Wednesday, November 15, 2017

HISTORIA FUPI YA DEKULA KAHANGA VUMBI


Vumbi Dekula Kahanga





Orch. Maquis Original 1987 Wapiwapi Chang'ombe Bar,kutoka kulia ni:
Mbuya Makonga "Adios",Dekula Kahanga"Vumbi",Mpoyo Kalenga na William Maselenge.
Alie chuchumaa ni Juma Choka

Kwa wapenzi wa muziki wa dansi Tanzania, jina la mpiga gitaa Dekula Kahanga Vumbi si geni, wengi hasa humfahamu kama mwanamuziki wa Maquis Original, na wanakumbuka mlio wa gitaa lake katika nyimbo kama Makumbele na Ngalula hasa pale ambapo Assossa anamhamasisha aongeze utamu kwa kutaja jina' Vumbi Vumbi'. Lakini Je, alianzia wapi? Kwanza kabisa  baba yake hakupenda kabisa apige gitaa, ulikuwa ugomvi mkubwa lakini bahati nzuri alikulia kwa bibi yake katika mji wa Uvira, mkoa wa Kivu, Jamhuri ya Kongo. Kwa bibi kama walivyo wabibi wengi, alikuwa na uhuru zaidi na akaanza kwa kutengeneza magitaa yake, ambalo yalikuwa yakivunjwa kila baba yake alipokuwa akija kumtembelea bibi yake. Jirani na alipokuwa akiishi kulikuweko na bar inaitwa Sikiya sosi ambapo palikuweko  na bendi ikiitwa Gramick Jazz, bendi iliyopitiwa na wanamuziki wengi ambao baadae walikuja Tanzania akiwemo Dr RemmyOngala. Vumbi alikuwa akisikiliza muziki ukipigwa ndani ya  hiyo bar na yeye akawa anafuatisha kwenye gitaa la kutengeza mwenyewe la nyuzi tatu, hatimae bibi yake akamnunulia gitaa dogo la nyuzi nne ambalo alikuwa anaenda nalo mpaka shule, ambapo mwalimu wake siku nyingine alikuwa akimwita awatumbuize wanafunzi wenzie. Hatimae akakutana na jamaa aliyekuwa akipiga katika bendi iliyokuwa ikimilikiwa na mapadri, akawa anamnunulia sigara huyu jamaa nae akaanza kumfundisha chords mbalimbali za kupiga gitaa. Aliendelea vizuri hatimae akajiunga na bendi hiyo ya mapadri iliyoitwa Kyalalo Band akiwa mpiga rhythm. Wanamuziki wa Kyalalo hawakuruhusiwa kujiunga na bendi zilizo kuwa zinapiga muziki kwenye bar, wala bendi yenyewe  haikuruhusiwa kwenda kupiga kwenye bar, kulikuweko na ukumbi mkubwa wa kanisa na hapo ndipo walipofanya mazoezi na maonyesho, lakini baadae Vumbi akajiunga na bendi Bavy National tena kama mpiga rhythm, 
Bavy National  Orchestre, kutoka kulia mstari wa nyuma ni Dekula (Rythm),Packot(Solo na Kiongozi),Maboko(Besi),
Merry-Djo (Drums).
Kutoka kulia mstari wa mbele,Waimbaji ni Djo-Mali,Issa Nundu na Simplice Mofeza.
Mwaka wa 1983  katika "Sikia Sosi Bar" Mjini  Uvira Mkoani Kivu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
na hapo akakutana na mwimbaji Issa Nundu ambae alikuwa anafanya hospitali na jioni kujiunga na bendi, hatimae Kyanga Songa ambaye kazi yake ilikuwa Bwana Shamba nae alijiunga nao.
Katika kipindi hicho wakazi wa Kongo ya Mashariki, ambako kunazungumzwa Kiswahili, walikuwa wakisikiliza na kuzijua bendi nyingi kutoka Afrika ya Mashariki, bendi kama Tabora Jazz, Mangelepa, Simba wa Nyika, Mlimani Park zilisikilizwa sana, na nyimbo kama Kassim ilikuwa moja ya nyimbo maarufu wakati huo na hivyo ikawa ndoto ya Vumbi na wenzie kuwa lazima siku moja waende huko unakotoka muziki mtamu huo ili nao waweze kushiriki. Katika kipindi hicho Kyanga Songa na Issa Nundu waliondoka  kwenye bendi yao ya Bavi National na kuelekea Tanzania. Bendi ikatetereka sana, lakini nae wakati huo akawa anahamu sana ya kuja  Afrika Mashariki. Bahati nzuri mtu mmoja Alida Shanga akamjia akiwa ametumwa na Marehemu Mzee John Luanda aliyekuwa anamiliki Chamwino Jazz kuja kutafuta wanamuziki toka Kongo, nae akawachukua wanamuziki kadhaa akiwemo Vumbi na kituo chao cha kwanza kilikuwa Tandale jijini Dar es Salaam. Na siku waliofika tu na wakaanza mazoezi siku hiyo hiyo. Wakiwa vijana bado yeye na wenzie watatu walikuja wakiwa na staili ya  kuimba na kucheza steji show ambayo wakati huo iliitwa sarakasi, na pia wao ndo kilikuwa kikundi cha kwanza kuanza kurap katikati ya nyimbo. Waimbaji wakiwa ni   Sisko Lunanga, Fanfan Bwami, na mwenzao mmoja Baposta Kilosho ambae hatimae alirudi Kongo. Recording ya kwanza ilimuacha Julius Nyaisanga akishangaa vituko vya vijana hawa. Katika bendi ya Chamwino wakati huo wapiga magitaa walikuwa Vumbi Dekula, Kazembe wa Kazembe (huyu alikuwa Msukuma ambaye aliishi kwa muda Kongo na alikuwa mpiga gitaa hodari sana), na Mzee Albert, na hatimae wakamchukua Muhidin ambae alikuwa mpiga bezi wa Dr Remmy. Siku moja walienda kuomba kupiga na Maquis Original(lift), wakati huo wakipiga nyimbo za kopi, nyimbo kama Mario, Maze na kadhalika, hivyo wakazipiga hizo na watu wakafurahi sana na kuwatuza  fedha nyingi, wakachanganyikiwa maana bendi yao ya Chamwino ilikuwa haina mshahara na si mara moja walitembea kwa miguu kutoka Buguruni hadi Tandale kwa kukosa hata nauli. Japo wakati huo walikuwa wadogo kwa umri na hata umbo walifika mahala marehemu Kasheba alikuwa anawaita ‘Vimario’, upigaji wao ulikuwa mzuri sana. Nguza aliwashauri wawe wanakuja kupiga kabla Maquis hawajaanza kupiga. Hivyo wakaamua kuacha Chamwino, na wakawa wanasindikizana na Maquis, hili lilimuudhi aliyewaleta na siku moja wakiwa Silent Inn, maafisa wa Uhamiaji walikuja kuwachukua wakalazwa Central Police na kisha kupelekwa gereza la Keko. Wakiwa huko walimwandikia Mzee Luanda kuwa wanarudi Chamwino, basi wakaachiwa na kurudi kusuka upya Chamwino Jazz. Lakini hawakukaa muda mrefu Mzee Makassy akaja kuwaomba waingie katika bendi yake, wenzake waimbaji  wakaenda  yeye akabaki Chamwino, lakini muda si mrefu Nguza akamwambia aandike barua ajiunge na Maquis. Nae akafanya hivyo na ndio kujiunga rasmi na Maquis kama mpiga gitaa la second solo. Aliwakuta wanamuziki kama Maneno Uvuruge, Omari Makuka, Keppy kiombile, Ilunga Lubaba, William Maselenge na wengine wengi.  Aliendelea kupiga second solo hadi siku moja bendi ilikuwa inapiga maeneo ya Ukonga, kwa kawaida Mzee Lubaba alikuwa anapiga kuanzia saa tatu mpaka saa sita, na  kisha Nguza Viking akiingia na kuendelea .
Maquis wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma,  wa pili toka kulia na shati jeusi Vumbi, wapili toka kushoto na suruali nyeusi Issa Nundu
Siku hiyo Nguza hakuonekana Vumbi  akaweza kupiga nyimbo zote za Nguza, na kesho yake  akaambiwa afike ofisini akasainishwa rasmi mkataba wa kuwa mwanamuziki wa Maquis.  Baada ya muda mfupi Nguza akaacha bendi.
Muda mfupi baada ya hapo walirekodi ule wimbo maarufu wa Makumbele, solo ya wimbo huu ilikuwa awali ikipigwa na Mzee Lubaba, lakini afya ya mzee Lubaba ilianza kuzorota nae akawa anawafundisha nyimbo zake wanamuziki wengine, wimbo wa Makumbele alifundishwa  Omari Makuka na akawa anaupiga katika maonyesho mbalimbali, lakini wakati wa kutaka kurekodi kamati ya uongozi ya Maquis iliamua Vumbi aufanyie mazoezi  na aurekodi. Kurekodi kwa album ya Makumbele ilitokana na safari ndefu ya bendi ambayo ilichukua miezi mitatu katika mikoa ya Ziwa, hivyo bendi iliporudi Dar  ilikuta sifa ya bendi imepungua, hivyo walirekodi album ya Makumbele iliyokuwa na nyimbo kama Tipwatipwa, Ngalula na Makumbele, sifa ya bendi ikarudi juu tena kwa mara nyingine. Na ni wakati huo ambapo bendi ilihamia katika ukumbi wa Lang’ata Kinondoni. Vumbi aliedelea kupiga katika bedi hii mpaka alipoamua kuhamia Sweden ambako yuko mpaka leo akiendelea kupiga muziki.




Sunday, November 12, 2017

JE UTAMU WA GITAA LA RYTHM UTAWEZA KURUDI TENA?

Harrison Siwale (Satchmo) mpiga rythm, Mbaraka Mwinyishehe mpiga solo, Abdul Mketema mpuliza saksafoni
Katika mfumo wa awali kuanzia miaka ya 50,  bendi zilikuwa  na mfumo wa kutumia magitaa matatu, Solo, rythm na Bass. Gitaa la solo lilikuwa na sauti ya juu, huku rythm ikiwa na sauti nzito kidogo ya kati, na mwisho Bass likiwa na sauti nzito kuliko magitaa mengine. Kimuundo gitaa la rythm na la solo hakuna tofauti. Yote yana nyuzi 6,lakini katika kutyuni kwenye amplifier, gitaa la rythm hunyimwa treble (ukali) kiasi na kuongeza bass zaidi kuliko gitaa la solo ambalo huwa na treble zaidi ya magitaa mengine. Mwanzoni mwa miaka ya 60 likaanza kutumika gitaa la nne lililojulikana kama 'second solo' au Wakongo waliliita 'mi solo'. Inasemekana kaka yake mpiga solo maarufu wa Kongo wa enzi hizo Dr Nico, ndie aliyeanzisha mtindo wa kuongeza gitaa hilo la nne. Hili lilikuwa likipigwa kwa mifumo mbalimbali katika bendi mbali mbali. Bendi nyingine zilitumia second solo kama gitaa lililokuwa linajibizana na solo, na bendi nyingine lilikuwa linajibizana na rythm,na hata kulikuweko mfumo ambapo gitaa hilo aidha lilikuwa likipiga 'harmony ya gitaa la solo au ya gitaa la rythm. Bendi nyingine , mfano  Cuban Marimba chini ya Juma Kilaza liliongeza ubunifu na kuongeza gitaa la 5 na kuliita 'chord guitar'. Ubunifu huu uliongeza sana uzito wa muziki na hata kuleta ladha mbalimbali za muziki wa dansi. Na uamuzi wa aina ya mpangilio wa magitaa uliweza kuleta tofauti kubwa kati yabendi moja na nyingine.
Lakini katika makala ya leo tuzungumzie gitaa la rythm. Chombo hiki bado kinapigwa katika bendi nyingi lakini umuhimu wake umeshuka sana. Katika kipindi cha miaka ya 60 na 70, gitaa hili lilikuwa na umuhimu mkubwa na wapigaji wake waliweza kubuni staili zao wenyewe. N kujijengea sifa kubwa. Kati ya wapiga rythm maarufu alikuweko Satchmo, hilo ndio lilikuwa jina la kisanii la Harrison Siwale, huyu alikuwa Mzambia aliyekuja weka masikani yake katika mji wa Tanga. Alipitia bendi kubwa za Tanga ikiwemo Atomic Jazz Band na hatimae Jamhuri Jazz Band. Satchmo alikuwa na staili peke yake ya kupiga rythm, sikumbuki kusikia mtu mwingine akipiga rythm ya aina yake kabla ya hapo, lakini hakika wapiga rythm wengi walichukua mtindo wake na kubuni vionjo vya aina yao. Rythm yake ilitawala nyimbo za Jamhuri Jazz Band wakati huo. Ufundi wake unaonekana sana katika nyimbo kama Mganga no 1 na 2, au Blandina. Kule Tabora  Mzee Kasim Kaluwona nae alikuwa na staili tofauti ya upigaji wa gitaa la rythm uliyoifanya Tabora Jazz kuwa na staili yake peke yake, kumbuka gitaa lake katika wimbo Asha, au Dada Lemmy. Charles Kazembe akiwa na Morogoro Jazz anakumbukwa katika upigaji wa rythm kwenye nyimbo kama Wajomba Wamechacha. Hao ni wachache tu kulikoweko na wengi marufu. Katika kipindi hiki huko Zaire kulikuwa na mipigo mbalimbali ya gitaa la rythm, ila kitu kipya kikaanzishwa ambapo katika ufungaji wa nyuzi ,wapiga rythm wakauondoa uzi namba nne katika gitaa hilo na kuweka uzi namba moja, hivyo kukawa na nyuzi namba moja 2 katika gitaa moja, hapo ndipo akina Vata Mombasa wakaweza kuleta utamu mpya katika upigaji wa rythm, ufungaji wa aina hii wa nyuzi za gitaa ulifahamika kama 'double string'. Wakati huo Orchestra Kiam wakawa wanajivunia kupiga rythm kwa spidi kali sana,vibao kama Kamiki, Bomoto ni ushahidi wa kazi hizo. Utamu wa ufungaji wa nyuzi kwa staili hii uliweza kusikika vizuri katika gitaa lililopigwa mwanzo kabisa wa wimbo Andoya. Umuhimu wa gitaa la rythm ulikuwa ukionekana kwa bendi nyingi kuwa na mtindo wa 'kuachia rythm', huo ulikuwa ni mpangilio ambapo gitaa la rythm liliachwa lipige peke yake wakati magitaa mengine yakiwa kimya. Hapo mpiga rythm aliachiwa kucheza na gitaa alivyotaka na  kuonyesha umahiri wake wote. Mtindo huu ulipendwa sana na wapenzi wa muziki. Utaratibu huu umerudi kwa njia ya ajabu sana, bendi nyingi za  taarab vimeanza 'kuachia rythm' lakini kwa kuwa bendi hizo hazitumii tena gitaa la rythm , jukumu hili linafanywa na mpiga solo, tena vipande vingi vinavyopigwa ni vile vilivyopigwa na bendi za zamani!!  matokeo ni yaleyale, wapenzi wa muziki hupanda mzuka na kucheza sana wakati wa kipindi hicho. 
Kwa ujumla bendi nyingi za dansi hazitilii umuhimu tena gitaa la rythm. Kinanda kimechukua nafasi ya gitaa hili. Kuna bendi ambazo zinalo gitaa la rythm lakini kwa mfumo wa sasa wa muimbaji kuchukua nafasi kubwa ya wimbo gitaa hilo limerudishwa nyuma sana. Lakini kwenye muziki kila kitu kina utamu wake kamwe chombo kimoja hakiwezi kuziba pengo la chombo kingine.