Sunday, October 20, 2013

BURIANI JULIUS NYAISANGAH.......UNCLE J

Nyaisanga( wakwanza kushoto) akiwa na wanamuziki wa Sikinde na MK Sound
Jina la Julius Nyaisanga hakika litabaki kutajwa katika historia ya muziki Tanzania. Mtangazaji huyu ambaye alitokea Kenya na kuja kujiunga na Radio Tanzania Dar es Salaam, alikuja na aina mpya ya utangazaji ambayo ilimfanya apate nafasi ya pekee katika nyoyo za wasikilizaji wa RTD kwa miaka yote aliyokuweko huko. Julius ambaye mwenyewe alisema alitengeneza staili yake ya utangazaji kwa kumuiga mtangazaji maarufu wa KBC Leonard Mambo Mbotela aliyejulikana sana kwa kipindi chake 'Je huu ni uungwana?' alikuja na utangazaji uliochangamsha sana kumsikiliza. Nyaisanga alikuwa Producer wa mamia ya nyimbo za bendi zilizorekodiwa na bendi mbalimbali katika studio za RTD miaka ya 80. Nilipata bahati ya kufanya nae kazi wakati nilienda kurekodi nikiwa katika bendi tatu tofauti, Orchestra Mambo Bado, Tancut Almasi Orchestra, na  Vijana Jazz Band. Alishauri vizuri na matokeo yake ni nyimbo nyingi zilizopitia mikononi mwake zingali zinapendwa mpaka leo.
Pamoja na utangazaji, na u producer wa muziki, Nyaisanga alipenda muziki na wanamuziki, alikuwa rafiki wa wanamuziki wengi sana, alikuwa na tabia ya kutembelea bendi zinapopiga na aliweza hata kutembelea bendi nne au tano kwa usiku mmoja. Na hasa kama bendi iko katika ratiba ya kurekodiwa. Aliwahi hata kufika Iringa kutembelea tancut Almasi Orchestra kabla ya kurekodi toleo lao lililokuwa naule wimbo usiochosha Masafa Marefu. Nyaisanga alipita kwenye bendi kadhaa kututaarifu kuhusu kuanza kwa radio mpya ambayo ingekuwa katika masafa ya FM, na ndipo muda si mrefu Radio One ikaingia hewani wakati huo ikiwa pale katika jengo la NASACO ambalo lilikuja kuungua na baada ya kukarabatiwa sasa linaitwa Waterfront. Pia akiwa Radio One Nyaisanga aliendelea kuwa Nyaisanga, japo sera za Radio One hakika zilikuwa tofauti na zile za RTD, lakini pia huko mchango wake katika muziki ulikuwa mkubwa sana. Hatimae Nyaisanga alihamia Abood Radio Morogoro ambako amekuweko mpaka hatimae usiku wa kuamkia leo 20 October 2013, umauti umemkuta katika hospitali ya Mazimbu Morogoro kutokana na kusumbuliwa kwa muda mrefu na Kisukari.
MUNGU AMLAZE PEMA PEPONI UNCLE J
 

Friday, October 11, 2013

VIDEO YA ONYESHO LA MWISHO LA FRANCO LWAMBO MAKIADI,,22 SEPTEMBA 1989



Ijumaa , Septemba 22, 1989 Franco Luambo Luanzo Makiadi alifanya onyesho lake la mwisho maishani mwake katika ukumbi wa De Melkweg jijini Amsterdam Uholanzi. Alipoingia tu katika ukumbi siku hiyo watu wote waliona kuwa Franco alikuwa katika hali mbaya kiafya, ilikuwa wazi siku hiyo kuwa wapenzi wa Franco walianza kukata tama kuhusu afya yake. Siku hiyo onyesho lilianza na kuendelea kwa karibu masaa mawili kabla Franco kuweza kupanda jukwaani. Siku hiyo kama ilivyokuwa kawaida MC alikuwa mpiga saxaphone wa OK Jazz Isaac Musekiwa, ambaye alikuwa na Franco toka 1957, na ndiye aliyemsaidia Franco kupanda jukwaani na kumuketisha kwenye kiti, lile jitu la miraba minne lilikuwa limepungua sana, hata kusimama ilikuwa ni mtihani.  Wimbo ambao ulikuwa upigwe ulikuwa ni Chacun Pour Soi, uliokuwa umetungwa na Josky Kiambukuta ambaye siku hiyo hakuweko. Alipoanza tu kupiga ikajulikana wazi alikuwa mgonjwa kiasi cha kushindwa hata kupiga gitaa. Ukisikiliza kwenye video hii utasikia jinsi anavyokosea kupiga utadhani anajifunza wimbo ambao alipiga mwenyewe, inasikitisha. Alijitahidi kuimba  sehemu zake na kujaribu kusimama kilipofikia kipande chake cha kucharaza solo hali ilikuwa mbaya wanamuziki wake walijaribu kumsaidia kusimama, lakini hakuweza kuendelea kupiga tena kwani alikuwa anakosea kosea hakuwa tena Franco yule. Ikalazimu kuacha jukwaa akiwaacha wanamuziki wake na wapenzi wake wakiwa wamechanganyikiwa kwa majonzi. Machozi yalikuwa yametanda ukumbi mzima. Siku 20 baada ya onyesho hilo tarehe 12 Oktoba 1989 L’Okanga Lwa Ndjo Pene Luambo Makiadi akiwa na umri wa miaka 51 tu alifariki katika hospitali mjini Namur Ubelgiji. 
MUNGU AMLAZE PEMA PEPONI AMEN