Thursday, December 21, 2017

SANAA KATIKA MIKAKATI YA KUWA NCHI YA VIWANDA

Sanaa ni pana sana. Ukiangalia kila kinachokuzunguka, kina usanii ndani yake. Mpangilio wa habari katika gazeti hili, mpangilio wa lugha, mpangilio wa picha, halafu ukinyanyua macho na kuangalia vitu vilivyokuzunguka, majengo, mavazi, samani, vyombo vya usafiri, mpangilio wa rangi wa vitu hivyo au ukisikia sauti za muziki  vyote ni kazi za aina mbalimbali za sanaa. Katika zama hizi za kauli mbiu ya ‘nchi ya viwanda’, inashangaza kuwa matayarisho ya wasanii wa kuambatana na nchi ya viwanda haitiliwi mkazo, lakini bidhaa zote za viwanda zinahitaji usanii, kama ni kuchora nembo nzuri au kuweka tangazo zuri la mali au hata kutengeneza sura nzuri ya bidhaa zitakazozalishwa katika ‘nchi ya viwanda’ ni kazi ya sanaa. Bila matayarisho ya wasanii bora tutakuwa na mali nzuri zisizo na sura ya kumvutia mlaji. Hakika mpaka leo naamini kuwa kama wasanii wangehusishwa katika kukamilisha lile gari lililotengenezwa Tanzania na kupewa jina ‘nyumbu’, mambo kadhaa yangekuwa tofauti, kwanza lingepatikana jina la kuvutia zaidi na pili gari lile lingebuniwa  sura ya kuvutia zaidi. Watu wengi hununua magari kutokana na muonekano wa gari, bila hata kujiuliza mambo mengine ya kiufundi kuhusu gari husika.
 Kama nilivyosema sanaa ni pana sana leo nizungumzie sanaa ya kutumia mdomo. Binadamu wote kwa kawaida tuna midomo na pia kwa kawaida wote tunaweza kutoa sauti mbalimbali na mdomo huo. Mungu kawapa watu mbalimbali vipaji vya kuweza kutumia mdomo huo, kuna waimbaji wa staili mbalimbali, wako watambaji, waghani wa mashahiri, wasimuliaji wa hadithi, watangazaji, wachekeshaji, wahubiri, wanasiasa, na wengine wengi wa aina yao, wote hawa wanafanya sanaa zao kwa kutumia mdomo, japokuwa katika hawa hawa wengine hujiona sanaa yao ni bora kuliko ya wengine na mara nyingi hukataa katakata kuitwa wasanii.  Jambo moja lisilo pingika ni kuwa kila msanii hupenda kupata jukwaa la kuonyesha sanaa yake, na ndio maana kulibuniwa majukwaa, na hatimae majumba makubwa ya kuonyesha sanaa ambayo nayo huwa na majukwaa makubwa ya kupendeza. Wasanii hutayarisha shughuli zao  na kisha hualika watazamaji au wasilikizaji. Msanii aliyetayarisha au kutayarishiwa shughuli ni wazi ndie anayestahili kuweko jukwaa kuu kwani hata wanaokuja kumtazama wangetaka iwe hivyo ili wamuome na kumsikia vizuri. Kwenye shughuli za wasanii ambao hutumia midomo yao kuhubiri siasa, mara nyingi huweza ikaonekana ni vizuri kualika wasanii wengine, kama vile wanamuziki au wacheza ngoma au wanamuziki wa bongofleva na kadhalika ili waje wafanye sanaa zao kuleta burudani au kutoa ujumbe wa siku hiyo, kabla msanii aliyetayarisha shughuli hajapanda jukwaani na kuhubiri siasa. Katika shughuli za namna hii huwa hakuna utata sana kwani jukwaa kuu huanza kutumika na wanasiasa bila ya kuingilia. Lakini kuna tabia moja ambayo imejijenga hapa kwetu wakati shughuli inafanywa na wasanii wasio wanasiasa, ambao ili kufanikisha shughuli yao hualikwa wanasiasa, ni kawaida sana katika shughuli za namna hii ukakuta wanasiasa wamepangiwa viti kwenye jukwaa kuu na wenye shughuli kulazimika kujengewa jukwaa dogo pembeni, au kulazimika kufanya shughuli zao za sanaa kwenye sehemu ambayo hawaonekani. Nitoe mfano, siku chache zilizopita kulikuwa na shughuli kubwa ambayo ilihusu wasanii kuhamasisha uzalendo, wasanii kutoka sehemu mbalimbali nchini walikusanyika Dodoma kwa ajili ya shughuli hiyo. Shughuli ilipangwa kufanyika katika ukumbi mzuri uliojengwa kitaalamu kwa shughuli kama hizi. Na shughuli hiyo ilikuwa ikionyeshwa mubashara nchi nzima, hii iliwezesha ambao hawakuweza kuja Dodoma wafaidi na kuelewa yanayofanyika Dodoma bila wasiwasi. Siku hiyo ukumbi huu ‘ukaboreshwa’ kwa ajli ya shughuli, na  jukwaa dogo lilitengenezwa pembeni, na hapo ndipo wasanii walipopangiwa kufanya shughuli zao, katika jukwaa kubwa vikapangwa viti vya kukalia viongozi watazamaji wa maonyesho ya sanaa. Jengo hili lenye sehemu ya kukaa yenye zaidi ya viti mia tano, ikaachwa na viti vikapangwa kwenye jukwaa ambapo ndipo sehemu sahihi ya kuonyeshea kazi za sanaa. Ni nini kinasababisha ukumbi mzuri ule usitumike inavyotakiwa? Kwani viongozi wakikaa viti vya mbele na kuangalia sanaa zikiendelea jukwaani itakuwa wamedharauliwa? Mkao huo unaleta utata mwingine mkubwa kwa wasanii wanaofanya onyesho, wanakuwa katika utata, je wanafanya onyesho kwa ajili ya hadhira hivyo wawape mgongo viongozi au wanafanya onyesho kwa ajili ya viongozi hivyo waipe hadhira mgongo? Kwa aliye angalia kupitia onyesho lile kupitia luninga, onyesho lilionekana ni la hovyohovyo tu, wasanii wakionekana hawajui wanataka kufanya nini.
Baada ya viongozi kumaliza kilichowaleta wakaondoka, viti viliendelea kuwa jukwaani hivyo wasanii wakawa wanafanya maonyesho yao   chini ya jukwaa, na hivyo kutokuonekana vizuri kazi yao na watazamaji kuamua kuondoka mmoja mmoja. Matayarisho yote yamekuwa bure. Hata ule moto wa uzalendo uliotegemewa kuwashwa umegeuka cheche tu. Ushauri tu kwa wasanii wote niliyowataja hapo juu, itapendeza kila moja akiheshimu kazi ya mwenzie na kuruhusu ifanyike katika sehemu stahili, na si kujali tu kiongozi atakuwa wapi na kutokujali mamia ya hadhira yatawezaje kufaidi sanaa iliyopo ambayo imetayarishwa kwa muda mrefu na gharama kubwa..


PAKUA ANKO KITIME APP


PAKUA APP YA ANKO KITIME KWENYE SIMU YAKO UPATE TAARIFA ZOTE ZITAKAZOTUNDIKWA KWENYE www.theiringa.blogspot.com 
HABARI vichekesho PICHA video