Saturday, March 25, 2017

MIAKA 22 TOKA KIFO CHA NGULI MARIJANI RAJABU


ALHAMISI, Machi 23 mwaka 1995 ni siku isiyosahaulika kwa wapenzi wa muziki wa zamani nchini. Siku hiyo ndipo tulipompoteza mwanamuziki kipenzi chetu, Marijani Rajabu. Alizikwa kesho yake Ijumaa Machi 24 kwenye makaburi ya Kisutu.

Historia ya gwiji huyu inaanzia siku alipozaliwa tarehe 3 Machi mwaka 1955, katika eneo la Kariakoo.  Mama yake alikuwa mama wa nyumbani wakati baba yake alikuwa na shughuli za uchapishaji. Maisha yake ya utoto yalikuwa ya kawaida ila alikuwa kipenda sana uimbaji wa Tabu Ley na mwimbaji mmoja wa Guinea Sorry Kandia.  Alisoma shule ya Msingi ikiambatana na elimu ya Madrasa.   Mwaka 1970 Akiwa bado shuleni, utaona umri wake ulikuwa miaka 15 tu,  alijiunga na STC Jazz, ikiwa chini ya mpiga gitaa maarufu wakati huo Raphael Sabuni, kabla ya hapo bendi hii ilikuwa unajulikana kama The Jets. Katika bendi hii Marijani aliweza kutoka nje ya Tanzania kwa mara ya kwanza ambapo alikwenda Nairobi na kurekodi nyimbo zilizotoka katika label ya Phillips., hili jambo la mwanafunzi kusafiri na bendi likaleta shida na kwa vile STC ilikuwa mali ya umma akaachishwa kazi na mwaka1972 alijiunga na The Trippers ya David Mussa ambayo kwa wakati huo ilikuwa inapiga zaidi nyimbo za hoteli na za kukopi na muimbaji wao kiongozi wakati huo alikuwa Ali Rajabu. Hapa ndipo ubora wake ulifunguka haswa na kuweza kuinyanyua Trippers, ambayo sasa ilibadili jina na kuwa Safari trippers kutokana na msimamo wa serikali wakati huo wa kutaka majina ya nyumbani yatumike bala ya yale ya kigeni na  kuwa moja ya bendi maarufu za wakati huo. Waliweza kutoa vibao vilivyopendwa mfululizo na kuweza kuzunguka nchi nzima. Vibao kama Rosa nenda shule, Georgina,Mkuki moyoni, viliweza kuuza zaidi ya nakala 10000 za santuri na hivyo kuwezesha bendi kuwa na vyombo vyake vizuri. Bendi wakati huo ikiwa na wanahisa wanne, ambao kwa bahati mbaya wakati bendi ndio iko juu, wakakosa kuelewana na ukawa ndio mwisho wa bendi hiyo. Marijani alishiriki kutunga, kuimba nyimbo karibu zote za Trippers sanjari na kupiga gitaa kwa baadhi ya nyimbo. Mfano wimbo Olila ambao alipiga rhythm na kuimba.
Mwaka 1976, Marijani na baadhi ya wanamuziki wa Trippers waliamua kuihama bendi na kwenda baadaye kuasisi Dar es salaam International chini ya umiliki wa Mzee Zakaria Ndabemeye ambaye bado yu hai hadi sasa. Baadhi ya wanamuziki hao ni pamoja na Abel Baltazar kutoka Msondo, Kassimu Mponda kutoka Trippers, Abdallah Gama, Joseph Mulenga, Haruna Lwali na George Kessy Omojo waliokuwa wanapiga muziki Magot pale, Said Mohamed kutoka Polisi Jazz, Cosmas Chidumule kutoka Urafiki, Belesa Kakere kutoka Biashara Jazz, Joseph Bernard kutoka Trippers, Ali Rajabu kutoka Trippers, na King Michael Enock kutoka Dar es salaam Jazz. Akiwa Dar Inter alishiriki kutunga nyimbo mbili, Betty na Sikitiko. Hata hivyo kama waswahili wanavyosema mafahari wawili hawakai zizi moja ndivyo ilivyotokea kati yake na Abel Balthazal kiasi cha hatimaye Marijani kufukuzwa ndani ya bendi kutokana na ubishi kuhusu wimbo aliotunga Marijani, kuna maelezo kuwa wimbo ulionekana unafanana na wimbo fulani toka Kongo na hivyo Marijani akatakiwa aubadilishe na ndipo ugomvi ukaanza. Hata hivyo mwishoni mwa mwaka 1978, Marijani alirejeshwa tena kundini kutokana na rundo la wanamuziki wa Dar Inter kuihama bendi kwa kishindo kikubwa na kwenda kuifungua bendi mpya kabisa ya Orchestra Mlimani Park. Aliporejeshwa Marijani alikuja na wanamuziki wengi wapya wakati huo kama akina Christopher Kasongo, Mohamed Tungwa, Mafumu Bilal, Hamis Milambo, Athuman Momba, Mzee Alex Kanyimbo na wengine na kuja na mtindo wa Super Bomboka. Katika kudhihirisha hasira zake kwa Abel, Marijani alimtungia Abel wimbo wa kumnanga ukiitwa Kidudu mtu ambao hata hivyo RTD waliukataa kuurekodi, jambo lililokuwa kawaida enzi hizo kwa redio kukataa wimbo. Sifa nyingine ambayo Marijani alikuwa nayo ni kuibua wanamuziki chipukizi kama alivyofanya mwaka 1983 alipomuibua kutoka Tanga kijana Mkuu Waziri Kungugu Kitanda Milima almaaruf Fresh Jumbe ambaye kwa hakika kabisa Marijani hakujutia kumchukua kijana huyo. Alimuamini kupita maelezo kiasi kwamba wakati mwingine alikuwa akimuachia bendi aongoze na yeye anapumzika nyumbani. Mbali na Fresh, wanamuziki wengine ni kama vile Tino Masinge, Mohamed Mwinyikondo, Juma Choka na wengine kibao. Ni vizuri kuelezea hapa kuwa kadri ya maelezo yake mwenyewe marehemu  baada ya kurekodi Zuena na Mwanameka na nuimbo nyingine katika album hiyo alichoambulia ni malipo ya nauli toka RTD ya sh 2500/- tu. Kilichosikitisha zaidi ni kuwa nyimbo zao tisa ziliuzwa kwa kampuni ya Polygram bila ridhaa yao.
Hata hivyo safari ya Dar International ilikoma mwaka 1987 kutokana na sababu za kawaida za kufa kwa bendi lakini kubwa ni uchakavu wa vyombo. Hata hivyo Marijani aliendelea kufanya muziki na kwa kipindi kifupi amewahi kucheza na Kurugenzi ya Arusha na Mwenge Jazz ambayo alirekodi nayo wimbo mmoja wa Ukimwi na hata kupitia bendi ya Watafiti ambayo hatimae ilikuja kuwa 38.. Mwaka huohuo wa 1987 Marijani na Muhidin Maalim Gurumo waliliongoza kundi la wanamuziki zaidi ya 50 kutunga nyimbo maalum hasa kwa maadhimisho ya miaka 10 ya CCM na 20 ya Azimio la Arusha. Naizungumzia Tanzania All Stars. Aidha mwaka 1994 aliwahi kurekodi zong zing na marehemu Eddy Sheggy. Bendi yake ya mwisho ilikuwa ni Africulture ama Mahepe Ngoma ya Wajanja, iliyokuwa mali ya Rogers Malila, alikokuwa na wanamuziki kadhaa kama akina  Hassan Kunyata, Mgosi na wengine. Bado Marijani ataendelea kukumbukwa na wapenda muziki kote nchini na hata Afrika kwa ujumla kwa nyimbo zake zenye mafundisho na tamu huku akienzi utamaduni na ngoma za kwao Kigoma.

ANGALIA VIDEO MARIJANI LIVE

Saturday, March 18, 2017

AMRI BILA TAFITI ZINAATHIRI SANA SEKTA YA MUZIKI


KATIKA shughuli ambazo watu wengi huona ni rahisi kuendesha na kutoa maamuzi bila utafiti ni soka na muziki. Ukisikiliza mazungumzo baada ya mechi za soka ndipo utakaposikia watu wanavyotoa ushauri au kukosoa wachezaji, kocha refa, chama cha mpira wa miguu, hakika ingewezekana watu hawa wakapata mamlaka, maamuzi yangekuwa ya ajabu sana.
Hali kadhalika kwenye muziki. Kwa mfano ukiuliza,   kwanini muziki wa bendi hauna umaarufu kama zamani? Hakika ukipita kila mtaa utapata majibu, wengine watakwambia kosa la vyombo vya utangazaji , wengine watakwambia wanamuziki wenyewe , wengine watakwambia serikali, na pia utapewa maelekezo mbalimbali ya nini kifanyike. Bahati nzuri majibu haya ya mtaani hayana madhara kwani huishia hapo hapo. Lakini bahati mbaya huja pale ambapo viongozi wenye mamlaka nao hugeuka wataalamu wa muziki na wao kutoa maamuzi kadri ya mtizamo wao, lakini maamuzi yao huwa amri, na amri inapotolewa bila utafiti wa kutosha madhara yake yanaweza kuendelea miaka mingi baadae. Ninaloweza kusema kwa uhakika, ni kuwa muziki wa Tanzania leo ungekuwa katika nafasi ya juu zaidi duniani kama isingekuwa maamuzi ambayo yalitolewa bila utafiti miaka ya nyuma. Labda nitoe mifano kadhaa. Mpaka miaka ya 70, wanamuziki wa Tanzania walikuwa wakienda sambamba na wanamuziki wa nchi nyingine nyingi Afrika, licha ya kutokuwa na miundo mbinu muhimu katika maendeleo ya muziki kama vile kutokuwa na kampuni za kurekodi na kutengeneza santuri. Lakini kimuziki, wanamuziki wa kipindi hiki walikuwa bega kwa bega na wenzao ambao walikuwa na miundo mbinu stahiki. Tanzania tulikuwa na bendi ambazo zilikuwa  zinapiga muziki wa rumba, nyimbo nyingi za wakati huo mpaka leo bado zinasifika na kupendwa katika anga za muziki. Pia tulikuwa  na wanamuziki vijana ambao wengi wao walikuwa mashuleni, hawa wakiwa na mtizamo mpana zaidi wa kutambulika duniani, wanamuziki hawa kama ilivyokuwa sehemu nyingi Afrika walianza kupiga muziki uliojulikana kama Afro Rock, muziki ambao ulichanganya mahadhi ya muziki asili wa Kitanzania na mapigo ya kizungu, wakifuatia nyayo za kundi la Osibisa, na wanamuziki kama Ransome Fela Kuti. Kukawa na makundi kama Afro 70, Trippers, Sun Burst, The Jets na kadhalika kwa kuyataja machache, makundi ambayo yalianza kuingiza muziki wa Tanzania kwenye soko kubwa zaidi la Kimataifa, kwa mfano wimbo wa Weekend wa Afro70 uliingia kwenye Top Ten Nigeria miaka hiyo, wakati huo muziki wa Nigeria haukuwa na umaarufu wowote nchini kwetu.  Kwa kuwa vijana hawa wengi walikuwa bado shuleni, na kufuatana na maadili ya wakati ule, wanafunzi hawakuruhusiwa  kushiriki madansa ya usiku, hivyo basi kulikuweko na utamaduni wa madansa ya mchana yaliyoitwa Bugi. Hapo vijana walikusanyika kupiga muziki wao kila mwisho wa wiki, shughuli zikianza saa nane mchana na kuisha saa kumi na mbili jioni. Lakini siku moja kiongozi mmoja akatokea na kupiga marufuku Bugi, hivyo kuwaondoa wanamuziki vijana wengi kwenye muziki kwani wasingeruhusiwa kushiriki madansi ya usiku.  Wakati vijana hao wanaacha muziki, vijana wengine Afrika waliendelea mbele. Hata majirani zetu Kenya na Zambia wakawa na wanamuziki wengi walioweza kuingia katika soko la Kimataifa, wanamuziki wetu walikosa fursa hiyo. Pengo hili linaendelea kuwepo mpaka leo. Kuziba pengo hilo kunahitaji kutafiti tulipojikwaa na kuangalia tunafanya nini kurekebisha hali iliyopo. Swala la kupiga marufuku kazi za muziki si jambo geni katika historia ya muziki, kulikuwa na maamuzi kadhaa ya kisiasa pia ambayo pia hayakuwa na utafiti hivyo kudhoofisha maendeleo ya muziki Tanzania. Kwa mfano kulishawahi kutolewa amri ya kupiga marufuku wacheza show, wakati huo karibu bendi zote kubwa za muziki wa rumba kote Afrika Mashariki na Kati zilihakikisha kuwa zinakuwa na kundi la wacheza show, na waimbaji maarufu kama Mbilia Bel na Tshala Mwana wote awali walikuwa ni wacheza show. Kwa kipindi kirefu kulikuweko na sinto fahamu ya wacheza show na ikalazimika taaluma hiyo irudi kinyemela kwani makundi yote ya muziki kutoka nje yalipokuja nchini yalisindikizana na wacheza show. Nyimbo kadhaa ziliwahi kupigwa marufuku na hatimae kuja kuonekana ni za muhimu katika jamii, ukiwemo wimbo maarufu wa Super Matimila, Mambo kwa Soksi, ambao ulipigwa marufuku na baade kuonekana ni wimbo muhimu kuhamasisha watu kutumia kinga katika zama hizi za balaa la Ukimwi. Upigaji marufuku wa tungo unakwaza watunzi na kuishia kutunga nyimbo nyepesi ambazo zina uhakika wa kutokupigwa marufuku. Katika miaka ya karibuni kumewahi kufanyika maamuzi kadhaa yasiyokuwa na utafiti kwa mfano,  serikali iliwahi kununua mashine iliyoitwa Mastering Mixer kwa gharama ya shilingi milioni 50, kwa maelezo kuwa ndio itakayowezesha kumaliza wizi wa kazi za muziki. Sio siri wizi uko palepale. Hayo yalikuwa maamuzi bila utafiti, ni vizuri kujua hiyo ‘mixer’  iko wapi ili kutathmini ni matokeo ya uamuzi huu uliogharimiwa na serikali. Uamuzi mwingine ulikuwa ni ule wa kutunga sheria ya kuweka stempu za TRA kwenye kazi za sanaa, kwa maelezo kuwa utamaliza wizi wa kazi za muziki na filamu. Si mara moja taarifa imatolewa kuwa serikali ilitoa milioni 20 kwa mtafiti toka ‘Chuo Kikuu’ kuhakiki kuwa njia hiyo ndio itamaliza wizi wa kazi za sanaa, hakuna ‘mtafiti’ anayejitokeza kuwa alipokea fedha na kufanya utafiti huo, wala hakuna nakala ya utafiti huo, ni aina nyingine ya maamuzi bila utafiti na matokeo yake wizi wa kazi za sanaa umeenea kila kona nchini na mauzo halali ya kazi za muziki yamepotea. Ushauri tu kwa viongozi kuwa muziki si shughuli ya kubahatisha ina misingi yake, ni muhimu kwa manufaa ya Taifa, umefika wakati wa kufanya utafiti kwanza kabla ya kutoa maamuzi.