Sunday, March 30, 2014
Saturday, March 22, 2014
MARCH 23 2014, MIAKA 19 TOKA KIFO CHA MWANAMUZIKI MARIJANI RAJABU-DOZA..BY FRED MOSHA
Machi 23 mwaka 1995 ni siku isiyosahaulika kwa wapenzi wa muziki wa zamani nchini. Siku hiyo ndipo tulipompoteza mwanamuziki kipenzi chetu, Marijani Rajabu. Alizikwa kesho yake yaani Machi 24 kwenye makaburi ya Kisutu.
Historia ya gwiji huyu inaanzia Machi mwaka 1955. Mara baada ya kumaliza elimu yake ya Sekondari, Marijani alijitosa moja kwa moja kwenye muziki licha ya kuwa awali aliwahi kuwa Mlinda Mlango hodari kwenye timu mbalimbali ikiwemo Timu yake ya Shule. Mwaka 1970 alikuwa miongoni mwa wanamuziki wa bendi ya STC Jazz na kushiriki kuimba na kutunga vibao kadhaa. Ewe mwana inaweza kuwa ndio wimbo maarufu zaidi. Mwaka 1972 alijiunga na The Trippers ya David Mussa ambayo kwa wakati huo ilikuwa inapiga zaidi nyimbo za hoteli na za kukopi na muimbaji wao kiongozi wakati huo alikuwa Ali Rajabu. Kuingia kwa Marijani kukaleta mapinduzi mapya kabisa ndani ya bendi na muziki wake. Ikiathiriwa zaidi na muziki wa vijana wakati huo, muziki wa Soul, Trippers ambayo punde ikaongeza neno Safari kwenye jina lake ilianza kupiga na kutunga nyimbo zake kali na ambazo hata leo hii bado zinakumbukwa. Wimbo Georgina ni mfano tu. Marijani alishiriki kutunga, kuimba nyimbo karibu zote za Trippers sanjari na kupiga gitaa kwa baadhi ya nyimbo. Mfano wimbo Olila ambao alipiga rhythm na kuimba. Safari Trippers-Marijani wa pili toka kulia waliosimama. Wa kwanza mwenye kofia ndie mtunzi wa wimbo Georgina- Uvuruge |
Tanzania All Stars..Marijani wapili toka kulia |
Sunday, March 9, 2014
URAFIKI JAZZ BAND 2
Urafiki Jazz Band |
Bendi ya Urafiki ikiwa katika hali yake ya uchanga mwaka 1970 ilipata ajali ya gari, wakati kundi zima likitoka katika onyesho huko Chang’ombe, gari lao aina ya Volkswagon Kombi liligonga mti maeneo kona ya Kigogo na Msimbazi Mission.
Baadhi ya wanamuziki waliumia sana na gari lao, likawa halifai kabisa.
Wapigaji walioumia walikuwa ni Hamisi Mashala – Drummer Boy - alivunjika mguu, Mohamed Bakari Churchil aliumia kichwani na kushonwa nyuzi kadhaa, na pia Ayoub Iddi Dhahabu na Maarifa Ramadhani walipata maumivu makali kwa ndani mwilini.
Wapigaji walioumia walikuwa ni Hamisi Mashala – Drummer Boy - alivunjika mguu, Mohamed Bakari Churchil aliumia kichwani na kushonwa nyuzi kadhaa, na pia Ayoub Iddi Dhahabu na Maarifa Ramadhani walipata maumivu makali kwa ndani mwilini.
Bendi ilisimamisha maonyesho yake kwa muda hadi wanamuziki wake walipopata nafuu na kuanza maonyesho tena. Hali ya ajali ile ilileta fikra mbaya kwa wanamuziki hao na wapenzi wao na ilionekana kana kwamba kulikuwa na mkono wa mtu katika ajali ile. Juma Mrisho ‘Ngulimba’ alitunga wimbo ‘Nimekosa Nini Jama’, wimbo ulioelezea kadhia hiyo. Katika kipindi hiki dhana ya ushirikina ilitawala sana katika bendi mbalimbali. Vifo vya wanamuziki mara nyingi vilihusishwa na upinzani katika bendi.
Kufikia miaka ya ‘80’ kati bendi ya Urafiki ikawa inasua sua kutokana na uchakavu wa vyombo na Menejimenti iliyokuwepo wakati huo haikuwa tayari kutoa pesa kununulia vyombo vipya. Bendi ya Urafiki ilifikia tamati katika miaka ya ‘80’ kati kati na bendi hiyo ikatoweka katika anga za muziki na kubaki historia.
URAFIKI JAZZ BAND 1
Meneja Mkuu wa kiwanda cha Urafiki Bw. Joseph Rwegasira aliubariki mpango huo wa kuanzishwa bendi ya dansi ya kiwanda na hivyo aliidhinisha malipo ya hundi ya Shs. 50,000/= kununulia seti ya vyombo vya muziki kutoka katika duka la Dar Es Salaam Music House ambalo mpaka leo lipo katika mtaa wa Samora Avenue – Dar Es Salaam.
Ili kupata kundi lililo bora, Menejimenti ya kiwanda cha Nguo cha Urafiki ilimuajiri Juma Mrisho Feruzi maarufu kwa jina la Ngulimba wa Ngulimba na kumuagiza atafute wapigaji kutoka popote ili kuunda kundi imara.. Katika kuhakikisha bendi hiyo mpya inasimama, Ngulimba alichukua wapigaji watano kutoka Orchestre African Qwillado, bendi ambayo aliipigia kabla ya kuanza Urafiki. Na hii ndio maana nyimbo za mwanzoni za Urafiki Jazz Band zilionekana kama zina mahadhi ya Orch. Qwillado.
Wanamuziki aliowachukua Ngulimba kutoka Orch. Qwillado walikuwa ni Michael Vincent Semgumi, mpiga gitaa la Solo, Ayoub Iddi Dhahabu – Besi, Abassi Saidi Nyanga – Tenor Saxophone na Fida Saidi, Alto Saxophone. Ngulimba yeye akawa Muimbaji na pia Kiongozi wa Bendi.
Wanamuziki wengine wa mwanzo ambao waliungana na hao watano waliotoka Orch. Qwillado ambao tayari walikwisha ajiriwa kiwandani Urafiki, walikuwa – Juma Ramadhani Lidenge – Second Solo, Mohamed Bakari Churchil – gitaa la kati (rhythm), Ezekiel Mazanda – rhythm, Abassi Lulela – Besi, Hamisi Nguru – Muimbaji, Mussa Kitumbo – Muimbaji, Cleaver Ulanda – Muimbaji, Maarifa Ramadhani – Tumba, Juma Saidi – Manyanga (maraccass) na Hamisi Mashala – mpiga drums.
Mtindo walioanza nao Urafiki ulijulikana ‘Mchaka Mchaka’ na baadae ukabadilika na kuwa ‘Chaka Chua’ na hatimae mwisho mwisho bendi inaelekea ukingoni walipiga mtindo wa ‘Pasua’ na ‘Patashika’
Mwaka 1971 Gidion Banda, mwanamuziki kutoka bendi ya Morogoro Jazz alijiunga na kundi akiwa mpigaji wa Saxophone.
Aidha, Bendi ya Urafiki ilipitiwa na wanamuziki wengi baadhi wakiwemo Gideon Banda mpuliza saxophone kutoka Morogoro Jazz wengine wakiwemo Thobias Cosmas Chidumule na Frank Mahulu – Waimbaji waliotokea Western Jazz (Saboso) mwaka 1973 na kuongeza nguvu katika safu ya uimbaji. Waimbaji hao walishiriki nyimbo nyingi baadhi zikiwa Tausi Karuka, Jembe na Panga (Geza Ulole), Kosa la Nani, Mauaji ya Soweto, Rukia Hukusikia, Maonyesho ya Mtu Mweusi n.k.
Pia waliongezeka Mkali na Hidaya kutoka Morogoro wakipuliza matarumbeta, hao walikuja 1973 na Ali Saidi alietokea Cuban Marimba akipiga gitaa la kati (rhythm) na baadae mwaka 1975, Mganga Hemedi kutoka Tanga, akitokea Atomic Jazz, nae alijiunga na kuwa upande wa solo na rhythm.
Urafiki Jazz imetunga nyimbo nyingi, zaidi ya mia tatu zinazoelekeza kwenye siasa, mapenzi, nasaha na mafundisho na pia kukosoa. Baadhi ya nyimbo zake za siasa zilizopata umaarufu ni kama zile Mwenyekiti Nyerere, Mauaji ya Soweto, Jembe na Panga n.k..
Mwaka 1975 Bendi ilishiriki katika mashindano ya bendi za muziki wa dansi yaliyofanyika Mnazi Mmoja – D’Salaam na kushika nafasi ya tatu na Mzee Ngulimba, kama Kiongozi wa Urafiki aliiwakilisha Tanzania pamoja na bendi ya Afro 70 iliyopata nafasi ya kwanza na baadhi ya vikundi vya utamaduni kutoka Tanzania Bara na Zanzibar nchini Nigeria katika maonyesho ya mtu mweusi yaliyofanyika huko.
Saturday, March 1, 2014
ASIA DARWESH DADA MPIGA KINANDA AMBAYE KAACHA REKODI YA PEKEE TOKA ALIPOFARIKI 1995
Asia Darwesh kwenye kinanda pembeni yake ni Johnny Rocks kwenye drums. Haba wakiwa Bandari Grill- New Africa Hotel-enzi za Ngoma za magorofani |
MAKALA HII IMEANDIKWA NA MWANDISHI FRED MOSHA
Jina Asia Daruwesh, sio jina geni kwa mashabiki wa muziki Tanzania na pengine Afrika mashariki kwa ujumla. Huyu Dada anaweza kutajwa kama mpiga kinanda wa kwanza kabisa mwanamke kuwahi kutokea kwenye rhumba letu la kitanzania ingawa siku za nyuma kuliwahi kuwa na bendi ya akinamama watupu ikiitwa Women Jazz ambayo kuanzia magitaa, masaxphones na kuimba walikuwa akinamama watupu. Asia Daruwesh alizaliwa mwaka 1964. Ingawa alikuwa na asili ya Zanzibar, maisha yake kwa kiasi kikubwa yalikuwa Zambia kuanzia utotoni hadi anakua na huko ndiko alikopata inspiration ya kuwa mwanamuziki. Kwa hapa kwetu Tanzania, jina la Asia Daruwesh lilisikika kwenye safu ya mwanzo kabisa ya King Kikii mwaka 1984 akiwa na Kikii mwenyewe, Mumba Kisi, Kapelembe Coco, Samba Wa Mikalay, Zahoro Bangwe, Mohamed Idd Control, Matei Joseph na wengine. Alishiriki kupiga kinanda kwenye nyimbo kadhaa za bendi hii iliyokuwa ikitumia mtindo wa Embalasasa Shika Break kama Kinyume, Dodoma Capital, Njimina, Mimi na we, Kibwanange, Malalamiko na nyingine kadhaa huku nyimbo kama Lamanda na Kitoto chaanza tambaa akimuachia Ally Hemed Star huyuhuyu ambaye leo anajulikana kama muimbaji na mtunzi mzuri wa Taarab. Hata hivyo mwaka 1986 mwishoni aliihama bendi hiyo na kujiunga kwenye safu ya mwanzoni ya MK Group wakati huo. Nyimbo karibu zote za kuanzia toleo la kwanza hadi la tatu la MK Group amepiga kinanda yeye. Hassan Rehani sijui anakumbuka nini ukimtajia MK Group!! Mwaka 1989 alikuwa miongoni mwa wanamuziki wanne walioihama MK Group na kwenda kuasisi Bicco Stars. Angekuwemo na Joseph Mulenga katika group hii lakini alirudi nyuma. Akiwa Bicco aliungana na akina Kinguti System, Fresh Jumbe, Athuman Cholilo Mashida, Seif Rengwe, Sid Morris, Mafumu Bilal, Andy Swebe Ambassadeur na wengine Katika bendi hii ndiko alikotunga wimbo wake wa kwanza wa Bwana Kingo na pia akashiriki kuimba na ameimbisha wimbo huo. Mwaka 1992 alianzisha bendi yake mwenyewe akiita Zanzibar Sound ikitumia mtindo wa Wesaka Dance akiwa na akina Bob Gad William, Hezron Ludala ama Bob Ludala, Fariala Mbutu, na baadaye akina Mohamed Idd Control na Shaban Lendi. Wimbo Banana ambao baadaye Bob Gad alikuja kuurudia akiwa na Twanga Pepeta ulirekodiwa kwa mara ya kwanza na bendi hii. Aidha wimbo Hadija ambao Fariala alikuja kuurudia na Kilimanjaro Connections ulirekodiwa nao huku Ludala akiwa muimbaji Kiongozi. Kufariki dunia kwa Asia Daruwesh ama kwa jina la utani Super Mama mwaka 1995 ndiko kulikohitimisha safari ya bendi hii. Ni hayo tu
Subscribe to:
Posts (Atom)