Shule zote zilikuwa na bendi ya shule. Ambayo kila asubuhi ilipiga muziki wakati wa wanafunzi kukaguliwa kama wamekuja shuleni wasafi, moja ya ndoto za wanafunzi wengi ni kuwa katika bendi ya shule. Aidha kuwa mpiga ngoma au mpiga filimbi na kubwa kuliko yote ni kupata bahati kuwa mshika kifimbo. Shule zilishindana kwa kuzivalisha bendi mavazi bora na upigaji kuwa makini na hivyo siku za sikukuu kila shule ilijitahidi bendi yake ndio iwe bora. Hakika nakumbuka raha iliyokuwepo wakati shule mbalimbali zilipokutana siku ya siku kuu au kukiwa na maandamo na kisha kila bendi kupita mbele ya mgeni wa heshima, wanafunzi tulijitahidi kuwa wakakamavu wenye nidhamu ili shule yetu ishinde. Kila shule ilikuwa na vikundi vya kwaya, ngoma za asili na nyingine kuwa na bendi za muziki wa kisasa. Nilisoma shule iliyokuwa na wahindi wengi, Iringa Aga Khan Primary School, bila kujali kabila wote tulicheza ngoma za asili. Hakika kulikuwa na wahindi wanajua kucheza sindimba kuliko waswahili. Siasa ya Ujamaa iliingia wakati niko darasa la saba 1967. Mambo mengi yalibadilika, nyimbo, ngoma ngonjera, mashahiri yakanza kuwa ni ya kisiasa, nyimbo nyingi za kiasili zikapewa maneno ya kisiasa, maafisa utamaduni ndio walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha hili, kwa kuzunguka kuhamasisha na hata kutoa adhabu kwa vikundi vilivyoonekana havitaki kuimba nyimbo za siasa. Mashuleni tulianza kuimba nyimbo za siasa kwa uwingi zaidi, somo la kuimba lilikuwa likifundisha nyimbo za siasa tu. Kwaya zilizokuwa na nyimbo mbalimbali za siasa kutoka kila upande wa nchi, zilirekodiwa na Radio ya Taifa ambayo kwa wakati huu iliitwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Uzalendo ulikuwa ndio ‘habari ya mjini’. Kila mwisho wa onyesho la muziki bendi zililazimika kupiga ule wimbo wa ‘Chama cha Mapinduzi chajenga nchi (pichani TANU Youth League Mwanza 1966 wakicheza ngoma)
TANU Youth League (TYL) ilikuwa na matawi kila mahala. Kimuziki TYL ilichangia sana, kwani kila kwenye tawi la TYL lazima kulikuwa na kundi la muziki aidha kwaya au ngoma, na mara nyingi vyote na sehemu nyingi TYL pia ilinunua vyombo vya bendi na hivyo karibu kila wilaya ilikuwa na bendi. Hapa ndipo wanamuziki wengi maarufu wa miaka hiyo na ambao nyimbo zao bado maarufu mpaka leo walikotokea. Pale Iringa, vyombo vya TYL hatimae viliishia kuwa chini ya shule ya Sekondary ya Mkwawa na hivyo pale kulikuwa na bendi nzuri sana ambayo iliweza kuja kurekodi RTD, kati ya waliokuwa wanamuziki wa bendi hiyo, mpia solo ni mzazi wa producer mmoja maarufu wa Bongo fleva na hata yeye alikuja kuwa na bendi yake TZ Brothers, mpiga rythm kwa sasa ana chuo kikubwa cha muziki pale Tabata, wakati muimbaji mmoja wa bendi hiyo alianzisha bendi maarufu pale Arusha.