Thursday, July 28, 2016

URAFIKI JAZZ BAND NYIMBO ZAKE APATA UHAI MPYA



Leo nimeamka na wimbo wa Kwa Mjomba wa Urafiki Jazz Band, wimbo huo ni utunzi wa Frank Masamba ambaye kwa sasa ni mpiga saksafon na mwalimu wa chombo hicho;
Nilipokwenda kwa mjomba, Nilikutana na binamu yangu,
Na kwa kweli tulipendana, wazazi wetu walitukatalia tusioane
Eti kwa sababu yeye ni mtoto wa mjomba,
Ndivyo ilivyokuwa vigumu kwetu kufunga ndoa
Nilipokwenda kwa mjomba, Nilikutana na binamu yangu,
Na kwa kweli tulipendana, wazazi wetu walitukatalia tusioane
Eti kwa sababu yeye ni mtoto wa mjomba,
Ndivyo ilivyokuwa vigumu kwetu kufunga ndoa

       Chorus
Wazazi ninansema nasononeka, kwa vile msichana nilimpenda
Basi mwanangu nakuomba usisikitike sana , tuliza roho dunia hii ni pana sana kijana
Wazazi ninansema nasononeka, kwa vile msichana nilimpenda
Utampata wako mwingine pia utampenda, mtoto wa mjomba kweli kuoana si vizuri

Wazazi ninansema nasononeka, kwa vile msichana nilimpenda
Basi mwanangu nakuomba usisikitike sana , tuliza roho dunia hii ni pana sana kijana
Wazazi ninansema nasononeka, kwa vile msichana nilimpenda
Utampata wako mwingine pia utampenda, mtoto wa mjomba kweli kuoana si vizuri

Katika  zama hizi ukisikia neno ‘kuchakachua’ maana yake huwa kufanya jambo ambalo si halali au sahihi. Lakini neno ‘Chakachua’ katika miaka ya 70 na 80 lilikuwa na maana ya mtindo wa bendi maarufu wakati huo, na neno hilo lilitokana na mtindo wa bendi hiyo iliyokuwa inapiga mtindo iliyouita Mchakamchaka, neno lililofupishwa na wanamuziki wa bendi hii na kuitwa ‘Chaka Chuwa’. Bendi hii iliitwa Urafiki Jazz Band. Bendi hii  ilianzishwa mwaka 1970 ikiwa inamilikiwa na  kiwanda cha nguo cha Urafiki kilichokuwa Ubungo. Jina rasmi la kiwanda hicho lilikuwa ni FRIENDSHIP TEXTILE MILL. Kiwanda kilijengwa kwa msaada wa watu wa Jamhuri ya China na kwa urafiki huo kilipewa jina la Friendship Textile. Bendi ilianzishwa ili kutangaza bidhaa hasa Khanga na Vitenge za kiwanda hiki kwani wakati huo kulikuwa na viwanda vingine kadhaa vya nguo nchini kama vile Mwatex, Mutex, Kiltex, na kadhalika. Meneja Mkuu wa kiwanda cha Urafiki Bw. Joseph Rwegasira aliubariki mpango huo wa kuanzishwa bendi ya dansi ya kiwanda na hivyo aliidhinisha malipo ya hundi ya Shs. 50,000/= kununulia seti ya vyombo vya muziki kutoka katika duka la Dar Es Salaam Music House ambalo mpaka leo lipo katika mtaa wa Samora Avenue Dar Es Salaam.
Uongozi wa kiwanda ulimuajiri muimbaji Juma Mrisho Feruzi aliyekuwa maarufu kwa jina la Ngulimba wa Ngulimba na kumpa jukumu la kutafuta wanamuziki kwa ajili ya bendi hii. Ngulimba alichukua wapigaji watano kutoka Orchestre African Qillado, bendi ambayo aliipigia kabla ya kujiunga na Urafiki. Wanamuziki aliowachukua walikuwa ni Michael Vincent Semgumi mpiga gitaa la Solo, Ayoub Iddi Dhahabu mpiga gitaa zito la Bass, Abassi Saidi Nyanga mpulizaji wa Tenor Saxophone na Fida Saidi mpulizaji wa  Alto Saxophone. Wanamuziki wengine walikuwa  tayari waajiriwa wa kiwanda cha Urafiki  kama vile Juma Ramadhani Lidenge mpiga gitaa la Second Solo, Mohamed Bakari Churchil aliyepiga gitaa la rhythm, Ezekiel Mazanda pia alipiga rhythm, Abassi Lulela  kwenye Besi, Hamisi Nguru  Muimbaji, Mussa Kitumbo  Muimbaji, Cleaver Ulanda  Muimbaji, Maarifa Ramadhani kwenye Tumba, Juma Saidi mpiga maraccass na Hamisi Mashala  mpiga drums. Hilo ndilo lilikuwa kundi la kwanza la Urafiki Jazz Band. Mtindo walioanza nao Urafiki ulijulikana ‘Mchaka Mchaka’ na baadae ukabadilika na kuwa ‘Chaka Chua’ na hatimae wakati bendi inaelekea ukingoni mwa uhai wake walipiga mtindo wa ‘Pasua’ na ‘Patashika’.
Katika uhai wake  bendi ya Urafiki ilipitiwa na wanamuziki wengi waliokuwa maarufu wakati huo na wengine kuja kuwa maarufu baadae,  wakiwemo Gideon Banda mpuliza saxophone kutoka Morogoro Jazz, Thobias Cosmas Chidumule na Frank Mahulu ambao walikuwa  waimbaji waliotokea Western Jazz waliingia mwaka 1973 na kuongeza nguvu katika safu ya uimbaji. Baadae wapiga trampeti Mkali na Hidaya kutoka Morogoro walijiunga wakifuatana na Ali Saidi alietokea Cuban Marimba akipiga gitaa la kati (rhythm) na baadae mwaka 1975, Mganga Hemedi kutoka Tanga, akitokea Atomic Jazz, nae alijiunga na kuwa upande wa solo na rhythm.

Urafiki Jazz Band ilirekodi nyimbo zaidi ya  mia tatu zilizoelezea siasa, mapenzi, nasaha na mafundisho na pia kukosoa. Baadhi ya nyimbo zake za siasa zilizopata umaarufu ni kama zile Mwenyekiti Nyerere, Mauaji ya Soweto, Jembe na Panga na kadhalika.
Mwaka 1975 Bendi ilishiriki katika mashindano ya bendi za muziki wa dansi yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja,  Dar Es Salaam na kushika nafasi ya tatu, hili lilimuwezesha Juma Mrisho Ngulimba wa Ngulimba, kama Kiongozi wa Urafiki kupata nafasi ya kusindikizana na bendi ya Afro 70 kwenda Nigeria kwenye maonyesho ya mtu mweusi yaliyofanyika huko. Urafiki Jazz band haipo tena lakini hakika nyimbo zake bado zinapendwa na kuna vikundi vya vijana vimeanza kurudia nyimbo hizo kwa staili mpya, na hata tungo zake nyingine zikisikika katika mtindo wa taarab. Makala hii niliitoa kwama mara ya kwanza katika gazeti la MWANANCHI JUMAMOSI, na kila Jumamosi usikose makala kama hizi

Tuesday, July 19, 2016

BAVON MDOGO WAKE FRANCO LUAMBO LWANZO



Ganda la Album iliyokuwa na wimbo Maseke ya Meme. Tshimanga Assossa  aliwa wa pili toka kulia
Wimbo Maseke ya Meme ulipigwa katika miaka ya 70 na bendi maarufu ya Negro Success. Kundi lililokuwa likiongozwa na mdogo wake Franco Luambo Luanzo Makiadi, nae si mwingine ila ni mpiga solo mkali Bavon Siongo au maarufu kama Bavon Marie Marie aliyezaliwa May 27, 1944 ambaye pia alitunga wimbo huu marufu. Wimbo huu Maseke ya Meme au kwa Kiswahili ‘Pembe za kondoo’ ulianza kusambazwa March 1970. Mashahiri ya wimbo huu yalileta utata sana baada ya kifo cha Bavon Marie Marie kilichotokea muda si mrefu baada ya wimbo huu kutoka hewani.  Sehemu ya mashahiri ya wimbo huu yalisema hivi;
Bavon Marie Marie
 Nalilia maisha yangu
Sijachoka kuishi
Lakini wanataka nitangulie
Naacha kuongea
Nasubiri kifo.
Bahati mbaya sana Agosti 5, 1970, siku ya Jumatano, Bavon Marie Marie akakumbwa na ajali ya gari iliyosababisha kifo chake katika mtaa wa Avenue Kasavubu, mjini Kinshasa. Wimbo ule ukaonekana kama ni utabiri wa kifo chake mwenyewe. Kwa vile Franco hakufurahia mdogo wake kuingia katika muziki,watu wakatafsiri kuwa alikuwa amemloga mdogo wake ambae alifariki akiwa na umri wa miaka 34 tu. Kuna hadithi nyingine inayosema kifo cha Bavon kilitokea muda mfupi baada ya ugomvi na kaka yake kwa kisa kuwa Franco alikuwa ametembea na Lucy aliyekuwa bibi wa Bavon. Inasemekana Bavon aliondoka spidi na gari akiwa na hasira na muda mchache baadae akaaingia chini ya lori.
Kuna nyimbo nyingi duniani ambazo watu hudhani ni kama utabiri wa wanamuziki kabla ya kufa. Wimbo Ee Mola wangu wa Salum Abdallah wa Cuban Marimba ni mfano mojawapo. Kuna wanamuziki wengi wanaogopa kuimba au kutunga nyimbo kuhusu kifo kwa imani kuwa ukitunga wimbo wa namna hiyo unaita kifo.