Thursday, February 13, 2014

ULALE PEMA KING KESTER EMENEYA


 Jean Emeneya Mubiala Kwamambu, maarufu kama King Kester Emeneya amefariki leo 13 February 2014 alfajiri saa kumi na moja na nusu katika hospitali ya  Marie Lannelongue katika jiji la  Paris akiwa na umri wa miaka 57.

Mwanamuziki huyu kiongozi na  mlezi wa kundi la Victoria Eleison. King alipata mshtuko wa moyo mara ya kwanza aliposikia kifo cha Tabu Ley mwezi November 2013 na akatibiwa katika hospitali hiyo ya Marie Lannelongue. Inaonekana  Kester Emeneya alishtushwa sana na kifo cha Tabu Ley ambaye alimuiga kwa mambo mengi. Rafiki wa Kester ambaye ni mwandishi wa habari Deck Mbutanganga alisema kuwa tangu kifo cha Tabu Ley, Kester hakurudia katika hali yake ya kiafya, alizidi kudhoufika mpaka alipofikia mauti yake..
King Kester alizaliwa mji wa Kikwit katika jimbo la Bandundu, magharibi mwa Jamhuri ya Kongo, alipofikia umri wa miaka 17 alianzisha kundi la muziki la Les Anges Noir, Malaika Weusi, akiwa na Lidjo Kwempa ambaye waliendelea kushirikiana katika muziki miaka mingi baadaye. Akiwa mwanachuo anaetafuta digrii ya Political Science katika Chuo Kikuu cha Lumbumbashi,  hamu ya kuwa mwanamuziki ikamzidia, mwaka 1977 akiwa na umri wa miaka 21 akaacha Chuo na kujiunga na kundi la Viva La Musica la Papa Wemba, akapata umaarufu mkubwa sana kama muimbaji, wakati mwingi ambapo Papa Wemba hakuwepo kwenye kundi hili Kester ndie aliyekuwa kiongozi. Hatimae tarehe 24 Desemba 1982 akazindua kundi lake la Victoria Eleison , kundi lililoleta ladha mpya katika muziki wa Kongo. Kester hutajwa kuwa mwanamuziki wa kwanza wa Afrika ya Kati kuingiza synthesizer kwenye muziki wake na album yake ya Zinzi, ambao wimbo huo ulitengenezwa studio tu, iliuza zaidi ya nakala milioni moja. Hakika alikuwa ndie mwanamuziki maarufu katika Afrika ya Kati katika miaka 1980-1990. Katika maisha yake Kester alipata Tuzo nyingi sana, kitaifa na kimataifa. Werrason na JB Mpiana walitumia nyimbo zake nyingi na mikongosio yake kutengeneza Wenge Musica. Amekwisha fanya maonyesho katika mabara yote matano duniani. Alijulikana kama Entertainer of the Year na magazeti mengi ya Kongo, katika onyesho lake moja Switzerland watu zaidi ya 12,000 walihudhuria, kitu ambacho kilitokea kwa mara ya kwanza kwa mwanamuziki kutoka Afrika kufanya katika nchi ile. Mwaka 1991 alihamia Paris na mwaka  1997 aliporudi Kongo kwa mara ya kwanza  baada ya miaka 6, onyesho alilolifanya Stade des Martyrs  lilihudhuriwa na watu 80,000.  Kester anasemekana alikuwa na nyimbo zaidi ya 1000.
 Marais wote wa Kongo waliwahi kumkaribisha katika Ikulu, Mobutu Sese Seko, Rais Laurent Kabila alimkaribisha ikulu mara tatu, na alishakaribishwa mara mbili na Rais wa sasa Joseph Kabila.
King Kester Emeneya amekuwa anaishi Ufaransa toka 1991 japo alikuwa na nyumba mbili Kinshasa katika eneo la watu wenye uwezo wa kifedha
Emeneya amekwenda lakini alichokiasisi kinaendelea katika jamii ya wapiga rumba Afrika
Mungu Mlaze Pema peponi.
Tumkumbuke kwa wimbo wa Zinzi hapa katika video hii;

No comments: