Thursday, January 4, 2018

MTUNZI WA LUNCHTIME MZEE GABRIEL OMOLO AFARIKI DUNIA



Mzee Gabriel Omolo Aginga anayejulikana kwa wapenzi wengi wa muziki wa zamani kwa wimbo wake Lunchtime, alikuwa ni mmoja wa wanamuziki wachache waliotamba Kenya katikamiaka ya 70 ambao walikuwa bado hai. Katika video moja iliyotoka karibuni ilimuonyesha Mzee Gabriel ambae uzeeni alikuwa mkulima akiangalia mifugo yake akiwa katika afya nzuri.
Gabriel Omolo
(Picha kwa hisani)
Gabriel alifariki baada ya kuugua kwa muda mfupi na kufariki katika hospitali ya Busia jana Jumatano usiku. Rafiki yake wa toka utotoni na mwanamuziki mwenzake Charles Makawita ambaye walitoka wote katika kijiji cha Nyabenda Uhoro, kwenye kaunti ya Siaya alisema Gabriel alikuwa na miaka 79 na alifariki kutokana na matatizo ya kushindwa kupumua. Mke wa marehemu Alice Adeya ndiye aliyemtaarifu Charles kuwa mwenzie anaumwa.
Gabriel alizaliwa 1939, alijifunza gitaa akiwa shule ya msingi ya St Peter Claver ambako pia alikuwa anaimba kwenye kwaya ya shule hiyo. Kwenye miaka ya 60 alijiunga na ile bendi maarufu ya Equator Sound Band ambayo wakati huo ilikuwa na miamba akina Peter Tsotsi, Nashil Pichen Kazembe, Daudi Kabaka na Fadhili William. Gabriel ndie aliyepiga gitaa la bezi kwenye wimbo Pole Musa wimbo uliotungwa na Peter Tsotsi. Marehemu Gabriel alipigia pia Eagles Band , Blue Shades na baadae Apollo Komesha Band
Septemba 1974 Gabriel alikuwa Mkenya wa kwanza kupata tuzo ya International Golden Disc kutokana na mauzo ya wimbo wake wa Lunchtime. Kampuni ya Phonogram Records ilihakikisha kuwa single ya wimbo huo iliuza nakala 150,000.Afrika ya Mashariki na Afrika Magharibi.

Remix ya wimbo huo ilifanywa mwaka 2005, ikiwa ni miaka 35 toka ilipoachiwa nyimbo hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 1970. Remix ilifanywa na mwanamuziki marehemu Poxi Presha na Paddy makani, Mkongo aliyekuwa akiishi Kenya. Tunamuomba Mungu Amlaze Pema Gabriel Omolo

No comments: