Friday, November 27, 2015

DAVID MUSA AFARIKI DUNIA


MWANAMUZIKI mwanzilishi wa kundi la Safari Trippers na aliyekuwa mwalimu wa wanamuziki wengi sana David Musa amefariki usiku wa kuamkia leo. Msiba uko nyumbani kwake Chang'ombe. Habari zaidi tutazileta kadri tutakavyozipata. 
safari trippers
Kushoto mwenye miwani David Musa, wa tatu Marijani Rajabu na kulia mwisho Jumanne Uvuruge mtunzi wa wimbo wa Georgina.
 Mungu amlaze pema

Monday, November 23, 2015

MFAHAMU MBARAKA YUSUPH MWANAMUZIKI WA NATIONAL PANASONIC NA POWER IRANDA

“NIMEACHANA na muziki wa dansi hivi sasa na nimeamua kugeukia sanaa ya filamu, ambapo sababu kubwa ni kupungua kwa kasi yangu ya ucharazaji gitaa, kutokana na kupata mara mbili kwa nyakati tofauti, ugonjwa wa kupooza.”
Hayo ni maneno ya Mbaraka Yusuph, kati ya wacharazaji mahiri wa zamani wa magitaa yote pamoja na Saxophone, aliyewahi kuzitumikia bendi mbalimbali hapa nchini, zikiwamo, The Smashers, National Panasonic, OSS ‘Power Iranda’, Seven Blind Beats na the Big Africa ya Arusha..ENDELEA HUKU

Monday, November 9, 2015

MWANAMUZIKI MKONGWE CAPT JOHN SIMON AFARIKI DUNIA


IMG_9699
 Capt John Simon
 MWANAMUZIKI mkongwe ambaye kwa siku za karibuni alikuwa kwenye bendi ya Shikamoo Jazz, Capt John Simon, amefariki dunia leo katika hospitali ya Muhimbili. Mzee huyu alikuwa mmoja ya waanzilishi wa NUTA Jazz band, na baadae kadri ya maelezo yake mwenyewe, Mheshimiwa Rashid Kawawa, ndie alimtoa NUTA Jazz na wanamuziki wengine na kwenda kuanzisha JKT Jazz Band, iliyopata umaarufu kama Kimbunga Stereo. 
FIL6
Waimbaji wa NUTA Jazz Band, toka kulia John Simon, Muhidin Gurumo, na kushoto Ally Akida
  Mzee John Simon pia alikuwa mwanzilishi wa Shikamoo Jazz Band, bendi ambayo ameitumikia mpaka siku zake za mwisho. Capt John Simon pia alikuwa makamu mwenyekiti wa CHAMUDATA mwishoni mwa miaka ya 90, akiwa makamu wa John Kitime, na hatimae kuwa mwenyekiti baada ya John kitime kujiuzuru nafasi yake. Taratibu za mazishi zitapatikana baada ya ndugu kukutana. Msiba uko nyumbani kwa marehemu Tabata Kimanga.