Thursday, July 28, 2016

URAFIKI JAZZ BAND NYIMBO ZAKE APATA UHAI MPYA



Leo nimeamka na wimbo wa Kwa Mjomba wa Urafiki Jazz Band, wimbo huo ni utunzi wa Frank Masamba ambaye kwa sasa ni mpiga saksafon na mwalimu wa chombo hicho;
Nilipokwenda kwa mjomba, Nilikutana na binamu yangu,
Na kwa kweli tulipendana, wazazi wetu walitukatalia tusioane
Eti kwa sababu yeye ni mtoto wa mjomba,
Ndivyo ilivyokuwa vigumu kwetu kufunga ndoa
Nilipokwenda kwa mjomba, Nilikutana na binamu yangu,
Na kwa kweli tulipendana, wazazi wetu walitukatalia tusioane
Eti kwa sababu yeye ni mtoto wa mjomba,
Ndivyo ilivyokuwa vigumu kwetu kufunga ndoa

       Chorus
Wazazi ninansema nasononeka, kwa vile msichana nilimpenda
Basi mwanangu nakuomba usisikitike sana , tuliza roho dunia hii ni pana sana kijana
Wazazi ninansema nasononeka, kwa vile msichana nilimpenda
Utampata wako mwingine pia utampenda, mtoto wa mjomba kweli kuoana si vizuri

Wazazi ninansema nasononeka, kwa vile msichana nilimpenda
Basi mwanangu nakuomba usisikitike sana , tuliza roho dunia hii ni pana sana kijana
Wazazi ninansema nasononeka, kwa vile msichana nilimpenda
Utampata wako mwingine pia utampenda, mtoto wa mjomba kweli kuoana si vizuri

Katika  zama hizi ukisikia neno ‘kuchakachua’ maana yake huwa kufanya jambo ambalo si halali au sahihi. Lakini neno ‘Chakachua’ katika miaka ya 70 na 80 lilikuwa na maana ya mtindo wa bendi maarufu wakati huo, na neno hilo lilitokana na mtindo wa bendi hiyo iliyokuwa inapiga mtindo iliyouita Mchakamchaka, neno lililofupishwa na wanamuziki wa bendi hii na kuitwa ‘Chaka Chuwa’. Bendi hii iliitwa Urafiki Jazz Band. Bendi hii  ilianzishwa mwaka 1970 ikiwa inamilikiwa na  kiwanda cha nguo cha Urafiki kilichokuwa Ubungo. Jina rasmi la kiwanda hicho lilikuwa ni FRIENDSHIP TEXTILE MILL. Kiwanda kilijengwa kwa msaada wa watu wa Jamhuri ya China na kwa urafiki huo kilipewa jina la Friendship Textile. Bendi ilianzishwa ili kutangaza bidhaa hasa Khanga na Vitenge za kiwanda hiki kwani wakati huo kulikuwa na viwanda vingine kadhaa vya nguo nchini kama vile Mwatex, Mutex, Kiltex, na kadhalika. Meneja Mkuu wa kiwanda cha Urafiki Bw. Joseph Rwegasira aliubariki mpango huo wa kuanzishwa bendi ya dansi ya kiwanda na hivyo aliidhinisha malipo ya hundi ya Shs. 50,000/= kununulia seti ya vyombo vya muziki kutoka katika duka la Dar Es Salaam Music House ambalo mpaka leo lipo katika mtaa wa Samora Avenue Dar Es Salaam.
Uongozi wa kiwanda ulimuajiri muimbaji Juma Mrisho Feruzi aliyekuwa maarufu kwa jina la Ngulimba wa Ngulimba na kumpa jukumu la kutafuta wanamuziki kwa ajili ya bendi hii. Ngulimba alichukua wapigaji watano kutoka Orchestre African Qillado, bendi ambayo aliipigia kabla ya kujiunga na Urafiki. Wanamuziki aliowachukua walikuwa ni Michael Vincent Semgumi mpiga gitaa la Solo, Ayoub Iddi Dhahabu mpiga gitaa zito la Bass, Abassi Saidi Nyanga mpulizaji wa Tenor Saxophone na Fida Saidi mpulizaji wa  Alto Saxophone. Wanamuziki wengine walikuwa  tayari waajiriwa wa kiwanda cha Urafiki  kama vile Juma Ramadhani Lidenge mpiga gitaa la Second Solo, Mohamed Bakari Churchil aliyepiga gitaa la rhythm, Ezekiel Mazanda pia alipiga rhythm, Abassi Lulela  kwenye Besi, Hamisi Nguru  Muimbaji, Mussa Kitumbo  Muimbaji, Cleaver Ulanda  Muimbaji, Maarifa Ramadhani kwenye Tumba, Juma Saidi mpiga maraccass na Hamisi Mashala  mpiga drums. Hilo ndilo lilikuwa kundi la kwanza la Urafiki Jazz Band. Mtindo walioanza nao Urafiki ulijulikana ‘Mchaka Mchaka’ na baadae ukabadilika na kuwa ‘Chaka Chua’ na hatimae wakati bendi inaelekea ukingoni mwa uhai wake walipiga mtindo wa ‘Pasua’ na ‘Patashika’.
Katika uhai wake  bendi ya Urafiki ilipitiwa na wanamuziki wengi waliokuwa maarufu wakati huo na wengine kuja kuwa maarufu baadae,  wakiwemo Gideon Banda mpuliza saxophone kutoka Morogoro Jazz, Thobias Cosmas Chidumule na Frank Mahulu ambao walikuwa  waimbaji waliotokea Western Jazz waliingia mwaka 1973 na kuongeza nguvu katika safu ya uimbaji. Baadae wapiga trampeti Mkali na Hidaya kutoka Morogoro walijiunga wakifuatana na Ali Saidi alietokea Cuban Marimba akipiga gitaa la kati (rhythm) na baadae mwaka 1975, Mganga Hemedi kutoka Tanga, akitokea Atomic Jazz, nae alijiunga na kuwa upande wa solo na rhythm.

Urafiki Jazz Band ilirekodi nyimbo zaidi ya  mia tatu zilizoelezea siasa, mapenzi, nasaha na mafundisho na pia kukosoa. Baadhi ya nyimbo zake za siasa zilizopata umaarufu ni kama zile Mwenyekiti Nyerere, Mauaji ya Soweto, Jembe na Panga na kadhalika.
Mwaka 1975 Bendi ilishiriki katika mashindano ya bendi za muziki wa dansi yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja,  Dar Es Salaam na kushika nafasi ya tatu, hili lilimuwezesha Juma Mrisho Ngulimba wa Ngulimba, kama Kiongozi wa Urafiki kupata nafasi ya kusindikizana na bendi ya Afro 70 kwenda Nigeria kwenye maonyesho ya mtu mweusi yaliyofanyika huko. Urafiki Jazz band haipo tena lakini hakika nyimbo zake bado zinapendwa na kuna vikundi vya vijana vimeanza kurudia nyimbo hizo kwa staili mpya, na hata tungo zake nyingine zikisikika katika mtindo wa taarab. Makala hii niliitoa kwama mara ya kwanza katika gazeti la MWANANCHI JUMAMOSI, na kila Jumamosi usikose makala kama hizi

No comments: