Friday, February 26, 2016
IJUE HISTORIA FUPI YA MZEE KASSIM MAPILI
Women Jazz band
Ni katika bendi ya Polisi katika mtindo wao wa Vangavanga ndipo jina la Mzee Mapili lilikuja julikana na sana, na hasa kutokana na tungo zake kama Dunia ulioimbwa na Moshi William, na Hayati Mzee Diwani. Baada ya miaka 16 katika bendi ya Polisi, tarehe 5 Mei 1981, Mzee Kassim Mapili alistaafu jeshi la Polisi. Baada ya kustaafu Mzee Mapili alijiunga na bendi ya Tanzania Stars iliyokuwa na makao yake katika hoteli ya Margot. Hoteli na bendi zilikuwa zikimilikiwa na Jumuiya ya Ushirika iliyojulikana kama Washirika na hatimae bendi hiyo ilikuja julikana kama Washirika Tanzania Stars.
Wanamuziki na viongozi wa Tancut Almasi Orchestra wakisherehekea ushindi katika Top Ten Show
Mwaka 1982 baada ya semina ya wanamuziki iliyofanyika Bagamoyo Mzee Mapili alikuwa mmoja wapo wa wanamuziki walioanzisha Chama Cha Muziki wa dansi Tanzania, na akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho. Akiwa Mwenyekiti wa chama hicho mwaka 1986, aliweza kukusanya kundi la wanamuziki 57 ambao walitengeneza kund lililoitwa Tanzania All Stars. Kundi hili lilirekodi muziki ambao mpaka leo umekuwa katika kipimo cha juu ambacho hakijafikiwa na wanamuziki wa sasa. Wakati wa uongozi wa Mzee mapili kwa kushirikiana na Umoja wa Vijana wa CCM, Radio Tanzania, BASATA na CHAMUDATA waliweza kufanya shindano la bendi ambalo aina yake haijawahi kurudiwa tena, shindano hili lililoitwa Top Ten Show lilishirikisha bendi kutoka karibu kila wilaya hapa nchini. Uongozi huu aliendelea mpaka mwaka 1990. Mwaka 1993 alikuwa mmoja wa waanzilishi wa Shikamoo Jazz Band na katika bendi hii alitunga wimbo wa Eva uliokuwemo katika album ya kwanza ya bendi hii. Alipoacha bendi hii Mzee mapili alipitia Super Matimila, Gold All Stars, na hata kujiunga na binti wa Mbaraka Mwinshehe katika bendi yake ya Volcano Stars, na kipindi cha karibuni alikuwa akishirikiana na Mrisho Mpoto na wasanii mbalimbali katika muziki. Mzee Mapili ameacha watoto watatu. Hakika Mzee Mapili alikuwa mtu wa watu.
Thursday, February 25, 2016
MZEE KASSIM MAPILI HATUNAE TENA
MZEE Kassim Mapili hatunae tena. Habari ilitufikia jioni hii kuwa Mzee aliingia chumbani kwake Jumanne usiku akitokea kuangalia mechi ya Arsenal na Barcelona, na toka alipoingia hakutoka tena, hivyo jioni ya leo majirani walilazimika kutoa taarifa ambapo polisi walivunja mlango wa chumba cha Mzee na kukuta amefariki. Kutokana na hali ya mwili inaonekana alifariki tangu juzi na hali ya mwili si nzuri. Mzee Mapili alilazwa miezi michache iliyopita Muhimbili kutokan na kuwa na tatizo la moyo, lakini alikusema mwenyewe hata wiki iliyopita kuwa kutokana na kusaidiwa na Salma Moshi, msanii mkongwe anaeishi Marekani kupata Bima ya Afya hali yake imeimarika kwani anapata dawa zote zinazohitajika bila ya matatizo. Siku ya Jumatatu Mzee mapili alishiriki kikamilifu katika kumzika mtangazaji Fred Mosha, na hata kumuimbia marehemu akisikitika kuondoka kwake mapema. MUNGU AMLAZE PEMA MZEE WETU MAPILI
Sunday, February 21, 2016
LEO NDIO SIKU YA MAZISHI YA RAFIKI YETU NA NDUGU YETU FRED CAMILLIUS MOSHA
| RIP FRED MOSHA |
RATIBA YA MAZISHI NI KAMA IFUATAYO;
- SAA 4-5 MWILI UTAPELEKWA NYUMBANI KWAKE CHAMAZI UKITOKEA MUHIMBILI
- SAA 7 MWILI KUPELEKWA KANISA LA RC CHANG'OMBE KWA MISA YA MAZISHI
- BAADA YA HAPO SAFARI ITAANZA YA KUELEKEA MAKABURI YA KINONDONI KWENYE MAKAZI YAKE YA MILELE
- MUNGU MALAZE PEMA PEPONI FRED MOSHA
Monday, February 8, 2016
WAKONGWE WA DANSI TANZANIA KATIKA WIMBO WA PAMOJA- MIAKA 50 YA UHURU
VIDEO HII YA WIMBO HUU MIAKA 50 YA UHURU INA KUMBUKUMBU NYINGI. HAPA WAPO PAMOJA JUKWAANI, KASONGO MPINDA NA KABEYA BADU
Subscribe to:
Comments (Atom)