Saturday, September 16, 2017

BURIANI SHABANI YOHANA MWANASANDE- SHABAN WANTED HATUNAE TENA

Jana mchana, siku ya Ijumaa nikiwa njiani natoka Tanga muda mfupi tu baada ya kupita Hale nilipigiwa simu na James Mawila, mpiga drums wa Msondo akinitaarifu kuwa Albert Chikopa, mwanamuziki mwenzetu aliyeko Botswana ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kuwa mpiga gitaa Shabani Yohana amefariki. Niliingia haraka katika ukurasa huo na kukuta habari hizo, pia Chikopa alikuwa ameweka namba ya mtu ambaye ana taarifa zaidi. Nilimpigia mtu huyo na alisema kuwa habari hizo ni kweli na kuwa Shabani alifariki akiwa peke yake chumbani na hivyo ilikuwa ni baada ya siku mbili ndipo jambo hilo lilipojulikana na hivyo polisi walikuwa wakitafuta ndugu zake. Bahati nzuri Rashid Pembe aliweza kumpata nduguye na taratibu za mazishi zinaendelea. Mpaka sasa kuna jitihada za kujaribu kurudisha mwili wa Shabani nyumbani. Michango inaendelea Botswana na hapa nyumbani katika makundi ya wapenzi wa muziki wa rumba.
Nilikutana na Shabani mara ya kwanza katika bendi ya Tancut Almasi Orchestra, yeye akitokea bendi ya Orchestra Vinavina, nami nikitokea Orchestra Seleleka, tulikuwa kati wa watu wa kwanza kujiunga na bendi hiyo hatimae wakaja kujiunga wanamuziki wengine kina Mafumu Bilali, Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa na pamoja tukaja kujenga bendi ambayo iliweza kuporomosha muziki mzuri sana. Katika album ya kwanza ya Tancut Almasi karibu nyimbo zote solo lilipigwa na Shabani Yohana kasoro wimbo wa Kiwele ambapo solo lilipigwa na Kawelee Mutimwana ambaye pia ndie aliyekuwa  mtunzi wa wimbo huo. Nyimbo hizo zilikuwa 
Nimemkaribisha nyoka
Kashasha
Tutasele
Kuwajibiika
Big Four
Mtaulage
Na hata album ya pili solo la Shabani linatambulika sana kwenye wimbo Masafa Marefu, lakini pia alipiga solo kwenye wimbo wa Wifi.
Shabani alihamia vijana Jazz band 1988 ambapo akapewa jina la Wanted, na katika bendi hii aliendelea kwa miaka 6 kuburudisha watu kwa ufanisi wake katika kupiga gitaa hili, nyimbo kama Ogopa Tapeli, Aza, Mama Wa Kambo Mundinde, Wifi Zangu, Penzi haligawanyiki, Thereza, Shoga, Heshima ya mtu na nyimbo nyingine nyingi za bendi hii. Baada ya safari ya Ujerumani ambapo tulikwenda mimi John Kitime, Mzee Small, Abadallah Mgonahazelu, Baker Semhando, na yeye mwenyewe Shabani, ndipo mwenzetu alipotutaarifu kuwa anataka kuhama bendi. Vijana Jazz tulimfanyia party ya kumuagana kumnunulia zawadi, jambo ambalo halikuwa la kawaida, na baada ya hapo akahamia Ngorongoro Heroes, huko nako alitingisha jiji kwa gitaa lake katika nyimbo za bendi hiyo. Hatimae akahamia Botswana, ambako kwa mujibu wa maandiko kwenye facebook baada ya kusikia kifo chake wanamuziki wa huko wameendelea kusifia ubora aliokuwa nao.
Mipango ya maziko inaendelea, jaribio kubwa ni kuchangishana kurudisha mwili wake hapa nyumbani. 
MUNGU AMLAZE PEMA SHABANI YOHANA WANTED

Thursday, September 7, 2017

UNAKUMBUKA SOCIAL EVENINGS?

KWA wengi waliokuwa wakisoma sekondari miaka ya 60 na 70, moja ya siku zilizokuwa zikisubiriwa kwa hamu ilikuwa siku ya ‘Social Evening’. Siku hii ilikuwa ndio siku ambayo wanafunzi walipata nafasi kusakata dansi na kupata marafiki wapya, na mara nyingine hata kuachwa na marafiki wa zamani. Mara nyingi dansi hili liliambatana na kualika wanafunzi kutoka shule nyingine za jirani. Na kawaida ilikuwa shule ya wavulana kualika wanafunzi kutoka shule ya wasichana na shule ya wasichana kualika wanafunzi kutoka shule ya wavulana. Matayarisho yalikuwa yanaanza mapema kwa waalikaji kuandika barua kwa Mwalimu Mkuu au mwalimu wa ‘Social’ wa shule wanayotaka kuialika. Baada ya hapo kazi kubwa ni kukusanya michango kutoka kwa wanafunzi wanaotaka kushiriki siku hiyo. Michango hii kazi yake ilikuwa kununua viburudisho kwa wageni; soda, biskuti au hata maandazi, na pia kununua betri za ‘player’ ya kupigia muziki. Umeme ulikuwa nadra kwenye mashule mengi. Kamati ya starehe ilikuwa ‘busy’ kutafuta santuri mpya, kwa kuazima popote pale, na kama kuna mwalimu ana record player ilikuwa jambo la heri sana.  Ukumbi ulipigwa deki vizuri ili wageni wakifika wasije wakawadharau. Hatimae siku huwadia, social evening mara nyingi zilikuwa Jumamosi kuanzia saa nane mchana na kuisha kati ya saa moja mpaka mbili usiku. Wageni hukaribishwa na burudani huanza. Baada ya hotuba na kugawa vinywaji, wenyeji huleta burudani kama vile kucheza jiving, baada ya hapo ‘Dada mkuu’ au mwenyekiti wa kamati ya social wa shule moja hufungua dansi na mwenzie wa upande wa pili. Na ndipo wengine mnajitosa kusaka mapatna. Kawaida ya miaka hiyo mwanaume unamfuata msichana kisha unainama kidogo kumuomba ucheze nae, anaweza akakubali au kukataa. Katika shughuli hizi waalimu wa kuangalia nidhamu walikuwa wakishiriki kuangalia kuwa maadili yanafuatwa. Wakati mnacheza mwalimu anapitapita kuangalia kama ‘hamsogeleani ‘ sana.  Kama nilivyosema hapo juu, muziki ulitoka kwenye record player ambayo ilikuwa na spika moja ndogo hivyo haikuwa na sauti kubwa. Ukiona ukubwa wa maspika siku hizi, unabaki kushangaa, tuliwezaje wanafunzi 200 hadi 300 kucheza muziki na kuusikia vizuri kwa kutumia spika moja  ya player yenye betri 6. Spika ambayo ili itoe bezi ililazimika kuwekwa juu ya pipa. Kulikuwa na nidhamu kubwa sana katika uchezaji, kulikuwa hakuna kupiga kelele, unasikia viatu tu vikisaga chini kwa kufuata mdundo wa muziki. Swala la kuwa pombe haikuhusika katika burudani hizi ni moja ya sababu ya kuwezekana kwa nidhamu hii. Mazungumzo yalikuwa ya chini chini mara nyingi yakihusu masomo.
Katika miaka ya 60 santuri za nyimbo kutoka Congo ndizo zilikuwa maarufu, magwiji wa muziki kama akina Franco, Johhny Bokelo, Dr Nico, Bavon Marie Marie na bendi zao maarufu, Ok Jazz, Negro Success, Co Bantuo, Conga Success na kadhalika, ndizo zilikuwa pendwa wakati huo. Kutoka  Marekani wanamuziki wa muziki wa country kama Skeeter Davis, Jim Reeves, Connie Francis ndio walitawala social evenings. Wavulana kwa wasichana walishiriki kuandika maneno ya nyimbo hizo kwenye madaftari yao na kubadilishana madaftari. Nyimbo maarufu katika madaftari ya wavulana zilikuwa ni nyimbo za Kikongo. Tambola na Mokili wa Johhny Bokelo na Conga Success na Bougie ya Motema wa Dr Nico na African Fiesta zilikuwa hazikosekana kwenye madaftari ya wavulana, wakati akina dada walipendelea sana kuandika maneno ya nyimbo za Skeeter Davis na Dark City Sisters kutoka Afrika ya Kusini. Kama nilivyosema hapo juu, umeme tu ulikuwa tatizo kweye shule nyingi, hivyo swala la kuwaona na kuwajua wanamuziki waliokuwa wakiporomosha muziki huo lilikuwa nadra sana. Magazeti yalikuwa machache, vyombo ambavyo siku hizi vinaonekana ni kawaida kabisa kama radio na TV navyo vilikuwa nadra sana. Lakini kwa njia ya ajabu watu walikuwa wanajua namna ya kucheza staili za muziki mbalimbali!! Chacha, pachanga, charanga, baadae soul, bumping na kadhalika. Kwenye shule mbalimbali kulikuwa na wanafunzi ambao walikuwa wanapata bahati kuwa na ndugu au marafiki ambao walikuwa wakibahatisha kuwafundisha uchezaji mbalimbali wakati wa likizo, basi mwanafunzi wa aina hiyo anakuwa maarufu sana mara arudipo shule na watu wote wanaanza kumuiga  uchezaji ili kujitayarisha kwa social evening.
Ili kujaribu kuwarudishia kumbukumbu wazee walioshiriki haya miaka hiyo na kuwaonyesha wale ambao hawakupitia  enzi hizo nimetayarisha ‘social evening’ kila Ijumaa kwenye ukumbi wa Salender Bridge Upanga, Dar es Salaam, kuanzia tarehe 8 Septemba 2017. Kuanzia saa moja jioni na kuendelea siku hiyo na kila Ijumaa baada ya hapo, muziki utarudishwa nyuma enzi za miaka ya 60,70, na 80. Saa moja usiku utaanza muziki laini, zikipigwa nyimbo laini zilizokuwa maarufu, hivyo sauti za Skeeter Davis, Bobby Bare, Jim Reeves, zitasikika tena, baada ya hapo kutakuwa na maonyesho ya video mbalimbali za wanamuziki wa zamani wakiwa jukwaani. Franco, Tabu Ley, Dr Nico, Bella bella, Lipua Lipua, na kutoka hapa kwetu video za Maquis enzi ya marehemu Chinyama Chiaza, Vijana Jazz, Simba wa Nyika na kadhalika, hatimae dansi rasmi litaanza kwa muziki wa aina mbalimbali na watakaofika wataweza tena kucheza nyimbo ambazo pengine hawajawahi kuzisikia tena toka walipocheza muziki walipokuwa sekondari miaka ya 60. Jioni hiyo itakuwa pia ya kukutana na marafiki na jamaa ambao wamepoteana miaka mingi na kukumbushana vituko vya ujana wao, hakika sasa imepatikana nafasi ya wazee nao kujipatia mahala pa kwenda kupata burudani ya enzi zao.