Saturday, March 22, 2014

MARCH 23 2014, MIAKA 19 TOKA KIFO CHA MWANAMUZIKI MARIJANI RAJABU-DOZA..BY FRED MOSHA


Machi 23 mwaka 1995 ni siku isiyosahaulika kwa wapenzi wa muziki wa zamani nchini. Siku hiyo ndipo tulipompoteza mwanamuziki kipenzi chetu, Marijani Rajabu. Alizikwa kesho yake yaani Machi 24 kwenye makaburi ya Kisutu.
Historia ya gwiji huyu inaanzia Machi mwaka 1955. Mara baada ya kumaliza elimu yake ya Sekondari, Marijani alijitosa moja kwa moja kwenye muziki licha ya kuwa awali aliwahi kuwa Mlinda Mlango hodari kwenye timu mbalimbali ikiwemo Timu yake ya Shule. Mwaka 1970 alikuwa miongoni mwa wanamuziki wa bendi ya STC Jazz na kushiriki kuimba na kutunga vibao kadhaa. Ewe mwana inaweza kuwa ndio wimbo maarufu zaidi. Mwaka 1972 alijiunga na The Trippers ya David Mussa ambayo kwa wakati huo ilikuwa inapiga zaidi nyimbo za hoteli na za kukopi na muimbaji wao kiongozi wakati huo alikuwa Ali Rajabu. Kuingia kwa Marijani kukaleta mapinduzi mapya kabisa ndani ya bendi na muziki wake. Ikiathiriwa zaidi na muziki wa vijana wakati huo, muziki wa Soul, Trippers ambayo punde ikaongeza neno Safari kwenye jina lake ilianza kupiga na kutunga nyimbo zake kali na ambazo hata leo hii bado zinakumbukwa. Wimbo Georgina ni mfano tu. Marijani alishiriki kutunga, kuimba nyimbo karibu zote za Trippers sanjari na kupiga gitaa kwa baadhi ya nyimbo. Mfano wimbo Olila ambao alipiga rhythm na kuimba.
Safari Trippers-Marijani wa pili toka kulia waliosimama. Wa kwanza mwenye kofia ndie mtunzi wa wimbo Georgina- Uvuruge
Mwaka 1976, Marijani na baadhi ya wanamuziki wa Trippers waliamua kuihama bendi na kwenda baadaye kuasisi Dar es salaam International chini ya umiliki wa Mzee Zakaria Ndabemeye ambaye bado yu hai hadi sasa. Baadhi ya wanamuziki hao ni pamoja na Abel Baltazar kutoka Msondo, Kassimu Mponda kutoka Trippers, Abdallah Gama, Joseph Mulenga, Haruna Lwali na George Kessy Omojo waliokuwa wanapiga muziki Magot pale, Said Mohamed kutoka Polisi Jazz, Cosmas Chidumule kutoka Urafiki, Belesa Kakere kutoka Biashara Jazz, Joseph Bernard kutoka Trippers, Ali Rajabu kutoka Trippers, na King Michael Enock kutoka Dar es salaam JazzAkiwa Dar Inter alishiriki kutunga nyimbo mbili, Betty na Sikitiko. Hata hivyo kama waswahili wanavyosema mafahari wawili hawakai zizi moja ndivyo ilivyotokea kati yake na Abel Balthazal kiasi cha hatimaye Marijani kufukuzwa ndani ya bendi kutokana na ubishi kuhusu wimbo aliotunga Marijani, kuna maelezo kuwa wimbo ulionekana unafanana na wimbo fulani toka Kongo na hivyo Marijani akatakiwa aubadilishe na ndipo ugomvi ukaanza. Hata hivyo mwishoni mwa mwaka 1978, Marijani alirejeshwa tena kundini kutokana na rundo la wanamuziki wa Dar Inter kuihama bendi kwa kishindo kikubwa na kwenda kuifungua bendi mpya kabisa ya Orchestra Mlimani Park. Aliporejeshwa Marijani alikuja na wanamuziki wengi wapya wakati huo kama akina Christopher Kasongo, Mohamed Tungwa, Mafumu Bilal, Hamis Milambo, Athuman Momba, Mzee Alex Kanyimbo na wengine na kuja na mtindo wa Super Bomboka. Katika kudhihirisha hasira zake kwa Abel, Marijani alimtungia Abel wimbo wa kumnanga ukiitwa Kidudu mtu ambao hata hivyo RTD waliukataa kuurekodi, jambo lililokuwa kawaida enzi hizo kwa redio kukataa wimbo. Sifa nyingine ambayo Marijani alikuwa nayo ni kuibua wanamuziki chipukizi kama alivyofanya mwaka 1983 alipomuibua kutoka Tanga kijana Mkuu Waziri Kungugu Kitanda Milima almaaruf Fresh Jumbe ambaye kwa hakika kabisa Marijani hakujutia kumchukua kijana huyo. Alimuamini kupita maelezo kiasi kwamba wakati mwingine alikuwa akimuachia bendi aongoze na yeye anapumzika nyumbani. Mbali na Fresh, wanamuziki wengine ni kama vile Tino Masinge, Mohamed Mwinyikondo, Juma Choka na wengine kibao.
Tanzania All Stars..Marijani wapili toka kulia
Hata hivyo safari ya Dar Inter ilikoma mwaka 1987 kutokana na sababu za kawaida za kufa kwa bendi lakini kubwa ni uchakavu wa vyombo. Hata hivyo Marijani aliendelea kufanya muziki na kwa kipindi kifupi amewahi kucheza na Kurugenzi ya Arusha na Mwenge Jazz ambayo alirekodi nayo wimbo mmoja wa Ukimwi. Mwaka huohuo wa 1987 Marijani na Muhidin Maalim Gurumo waliliongoza kundi la wanamuziki zaidi ya 50 kutunga nyimbo maalum hasa kwa maadhimisho ya miaka 10 ya CCM na 20 ya Azimio la Arusha. Naizungumzia Tanzania All Stars. Aidha mwaka 1994 aliwahi mkurekodi zong zing na marehemu Eddy Sheggy. Bendi yake ya mwisho ilikuwa ni Africulture ama Mahepe Ngoma ya Wajanjailiyokuwa mali ya Rogers Malila, alikokuwa na wanamuziki kadhaa kama akina  Hassan Kunyata na wengine. Bado Marijani ataendelea kukumbukwa na wapenda muziki kote nchini na hata Afrika kwa ujumla kwa nyimbo zake zenye mafundisho na tamu huku akienzi utamaduni na ngoma za kwao Kigoma.Chini hapa ni video ya Marijani akipiga gitaa na kuimba wimbo aliotunga enzi za Dar International hapa alikuwa na kundi la Africulture katika ukumbi wa Mango.

No comments: