuziki wa Cercul Jazz, band iliyoanza miaka ya 50 ikiwa chini ya chama cha vijana kilichokuwa kikipata ufadhili wa serikali ya Ufaransa, chama hicho kiliitwa Cercule Culturel de Bacongo. Hatimae Boukaka alikuja kuwa kiongozi wa chama hiki na kikawa na umaarufu wa mkubwa. Wimbo wa bendi hiyo "Pont Sur le Congo" (Daraja juu ya Mto Congo), wimbo ambao ulikuwa una hamasisha kuunganika kwa Congo Kinshasa na Kongo Brazzaville baada ya nchi hizo kupata uhuru. Wimbo uliopata umaarufu kuliko nyimbo zote za bendi hiyo. Baadaye Franklin akiwa na gitaa lake kavu akaanzisha kikundi ambacho kilikuwa na wapiga marimba wawili akaweza kufanya ziara kadhaa hata nje ya nchi yake na kundi hili. Mwaka 1970 ndipo Boukaka alipo rekodi nyimbo 12 zilizopangwa vyombo na Manu Dibango na hapo ndipo nyimbo Nakoki na Le Bucheron zilipopatikana. Baada ya hapo Franklin alijiunga na wenzie waliotaka kuipindua serikali ya Congo Brazzaville wakati huo ikiwa chini ya Rais Marien Ngouabi(aliyetuletea suti za Ngwabi). Jaribio hilo lililofanyika tarehe 22 February 1972 lilishindwa na siku chache baadae kifo cha Boukaka kilitangazwa.
Tuesday, January 14, 2014
Saturday, January 11, 2014
WAKUMBUKE ORCHESTRA MAQUIS ORIGINAL MAY 1996 -VIDEO
June 1, 1996 Jumamosi kulifanyika Tamasha kubwa la muziki katika viwanja vya Mnazi Mmoja, ilikuwa ni kuhamasisha utunzaji wa mazingira. Huu ulikuwa wimbo mmoja wa Maquis katika matayarisho ya siku hiyo.
Friday, December 20, 2013
UNAKIJUA KILICHOIUA ORCHESTRA SOSOLISO? ANGALIA NA VIDEO YA LIVE SHOW ZAO
Miaka ile ya mwanzoni ya 70, Kiamwangana Mateta Verckys, aliyejulikana kama mpiga sax mwenye mapafu ya chuma, alikuwa ndio katika umaarufu wa hali ya juu bendi yake ikitoa kibao baada ya kibao ambavyo vyote vilitingisha nchi yake ya Kongo na nchi za jirani, Tanzania ikiwa mojawapo. Kama methali ya Kiswahili isemayo ‘ngoma ikivuma sana hupasuka’ ndicho kilichotokea kwa bendi yake ya Orchestre Veve, waimbaji wake nyota watatu wakaona wanabanwa, wakachoropoka na kuanzisha kundi lao. Matadidi " Buana Kitoko " Mario, Bonghat Tshekabu "Saak Sakoul" na Masengo Djeskain Loko, ( labda niseme hapa bendi ya Mapacha Watatu ilipoanza nilikuwa napata kumbukumbu ya kundi hili, kuna mengi walifanana). Nyota hawa wakaanzisha bendi walioiita Orchestra Sosoliso Trio Madjesi . Bendi hii changa ilipata umaarufu mkubwa mara baada ya kuanza. Maonyesho ya Trio Madjesi kwenye maeneo kama vile Place de la Voix du Zaire au maeneo ya Itaga katikati ya jiji la Kinshasa ilikuwa moto chini, watu waliumizana kwa kujazana kwenye maonyesho ya hawa vijana, kuna siku walikuwa wanafanya onyesho, na kundi la vijana wakawa wamepanda kwenye paa la kanisa la Mtakatifu Andrew maeneo ya Mature, ili wawaangalie, paala kanisa likavunjika, kukaweko na majeruhi na inasemekana hata vifo.
Trio Madjes na Sosoliso wakaendelea kuwasha moto na vipao vyao, wakaanza kupata mialiko hata nje ya Kongo. Wakongwe wa muziki wa Kongo hawakufurahia umaarufu wa ghafla waliokuwa wakipata hawa vijana, wakaapa lazima kulimaliza kundi hili, na hasa kundi lilipopata mwaliko wa kukaribishwa Paris na kupiga katika ukumbi wa Olympia, wazee waliokuwa wakijiita the Three Musketeers Luambo Makiadi Franco, Tabu Ley Rochereau na Kiamwangana Mateta Verckys wakaona kama vile utawala wao katika muziki wa Kongo unataka kuingiliwa na mpango ukaundwa wa kuimaliza Sosoliso. Katibu mipango mmoja akapenyezwa kwa ujanja na kujiunga na bendi hii, hivyo wazee wakawa wanapata kila plani inayofanywa na vijana hawa.
Siku moja Trio Madjesi wakakaribishwa kwenye onyesho walilolifanya Bangui CAR, walipolipwa fedha zao kwa pesa ya Kifaransa, wakaamua kubadilisha fedha zao kuwa za Zaire kwa njia ya magendo badala ya kutumia benkii ya Zaire ili wapate fedha nzuri, jambo ambalo lilikuwa ni kosa la jinai. Three Musketeers wakapewa taarifa, haraka sana mambo yakasukwa na chama cha wanamuziki cha Kongo wakati huo kikiitwa UMUZA-Union des Musiciens du Zaïre kikatoa adhabu ya kuifungia bendi ya Sosoliso na viongozi wake kutofanya shughuli za muziki kwa miezi sita, safari ya Paris ikafa na mwanzo wa mwisho wa Sosoliso ukawadia.
Baada ya muda Matadidi Mario akaamua kurudi kwao Angola. Loko Masengo akahamia Congo Brazzaville, Saak Sakoul akapanda ndege na kuelkea Ufaransa. Wanamuziki nao wakasambaratika mpiga gitaa Makoso akajiunga na TP OK Jazz . Katibu Mipango aliyeimaliza bendi, Manzenza Nsalamu Nsala akarudi kwa Luambo Makiadi kamaliza kazi aliyotumwa.
Friday, December 13, 2013
GURUMO 53-TAMASHA LA KUSTAAFU MUHIDIN MAALI GURUMO
Wanamuziki kadhaa wenye heshima katika muziki wa dansi watakuweko katika Tamasha la Gurumo 53, ambalo ni tamasha la kustaafu muziki mwanamuziki mkongwe Muhidin Maalim Gurumo. Kati ya wanamuziki watakao panda jukwaani ni Komandoo Hamza Kalala, Mzee Makassy, wanamuziki nyota waliowahi kutamba na bendi ya DDC Mlimani Park , Cosmas Chidumule, Abdallah Gama, Hussein Jumbe, Mashaka Shaaban, Kalamazoo, Henry Mkanyia na Karama Legesu. Wengine ni Ali Yahaya na Boniface Kachala, Tshimanga Kalala Assossa, Shaaban Lendi na Ibrahim Mwinchande. Pia wapulizaji wakongwe Majengo na King Maluu watakuweko na wote kwa pamoja wataporomosha show kubwa Jumamosi hii ndani ya TCC Club Chang’ombe. Wakali hao jana Alhamisi walihitimisha mazoezi ya nyimbo tano watakazopiga katika tamasha hilo. Mazoezi hayo makali yalifanyika Amana Club ambako kwa wiki nzima wanamuziki watakaoshiriki tamasha hilo wamekuwa wakikutana hapo na kupiga mazoezi ya kufa mtu. Baadhi ya nyimbo zilizofanyiwa mazoezi ni pamoja na “Selina” utunzi wake Gurumo kwa kushirikiana na marehemu Joseph Mulenga, “Barua kutoka kwa Mama” uliotungwa na Cosmas Chidumule na “Gama” (Tshimanga Kalala Assossa). Tamasha la Gurumo 53 ni maalum kwa ajili ya kuhitimisha miaka 53 ya utumishi uliotukuka katika muziki wa dansi kwa Muhidin Maalim Gurumo ambaye ametangaza rasmi kustaafu muziki. Wasanii wengine wanaoshiriki mazoezi hayo ni Miraji Shakashia, Hafsa Kazinja, Juma Katundu, Edo Sanga. Burudani zingine zitakazokuwepo siku hiyo ni pamoja na bendi za Msondo Ngoma Music Band, Talent Band, na Twanga Pepeta.
Wednesday, December 11, 2013
WANAMUZIKI WA KONGO WATAKA SIKU ALIYOFARIKI TABU LEY KUWA SIKU YA MAPUMZIKO KITAIFA..ANGALIA VIDEO
GOVERNOR WA KINSHASA ALITANGAZA SIKU ILE YA MAZISHI KUWA BARABARA YA TOMBALBAYE AVENUE SASA ITAITWA TABU LEY AVENUE
Sunday, December 8, 2013
MZEE CHEKECHA HATUNAE TENA
WAPENZI WA MAQUIS WATAMKUMBUKA MKONGWE HUYU MZEE MWEMA ALIYEKUJA FAHAMIKA ZAIDI KAMA MZEE CHEKECHA.
PICHA MBILI HAPO JUU NI ZA MZEE CHEKECHA AKIWA KWENYE MAZISHI YA KABEYA BADU MIEZI MICHACHE ILIYOPITA. HABARI ZILIZOTUFIKIA PUNDE NI KUWA MZEE ALIFIA HOSPITALI YA AMANA SIKU YA IJUMAA TAREHE 6 DESEMBA NA KUZIKWA MAKABURI YA MAGOMENI KAGERA
MUNGU AILAZE PEMA PEPONI ROHO YA MZEE MWEMA MUDJANGA
Subscribe to:
Posts (Atom)



