Thursday, July 24, 2014

ABBA KUNDI LA MUZIKI TOKA SWEDEN, LILILOWAHI KUTINGISHA DUNIA



Kundi la ABBA lilianza mwaka 1972, na lilikuwa ni la vijana wanne wa Kiswidi Agnetha Fältskog, Björn Ulvaeus, Benny Andersson, and Anni-Frid Lyngstad. Na kutokana na herufi za kwanza za majina yao ndio wakapata jina la kundi lao ABBA. Katika historia ya muziki wanasemekana ndilo kundi lililofanikiwa sana kibiashara kwa kuwa katika top ten ya mauzo katika nchi mbalimbali duniani kwa kipindi cha miaka 7 kati ya 1975 mpaka. Mwaka 1974 kundi hili ndipo lilipojitokeza kwa kushinda yale mashindano ya muziki wa nchi za Ulaya ya Eurovision Song Contest. Na hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza katika historia ya shindano hilo kwa kundi toka Sweden kushinda,  na pia kwa mara ya kwanza Sweden kuwa na kundi ambalo lilikuja julikana dunia nzima. Kundi la ABBA liliuza zaidi ya album na singles milioni 380. Agnetha na Bjorn  walioana na pia Anni-Frid na Benny walikuwa ndani ya ndoa japo ndoa zote zilikuja vunjika.  Ndoa zao kufikia 1981 zilikuwa zimekwisha vunjika, tatizo kubwa ni kutokana na mzigo wa umaarufu.
Mwaka 1982 kundi lilivunjika japo haijawahi kutangazwa rasmi kuwa kundi lilivunjwa. Wanaume katika kundi hili waliendelea kuwa pamoja wakitunga nyimbo kwa ajili ya michezo ya jukwaani(musicals), wakati akina mama kila mmoja akaanza shughuli kivyake (solo), na umaarufu wa kundi ukaanza kushuka. Filamu ya Mama Mia iliyotoka 1999 ikiwa na nyimbo nyingi za ABBA ilitengenezwa baada ya mchezo wa kuigiza (musical), wenye jina hilo kupata umaarufu sana. Filamu hiyo ndiyo iliyoingiza pesa nyingi zaidi ya filamu nyingine nchini Uingereza kwa mwaka huo. Wimbo wa ABBA, Waterloo,  ambao ndio ulioweza kuwafanya washindi wa Eurovisiona Song Contest ulichaguliwa kuwa ndio wimbo bora uliowahi kutokea katika shindano hili.


Sunday, July 6, 2014

KAMA KAWA EFM 93.7FM INAKULETEA MUZIKI ULITINGISHA ZAMA ZILE, LEO HEWANI TENA USIKOSEE

JUMAPILI NYINGINE NDIO NIMEMALIZA KUKUKUSANYIA NYIMBO NTAKAZOKUPIGIA LEO...LA BAMBA UNAJUA ILITOKA WAPI? DOUBLE OO, NA NYIMBO SITA AMBAZO N SURPRISE, SIKIA SAUTI YA MOSHI WILLIAM TX ALIPOKUWA MDOGO, MSIKILIZE TENA SKEETER DAVIS EFM 93.7FM KUANZIA SAA 2-5 USIKU LEO KWA WENYE INTERNET ANUANI NI HII http://tunein.com/radio/E-FM-Radio-937-s224740/

Friday, July 4, 2014

IJUE BEMBEYA JAZZ YA GUINEA


Bembeya Jazz, hutajwa kama ni nguzo ya historia ya muziki wa kisasa wa Afrika Magharibi. Bendi hii ilianza vipi?
Mwaka 1958 kulikuweko na kura ya maoni katika nchi zilizotawaliwa na Wafaransa Afrika Magharibi ambapo wananchi waliulizwa kama wanataka kuendelea kuwa chini ya Ufaransa, Guinea ndio nchi pekee iliyokataa. Sekou Toure akachaguliwa Rais  wa nchi hiyo, na kati ya vitu alivyoanzisha mara  moja ilikuwa ni Bendi ya Taifa iliyoitwa Syli National Orchestra. Bendi hii iliyokuwa na maskani katika jiji la Conakry iliendelea kukuwa na kuwa kubwa hatimae  mwaka 1961 ikagawanyika katika makundi mawili Bala et ses Balladins na Keletigui et ses Tambourinis. Kutokana na  upenzi wake wa sanaa Sekou Toure alitengeneza bendi za mikoani, ambazo alizifadhili kwa vyombo na fedha. Katika jiji la Beyla kusini mashariki mwa Guinea kwenye mwaka 1961 Gavana wa mkoa huo Emile Conde alianzisha kakundi kake kadogo kakiwa na gitaa moja tu kavu na bila uzoefu mwingi lakini taratibu kakanza kujitokeza. Kabendi haka toka mikoani kalishinda mashindano mengi na kakajulikana sana Conakry, hatimae chama tawala kiliitaka Bembeya ihamie Conakry mwaka 1965, na kakataifishwa na kufanywa bendi ya Taifa kama zile nyingine mbili. Bendi hii ilianza kwa kuitwa Beyla Jazz, lakini siku moja April 1961, katika mkutano wa bendi wakaamua kujiita Mbembeya Jazz
 Wakati huo Guinea kulikuwa na aina mbili za wanamuziki wale waliopiga muziki kutumia muziki wao wa  asili na wale waliotoka kwenye mashule ya Kifaranza amabo walipiga muziki wa asili ya Cuba, kuna amri iliyotolewa na serikali kueleza wanamuziki wapige muziki kutokana na vionjo vya kwao kwenye katikati ya miaka ya 60. Hivyo ukisikia nyimbo za Bembeya Jazz kabla ya hapo unasikia vionjo vya Cuba kama vile Whisky Soda na Mamiwata  ni mfano wa upigaji huo, baada ya hapo na mpaka ilipokuja kurekodi mara ya mwisho bendi hiyo imekuwa na vionjo vya muziki wa asili wa  Guinea
Wakati wa uhai wa Sekou Toure, nchi hiyo ilianzisha record label iliyoitwa Syliphone, ilikuwa label ya Taifa, jambo hilo halikuwahi kufanyika popote Afrika, Tanzania ilijaribu kuiga mfumo huu na iliweza kutoa kazi chache kwa kutumia Tanzania Film Company na  kuwa na label kama TFC na Sindimba.
 Bahati mbaya hali ya uchumi wa Guinea ulipoharibika miaka ya 70 label hiyo ambayo iliyoweza kutoa album 80 ilikufa, na ndipo wanamuziki wa nchi hiyo wakaanza kuelekea Ufaransa. Sekou Toure alifanya kazi kubwa kwa nchi yake kwa upande wa sanaa na kuweza kuifanya Guinea kuwa kati ya nchi zilizoongoza Afrika katika utamaduni wa muziki. Bahati mbaya taratibu alianza udikteta na watu waliompinga wakaanza kupotea au kuuwawa, kama ilivyotokea kwa Fodeba Keita msanii aliyeanzisha kundi la kwanza la Ballet nchini Guinea na Sekou Toure akamfanya Waziri wa Mambo ya Ndani, lakini kufikia mwishoni mwa miaka ya 60, Sekou Toure akawa na wasiwasi kuwa Fodeba atampindua, basi alimfunga na hatimae mtu huyu akapotea, haijulikani alikufa vipi au lini. Pamoja na udikteta huo alikuwa tofauti na Mobutu. Alikuwa mzalendo hakuwa fisadi wa kuiba mabilioni na kuyatorosha nje kama Mobutu, bali aligeuka kuwa katili wa kulinda utawala wake. Pamoja na maelfu ya Waguinea kuikimbia nchi yao kutokana na utawala huu wanamuziki wachache walimlaani kwani wengi walifaidika na fadhila zake katika tasnia ya muziki.

Kufikia mwaka 1980 Bembeya Jazz  ilikuwa haipigi tena maonyesho ya kawaida  labda kwa kukodishwa. Kati ya mambo makubwa ya kusikitisha yaliyokikumba kikundi hiki ni kifo cha muimbaji wao Demba Camara ambaye alifariki gari lao lililokuwa likiendeshwa na dereva wa bendi kupinduka wakiwa safarini, katika gari hilo pia alikuweko Sekou 'Bembeya' Diabate (Diamond Finger). Demba alikutwa ametupwa nje ya gari walipowasili wanamuziki wengine waliokuwa katika gari jingine.
Sekou 'Bembeya' Diabate

Sekou 'Bembeya' Diabate bado anafanya maonyesho lakini hasa nje ya Guinea
Kwa wale wanaojua historia ya sanaa ya Tanzania watajua kuwa Tanzania iliiga baadhi ya taratibu za sanaa za Rais Sekou Toure wa Guinee, kuanzishwa kwa kundi la sanaa la Taifa na hata kuanzishwa kwa bendi ya wanawake,  yalitokana na ziara za Rais huyo hapa kwetu ambapo alikuja kasindikizana na kundi kubwa la wasanii wa kundi la Taifa.