Sunday, September 8, 2013

HARRISON SIWALE ALIISHIA WAPI? NI HABARI YA KUSIKITISHA

HARRISON SIWALE, MBARAKA MWINYSHEHE MWALUKA NA ABDUL MKETEMA


Nimetoka kuongea na Mzee mmoja ambaye nilimuomba anitafutie habari za Harrison Siwale  aka ‘Satchmo’, ambaye alikuwa mpiga rhythm mahiri na maarufu sana katika miaka ya sabini, Harrison alikuwa na staili ya pekee ya upigaji wa gitaa wa kudokoa nyuzi na kupata aina ya pekee ya mlio wa gitaa. Kati ya nyimbo ambazo upigaji huu unasikika ni katika nyimbo za Jamhuri Jazz Band kama vile Mganga 1  na 2, Blandina na kadhalika. Pamoja na bendi nyingine Harisson aliwahi kupigia Atomic na Jamhuri Jazz Band zote za Tanga, na kisha kuvuka mpaka na kuwa na makazi Mombasa kwa muda mrefu ambako aliendelea na muziki. Kwa kadri ya maelezo niliyopewa leo na huyu Mzee niliyemuomba anitafutie habari ili nijue yu wapi huyu mwanamuziki siku hizi? Haya ndio aliyonambia.
Baada ya kufa kwa yale makundi ya Simba wa Nyika na Les Wanyika, Harrison Siwale alianza kupiga muziki wa Injili katika eneo la Kilifi. Akawemo katika kundi lililokuwa likifanya maonyesho yake katika miji mingi ikiwemo Mombasa na Nairobi. Umahiri wake wa kazi ukamfanya mwenye vyombo vya hilo kundi alilokuwemo Harrison kumuamini sana na kumuachia awe kiongozi wa kundi hilo na kuwa huru kuzunguka sehemu mbalimbali. Inasemekana Harrison akapata tamaa ya kuingia mitini na vyombo vile, hivyo ghafla akapotea. Taarifa zikamfikia mwenye vyombo kuwa vyombo vyake viko njiani kuvushwa kungia Tanzania kupitia mji wa Lungalunga. Mwenye vyombo akaweka mtego hapo na Harrison akakamatwa hapo akiwa na vyombo hivyo, kesi ilifika mahakamani na akahukumiwa kifungo cha miaka mitatu. Baada ya hapa kuna hadithi mbili, moja ikisema alifia gerezani Shimo la Tewa, na nyingine ikisema alifariki baada ya kumaliza kifungo chake.
Je, nini hasa kilitokea? Najaribu kuwasiliana na watu mbalimbali kupata hadithi zaidi kuhusu mwanamuziki huyu.

No comments: