Wednesday, November 20, 2013

HISTORIA FUPI YA TINO JOAKIM MASENGE 'ARAWA'

TINO (mwenye chupa ya maji) akiwa na kundi zima la Sikinde
Tino Joakim Masenge, kwa wengi alijulikana kama Tino Masinge Arawa,    alizawa kijijini Maharo, wilaya ya Rombo mwaka 1961 .!969 alianza shule katika shule ya Mkuu Extendes Primary school   na mwaka 1972, na akajiunga Kawe Primary School, akajiunga na Mzizima Secondary na kumaliza kidato cha nne 1980.
Muziki kwake ni uhakika yako katika damu. Alianza kuimba kwaya primary na pia alikuwa anapiga accordion. Babu yake alikuwa mpiga mbiu, iranda. Baba yake mdogo Francis Petro Masenge alikuwa mpiga accordion na alikuwa maarufu kwa kusindikiza harusi Rombo, na hata kutunga nyimbo zilizokuwa na hisia katika jamii, kuna wakati aliwahi kumtungia wimbo binamu yake ambaye ni Baba wa Wabunge wawili maarufu akiimba kuwa mzee huyo akafungwe Sumbawanga kutokana na tatizo la kifedha lililotokea pale kijijini kwao. Wakati huo kufungwa Sumbawanga ilikuwa jambo kubwa na baya kwa mwenyeji wa Rombo. Wimbo ulipata umaarufu katika jamii pale Rombo.
Bendi  ya kwanza ya Tino ilikuwa Dar International Orchestra, alijiunga 1983 na kukaa nayo mpaka 1985. Alivutiwa na Marijani na akaanza kuimba nyimbo zake kabla hata ya kujiunga na Dar International. Na hii ilimrahisishia hata kuingia katika bendi hii na pia kuachiwa kuimba nyimbo nyingi za Marijani. Hakujiendeleza katika vyombo alitaka  ajikite zaidi katika uimbaji zaidi. Katika kipindi cha Dar International alijikuta amekuwa simulizi kiasi cha kwamba baada ya Fresh Jumbe kuondoka JUWATA alifuatwa ili kujaza pengo la Fresh. Katika bendi ya Dar International alishiriki kurekodi nyimbo kama Masudi, Ubaya wa Jirani na kadhalika.
Alikaa JUWATA JAzz kwa muda wa miaka mitano 1985 -1990, recording yake ya kwanza ilikuwa wimbo wa Solemba, baadae akafuatwa na OSS Ndekule na kusaini mkataba wa miaka miwili lakini akadumu kwa mwaka mmoja kutokana na hali ya kutokuelewana na wenye bendi. Kwa kadri ya Tino katika mazungumzo yake siku moja alisema kuwa  kulikuwa ni maslahi madogo na maelewano madogo kati ya wanamuziki na uongozi. Akajiunga na Sikinde 1991. Akiwa na kundi la Sikinde alitunga kibao cha Arawa kilichompa umaarufu na hata kubakia na jina jipya la Arawa maisha yake yote.Akiwa Sikinde pia alitunga wimbo ulioitwa Jino la embe si dawa ya pengo. Baada ya hapo yeye na wenzie watano walitoka bendi hiyo na kuanzisha kundi la TZ Brothers. Tino aliwahi kusema moja wapo ya kitu kilichomfanya ahame Sikinde ni hali ya kuona kabanwa sana kiusanii akashindwa kuonyesha uwezo wake wote, na kujiona ni mtu wa kuitikia tu katika nyimbo licha ya kuimba na watu kama Marijani Rajabu  na Niko Zengekala.
Kundi la TZ Brothers lilipata ufadhili mkubwa kutoka kwa mwanamuziki wa zamani ambaye ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Mlimani ambaye alitoa vyombo na kuwaeleza wanamuziki kuwa wajitegemee wakati huohuo wakimpa sehemu ya mapato katika kumrudishia gharama za kununua vifaa. Walioanzisha TZ Brothers walikuwa Tino Masenge, Henry Mkanyia, Julius Mzeru Gaspar Kanuti, Kejeli mfaume, Kalamazoo Nyembo, Siraji Lumumba, na Mzee Sewando Mwenyewe (ukitaka kujua hadith ya Mzee Sewando BONYEZA HAPA. Kati ya kibao kilicho tikisa sana cha bendi hii kilikuwa kibao Blandina Stanley au maarufu Funga Mtaa, kilichoanza kwa rumba lililoimbwa vizuri sana na Tino na kumalizika na mtindo wa Vanga. Bahati mbaya bendi ya TZ Brothers ilisambaratika na Tino Masinge hatunae tena duniani MUNGU AMLAZE PEMA ARAWA

No comments: