Thursday, February 27, 2014

HISTORIA YA MANENO UVURUGE

Mawazo Hunja kwenye trumpet, Maneno Uvuruge kwenye gitaa
Maneno Uvuruge ni moja ya wanamuziki waliotoka katika familia ya wanamuziki ya ukoo wa Uvuruge. Kaka zake Jumanne, Stamili, na Huluka ni kati ya wapiga magitaa walioheshimika sana katika jamii ya wanamuziki wa bendi Tanzania.
Jumanne Uvuruge ambae alikuwa mkubwa wa akina Uvuruge wote, ndie aliyetunga kibao maarufu cha Georgina, kilichopigwa na Safari Trippers na kuimbwa na Marijani Rajabu. Siku zake za mwisho za maisha Jumanne alikuwa anajishughulisha na kupata riziki yake kwa kuzunguka katika mabaa mbalimbali na gitaa na kupiga maombi mbalimbali ya wanywaji, na kisha kuhama na kuelekea baa nyingine. Hayakuwa maisha rahisi.
Maneno Uvuruge hana kumbukumbu ya jinsi gani Jumanne alijifunza gitaa, lakini anajuwa kuwa Stamili alifundishwa na Jumanne. Anakumbuka zaidi jinsi Huluka alivyojifunza kwani ndie alikuwa kaka yake waliefuatana kuzaliwa. Huluka alijifunza gitaa kwa kuanza kuchonga gitaa lake mwenyewe, aliiba mishipi ya kuvulia ya baba yake na ndio zikawa nyuzi za gitaa lake, siku babake alipogundua wizi huo alivunja vunja gitaa na kumkataza asiguse mishipi yake tena, lakini akamwelekeza inakonunuliwa, Huluka alitafuta pesa na kwenda kununua mishipi na kuendelea na gitaa lake la kopo. Wakati huo Huluka alikuwa anasoma, naye Maneno akaanza hamu ya kutaka kujua kupiga gitaa akawa anaiba gitaa la kaka yake kila alipoenda shule, ilikuwa ni ugomvi kila alipokata nyuzi kwani alikuwa bado anajifunza. Jumanne na Stamili wakaanza rasmi kumfundisha gitaa Huluka nae akalijua vizuri sana. Si muda mrefu baadae nae akaanza rasmi kumfundisha mdogo wake. Maneno anasema wimbo wa kwanza kakake kumfundisha ni ile rhythm ya wimbo Novelle Geneation wa Orchestra Lipualipua, wimbo huu ulikuwa ni kipimo muhimu kwa wapiga rythm enzi hizo. Freddy Benjamin ndie aliyemshauri kujiunga na Bendi. Alimkaribisha UDA Jazz ambako alikuwa akiimbia na pamoja na kuweza kupiga gitaa alifanyiwa mizengwe na mpiga rhythm aliyekuweko na ambae pia alikuwa katibu wa bendi. Freddy alimuombea kazi Super Rainbow iliyokuwa na makao yake makuu pale Sunlight Bar Mwananyamala B. Na hapo akakutana na wanamuziki kama Hatibu Iteytey, Nuzi Ndoli, Rocky, Mzee Bebe, Akina Eddy Sheggy walikuwa bado hawajajiunga na bendi hii wakati huo.
 
Keppy Kiombile Bass, Maneno Uvuruge Rythm, Makuka Second solo, Juma Choka Drums, Lubaba Solo enzi ya Maquis

Katika kipindi ambapo Maneno Uvuruge alikuwa akipigia Super Rainbow ndipo Eddy Sheggy na Emma Mkello walipojiunga, hawa hukumbukwa sana kwenye bendi hii kwa ajili ya ule wimbo Milima Ya Kwetu, pia nae Banza Tax akajiunga kipindi hiki. Na kule Mabibo bendi ya Mambo Bado ilipata msukosuko na kuvunjika kwa mara ya kwanza na hivyo wanamuziki wake Juma Choka mpiga drums, Lodji Mselewa na Nana Njige pia wakajiunga na kundi na Super Rainbow, lakini hawakukaa sana Assossa aliweza kuifufua tena Mambo Bado na wote wakarudi wakifuatana na Maneno Uvuruge. Lakini tayari bendi ilikuwa iko katika hali mbaya kwani Assossa aliacha tena akiwa katika harakati ya kuunda bendi mpya na Mambo Bado ikafa rasmi. Juma Choka akamtaarifu Maneno kuwa Urafiki Jazz kuna nafasi ya kazi na hapo akenda na kusailiwa na Ngulimba wa Ngulimba, Marehemu Mzee Juma Mrisho, Urafiki nayo ilikuwa katika siku zake za mwisho lakini bado yule mpiga solo mahiri Michael Vicent alikuweko. Kipindi hiki pia waliingia Mohamed Gota gota na Hussein Jumbe. Maneno Uvuruge sasa alianza kufahamika kwa wanamuziki wengine kuwa ana uwezo mkubwa na bendi zikaanza kumsaka, na kuanzia hapo amekuwa hatafuti kazi bali anatafutwa. Bendi ya kwanza kumchukua ilikuwa ni Maquis, alichukuliwa ili awe mpiga gitaa la rhythm, aliwakuta wapiga rhythm wawili, huko, Mbwana Cox na Makuka. Akawa mwanamuziki wa Maquis wakati huo wapiga solo wa bendi hiyo walikuwa ni Nguza Viking, na Mzee Lubaba.
Mwanamuziki Belly Kankonde akakutana na Marehemu Mzee Mwendapole na kuamua kuipa uhai bendi ya Afrisongoma. Kankonde akawashawishi wanamuziki wenzie wanne wa Maquis, Maneno Uvuruge (guitar),Kiniki Kieto(mwimbaji), Comson Mkomwa(saxophone) na Keppy Kiombile(bass) wakahamia Afrisongoma. Maneno hakukaa muda mrefu kwani Nguza alimfuata yeye na Comson na kuwarudisha Maquis , na kwa kuwa walikuwa wamekwishapokea fedha za Mzee Mwendapole kesi ilifika polisi na ikalazimu Maquis warudishe fedha hiyo. Lovy Longomba alijiunga na Maquis nae hakukaa muda mrefu Mwendapole akamshawishi akaunde upya kundi la Afrisongoma ambalo katika awamu ya kwanza liliishia kurekodi mara moja na kutokuwa na maendeleo. Lovy pia tena akamuondoa Maneno na kuhamia nae Afrisongoma.
Wakati huo Mosesengo Fan Fan yule mpiga gitaa mahiri aliyetoka kwa Franco na kupigia Matimila na Makassy alikuwa amehamia Uingereza na akawa amemtaka Kiniki Kieto awashawishi Maneno Uvuruge, Keppy Kiombile, na Vivi Kapaya wamfuate,lakini mpango huo uliishia kwa Kiniki na Vivi kuendelea na Fanfan wakati Maneno na Keppy wakahamia Afrisongoma wakiwa na Lovy. Wanamuziki kadhaa walihamia Afriso wakati huo wakiwemo Kalamazoo, na Mzee Mponda ambae baada ya kutoka Msondo alikuwa kapita Sikinde na akatua Afrisongoma. Na hapo ndipo msondo wakamchukua Maneno kwa mara ya kwanza. Alikaa kwa muda na rafiki zake akina Benno Vila Anthony wakaweza kumshawishi ahamie Sikinde. Baada ya muda si mrefu Nguza akamfuata ili kumshawishi ajiunge na Orchestra Sambulumaa. Ilikuwa ni ushawishi wa Skassy Kasambula na Emmanuel Mpangala aliyekuwa mkurugenzi wa bendi ndio ulioweza kumfanya Maneno ahamie Sambulumaa

ORCHESTRE SANTA FE ILIKUWA BENDI YA KWANZA YA WAKONGO WATUPU NCHINI?

Kati ya maswali amabayo yamewahi kuulizwa humu ni kuhusu bendi hii Orchestra Santa Fe. Hii ilikuwa mwanzo ni bendi yenye asilimia kubwa ya wanamuziki Wakongo. Kuna wakati Blogger Kiongozi Issa michuzi aliwahi kuuliza kama Je,Sante Fe ndio ilikuwa Bendi ya kwanza ya Kikongo? Sina jibu bado kuhusu hili. Wenye taarifa zaidi kuhusu Bendi hii karibuni. Bendi hii ilikuwa ikipiga pale Gateways Mnazi Mmoja maeneo ambayo kuna wakati yalikuwa maeneo muhimu katika shughuli za starehe jijini Dar es Salaam.Kuna maoni yaliwahi kutoleaa kuhusu mada hii katika blog iliyokuwa kabla ya kuzaliwa hii na haya ndio yalikuwa maelezo yao:

      1. BLACKMANNEN said...
Orchestra Santa Fe, haikuwa ya Wakongo. Bendi za Fouvette na akina "Papa Mikey" ndiyo waliokuwa Wakongo wa mwanzo Tanzania.

Orchestra Santa Fe, Tanzania Jazz Band, King Africa Jazz Band na Orchestra Quilado zote zilikuwa za Kitanzania, ila habari zake wengi hatuzijui.

It's Great To Be Black=Blackmannen
2. 
Anonymous said...
TP SANTA FE ILIKUWA NI BENDI YA WAKONGO ILINGIA NCHINI IKITOKEA ZAMBIA NA BAADHI YA WANAMUZIKI WA ZAMBIA MMOJA WAPO NI MPIGA BASS JOSEPH MULENGA,WAKATI TP SANTA FE INAPIGA GOROFA YA TANO GATE WAYS SAFARI TRIPPES ILIKUA ATUA CHACHE PRINCESS BAR KUNA SIKU MPIGA BASS WA TRIPPERS MAREHEMU CHRISTIAN KAZINDUKI ALIPATA AJALI YA PIKIKI PALE KONA YA CENTRAL POLICE KUKAWA HAKUNA MPIGA BASS ILIBIDI MASHABIKI TUTOKE KWENDA KUMUZIMA MULENGA ILI DANSI LETU LIPIGWE NANDIO UKAWA MWANZO WA NYOTA YAKE KUNG'AA ALIJIUNGA NA TRIPPERS NA NYIMBO YAKE YA KWANZA KUREKODI MATESO DHIKI NA MATESO AKIPIGA RIDHIM GITAA ,ABDALA GAMA SOLO,BENNY PETTY SECOND SOLO,KAZINDUKI BASS,KABLA YA KUHAMIA DAR INTERNATIONAL NA KUKUTANA NA MZAMBIA MWENZI MKUBWA WAKE MICHAEL ENOCK ALIE MTRAIN KUWA MPIGA SOLO SIKILIZA NYERERE BABA MLEZI NYERERE MWANA MAPINDUZI THEN AKAENDA SIKINDE.

Thursday, February 13, 2014

ULALE PEMA KING KESTER EMENEYA


 Jean Emeneya Mubiala Kwamambu, maarufu kama King Kester Emeneya amefariki leo 13 February 2014 alfajiri saa kumi na moja na nusu katika hospitali ya  Marie Lannelongue katika jiji la  Paris akiwa na umri wa miaka 57.

Mwanamuziki huyu kiongozi na  mlezi wa kundi la Victoria Eleison. King alipata mshtuko wa moyo mara ya kwanza aliposikia kifo cha Tabu Ley mwezi November 2013 na akatibiwa katika hospitali hiyo ya Marie Lannelongue. Inaonekana  Kester Emeneya alishtushwa sana na kifo cha Tabu Ley ambaye alimuiga kwa mambo mengi. Rafiki wa Kester ambaye ni mwandishi wa habari Deck Mbutanganga alisema kuwa tangu kifo cha Tabu Ley, Kester hakurudia katika hali yake ya kiafya, alizidi kudhoufika mpaka alipofikia mauti yake..
King Kester alizaliwa mji wa Kikwit katika jimbo la Bandundu, magharibi mwa Jamhuri ya Kongo, alipofikia umri wa miaka 17 alianzisha kundi la muziki la Les Anges Noir, Malaika Weusi, akiwa na Lidjo Kwempa ambaye waliendelea kushirikiana katika muziki miaka mingi baadaye. Akiwa mwanachuo anaetafuta digrii ya Political Science katika Chuo Kikuu cha Lumbumbashi,  hamu ya kuwa mwanamuziki ikamzidia, mwaka 1977 akiwa na umri wa miaka 21 akaacha Chuo na kujiunga na kundi la Viva La Musica la Papa Wemba, akapata umaarufu mkubwa sana kama muimbaji, wakati mwingi ambapo Papa Wemba hakuwepo kwenye kundi hili Kester ndie aliyekuwa kiongozi. Hatimae tarehe 24 Desemba 1982 akazindua kundi lake la Victoria Eleison , kundi lililoleta ladha mpya katika muziki wa Kongo. Kester hutajwa kuwa mwanamuziki wa kwanza wa Afrika ya Kati kuingiza synthesizer kwenye muziki wake na album yake ya Zinzi, ambao wimbo huo ulitengenezwa studio tu, iliuza zaidi ya nakala milioni moja. Hakika alikuwa ndie mwanamuziki maarufu katika Afrika ya Kati katika miaka 1980-1990. Katika maisha yake Kester alipata Tuzo nyingi sana, kitaifa na kimataifa. Werrason na JB Mpiana walitumia nyimbo zake nyingi na mikongosio yake kutengeneza Wenge Musica. Amekwisha fanya maonyesho katika mabara yote matano duniani. Alijulikana kama Entertainer of the Year na magazeti mengi ya Kongo, katika onyesho lake moja Switzerland watu zaidi ya 12,000 walihudhuria, kitu ambacho kilitokea kwa mara ya kwanza kwa mwanamuziki kutoka Afrika kufanya katika nchi ile. Mwaka 1991 alihamia Paris na mwaka  1997 aliporudi Kongo kwa mara ya kwanza  baada ya miaka 6, onyesho alilolifanya Stade des Martyrs  lilihudhuriwa na watu 80,000.  Kester anasemekana alikuwa na nyimbo zaidi ya 1000.
 Marais wote wa Kongo waliwahi kumkaribisha katika Ikulu, Mobutu Sese Seko, Rais Laurent Kabila alimkaribisha ikulu mara tatu, na alishakaribishwa mara mbili na Rais wa sasa Joseph Kabila.
King Kester Emeneya amekuwa anaishi Ufaransa toka 1991 japo alikuwa na nyumba mbili Kinshasa katika eneo la watu wenye uwezo wa kifedha
Emeneya amekwenda lakini alichokiasisi kinaendelea katika jamii ya wapiga rumba Afrika
Mungu Mlaze Pema peponi.
Tumkumbuke kwa wimbo wa Zinzi hapa katika video hii;