HALILA TONGOLANGA, mwanamuziki wa siku nyingi ambaye alikuwa amelazwa katika hospitali ya Muhimbili amefariki dunia usiku wa kuamkia leo. Halila alikuwa amesafirishwa kutokea Ndanda kuja Muhimbili akihisiwa kuwa na matatizo ya figo. Licha ya kuwa alifika Muhimbili juzi Ijumaa usiku, lakini alikuwa hakufanyiwa vipimo vyovyote vikubwa mpaka umauti unamkuta. Jana Jumapili ililazimika kuanza kufanya jitihada za kupata daktari ambaye angemshughulikia kwa karibu zaidi, na daktari alipatikana ambaye aliahidi angeanza kufwatilia swala lake leo asubuhi lakini mapenzi ya Mungu yalikuwa tofauti. Juzi nilipomuona alinambia kuwa ana mengi anataka kunambia, lakini moja aliloweza kunambia pale ni kuwa yeye anajihisi ana kansa, 'Nilimuuliza anajuaje hilo, kwa vile hajapimwa hakuwa na jibu"
Wengi tutamkumbuka Tongolanga kwa wimbo wake wa Kimakonde aliouimba kwa mara ya kwanza akiwa na Les Mwenge 'Kila Munu Ave Na Kwao"
Mwili wa marehemu unategemewa kusafirishwa leo saa tano kuelekea kwao Newala. Habari zaidi zitawafikia kupia hapa
Mungu amlaze Pema peponi Halila Tongolanga
Sunday, June 4, 2017
Saturday, June 3, 2017
TONGOLANGA ANASUBIRI VIPIMO
![]() |
| Katibu Mtendaji wa BASATA mwenye kitenge akiwa na Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi, walipomtembelea Tongolanga asubuhi ya leo. |
Halila Tongolanga kwa kweli anaumwa. Kwa maelezo ya mdogo wake, ni mwezi wa tatu sasa anaingia na kutoka hospitali mbalimbali. Mpaka jana alikuwa katika hospitali ya Ndanda, na kwa msaada wa Mbunge wa Tandahimba aliweza kupatiwa Ambulance na kufikishwa Muhimbili ambako amelazwa Kibasila No 10. Mpaka jioni ya leo alikuwa anasubiri vipimo.
Tongolanga ndie mtunzi na mwimbaji wa wimbo maarufu wa 'Kilamunu ave na kwao' aliouimba kwanza akiwa Les Mwenge bendi iliyo mali ya JWTZ.
Tongolanga ndie mtunzi na mwimbaji wa wimbo maarufu wa 'Kilamunu ave na kwao' aliouimba kwanza akiwa Les Mwenge bendi iliyo mali ya JWTZ.
NIDHAMU NA MAENDELEO YA MUZIKI KATIKA BENDI ZETU
Miezi michache iliyopita rafiki yangu mmoja alinambia ameamua kuunda bendi mpya kabisa, alikuwa na lengo la kuleta muziki mpya kabisa katika anga ya muziki Tanzania. Aliongea kwa furaha na ni wazi alikuwa ana nia ya kufanya kitu kikubwa, maana alikuwa amegharamia fedha nyingi kununua vifaa vipya kabisa vya kuanzisha bendi. Mwezi mmoja baada ya mazoezi kuanza alinitafuta na kunambia ameamua kuvunja bendi na vyombo anauza. Nilipomuuliza kwanini kabadili mawazo katika kipindi kifupi vile, hata onyesho moja halijafanyika? Akanijibu. ’Wanamuziki wamenishinda, wana matatizo makubwa ya ndhamu’. Kiukweli sikushangaa sana kwani jambo hili si geni kabisa kwenye tasnia ya muziki kwa siku hizi. Mfumo wa uendeshaji bendi siku hizi ni tofauti sana na miaka ya nyuma.
Nichukue mfano wa bendi Vijana jazz Band, bendi ambayo nilijiunga mwaka 1989. Kujiunga na bendi hii kulitokana na mwaliko niliyoupata kupitia kwa muimbaji rafiki yangu Marehemu Mohamed Shaweji. Shaweji tulikuwa wote Tancut Almasi Orchestra kisha yeye akaniacha kule na na kujiunga na Vijana Jazz Band, yeye na muimbaji mwingine Marehemu Gota gota wakiwa wamemfuata mpiga gitaa Shaaban ‘Wanted’ Yohana, aliyetoka Tancut pia na kuhamia Vijana Jazz Band miezi michache kabla. Hivyo siku moja nikiwa na bendi ya Tancut Almasi kwenye onyesho kwenye ukumbi wa CCM kata ya 14 Temeke, Shaweji alikuja na kunambia kuwa Hemed Maneti, kiongozi wa Vijana Jazz Band alikuwa anataka nijiunge na bendi yake. Nilikubali na mwezi Oktoba 1989 nilijiunga na Vijana Jazz. Kufikia mwezi wa Desemba mwaka huohuo nikawa nimepewa wadhifa wa kuwa Band Master, kazi za Band Master ni kuangalia nidhamu ya jumla ya wanamuziki, ikiwemo mahudhurio mazoezini na kazini, uchelewaji, ulevi, usafi binafsi wa mwanamuziki na pia kupanga ratiba ya nyimbo ambazo zinatakiwa kupigwa katika onyesho. Kwa mfumo uliokuweko, Band Master aliweza kumsimamisha mwanamuziki yoyote aliyekiuka sheria za bendi, au kutoa adhabu ya kukatwa fedha kutoka kwenye mafao yake ya kila wiki ikiwa ni adhabu kwa makosa mbalimbali. Nguvu hizi zilifanya wanamuziki kuwa na nidhamu wakati wote wawapo kwenye shughuli za bendi. Ikumbukwe kuwa katika bendi kulikuweko na kiongozi mkuu Band Leader. Huyu alikuwa na mamlaka ya kufukuza mtu kazi na pia kuajiri na ndie anaepanga hata ukubwa wa mshahara, lakini alikuwa haingilii madaraka ya Stage Master. Kwa kawaida wanamuziki waliona ni heri matatizo yao yaishie kwa Band Master kwani yakifika kwa Band Leader yanakuwa ndio yamefika hatua ya mwisho isiyo na rufaa na inaweza kuwa hasara kubwa. Ili kuonyesha Band Master alivyokuwa na nafasi ya pekee, siku moja wakati niko Vijana jazz band, ilikuwa twende kwenye moja ya maonesho na kuna gari ilikuwa inatupitia wote majumbani kwetu, tulipofika nyumbani kwa Band Leader Hemed Maneti, alitoka nje akiwa na karatasi kutoka hospitali akaja kunitaarifu kama Band Master, kuwa hataweza kuja kazini kwani anaumwa, Maneti alikuwa Band Leader lakini alikuwa akiheshimu nafasi ya Band Master, tena nilikuwa bado mgeni katika bendi. Hii ilikuwa ni ishara wazi kwa wanamuziki wengine kuwa Band Master lazima aheshimiwe na wote.
Hali si hivi katika bendi nyingi siku hizi. Ngumu kujua nani mwenye madaraka gani kwani bendi zinakuwa na mwenye bendi, mkurugenzi wa bendi, meneja, maseneta, kiongozi wa bendi, wadau wa bendi. Wote hawa wana mamlaka zisizo na mipaka, wanaweza kuamua wimbo gani upigwe, wanaweza kuamua nani atimuliwe au nani aingizwe kwenye bendi, mmoja akimsimamisha mwanamuziki kwa utovu wa nidhamu mwingine anaweza akamrudisha, hakuna mtu mwenye amri ya mwisho kuhusu lolote lile, hivyo nidhamu imeshuka sana, na pasipo na nidhamu si rahisi kuweko na maendeleo yoyote yenye tija.
Sasa nizungumzie kosa la rafiki yangu aliyetaka kuanzisha bendi na ikamshinda, kwanza baada ya kununua vyombo, aliaanza kutafuta wanamuziki akisaidiana na watu wake wa karibu, kisha akamteua kiongozi wa bendi, ambae kimsingi kilikuwa kilemba cha ukoka kwani rafiki yangu ndie aliyekuwa na amri ya mwisho kuhusu lolote katika bendi. Na kwa kuwa hakuwa na muda wa kushinda kila mahala na bendi, kundi likawa halina kiongozi mwenye mamalaka na mwisho kila mtu akawa anafanya lake, walevi wakalewa sana, wachelewaji wakendelea na uchelewaji wao, hakukuwa na mtu aliyekuwa na uwezo wa kutoa mwelekeo wa bendi kinidhamu wala kimuziki. Muziki wa bendi kwa ujumla umekumbwa na tatizo hili la kukosa uongozi, maamuzi mengi yanafanyika kwa vikao, hata maamuzi yale ambayo ni ya kitaaluma yanangoja makubaliano ya wengi, na kwa mtindo huu bendi zitachelewa sana kujikwamua kwenye tope ambalo zimenasa. Ushauri kwa wanaotaka kufungua bendi, ni bora kumtafuta mwanamuziki mmoja ambaye unaamini anaweza kutengeneza muziki unaoutaka au unaodhani utakuletea biashara kisha umwachie aijege hiyo bendi na wanamuziki anaoona yeye wanafaa, hapa tayari utakuwa umejenga utawala unaoeleweka. Mwenye vyombo usiingilie moja kwa moja mambo ya bendi, wanamuziki wakishajua kuwa kiongozi wa bendi hana mamlaka kamili, nidhamu inavunjika.
Friday, June 2, 2017
HABARI NJEMA, HALILA TONGOLANGA AMEPATA USAFIRI WA KUJA DAR ES SALAAM NA YUKO NJIANI, ANATEGEMEA KUFIKIA HOSPITALI TA REGENCY
MWANAMUZIKI HALILA TONGOLANGA AMEWEZA KUPATA BAHATI YA KUPATA USAFIRI UTAKAOMLETA KWENYE MATIBABU DAR ES SALAAM. TONGOLANGA ANATEGEMEWA KUFIKIA HOSPITALI YA REGENCY. ANASINDIKIZWA NA WADOGO ZAKE WAWILI. TUZIDI KUMUOMBEA NDUGU YETU
Thursday, June 1, 2017
HALILA TONGOLANGA ANAUMWA ANAHITAJI MSAADA WA HARAKA SANA
MWANAMUZIKI HALILA TONGOLANGA MTUNZI WA WIMBO MAARUFU WA KILA MUNU AVE NA KWAO, AMEUGUA GHAFLA AKIWA KATIKA ZIARA YA MUZIKI MIKOA YA KUSINI. ANATAKIWA KURUDISHWA DAR ES SALAAM MAPEMA APATE MATIBABU YA HARAKA MUHIMBILI. KWA SASA AMELAZWA KATIKA HOSPITALI YA NDANDA. ANAE ONA AMEGUSWA NA ANAWEZA KUTOA USAFIRI AU MSAADA WOWOTE APIGE SIMU 0713644439 ILI KUWASILIANA NA KATIBU MTENDAJI WA BARAZA LA SANAA LA TAIFA.
NI MIAKA 27 TOKA KIFO CHA HEMEDI MANETI
Mara ya kwanza kukutana uso kwa uso na Hemedi Maneti ilikuwa ni wakati Vijana Jazz band ilipita Iringa ikielekea Songea mwaka 1989. Wakti huo nilikuwa mwanamuziki wa Tancut Almasi Orchestra, na kama ilivyokuwa ada miaka ile, bendi ikipita katika mji ambao kuna bendi wanamuziki walikuwa wakipiga muziki pamoja. Tuliongea nae machache lakini aliongea kuhusu kufurahishwa na setting ya vyombo vyetu, alisema inafanya vyombo vyote visikike. Wakati huo hatukujua lakini kumbe alikuwa kishaongea na Shaaban Wanted, Mohamed Gotagota na Mohamed Shaweji ili wajiunge na Vijana Jazz band, na hakika walihamia bendi hiyo wiki chache zilizofuata.
Katika mlolongo huohuo nilijikuta nikiitwa kujiunga na Vijana Jazz Band mwezi wa September mwaka huohuo na kufikia Oktober 1989 niliwasili Dar es Salaam kujiunga na Vijana Jazz Band. Siku ya kwanza nilipofika Vijana maneti alinipa shilingi 300 za kuanza maisha. Nitafute guest house ya kuishi na chakula kwa wiki moja. Hiyo ndiyo kumbukumbu yangu ya kwanza ya Maneti ambaye miezi michache baadae, tarehe 31 May 1990 siku ya Alhamisi majira ya saa kumi na moja jioni, Hemed Maneti alifariki katika hospitali ya Mwananyamala. Alikuwa ameanza kuwa na matatizo ya afya miezi kadhaa kabla ya hapo na hatimae kupelekwa Tanga kwa ajili ya matibabu. Hali yake ilipozidi kuwa mbaya alirudishwa kwa ndege kuwasili Dar Jumatano 30 May na kupelekwa moja kwa moja hospitali ya Mwananyamala ambapo alilala na kufariki kesho yake. Marehemu alisafirishwa kwenda kuzikwa Tanga siku moja baadae.
Wimbo wa mwisho kurekodi ulikuwa wimbo Nelson Mandela uliotungwa nami, ukiwa wimbo uliokuwa matayarisho ya ziara ya Nelson Mandela.
Katika mlolongo huohuo nilijikuta nikiitwa kujiunga na Vijana Jazz Band mwezi wa September mwaka huohuo na kufikia Oktober 1989 niliwasili Dar es Salaam kujiunga na Vijana Jazz Band. Siku ya kwanza nilipofika Vijana maneti alinipa shilingi 300 za kuanza maisha. Nitafute guest house ya kuishi na chakula kwa wiki moja. Hiyo ndiyo kumbukumbu yangu ya kwanza ya Maneti ambaye miezi michache baadae, tarehe 31 May 1990 siku ya Alhamisi majira ya saa kumi na moja jioni, Hemed Maneti alifariki katika hospitali ya Mwananyamala. Alikuwa ameanza kuwa na matatizo ya afya miezi kadhaa kabla ya hapo na hatimae kupelekwa Tanga kwa ajili ya matibabu. Hali yake ilipozidi kuwa mbaya alirudishwa kwa ndege kuwasili Dar Jumatano 30 May na kupelekwa moja kwa moja hospitali ya Mwananyamala ambapo alilala na kufariki kesho yake. Marehemu alisafirishwa kwenda kuzikwa Tanga siku moja baadae.
Wimbo wa mwisho kurekodi ulikuwa wimbo Nelson Mandela uliotungwa nami, ukiwa wimbo uliokuwa matayarisho ya ziara ya Nelson Mandela.
Subscribe to:
Posts (Atom)




