Wednesday, September 7, 2016

WESTERN JAZZ BAND MOJA YA BENDI ILIYOKUWA MAARUFU TANZANIA

Mzee Iddi Nhende ndiye aliyepata wazo la kuanzisha bendi maarufu ya Western Jazz. Iddi Nhende alianza muziki akiwa bado mdogo katika bendi ya shule alipokuwa Primary huko Nzega, mwaka 1944 alijiunga na Tabora Boys Secondary na hapa akajiunga na Brass Band ya shule ambapo alikuwa mpigaji wa Cornet. Alimaliza shule na kuja Dar es Salaam kujiunga na Chuo cha Afya, Sewa Haji Medical Training Center. Baada ya kumaliza mafunzo akaajiriwa Bohari ya madawa na kisha mwaka 1957 alihamishiwa Muhimbili. Upenzi wake wa muziki ulimfanya mwaka huohuo ajiunge na Rufiji Jazz Band kama mpiga trumpet, bendi hii wakati huo ilikuwa ikifanya maonyesho yake Minazini Community Centre iliyokuwa eneo linaloitwa siku hizi Mchikichini na pia walikuwa wakipiga muziki katika ukumbi wa Arnatougro.
Kutokana na miji kuwa ndio ilikuwa inaanza, watu wengi kutoka maeneo mbalimbali walihamia mijini na kujaribu kutafuta wenzao waliotoka sehemu moja na kuwa na vikundi vya kusaidiana au kuwaunganisha, watu wa sehemu mbalimbali walianzisha bendi wakazipa majina ya wanakotoka, hivyo waanzilishi wa Rufiji Jazz walitoka Rufiji, na ndivyo ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga jazz na kadhalika. Hivyo Iddi Nhende aliyekuwa ametoka Nzega akaamua kuanzisha bendi ya watu kutoka Magharibi, kwa kuwa nchi ilikuwa imegawanywa katika majimbo, yakiweko majimbo kama Northern Province, Southern Highlands Province, Western Province na kwa vile Nhende alitoka Western province akaanzisha Western Jazz Band 1959. Akanunua vyombo aina ya Grampian toka duka la Souza Junior duka la vyombo vya muziki lililokuwepo mtaa wa Mkwepu. Aliweza kupata fedha baada ya kuuza ng’ombe kadhaa wa mamake. Wakati huo katika bendi za aina yake ni Dar es Salaam Jazz Band peke yake waliokuwa na magitaa ya umeme, hivyo Nhende akawa na kazi ya kuwatafuta wapigaji ambapo alimfuata mpiga gitaa la umeme wa kwanza Haus Dibonde(Msukuma), aliyekuwa anapigia Dar es Salaam Jazz Band(hii ilikuwa chini ya Mzee Muba), baada ya hapo akawapata wanamuziki wengine kutoka Ulanga Jazz Band, wakati huo chombo cha banjo kilikuwa muhimu hivyo akamtafuta mpiga banjo toka Cuban Marimba tawi la Dar es Salaam. Cuban Marimba wakati huo ilikuwa na tawi Dar Es Salaam lililokuwa chini ya Mzee Mwaipungu. Mwaka mmoja baadae alipata transfer ya kwenda Morogoro, hivyo huku nyuma alilazimika kuongeza wasanii ili kuimarisha bendi wakati hayupo. Akampata David Makwaya mwimbaji, na Ally Rashid(huyu ameacha muziki karibuni akiwa Msondo), mpiga Saxaphone toka Zanzibar. Bahati mbaya yule mpiga gitaa Haus akapata kichaa katika mazingira yaliyohusishwa na ushirikina kutokana na ushindani wa bendi uliokuwepo. Hivyo basi walifuatwa wanamuziki watatu toka Tabora Jazz, wanamuziki hao walikuwa wametoka pamoja katika bendi iliyokuwa na makazi Mwanza ikiitwa Kimbo Twist Band na wakahamia Tabora Jazz, na kutoka hapo wakachukuliwa na Western Jazz. Wanamuziki hao walikuwa
Rashid Hanzuruni, Kassim Mponda na Omary Kayanda. Baada ya kazi nzuri sana, Hanzuruni Nae akarukwa na akili katika mazingira yale ya yule mpiga solo wa kwanza akalazimika kurudishwa Tabora ambako alikaa mpaka mauti yake. Wema Abdallah akachukua nafasi ya mpiga solo katika bendi ya Western. Tatizo la kinidhamu lilifanya Wema aondolewe Western, na mpigaji mwingine mzuri sana Shamba Abbdallah akachukua nafasi, solo la huyu bwana linasikika kwenye nyimbo ka Rosa na kadhalika.
Hall la nyumbani la Western Jazz lilikuwa Alexander Hall, ambalo lilikuja kuwa hall la DDC Kariakoo. Western walinunua drums baada ya Kilwa Jazz kununua drums na kuzipitisha kwao kuwaringia. Walinunua toka kwa bendi moja ya Wagoa iliyoitwa De Mello Brothers. Western walirekodi santuri kadhaa chini ya mkataba waliyousaini na lebo ya Phillips ya Kenya. Hatimae Western na mtindo wao wa Saboso walitoweka katika anga za muziki miaka ya mwisho ya sabini. Kati ya nyimbo zao nyingi ni hizi hapa; Rosa, Vigelegele, Jela ya Mapenzi, Helena no 1 na 2.

Friday, August 19, 2016

MAZISHI YA BI SHAKILA , YATAFANYIKA LEO MBAGALA CHARAMBE

Mazishi ya Bi Shakila yatakuwa leo Jumamosi 20 AGOSTI 2016. Mbagala Charambe, saa kumi alasiri Uwanja wa Ninja.
 Namna ya kufika msibani nyumbani kwa marehemu kwa kutumia daladala. Unapanda magari ya Mbagala Rangi Tatu, ukifika mwisho unachukua basi la Nzasa na unashuka Mnara wa Voda hapo unauliza kwa Bi Shakila utaonyeshwa

Sunday, August 7, 2016

LEO TUNATIMIZA MIAKA 12 TOKA KIFO CHA PATRICK BALISDYA


Jina Patrick Balisdya halitakuwa geni kabisa kwa wadau wa blog hii,lazima roho zimeanza kuwadunda kama inavyokuwa kwangu kila nikimkumbuka Blai. Patrick Pama Balisidya alizaliwa Mvumi Dodoma tarehe 18 April 1946. Kabila lake alikuwa Mgogo , kabila ambalo lina wanamuziki wengi maarufu kutokana na muziki kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kabila hilo. Mama yake alikuwa anapiga kinanda kanisani na hivyo basi kutokana na asili ya kabila lake na pia kutokana na mama yake, hakika huyu angeweza kujisifu kuwa muziki uko katika damu yake. Mdau mmoja alitutaarifu kuwa Balisidya alikuwa kiongozi wa Bendi ya shuleni kwake Dodoma secondary School. Ambapo kutoka hapo alijiunga na Chuo cha Ufundi , na baada ya kumaliza mafunzo alifanya kazi hiyo kwa muda na 1967 akawa tayari anapiga muziki Dar Es Salaam Jazz B. Kufikia mwaka 1970 Patrick alikuwa ameanzisha kikosi chake mwenyewe Afro70, kikiwa na mtindo wake Afrosa. Alikuwa mbunifu katika muziki wake, na kwa muda mrefu alikwepa sana kuingia katika wimbi la kufuata mapigo ya Kikongo kitu ambacho hata wakati huo bendi nyingi zilikifanya, japokuwa kukutana na Franco wakati alipofanya moja ya ziara zake nchini humu kulimfanya abadili mtindo kwa kipindi kifupi na katika nyimbo moja wapo aliiga kabisa solo la Franco alilolipiga kwenye wimbo wake Georgette. Afro70 iliwakilisha wanamuziki wa Tanzania katika maonyesho ya mtu mweusi Lagos, Nigeria. (FESTAC festival 1977). Vyombo alivyotumia katika maonyesho haya vilimsumbua akili mpaka alipofariki, kwani muda mchache kabla ya Festac, wakati huo serikali ikiwa imeshamtaarifu kuwa ndie atakuwa mwakilishi wa Tanzania, vyombo vyake vyote vilihalibika katika ajali ya gari. Serikali ilikuwa imenunua vyombo vipya kwa ajili ya bendi yake ya Wizara ya Utamaduni wakati huo, ambavyo siku zote Balisdya alisema aliambiwa ni vyake baada ya maonyesho. Aliporudi kutoka Nigeria Kiongozi mwingine wa serikali aliamuliwa arudishe hivyo vyombo virudishwe serikalini na kwa kitendo kile kutangaza kifo cha Afro70. Vyombo hivyo vilitumika kuanzisha bendi ya Asilia Jazz ambayo ilikuwa Bendi ya Wizara ya Utamaduni na Vijana. Balisdya alitumia muda mwingi kujaribu kudai haki yake hiyo ambayo ilimkwepa mpaka mwisho wa maisha. Mwaka 1979, Balisidya alikwenda Sweden na kushirikiana na kikundi cha Archimedes akatoa album nzuri sana iliyoitwa Bado Kidogo. Kuna wakati Patrick alijiunga na Orchestre Safari Sound, (masantula) na kupiga piano katika ule wimbo maarufu, ‘Unambie siri’, Patrick pia alikuwa mpigaji mahiri wa keyboards. Kwa kweli nyimbo za Patrick zilizokuwa juu katika chati ni nyingi. Harusi, Dirishani, Weekend, Tausi, Pesa, Nakupenda kama Lulu, Ni mashaka na mahangaiko, Afrika. Patrick alifariki tarehe 7, Agosti 2004 na kuzikwa 12 Aug katika makaburi ya Buguruni Malapa. Daima tutakukumbuka Patrick Pama Balisidya, Mungu akulaze pema peponi


NI MIAKA 46 TOKA KIFO CHA BAVON MARIE MARIE






Bavon Marie Marie, mdogo wake Franco Luambo,
alizaliwa May 27, 1944 katika jiji la Kinshasa na kupewa jina la Siango Bavon Marie Marie. Alipokuwa mdogo hakuwa mtukutu lakini alikuwa na akili sana, akajulikana sana kwenye eneo alilokulia   wilaya ya Bosobolo. Kadri alivyokuwa akaanza kuishi maisha ya  makeke zaidi kwa kuwa mlevi mzuri wa pombe na msafi aliyechichumbua kisawasawa kama ilivyokuwa desturi ya vijana wa Kinshasa wakati ule. Kama alivyokuwa kaka yake Franco Makiadi naye alikuwa mpiga gitaa mzuri sana. Alipigia bendi kama Cubana Jazz akiwa na mwanamuziki Bumba Massa, akapigia Orchestre Jamel kabla ya kuingia Negro Succes, bendi ambayo ilianzishwa 1960 za Vicky Longomba (Baba wa Awilo Longomba). Vicky aliwahi kuwa mmoja wa wanamuziki wa TP OK Jazz, sasa yeye  pamoja na wenzie Leon’ Bholen’ Bombolo, na mwimbaji mwenzie Hubert ‘Djeskin’Dihunga, mpiga sax Andre Menga, rhythm Jean Dinos, mpiga bezi Alphonse ‘Le Brun’ Epayo, mpiga drum Sammy Kiadaka na mwimbaji mwingine Gaspard ‘Gaspy; Luwowo wakaanzisha hiyo bendi kali kabisa  Negro Succes . Bavon akawa mpiga gitaa wa bendi hii baada ya mwaka 1965, yeye na mwenzie Bholen wakawa viongozi na masupastar wa wakati huo kwa vijana wa Kinshasa. Pamoja na kuwa kaka yake Franco  ndie aliyekuwa akijulikana kama Mwalimu Mkuu wa Rhumba la Kongo yeye pia alikuwa kipenzi  vijana kutokana na upigaji wa solo lake lililokuwa na uchangamfu zaidi .



Tarehe 5 Agost 1970 Bavon Marie alifariki katika ajali ya gari baada ya ugomvi uliotokana na mpenzi wa Bavon aliyeitwa Lucy, ambapo Bavon alimshutumu kaka yake kuwa kalala na mpenzi wake huyo. Ajali hiyo ilisababisha Lucy akatike miguu. Kuna watu wengine wanasema kisa kilikuwa ni ulevi tu wa Bavon ulisababisha bendi yake ishindwe kufanya show nae akawa kakasirika kwa hilo na kuendesha gari kwa fujo na kuishia chini ya uvungu wa roli kwenye njia panda. Pamoja na upigaji wa gitaa Bavon pia alikuwa mtunzi mzuri sana wa mashahiri ambayo yaliwagusa watu. Kwa mfano wimbo wake wa 'Mwana 15 Ans'…Mtoto wa miaka 15, Bavon aliongea kama binti wa miaka 15 ambae ana uchungu kwa kuwa familia yake inamtafutia mchumba japo yeye anataka kwenda shule. Hadithi ambayo wote tutakubali mpaka leo inamaana sana katika jamii za Kiafrika

Wednesday, August 3, 2016

TODAY I WOKE UP WITH THE SONG KWA MJOMBA BY URAFIKI JAZZ BAND


I woke up today with a 1970s Urafiki Jazz Band's tune Kwa Mjomba singing in my brain. The song was composed by Frank Masamba who was a vocalist then but now a saxaphonist and also teaches saxophone. The lyrics of this song  talk about this young guy who visited his uncle and met his beautiful cousin and fell in love with her, but was told he could not marry his cousin but wait for any other girl and someday will fall in love again. The song was very popular during its days, and is still being aired in some radio programs to date. Here are the lyrics;
Nilipokwenda kwa mjomba, Nilikutana na binamu yangu,
Na kwa kweli tulipendana, wazazi wetu walitukatalia tusioane
Eti kwa sababu yeye ni mtoto wa mjomba,
Ndivyo ilivyokuwa vigumu kwetu kufunga ndoa
Nilipokwenda kwa mjomba, Nilikutana na binamu yangu,
Na kwa kweli tulipendana, wazazi wetu walitukatalia tusioane
Eti kwa sababu yeye ni mtoto wa mjomba,
Ndivyo ilivyokuwa vigumu kwetu kufunga ndoa

       Chorus
Wazazi ninansema nasononeka, kwa vile msichana nilimpenda
Basi mwanangu nakuomba usisikitike sana , tuliza roho dunia hii ni pana sana kijana
Wazazi ninansema nasononeka, kwa vile msichana nilimpenda
Utampata wako mwingine pia utampenda, mtoto wa mjomba kweli kuoana si vizuri

Wazazi ninansema nasononeka, kwa vile msichana nilimpenda
Basi mwanangu nakuomba usisikitike sana , tuliza roho dunia hii ni pana sana kijana
Wazazi ninansema nasononeka, kwa vile msichana nilimpenda
Utampata wako mwingine pia utampenda, mtoto wa mjomba kweli kuoana si vizuri

The bands style was 'Mchakachaka' but fondly named 'Chakachua'. The word has changed its meaning now mostly because politicians have made it famous making it mean hoodwinking.  Urafiki Jazz Band was formed in 1970. It was owned by a textile mill known then as  FRIENDSHIP TEXTILE MILL. The company was so named as a sign of friendship between Tanzania and China. It was the Chinese who built the mill.The bands main purpose was to advertise the Khanga and Vitenge products that were being manufactured by the mill. At the time there was stiff competition from other textile mills like Mwatex , Kiltex, Mutex, and so on. The then General Manager of the mill, Mr Joseph Rwegasira (late) dished out 50,000/- which was enough to buy a set of music instruments from Dar es Salaam Music House. The shop is still in business to date. The company management engaged Mr Juma Feruzi Mrisho aka Ngulimba wa Ngulimba a veteran vocalist to come up with a band. Ngulimba took 5 musicians from the band he had just left, African Quilado and they became the core of the new band. He brought in  Michael Vincent Semgumi a lead guitarist, to date one of the best lead guitarists Tanzania has ever come up with, Ayoub Iddi Dhahabu on the bass guitar, Abassi Saidi Nyanga,Tenor Sax, Fida Saidi on Alto Sax. Other musicians were already employees of the company, like Juma Ramadhani Lidenge on the Second Solo guitar, Mohamed Bakari Churchil on rhythm guitar, Ezekiel Mazanda also a  rhythm guitarist, Abassi Lulela another bass guitarist, Hamisi Nguru, Mussa Kitumbo, Cleaver Ulanda all being vocalists, Maarifa Ramadhani on the congas, Juma Saidi on maraccass and Hamisi Mashala playing the drums . That was the firs line up of Urafiki Jazz Band. The band began with its 'Mchakamchaka' style later on changed to 'chakachua' and in its last day in the 80s went on to ‘Pasua’ and lastly ‘Patashika’. Many musicians joined and left this band other famous names of the time include Gideon Banda the saxophonist from  Morogoro Jazz, Thobias Cosmas Chidumule still famous vocalist who has now turned to gospel music, who together with Frank Mahulu joined the group coming from another great group The Western Jazz Band that was sometimes in 1973. Mkali and Hidaya,Trumpet blowers from the nearby town Morogoro accompanied by Ali Saidi, a rythm guitarist from Cuban Marimba, joined the band and in 1975 Mganga Hemedi a rythm guitarist from Atomic jazz band of Tanga joined this great group. Urafiki Jazz Band recorded more than three hundred songs covering subject like love, politics and everyday life in Tanzania at the time. A number of its songs are still being aired and some groups have even recorded their version of the songs. In
1975 the band took part in a Band competition which was held at Mnazi Mmoja Grounds and came third, this gave a ticket to the Band leader Ngulimba to travel with the band that won ( Afro 70 Band) to Lagos for the FESTAC festival held that year.

Thursday, July 28, 2016

URAFIKI JAZZ BAND NYIMBO ZAKE APATA UHAI MPYA



Leo nimeamka na wimbo wa Kwa Mjomba wa Urafiki Jazz Band, wimbo huo ni utunzi wa Frank Masamba ambaye kwa sasa ni mpiga saksafon na mwalimu wa chombo hicho;
Nilipokwenda kwa mjomba, Nilikutana na binamu yangu,
Na kwa kweli tulipendana, wazazi wetu walitukatalia tusioane
Eti kwa sababu yeye ni mtoto wa mjomba,
Ndivyo ilivyokuwa vigumu kwetu kufunga ndoa
Nilipokwenda kwa mjomba, Nilikutana na binamu yangu,
Na kwa kweli tulipendana, wazazi wetu walitukatalia tusioane
Eti kwa sababu yeye ni mtoto wa mjomba,
Ndivyo ilivyokuwa vigumu kwetu kufunga ndoa

       Chorus
Wazazi ninansema nasononeka, kwa vile msichana nilimpenda
Basi mwanangu nakuomba usisikitike sana , tuliza roho dunia hii ni pana sana kijana
Wazazi ninansema nasononeka, kwa vile msichana nilimpenda
Utampata wako mwingine pia utampenda, mtoto wa mjomba kweli kuoana si vizuri

Wazazi ninansema nasononeka, kwa vile msichana nilimpenda
Basi mwanangu nakuomba usisikitike sana , tuliza roho dunia hii ni pana sana kijana
Wazazi ninansema nasononeka, kwa vile msichana nilimpenda
Utampata wako mwingine pia utampenda, mtoto wa mjomba kweli kuoana si vizuri

Katika  zama hizi ukisikia neno ‘kuchakachua’ maana yake huwa kufanya jambo ambalo si halali au sahihi. Lakini neno ‘Chakachua’ katika miaka ya 70 na 80 lilikuwa na maana ya mtindo wa bendi maarufu wakati huo, na neno hilo lilitokana na mtindo wa bendi hiyo iliyokuwa inapiga mtindo iliyouita Mchakamchaka, neno lililofupishwa na wanamuziki wa bendi hii na kuitwa ‘Chaka Chuwa’. Bendi hii iliitwa Urafiki Jazz Band. Bendi hii  ilianzishwa mwaka 1970 ikiwa inamilikiwa na  kiwanda cha nguo cha Urafiki kilichokuwa Ubungo. Jina rasmi la kiwanda hicho lilikuwa ni FRIENDSHIP TEXTILE MILL. Kiwanda kilijengwa kwa msaada wa watu wa Jamhuri ya China na kwa urafiki huo kilipewa jina la Friendship Textile. Bendi ilianzishwa ili kutangaza bidhaa hasa Khanga na Vitenge za kiwanda hiki kwani wakati huo kulikuwa na viwanda vingine kadhaa vya nguo nchini kama vile Mwatex, Mutex, Kiltex, na kadhalika. Meneja Mkuu wa kiwanda cha Urafiki Bw. Joseph Rwegasira aliubariki mpango huo wa kuanzishwa bendi ya dansi ya kiwanda na hivyo aliidhinisha malipo ya hundi ya Shs. 50,000/= kununulia seti ya vyombo vya muziki kutoka katika duka la Dar Es Salaam Music House ambalo mpaka leo lipo katika mtaa wa Samora Avenue Dar Es Salaam.
Uongozi wa kiwanda ulimuajiri muimbaji Juma Mrisho Feruzi aliyekuwa maarufu kwa jina la Ngulimba wa Ngulimba na kumpa jukumu la kutafuta wanamuziki kwa ajili ya bendi hii. Ngulimba alichukua wapigaji watano kutoka Orchestre African Qillado, bendi ambayo aliipigia kabla ya kujiunga na Urafiki. Wanamuziki aliowachukua walikuwa ni Michael Vincent Semgumi mpiga gitaa la Solo, Ayoub Iddi Dhahabu mpiga gitaa zito la Bass, Abassi Saidi Nyanga mpulizaji wa Tenor Saxophone na Fida Saidi mpulizaji wa  Alto Saxophone. Wanamuziki wengine walikuwa  tayari waajiriwa wa kiwanda cha Urafiki  kama vile Juma Ramadhani Lidenge mpiga gitaa la Second Solo, Mohamed Bakari Churchil aliyepiga gitaa la rhythm, Ezekiel Mazanda pia alipiga rhythm, Abassi Lulela  kwenye Besi, Hamisi Nguru  Muimbaji, Mussa Kitumbo  Muimbaji, Cleaver Ulanda  Muimbaji, Maarifa Ramadhani kwenye Tumba, Juma Saidi mpiga maraccass na Hamisi Mashala  mpiga drums. Hilo ndilo lilikuwa kundi la kwanza la Urafiki Jazz Band. Mtindo walioanza nao Urafiki ulijulikana ‘Mchaka Mchaka’ na baadae ukabadilika na kuwa ‘Chaka Chua’ na hatimae wakati bendi inaelekea ukingoni mwa uhai wake walipiga mtindo wa ‘Pasua’ na ‘Patashika’.
Katika uhai wake  bendi ya Urafiki ilipitiwa na wanamuziki wengi waliokuwa maarufu wakati huo na wengine kuja kuwa maarufu baadae,  wakiwemo Gideon Banda mpuliza saxophone kutoka Morogoro Jazz, Thobias Cosmas Chidumule na Frank Mahulu ambao walikuwa  waimbaji waliotokea Western Jazz waliingia mwaka 1973 na kuongeza nguvu katika safu ya uimbaji. Baadae wapiga trampeti Mkali na Hidaya kutoka Morogoro walijiunga wakifuatana na Ali Saidi alietokea Cuban Marimba akipiga gitaa la kati (rhythm) na baadae mwaka 1975, Mganga Hemedi kutoka Tanga, akitokea Atomic Jazz, nae alijiunga na kuwa upande wa solo na rhythm.

Urafiki Jazz Band ilirekodi nyimbo zaidi ya  mia tatu zilizoelezea siasa, mapenzi, nasaha na mafundisho na pia kukosoa. Baadhi ya nyimbo zake za siasa zilizopata umaarufu ni kama zile Mwenyekiti Nyerere, Mauaji ya Soweto, Jembe na Panga na kadhalika.
Mwaka 1975 Bendi ilishiriki katika mashindano ya bendi za muziki wa dansi yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja,  Dar Es Salaam na kushika nafasi ya tatu, hili lilimuwezesha Juma Mrisho Ngulimba wa Ngulimba, kama Kiongozi wa Urafiki kupata nafasi ya kusindikizana na bendi ya Afro 70 kwenda Nigeria kwenye maonyesho ya mtu mweusi yaliyofanyika huko. Urafiki Jazz band haipo tena lakini hakika nyimbo zake bado zinapendwa na kuna vikundi vya vijana vimeanza kurudia nyimbo hizo kwa staili mpya, na hata tungo zake nyingine zikisikika katika mtindo wa taarab. Makala hii niliitoa kwama mara ya kwanza katika gazeti la MWANANCHI JUMAMOSI, na kila Jumamosi usikose makala kama hizi

Tuesday, July 19, 2016

BAVON MDOGO WAKE FRANCO LUAMBO LWANZO



Ganda la Album iliyokuwa na wimbo Maseke ya Meme. Tshimanga Assossa  aliwa wa pili toka kulia
Wimbo Maseke ya Meme ulipigwa katika miaka ya 70 na bendi maarufu ya Negro Success. Kundi lililokuwa likiongozwa na mdogo wake Franco Luambo Luanzo Makiadi, nae si mwingine ila ni mpiga solo mkali Bavon Siongo au maarufu kama Bavon Marie Marie aliyezaliwa May 27, 1944 ambaye pia alitunga wimbo huu marufu. Wimbo huu Maseke ya Meme au kwa Kiswahili ‘Pembe za kondoo’ ulianza kusambazwa March 1970. Mashahiri ya wimbo huu yalileta utata sana baada ya kifo cha Bavon Marie Marie kilichotokea muda si mrefu baada ya wimbo huu kutoka hewani.  Sehemu ya mashahiri ya wimbo huu yalisema hivi;
Bavon Marie Marie
 Nalilia maisha yangu
Sijachoka kuishi
Lakini wanataka nitangulie
Naacha kuongea
Nasubiri kifo.
Bahati mbaya sana Agosti 5, 1970, siku ya Jumatano, Bavon Marie Marie akakumbwa na ajali ya gari iliyosababisha kifo chake katika mtaa wa Avenue Kasavubu, mjini Kinshasa. Wimbo ule ukaonekana kama ni utabiri wa kifo chake mwenyewe. Kwa vile Franco hakufurahia mdogo wake kuingia katika muziki,watu wakatafsiri kuwa alikuwa amemloga mdogo wake ambae alifariki akiwa na umri wa miaka 34 tu. Kuna hadithi nyingine inayosema kifo cha Bavon kilitokea muda mfupi baada ya ugomvi na kaka yake kwa kisa kuwa Franco alikuwa ametembea na Lucy aliyekuwa bibi wa Bavon. Inasemekana Bavon aliondoka spidi na gari akiwa na hasira na muda mchache baadae akaaingia chini ya lori.
Kuna nyimbo nyingi duniani ambazo watu hudhani ni kama utabiri wa wanamuziki kabla ya kufa. Wimbo Ee Mola wangu wa Salum Abdallah wa Cuban Marimba ni mfano mojawapo. Kuna wanamuziki wengi wanaogopa kuimba au kutunga nyimbo kuhusu kifo kwa imani kuwa ukitunga wimbo wa namna hiyo unaita kifo.